|
|
| Serikali
kuzuia mahubiri ya Waislamu,
kuvamia Msikiti, kukamata, kudhalilisha na kuua Wananchi ni kuvunja Katiba na Sheria za Nchi Hivi karibuni palijitokeza dhulma na mauaji yaliyofanywa na jeshi la polisi Tanzania dhidi ya Waislamu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Vurugu hizo zilianza mnamo tarehe 12/2/98 pale polisi walipomkamata kiholela na pasipo nidhamu Sheikh Magezi kwa madai kuwa siku za nyuma alifanya mhadhara wa kashfa. Tukio la kukamatwa kwa Magezi lilifuatiwa na matukio mengine ya kinyama ambapo katu yalisingetegemewa kutokea katika nchi kama Tanzania inayodai kuongozwa na misingi ya demokrasia na haki za binaadamu. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na kuvunjwa milango ya msikiti, kupigwa mabomu ya sumu ndani ya msikiti, kuwapiga na kuwadhalilisha Wanawake wa kiislamu kijinsia, kuuawa pamoja na kujeruhi watu wengi kwa bunduki na mabomu. Mambo yote haya yalifanywa huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Makamba) Kamanda wa polisi wa Mkoa bwana Gewe na viongozi wengine wa serikali wakishangilia kwa furaha na kujipongeza. Hatuna hakika na Rais Mkapa kwani kimya kinatafsiri nyingi. Katika tukio hili kuna mambo mengi zaidi ambayo yanakiuka katiba ya nchi, sheria mbalimbali za nchi na mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binaadamu ambapo Tanzania ni msaini au imeipitisha. Ni mambo hayo yanayotufanya tujiulize mara mbilimbili kama kweli serikali ya Rais Mkapa bado inaheshimu misingi ya demokrasia na haki za binaadamu au inachukua muelekeo mwingine! Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayokiuka misingi ya haki za binaadam. (a) Kuvunja msikiti na kuwapiga Waislamu. Mambo yote haya yalifanywa usiku wakati palikuwa na utulivu mkubwa na waislamu wakiwa katika ibada zao. Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba mara baada ya kuvunja milango ya msikiti askari waliingia na buti zao na kuanza kuwapiga mabomu, virungu na kuwavua nguo wanawake wa kiislamu ambao hawakuwa na silaha yoyote na wala hawakukataa kukamatwa. Inashangaza sana kuwa hata baada ya kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi Waislamu hawa waliendelea kupigwa na virungu vichwani na sehemu zingine za mwili. Hii inapingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo sheria mama. Kifungu cha 13(6)(d) kinasema: "Kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binaadamu, heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai na katika shughuli nyingine ambapo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru, au katika kuhakikisha utekelezaji wa adhabu". Tukio zima la kuvunja msikiti na kuwapiga mabomu, marungu pamoja na kuwadhalilisha kimwili Wanawake wa kiislamu ambao hawakufanya jaribio lolote la kujitetea kwa nguvu zozote ni uvunjaji wa katiba kama kifungu hapo juu inavyojieleza. Kifungu 13(6)(e) kinasema: "Ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha." Kitendo cha kupiga mabomu ya sumu msikitini,askari wa kiume kuwavua nguo Wanawake na kuwapiga virungu ni vya kinyama na hivyo vinadhalilisha na kuwatweza na kwa hivyo ni kinyume cha katiba. Kifungu cha 18 cha katiba ya muungano kinatoa uhuru wa kuabudu na kwamba serikali inathamini na kuheshimu dini zote. Je, uhuru huo na heshima itapatikana wakati waumini