AN-NUUR
Na.156 Rabi' Awal 1419, Julai 4 - 9, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mafumbo ya imani yabakie ndani ya Makanisa

Na J. Hussein

DHANA ya fumbo la imani si ngeni miongoni mwa jamii mbali mbali ulimwenguni, hususan zile ambazo katika mchanganyiko wake kuna idadi isiyo haba ya waumini wa dini ya Kikristo. Hali hii inatokana na ukweli kwamba mafundisho mengi ya dini hii yanapigana na hoja za kifalsafa na kweli za kisayansi – hivyo basi ili kukabiliana na udadisi ambao ni hulka ya akili ya mwanaadamu ni lazima yapewe pa kushika. Mshiko huu ndio unaoitwa fumbo la imani. Hii basi ina maana kwamba katika imani ya Ukristo nguvu ya hoja haina nafasi.

Haina nafasi kwa sababu ili hoja iwe na nguvu ni sharti iwe imejengwa au katika nadharia ya kifalsafa – yaani mpangilio wa maswali na majibu usio kanushika, au katika kweli tunazozijua kupitia katika sayansi ya maada (Physical sciences).

Mtu yeyote atakayejaribu kutoa nafasi kwa nguvu ya hoja katika imani yaUkristo atajikuta anakwenda haraka sana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mara tu pale mtiririko wa hoja utakapoonekana kushinda ghafla mtoa hoja atajikuta akijikwaa katika kisiki cha FUMBO LA IMANI. Yaani atajikuta akiambiwa kuwa chochote kile ambacho kwa mujibu wa hoja zake hakiingii akilini katika imani hiyo, hilo ni fumbo la imani. Kama mhusika ni Mkristo atajikuta anakabiliwa na uchaguzi wa moja kati ya mambo mawili: Au afikie uamuzi kuwa hoja zake zote hazikuwa na maana yeyote na hivyo aachane nazo na kuendelea na imani yake ya Ukristo, au ang’ang’anie hoja zake – akatae kuburuzwa, na hivyo ashuhudie Ukristo wake ukisambaratika.

Hata hivyo anasa hii ya uchaguzi anayo Mkristo wa zama hizi tu. Zama zilizotangulia – kama historia ya zama za kati katika Ulaya (Kitovu cha Ukristo) inavyoonesha, mkiristo yeyote aliyeng’ang’ania nguvu ya hoja alijikuta akitangazwa kuwa ni mwasi na adhabu ya mwasi ilikuwa ni kuuwawa – angalabu kwa kuchomwa moto akiwa hai na huku akiwa amefungwa madhubuti kwenye kigingi. Kama historia ilivyorekodi, watu wengi kule Ulaya walikumbana na mauti ya aina hii.

Ni muhimu ikaeleweka kuwa katika zama tulizonazo,mbali ya kwamba hakuna hatari tena kwa Mkristo yeyote kuuawa kwa sababu mbali mbali bado Ukristo una wafuasi wengi Ulimwenguni. Hawa kwa kutumia uzito wa fumbo la imani wanaendelea kuamini kuwa: Ulimwengu na kila kilichomo vilumbwa katika muda wa siku sita – na katika siku hizi sita jua liliumbwa katika siku ya nne! Baba ni Mungu, Mwana naye ni Mungu, na Roho Mtakatifu ni Mungu – ila hakuna Miungu watatu bali ni mmoja tu! Kujificha kufuatia kitendo chao cha kula katika mti uliokatazwa; Mungu alipigana mieleka na Yakobo (mwanadamu) na kushindwa; Yesu na Baba umri wao ni mmoja lakini Yesu ndiye mwana pekee wa Mungu wa kumzaa; Yesu ndio Mungu Mkuu na Mwokozi wao (Wakristo); baada ya kusulubiwa siku ya Ijumaa saa tisa jioni Bwana Yesu alikaa kaburini kwa muda wa siku tatu mchana na usiku, mbali ya kwamba alifufuka saa nne asubuhi ya siku ya Jumapili; wao ni Waisraeli wa Kiroho. Kwa kuwa Bwana Yesu hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israel; n.k.

Imani ni imani na ni lazima ieleweke kuwa Mkristo ana haki ya kuyaamini yote haya na mengine mengi zaidi ukitaka. Hata hivyo ni lazima zaidi ieleweke kwamba imani kama hizi hazina nafasi kabisa katika ulimwengu ambao maamuzi yake ni matokeo ya fikra zilizochunjwa na hoja zisizo kanushika. Kwa kifupi, nje ya kuta nne za kanisa. Kinyume cha utaratibu huu ni migongano isiyo na maana na ambayo inaweza ikawa hata ya hatari sana kamailivyotokea Ulaya katika karne za nyuma pale watakatifu wa huko walipojaribu kusimika imani zao katika sera zilizoongoza maisha ya kila siku ya wananchi.

Nimelazimika kuuweka huu utangulizi mrefu ili utusaidie kuielezea nukta ambayo kwa mawazo yangu ni ndogo sana japo madalali wa fitna kama kawaida yao wameshaanza kujaribu kuipa ukubwa wa mlima Kilimanjaro. 

Nukta yenyewe ni kuhusu kuzinduliwa kwa DAR ES SALAAM ISLAMIC CLUB. Klabu hii ya kijamii imeundwa kwa minajili ya kuwakutanisha Waislamu wa kada mbali mbali ili mbali ya kujuana na kuwa karibu waweze kwa pamoja kushauriana na kupanga harakati za kuuendeleza Uislamu.

Miongoni mwa walioshiriki uzinduzi huu ni pamoja na baadhi ya maafisa wa jeshi ambao ni Waislamu, baadhi ya wafanyabiashara maarufu wa Kiislamu, na baadhi ya Wabunge Waislamu. Pamoja na wote hawa pia alikuwamo Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Alhaj Ali Hassan Mwinyi ambaye imeelezwa kuwa ndiye mlezi wa Klabu hiyo.

Katika nchi ya kawaida – kwa maana kwamba wananchi wake ni watu wa kawaida – yaani wenye uwezo mzuri wa kufikiri na kunena kwa hoja zisizo na mashaka, uzinduzi wa klabu kama hiyo ungeonekana ni jambo la kawaida na ambalo lisingeweza kumpotezea mtu muda wake mwingi kuliandikia makala. Lakini Tanzania sio nchi ya kawaida. Ni nchi ambayo wananchi wengi hususan wale ambao si Waislamu wanapata matatizo ya kuyaona mambo katika uhalisi wake. Ni nchi ambayo serikali inayodai kutoegemea upande wowote kidini haioni mgongano wowote kumkamata na kumweka ndani mwananchi ambaye ameiremba baiskeli yake kwa maandishi "YESU SI MUNGU’ na kumwachia kila anayetaka aandike madala dala yake kuwa "Yesu ni Mungu". Kwa kifupi Tanzania ni nchi ambayo imani za mafumbo zinashinikizwa – kwa kutumia nguvu za dola pale inapobidi, ziwe ndio mwongozo wa taifa.

Katika mazingira kama haya haishangazi hata kidogo basi kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kuhoji: Ni vipi Waislamu waachiwe waanzishe klabu yao? Ni vipi rais Mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aachiwe aendelee kuwa mlezi wa klabu hiyo kwa utulivu? Kuwa Wakristo nchini wanazo taasisi na klabu kama hiyo lukuki hilo kwa vyombo hivi vya habari sio suala. Kwao suala ni kwa nini na Waislamu nao? Au kuwa baadhi ya viongozi wa Kikristo serikalini si tu kwamba ni wanachama maarufu wa baadhi ya taasisi za Kikristo, bali vile vile ni viongozi katika taasisi hizo kwa vyombo hivi vya habari kwao sio suala. Suala kwao ni kwa nini na Waislamu nao?

Ni dhahiri kabisa kuwa watu wasiojua thamani ya nguvu ya hoja ni kupoteza muda kuongea nao kwa utaratibu huo. Ni kwa mantiki hiyo ningependa kuwasiliana na magazeti ya Mfanyakazi na lile la Kiongozi kwa mtindo ufuatao:

Gazeti la Mfanyakazi Na. 12128 la Jumamosi, tarehe 13 Juni, 1998 limejaribu sana kumjengea msomaji taswira kwamba uzinduzi wa Dar es Salaam Islamic Club hauna nia yoyote zaidi ya udini. Kwa hoja kwamba, klabu hiyo inabagua wasio Waislamu. Ni kweli kabisa hii ni klabu ya Waislamu watupu hivyo basi kama yuko yeyote asiye Muislamu ambaye amevutiwa nayo na angependa kujiunga aende akasilimu kwanza! Kama mabwana na mabibi Mfanyakazi mnaona kuwa sharti hili linakiuka sheria za nchi basi kafungueni kesi mahakamani ambapo nina uhakika kabisa kuwa suala la nani ana udini kati yenu na wenye klabu yao litwawekwa bayana. 

Hata hivyo nachukua fursa hii kuwapongezeni kwa kutuandikia orodha ndefu ya Waislamu mashuhuri wageni waalikwa kwenye uzinduzi wa klabu hiyo. Inatia faraja kugundua kuwa kumbe kuna Waislamu wengi tu mashuhuri kiasi cha kuonewa kijicho ilhali tumeshazoea kuambiwa mara kwa mara kwamba vinafasi vichache tunavyopata katika mgawanyo wa madaraka nchini tushukuru kwani Waislamu wenye sifa ni adimu kupatikana.

Nalo gazeti la Kiongozi toleo la June 13-19,1998 kupitia kwa Mchungaji Christopher Mtikila, limemshutumu Alhaj Ali Hassan Mwinyi kwa kujihusisha na shughuli za Dar es Saaam Islamic Club. Katika shutuma zake limemtaja Alhaji Mwinyi kama kiongozi anayepaswa kuheshimiwa na hivyo ana wajibu wa kusaidia umma wote wa Watanzania wote bila kujali dini. Upuuzi wa madai kama haya unatisha. Alhaj Mwinyi hivi leo ni kiongozi? Kwa mujibu wa Katiba ipi? Ama kuhusu wajibu wa Alhaj Mwinyi kuwasaidia wananchi wote bila kujali dini zao, ningemshauri Bwana Mtikila amsihi Alhaj Mwinyi awe mlezi wa kitengo chake cha Liberty Desk ambacho kinaonekana kupwaya sana hivi sasa. Mtikila asiwe na wasiwasi kwani sifa aliyonayo Alhaj Mwinyi ya huruma, ukarimu na roho isiyo na magutugutu inaeleweka hata kwa watoto wadogo. Nina hakika kabisa kuwa kama Alhaj Mwinyi atakuwa hana shughuli nyingi bila shaka yoyote atalikubali ombi kama hilo kwa moyo mkunjufu na uso wa bashasha hata kama litakuwa linatoka kwa mtu yule yule ambaye enzi za Urais wake, aliongoza kundi la wale waliokuwa wakimshutumu.
 

Juu 
 

YALIYOMO
 
TAHARIRI 

Maoni yetu:Tusianze kuulizana tena shida yenu nini 

Agizo la Rais Mkapa lapuuzwa:Wazee wa miaka 80 wateseka Gerezani

Wanawake wasema hawatarudi nyuma mpaka dhulma iondoke

Serikali kuzuia mahubiri ya Waislamu, kuvamia Msikiti, kukamata, kudhalilisha na kuua Wananchi ni kuvunja Katiba na Sheria za Nchi

Kujua lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah
Na Sadick M. Sadick"

Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi

Intifada ndio jibu (2)
Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Kusema ukweli ni sehemu ya uadilifu
A.S. Chachika

Mafumbo ya imani yabakie ndani ya Makanisa
Na J. Hussein

Majibu kwa Kamara Kusupa

Tamko la Wanawake wa Kiislamu mkoa wa Morogoro kuhusu kadhia ya Mwembechai

Asiye na elimu kwa mujibu wa Biblia
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

TAMTA yaadhimisha miaka 36
Na Masoud Mohamed Said, Tanga

Muumini aliyeachiwa aeleza jinsi Waislamu wanavyoteswa Segerea
Na Muhibu Said

Wakwama kujenga msikiti kwa miaka 30

Habari za Madrasa

Barua 

Mashairi 

Lishe : Mtoto anyonye maziwa ya mama miaka miwili 
Na Dk. Ali. A. Mzige
  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita