AN-NUUR
Na.156 Rabi' Awal 1419, Julai 4 - 9, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
HABARI ZA MADRASA
[Assasidyiin, Morogoro] [Shamsiya, Handeni] [Akhlaqil Islamiya, Magomeni, DSM]

Assasidyiin Madrasat na Islamic Centre Morogoro

Taasisi ya Kiislamu iliyopata mafanikio Kitaaluma 
 

Inafuata mfumo wa kisasa wa ufundishaji.
Hata hivyo inasumbuliwa na ukata mkubwa

Na Mussa Ally
 

BAADA ya miaka 17 tangu kuanzishwa kwake, leo kituo cha Kiislamu cha Assasdiyiin kimepata mafanikio makubwa hasa kitaaluma, hata hivyo matatizo ya kiuchumi yanakijengea ukuta, gazeti hili limekitembelea kituo hicho hivi karibuni.

Jii,aaa, sam, su, uu, hao….." Hiyo ni sauti ya mmoja wa wakufunzi wa madrast Assasdiyiin akifunza somo ya sanaa ya mapigano (marhsart) ambalo ni moja la masomo muhimu sana chuoni hapo.

Wanaonekana vijana wa kike na wa kiume wakijifunza jinsi ya kushambulia, kukwepa mapigo na kujikinga.

Nyuma ya darasa wapo wanashule wadogo wanaofundishwa mazoezi ya viungo (physical training) wakipasha moto viungo vyao.

Si hayo tu ya kuvutia, bali lugha ya Kiarabu na Kiingereza kufanywa ndiyo lugha rasmi za mawasiliano madrasani hapo ni kitu kingine ambacho taasisi hiyo inapaswa kujivunia.

Masomo kama Hisabati, Sayansi, Akhlaq, Sira, Fiqh, Tawheed, Hadithi, Qur-ran na tafsiri yake yanafunzwa chuoni hapo ili kumpika vyema kijana wa Kiislamu na kumuipua akiwa na msingi imara wa dini yake kama si mustakabali unaoeleweka kwa maisha yake ya baadaye hapa ulimwenguni na kesho Akhera.

Madrasa hiyo na kituo chake cha huduma za jamii, kwa Waislamu, ilianzishwa na Sheikh Ayoub Salum Muwinge, mwaka 1981 katika kata ya Chamwino (ambayo ndiyo makao yake makuu).

Ikiwa katika jengo duni la tope lililoezekwa kwa karatasi kuukuu za kufungia tumbako, taasisi hiyo ilianza na wanafunzi 85 kuufunza Uislamu.

Hadi sasa Assasidyiin Madrassat na Islamic Centre ina jumla ya wanafunzi 150 katika matawi yake mawili yaliyoko katika Kata ya Uwanja wa Ndege na wale wa kituo cha Chamwino.

Kila mwaka kituo hicho kinatoa zaidi ya wanafunzi 30.

Zaidi ya kutoa wahadhiri, waalimu wa dini (wa shule za awali, madrasa za mtaani, msingi, sekondari na vyuo), makhatibu wa misikiti na maimamu, taasisi hiyo pia inaendesha darsa la watu wazima (wake kwa waume).

Akiongea na gazeti hili katika maonyesho ya kitaaluma ya wana wa madrasa hiyo yaliyofanyika Chamwino hivi majuzi, Amiri Mkuu wa taasisi hiyo Sheikh Ayoub Muwinge aliyataja malengo ya baadaye ya taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kujenga kituo cha Afya, kituo cha kulelelea mayatima, shule ya sekondari na ya msingi; halikadhalika kuanzisha mradi wa kilimo cha mazao ya biashara.

"Tumekwishapata eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi huo, na tumepata shamba tayari kwa uzalishaji, tatizo tulilonalo sasa ni la kiuchumi; tunategemea kwa kupitia gazeti hili kuwaomba watu binafsi, makampuni na taasisi nyingine kutusaidia kufanikisha malengo yetu". Amesema kiongozi huyo.

Mwandishi wa makala hii pia alitembelea darasa la shule ya watoto wadogo (Nursery School) iliyoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya tisini kituoni hapo ambayo imesimama kwa zaidi ya mwaka sasa kutokana na matatizo ya kifedha yaliyokikalia kooni kituo hicho.

Hali hiyo ya ukata imeicha madrasat Assasdiyiin ikiwa haina vifaa vya kufundishia na walimu wake wa kujitolea wakifunza chini ya uwezo wao.

Samani zinaelekea ukingoni na jengo lake dogo la makao makuu ambalo bado halijakamilika kutokidhi haja ukizingatia idadi ya wanafunzi.

"Tatizo lingine tulilonalo, ni kukosa ushirikiano toka taasisi za Kiislamu za Kimataifa zilizopo nchini, hususan tunapowaombea nafasi za elimu ya juu vijana wetu wenye sifa za kujiunga na shule za sekondari, vyuo au vyuo vikuu kutokana na hali mbaya kiuchumi ameongeza Ustaadh Habib Salum, mmoja wa walimu waandamizi wa Assasidyii.

Gazeti hili limeshuhudia maendeleo ya madrasa hii pamoja na ukata unaokikabili.

Hivyo, linatoa wito kwa Waislamu ndani na nje ya Tanzania wapelekea misaada ya fedha na vifaa ili kudumisha na kuboresha maendeleo yaliyopo sasa katika madrasa hiyo.

Mawasiliano yafanywe kupitia gazeti hili kwa anuani ifuatayo:

Sheikh Ayoub Muwinge,
Madrasat Assasidyin,
Box 55105,
Simu Na: 181365,
Dar es Salaam.

Wale ambao wangependa kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na madrasa hiyo tunaahidi kuwapa anuani toleo lijalo Insha Allah.