wanadharauliwa imani zao kwa mtu kuingia na viatu msikitini na kuwadhalilisha wake za watu? Kwa mjibu wa kifungu cha 26 cha Sheria za mwenendo wa Jinai (Criminal procedure Act of 1984) pale inapobidi mwanamke kusachiwa, askari wa kike ndiyo atakayefanya hivyo. Kama palikuwa na sababu yoyote ya wanawake waliopigwa na kuteswa ndani ya msikiti kusachiwa, Jeshi la polisi kama lingetaka kupata uhalali wa kisheria lingewatumia askari wa kike kuingia upande wa wanawake na kuwasachi, lakini siyo maaskari wa kiume kuwavua nguo akina mama ambao wengine ni umri wa mama zao. (b) Kupiga risasi ovyo na kuuwa, kutesa na kukamata ovyo raia Siku iliyofuata askari polisi wote hata waliokuwa na mapumziko ya ugojwa walijazana maeneo ya Mwembechai wakiwa na silaha kali. Wengi tulishuhudia kupitia televion ya I.T.V na wengine kwa macho yetu, raia wasiokuwa na silaha zaidi ya mawe wakipigwa risasi ovyo na mapolisi ambao si ajabu walikuwa wengi kuliko raia. Hata kama hao raia walikuwa na kosa na walipinga kukamatwa na polisi kwa kutumia nguvu ya mawe, bado polisi hawakuwa na haki wala sababu yoyote ya kimazingira kutumia mauaji ya kikatili kama walivyofanya. Vurugu nyingi kama hizi zimetokea katika nchi mbalimbali kama vile Palestina, Kenya na hata hapa Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambapo watu walifikia hata kuuana huko Arusha, lakini bado mauaji ya kinyama kama haya hayakufanywa na Jeshi la polisi. Kifungu cha 21 cha sheria za mwenendo wa Jinai 1984 (CPA) inamruhuru ofisa wa polisi kutumia nguvu ambazo ni stahili (reasonable) pale mtuhumiwa anapopinga kukamatwa. Katika mazingira ya tukio la Mwembe Chai nguvu zilizotumika hazikustahili (unreasonable) katika mazingira ambayo Wananchi walikuwa na mawe tu na polisi walikuwa mamia ingekuwa rahisi kuwatenganisha kwa kutumia mabomu ya machozi tu. Kutokana na taratibu za polisi (police regulations) katika mazingira kama ya mwembechai hata kama ingebidi kutumia risasi wangetumia risasi za mipira (plastic bullets) na siyo risasi za moto (live bullets) kama wanapigana vita na jeshi lingine. Na hata kama wangekuwa hawana njia nyingine wangepiga miguuni kama taratibu za polisi zinavyosema. Tofauti ni kwamba, ofisa wa polisi alikuwa akitoa amri zinazothibitisha wazi kuwa walikuwa na lengo la kuuwa hata watu wote. Kifungu cha 4(1) cha mkataba wa kimataifa dhidi ya utesaji, ukatili na unyama mwingine (convention againts Torture and other Cruel, in human or degrading Treatment or purnishment) (1984) ambapo Tanzania ni msajili kinasema: Kila nchi mwanachama itahakikisha kwamba vitendo vyote vya utesaji vinafanywa kuwa makosa ya jinai. Tanzania kama nchi mwanachama imetekeleza hayo kwa kuingiza katika katiba ya Jamhuri ya Muungano, Bills of Rights ambapo kifungu cha 13(6)(e) kama tulivyokinukuu juu kinafanya kitendo hicho kuwa kosa la jinai hata kama zimefanywa na polisi (Taz pia mkataba wa kimataifa wa mambo ya ndani ya kisiasa na kiraia). Katika kesi ya Kombe askari wawili walioshiriki katika mauaji ya kinyama ya marehemu Kombe walihukumiwa kifo pamoja na kwamba walifanya kitendo hicho wakiwa kazini chini ya msimamizi wao. Kubwa zaidi ni kwamba vitendo vilivyofanywa na polisi mwembechai vimekiuka msingi mkubwa wa haki za binaadamu unaojulikana kama haki ya kuishi (right to life) ambayo imezungumziwa katika kifungu cha 14 cha katiba na Jamhuri ya Muungano kama kinavyonukuliwa hapo chini: "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata toka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria" Polisi hawakuwa na haki yoyote ya kisheria kudhulumu haki za raia wake za kuishi. Hata kama raia hawa walifanya makosa dhidi ya serikali bado serikali siyo mahakama. Kifungu cha 4 cha katiba kinaeleza wazi kuwa haki ya kuhukumu iko chini ya mahakama. Na kubwa zaidi ni kuwa polisi hawana uwezo wa kisheria wa kujua kuwa mtu fulani amefanya kosa, kazi na ujuzi huo uko chini ya mahakama na hata kama wana ujuzi huo, hawawezi kumhukumu mtu bila kumpa nafasi ya kujitetea na pia hukumu ya kufanya mihadhara ya kashfa au kutotii amri ya polisi siyo kifo. Kifungu 13(6)(b) cha katiba kinasema: kwamba Ni marufuku kwa mtu aliyeshitakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. (Tz pia tamko la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa). Ni dhahiri kwamba vitendo vilivyofanywa na jeshi la polisi kuwauwa raia zake hata watoto wasio na hatia, kuvamia nyumba za watu, kuvunja msikiti, kudhalilisha akina mama na kutumia risasi ovyo na kuelekeza mbele ya kundi la watu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu ambao usingefanywa hata na serikali ya kikoloni na ile na vinapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria. (c) Mihadhara ya kashfa kama chanzo Siku chache kabla ya tukio, Askofu Pengo na Paroko wa Kanisa la Katoliki ya Mayahudi dhidi ya Wapalestina na alitoa tamko la kuikemea serikali kuwa imeshindwa kuidhibiti vikundi vya Waislamu wanaoendesha mihadhara ya kashfa. Tulitegemea kuwa serikali ingetoa onyo kali kwa Paroko huyo, lakini kilichofuatia ni serikali kutangaza vita na waumini wa Msikiti wa Mwembechai chini ya Bwana Makamba. Alipotakiwa atoe tafsiri ya kashfa Bwana Makamba na hata Waziri Ameri hawakufanya hivyo, pengine ni kwa sababu hawajui sheria. Katiba ya Jamhuri kifungu 19(i) + (ii) kinatoa uhuru wa kutangaza, kuchunguza na kutoa mawazo juu ya dini yake ama nyingine. Haki hiyo hiyo inatolewa na mkataba wa kimataifa wa mambo ya ndani ya kisiasa na kijamii (Internal covenant on Civil and Political rights) kifungu 18(1), (2). Serikali baada ya kuelezwa kuwa viongozi hawa hawa wa kikatoliki wanashiriki katika kuuza vitabu vya kashfa dhidi ya Uislamu katika maduka yao ya vitabu hamna ilichofanya. Katika duka la vitabu la M. Joseph mjini Dar es Salaam na la Msimbazi Mission vitabu vingi vinavyokashifu dini ya kiislamu vilivyoandikwa kwa kutumia aya za Qur’an na biblia vinauzwa. Mfano kitabu cha Wana wa Ibrahim kilichoandikwa na Padri Angelu) (ambaye sasa ni marehemu). Mbona Kadinari, Mheshimiwa Pengo hilo halioni kuwa baya wakati wino ni mzito kuliko ulimi". Si hivyo tu huko Kigoma Muhubiri mmoja wa kikristo aitwaye L.M. Charange wa T.A.G tarehe 1/9/1995 alichoma moto Qur’an na alijigamba kwa dharau kwamba kama angelikuwa amebanwa na mkojo angekojolea Qur’an hiyo. Taarifa zilifikishwa polisi na muhusika alikiri kosa hilo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yake. Vile vile mnamo tarehe 1/12/1997 muhubiri mwingine wa Kikristo wa dhehebu la Pentekoste alihubiri katika kanisa moja Kakonko wilaya ya Kibondo mkoa wa Kigoma, katika mahubiri yake alitoa matusi na Kashfa nyingi dhidi ya Waislamu na Mtume Muhammad (S.A.W) miongoni mwa matusi na Kashfa hizo ni: 1. Wanawake Waislamu huingia Msikitini bila ya kuvaa Chupi ili waziniwe na majini Msikitini. 2. Alitafsiri Suratil Faatiha kimatusi. 3. Waislamu wanakula utumbo wa maiti kwenye Futari ya mwezi wa Ramadhani na kwenye Maulid. 4. Waislamu ni magudulia. 5. Muhammad ni Mshenzi. 6. Muhammad ni mgonjwa wa Kifafa 7. Muhammad ni mwizi aliiba Fimbo. Waislamu wa Kakonko wakiongozwa na Sheikh wao wa Wilaya Sheikh Iliyasa S. Bulyo walimfikisha Muhubiri huyo Mahakamani, Mahakama ilimpa haki ya dhamana. Pamoja na kuwa alikuwa chini ya dhamana muhubiri huyo aliendelea kutoa kashfa na matusi dhidi ya Waislamu. Kutokana na hali hiyo Sheikh wa wilaya alimuandikia barua mkuu wa Wilaya yenye Kumb. Na. BWT/W/KBD/47/25 ya tarehe 9/01/1998 nakala za Barua hiyo zilipelekwa kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa polisi wa mkoa, mkuu wa polisi wa Wilaya. Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na dhidi ya muhubiri huyo hadi hii leo. (i) Mihadhara ya Waislamu haiwezi kuvuruga amani Katika gazeti la Heko la tarehe 18/2/98 mapadri, maaskofu na wachungaji wa makanisa mbalimbali ya kikristo walionyesha kuwa tayari kuishi kwa amani na Waislamu na kuheshimu mihadhara ya dini zote. Wapagani, wahindu wamekuwa wakivumilia siku zote dini zao zikikashifiwa na wakristo, kama vile Mungu wa wahindu kuuzwa buchani, dini za kipagani kuitwa za kishenzi na hata hirizi zao kuchomwa makanisani, misikitini na katika mihadhara ya kidini. - Kwa nini serikali inawaendekeza wakatoliki kutaka kuwalazimisha watu waseme ndiyo katika mafundisho yote ya kikatoliki hata kama yanahitilafiana na mafunzo ya dini yao. Ni wajibu wao wa kisheria kuvumilia, kwani siyo lazima imani na vitendo vya dini nyingine ziwafurahishe wao. - Mbona Waislamu tunavumilia kusikia mkatoliki anasema Yesu ni Mungu wakati Quraani inasema nchi na mbingu hutikisika kwa kusikia kauli hiyo? Kama askofu anashindwa kuvumilia aache uaskofu, isitoshe dini siyo mali yake. HITIMISHO (i) Tunaiomba serikali na vyombo vinavyohusika kuwachukulia hatua kali wote waliohusika na mauaji hayo ya kinyama. (ii) Tunamuomba Rais ili kupunguza aibu taifa iliyopata kuwawajibisha Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam. (iii) Serikali iwe ya watu wote na siyo inayosikiliza watu wa dhehebu moja tu. Mihadhara iendelee kama kuna mtu au dhehebu linalokashifiwa wakalalamike polisi na siyo kwa Rais, na yoyote atakayeshindwa kuvumilia na akavuruga amani akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria. |
Maoni yetu:Tusianze kuulizana tena shida yenu nini Agizo la Rais Mkapa lapuuzwa:Wazee wa miaka 80 wateseka Gerezani Wanawake wasema hawatarudi nyuma mpaka dhulma iondoke Kujua
lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah
Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi Intifada
ndio jibu (2)
Kusema
ukweli ni sehemu ya uadilifu
Mafumbo
ya imani yabakie ndani ya Makanisa
Tamko la Wanawake wa Kiislamu mkoa wa Morogoro kuhusu kadhia ya Mwembechai Asiye
na elimu kwa mujibu wa Biblia
TAMTA
yaadhimisha miaka 36
Muumini
aliyeachiwa aeleza jinsi Waislamu wanavyoteswa Segerea
Wakwama kujenga msikiti kwa miaka 30 Lishe
: Mtoto anyonye maziwa ya mama miaka miwili
|