|
|
|
Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi KWA kuwa watu wengi wametoa nasaha zao kuhusu serikali yatu ya ukweli na uwazi na ya wachamungu ilivyoshughulikia suala la vurugu za Msikiti wa Mwembechai. Na kwa kuwa mpaka sasa serikali yetu bado imekaa kimya kuhusu dhuluma za wazi wanazotendewa Waislamu kinyume cha katiba na sheria za nchi, na kwa kuwa kuna usemi unasema kuwa tembo anauawa kwa mishale mingi, nimeona nami nitoe mchango wangu. Mwandishi wa makala hii S.M. Msuya anaelezea zaidi. Historia ya nchi hii inaeleza wazi kuwa Waislamu ndio walianzisha harakati za kudai uhuru kutoka kwa Wakoloni na wakashiriki kikamilifu kuhamasisha wananchi mpaka uhuru ukapatikana 1961. Baada ya kupata uhuru mbinu zilitumika kuwaengua Waislamu katika uongozi – nafasi zote nzuri wakapewa Wakristo ingawa wakati wa kupigania uhuru kanisa lilikuwa limeungana na wakoloni kupinga harakati za kudai uhuru. Bila shaka kanisa mwanzoni lilikuwa na haki ya kuungana na serikali ya Kikoloni kupinga harakati za kudai uhuru kwani walikuwa wakinufaika! Sababu ya pili ni kwamba kanisa tangu mfalme Kostantine limekuwa likiegemea kwenye serikali zinazotawala ili liweza kudumu. Kwa kuwa serikali ya Kikoloni ilikuwa inapiga vita Uislamu ikishirikiana na kanisa – baada ya uhuru kanisa lilihakikisha kuwa uongozi wa nchi unashikwa na Wakristo ili kuendelea kuzima harakati zozote za kuendeleza. Uchaguzi wa Viongozi Ingawa katika awamu zote wamekuwapo viongozi wachache Waislamu katika ngazi mbali mbali serikalini lakini ni ili tu Waislamu waamini kuwa serikali haina ubaguzi wa dini. Kuchaguliwa kwa Waislamu katika madaraka yajuu serikalini kuwaangaliwa zaidi msimamo wao katika Imani ya dini yao – wenye imani na msimamo wa dini wanaonekana ni hatari kupewa madaraka ya juu. Viongozi hao, aidha kwa kutojua au kwa ajili ya maslahi ya kidunia wamekuwa wakitumiwa mara zote kuzima harakati za Waislamu kueneza dini yao au kudai haki zao za kikatiba na sheria. Hekima ya kukaanga pweza kwa mafuta yake ndiyo inayotumika. Mwaka 1968 viongozi Waislamu waliokuwa madarakani walitumiwa kuunda BAKWATA ili kuzima maendeleo ya Waislamu na Uislamu baada ya serikali kuvunja chombo halali cha Waislamu E.A.M.W.S. (East African Muslim Welfare Society). Ni miaka 30 sasa tangu dude hili BAKWATA lianzishwe lakini Waislamu bado wako nyuma ki-elimu,ki-afya na ki-uchumi. BAKWATA imekuwa ikitumiwa na serikali kujibu malalamiko ya Waislamu dhidi ya Serikali. Taasisi yoyote ikitaka kufanya jambo lolote la kusaidia Uislamu na Waislamu BAKWATA INALETA VIPINGAMIZI NA VISINGIZIO MBALIMBALI. Serikali inafahamu wazi kuwa Waislamu wa Tanzania hawapendi uongozi uliopo madarakani kwenye BAKWATA. Ndiyo sababu Waislamu wakalazimika kuanzisha taasisi nyingine zitakazojali maendeleo ya Waislamu ya Uislamu. Lakini kwa kuwa serikali inatambua BAKWATA tu, taasisi zingine hata zikitoa hoja yeyote hazisikilizwi. Ni hivi karibuni tu taasisi hizo zimetishiwa kufungwa. Mapambano ya Mwembechai Ingawa inaeleweka wazi kuwa serikali ndiyo iliyoanzisha vurugu hizo baada ya kushinikizwa na Paroko Lwambano kuwa Yesu ametukanwa serikali kabla ya kufanya uchunguzi imewaua Waislamu na kujeruhi wengi na wameswekwa rumande wengi na mpaka sasa wamenyimwa dhamana. Wakristo walioshikwa pamoja na Waislamu wamepewa dhamana. Kina mama waliokuwa wanafanya Ibada Msikitini siku hiyo walisombwa na polisi baada ya kupigwa sana. Huko rumande walidhalilishwa kiasi kisichoelezeka. "Ingawa waliachiliwa baadaye bila ya kupelekwa mahakamani ikafahamika kosa lao. Waislamu wengine mpaka sasa wanateseka rumande, kesi zao hazijaanza kusikilizwa mpaka sasa. Tunategemea kuwa wakati kesi za akina Magezi zitakapoanza kusikilizwa, Paroko Luambano ataitwa kutoa ushahidi ili haki iweze kutendeka. Kama serikali itaamua kuwaachia bila kesi zao kusikilizwa hatuwezi kuamini kuwa wamehurumiwa basi tutaamini ni mbinu za kuwakomoa na kuwaziba midomo. Propaganda ya vyombo vya habari Baada ya mapambano ya Mwembechai vyombo vyote vya habari nchni vimekuwa msitari wa mbele kuendesha propaganda za shutuma dhidi ya Uislamu na Waislamu. Majina kama mjahidina, siasa kali, msimamo mkali yamekuwa yakitumika kumaanisha kuwa Waislamu wa aina hiyo ni watu wa hatari kwa jamii. Hata hivyo tunashukuru kwa kuwa vyombo vingine vinatumia jina la -–Mjahidina – ingawa wanatumia jina hilo kwa nia mbaya. Matukio yanayowahusu Waislamu na Uislamu yasiyopendeza yamekuwa yakipigiwa ngoma na vyombo vya habari. Yale mazuri kwa Waislamu yamekuwa yakipotoshwa au kutangazwa kwa kejeli. Hii inadhihirisha chuki iliyopo dhidi ya Uislamu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu katika Qur-ani Sura 3:118-120 ametutahadharisha juu ya hilo. Mbinu za kudhibiti harakati za Uislamu Pamoja na kwamba tumeambiwa kuwa serikali inatambua haki ya dini zote na Rais anawapenda sana Waislamu tunakukuwa na wasi wasi kuwa upendo huo mbona unafanana na ule wa simba na punda wa dobi? Upendo wa kuraruliwa kwa makucha na kuliwa! Tumelazimika kuamini hivyo kwa sababu zifuatazo:- Baada ya tukio la Mwembechai Waislamu wameomba ruhusa kuandamana kwa amani kupeleka malalamiko yao kwa viongozi wa serikali lakini walinyimwa kibali. Siku hiyo tulishangaa kuona ndege za helikopta zikizunguka jiji la Dar es Salaam eti kuzuia maandamano ya Waislamu. Laiti helikopta hizo zingetumika wakati ule wa ajali ya M.V. Bukoba zingeokoa watu wengi ambao baada ya meli kupinduka walikuwa wakielea kushikilia mikungu ya ndizi mpaka wakaishiwa nguvu na kufa maji. Kina mama walitaka kufanya mkutano wao kuelezea madhila ya wenzao waliyofanyiwa huko rumande wakanyimwa kibali – eti kwa ajili ya usalama. Ingawa mkutano huo ulifanyika hivi majuzi katika msikitiwa Sinza haukupewa hadhi yeyote. Viongozi wetu wa dini waliendelea kukamatwa bila taratibu usiku wa manane bila hata hati zinazotambulika ki-sheria. Viongozi wetu waliokamatwa tangu mwezi Februari mpaka sasa wanasota rumande lakini Wakristo ambao wanatuhumiwa pamoja wamepewa dhamana wako nje. Chuki Athumani, mtoto wa shule ambaye alipigwa risasi na polisi siku hiyo ya tukio bado anateseka Muhimbili. Binadamu yeyote aliye na huruma akimwona Chuki Athumani hali yake ilivyo anatokwa na machozi. Ingawa tuliambiwa kuwa vurugu za Mwembechai zilisababishwa na wakorofi wachache – tunashangaa mpaka sasa msikiti unalindwa na polisi usiku na mchana – na wanasali watu wachache tu. Tulitegemea kuwa kwa kuwa wakorofi wamekamatwa wako rumande na hakuna vurugu tena msikiti ungerudia hali yake ya kawaida. Hao wanaoitwa wadhamini wa msikiti waliokabidhiwa msikiti ambao askari wanawalinda sijui watalindwa mpaka lini kwani mjahidiana wanazaliwa kila siku. Mwisho tunaomba Mwenyezi Mungu awape subra ndugu
zetu wote wanaoteseka huko rumande/jela kwa sababu tu ya kutangaza Imani
yao na wale tutakaofuata. Pia awarehemu na kuwapa Pepo ya Firdous wote
waliokufa na watakaokufa katika harakati ya kuusimamisha/kuutetea Uislamu.
|
TAHARIRI Maoni yetu:Tusianze kuulizana tena shida yenu nini Agizo la Rais Mkapa lapuuzwa:Wazee wa miaka 80 wateseka Gerezani Wanawake wasema hawatarudi nyuma mpaka dhulma iondoke Kujua
lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah
Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi Intifada
ndio jibu (2)
Kusema
ukweli ni sehemu ya uadilifu
Mafumbo
ya imani yabakie ndani ya Makanisa
Tamko la Wanawake wa Kiislamu mkoa wa Morogoro kuhusu kadhia ya Mwembechai Asiye
na elimu kwa mujibu wa Biblia
TAMTA
yaadhimisha miaka 36
Muumini
aliyeachiwa aeleza jinsi Waislamu wanavyoteswa Segerea
Wakwama kujenga msikiti kwa miaka 30 Lishe
: Mtoto anyonye maziwa ya mama miaka miwili
|