Juu
Ijue Madrasat-Shamsiya Kwediboma, Handeni

MADRASAT Shamsiya inaendeshwa na Ustaadhi Ibrahim Said Makusi mwenye umri wa miaka 32.Yeye binafsi ndiye muasisi wa madrasa hii iliyopo kwenye kitongoji cha Kwa-muonga.

Akizungumza nami kijijini hapo, Ustaadhi Ibrahim alisema jina Shamsiya amelichagua kwa heshima ya madrasa aliyosomea Bwembwera wilayani Muheza. Hata hivyo madrasa hiyo ya Almarhum Sheikh Zubeir Juma sasa imebadilishwa jina na kuitwa Darul-Ulum kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Sheikh Othman Zubeir mwaka 1986.

Madrasat Shamsiya ilianza na wanafunzi 80 wavulana kwa wasichana lakini kwa sasa imebakiwa na wanafunzi wasiozidi 50, kutokana na kwamba wazaziwengi hawawahimizi watoto wao kuhudhuria madrasa.

Watoto wanasoma bila malipo na mwalimu mwenyewe anafundisha bila mshahara. Hii ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kushindikana kuvunja jengo la miti na nyasi na kujenga imara zaidi.

Masomo yanayofundishwa ni Qur’an, Hadith na Fiqh. Kwa upande wa lugha (Kiarabu) na tafsiri ya Wur’an bado hayafundishwi kwa vile Ustaadh Ibrahim anasema mwenyewe bado hayamudu vizuri.

Tatizo la masomo hayo mawili huenda likamalizika karibuni angalau kwa kiwango kidogo kufuatia azimio la pamoja na waalimu wa madrasa tano za Kwediboma; ambapo wale wenye mwangaza watakuwa wakizipitia madrasanyengine kwa zamu.

Utaratibu huo wa kutembeleana ulikubaliwa hapo tarehe 7 Juni 1998, wakati walimu hao walipokutana. Waliokutana ni Ustaadh Shaaban Rashid, Ustaadh Juma Mdingo, na Ustaadhi Omar Ali Maguleti.

Wengine ni Ustaadh Juma Bakar na Ustaadhi Omar Ali Kibwana.

Matatizo sugu ya Madrasat Shamsiya ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na vya kusomea kama vile Chaki, Juzuu, madaftari na vikalio.

Juu

Ijue Madrasatul – Akhlaqil – Islamiya Magomeni Mapipa

Madrasatul Akhlaqil – Islamiya iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam Magomeni Mapipa katika Mitaa ya Magomeni na Mburahati ni maarufu kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na Ufundishaji wake mzuri. Na madrasa hii iliasisiwa na Muasisi Ustadh Salum Mohamed mnamo mwaka 1994 ambapo madrasa hii ilianza ikiwa na wanafunzi 12 na mwalimu mmoja kwa kipindi hicho ilikuwa pale mtaa wa Mburahati. 

Lakini kutokana na ufundishaji mzuri wa mwalimu Idadi ya wanafunzi ilizidi kuongezeka hadi ilipofika mwaka 1995 wanafunzi walikuwa 90. Ndipo madrasa ilihamia mtaa wa Mburahati Na. 28 kwa Mzee Hussein Ally na hapo madrasa ikawa na idadi ya wanafunzi 104 na ikawa na walimu wawili. Na kutokana na ufundishaji mzuri wanafunzi walikuwa wanaogezeka siku baada ya siku hadi kufikia 170 na wakawa wanaongezeka hadi leo wanafunzi wapo 208 na walimu watatu na wasaidizi wawili ambao ni wanafunzi waliosomea hapa hapa chuoni. 

Wanafunzi 180 nafasi ya kukaa ikawa ndogo ndipo ilipobidi kutafuta sehemu nyingine ya kuwaweka wanafunzi na akajitokeza Bibi Mlekwa na kutoa nafasi hapo Mtaa wa Magomeni Na. 6 na ina nafasi nyingine kwa nyuma. 

Kuna kiwanja kizima cha kujenga chuo.

MATATIZO

Madrasa hii ina kiwanja hapo Mtaa Magomeni No. 6 ambacho inatarajia kukijenga kwa hiyo inaomba mtu mwenye uwezo wa kuweza kujenga ili kuukoa jamii ya Kiislamu.

Juu 
 

YALIYOMO
 
TAHARIRI 

Maoni yetu:Tusianze kuulizana tena shida yenu nini 

Agizo la Rais Mkapa lapuuzwa:Wazee wa miaka 80 wateseka Gerezani

Wanawake wasema hawatarudi nyuma mpaka dhulma iondoke

Serikali kuzuia mahubiri ya Waislamu, kuvamia Msikiti, kukamata, kudhalilisha na kuua Wananchi ni kuvunja Katiba na Sheria za Nchi

Kujua lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah
Na Sadick M. Sadick"

Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi

Intifada ndio jibu (2)
Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Kusema ukweli ni sehemu ya uadilifu
A.S. Chachika

Mafumbo ya imani yabakie ndani ya Makanisa
Na J. Hussein

Majibu kwa Kamara Kusupa

Tamko la Wanawake wa Kiislamu mkoa wa Morogoro kuhusu kadhia ya Mwembechai

Asiye na elimu kwa mujibu wa Biblia
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

TAMTA yaadhimisha miaka 36
Na Masoud Mohamed Said, Tanga

Muumini aliyeachiwa aeleza jinsi Waislamu wanavyoteswa Segerea
Na Muhibu Said

Wakwama kujenga msikiti kwa miaka 30

Habari za Madrasa

Barua 

Mashairi 

Lishe : Mtoto anyonye maziwa ya mama miaka miwili 
Na Dk. Ali. A. Mzige
  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita