AN-NUUR
Na.156 Rabi' Awal 1419, Julai 4 - 9, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MAKALA
 

Intifada ndio jibu (2)

Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Ninamshukuru Allah (s.w.) aliyenitia nguvu ya kuandika ili kuwazindua ndugu zangu. Namtakia rehema na amani mtume wetu (s.a.w.).

Katika toleo la ANU-NUUR Na.135 ukurasa wa 11, kulikuwa na maoni yaliyoandikwa na Ndugulile R.A. Ndugulile yenye anuani isemayo "Intifada ndio jibu." Maelezo yake yalinivutia mno hadi kupelekea nami kuandika maoni yangu ili wasomaji wa gazeti hili tukufu na wapenda haki wote wafahamu dhulma zinazofanywa dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Kama ilivyoelezwa kwamba Uislamu uliingia nchini katika karne ya saba, na tangu wakati huo sharia ya Allah (s.w.) ilitawala katika ardhi yetu kwa miaka mia nne na ishirini na sita chini ya uongozi wa misikiti mwili ya Mji wa zamani wa Kaole.

Misikiti hiyo hivi sasa inafikiriwa kujengwa hoteli ya kitalii kwanini? Kwa sababu haina mwenyewe! Mtunzaji wa Magofu ya Kaole ilipo misikiti hiyo (Mwislamu) na huwa anawatembeza Wazungu (watalii) ndani ya eneo la misikiti hiyo huku wakiwa na viatu, na wakati mwingine hunywa pombe humo na katika makaburi ishirini na mbili yaliyopo hapo, ambayo mengine yana minara ili wafanikiwe kuendeleza uharibifu wao katika ardhi ya mwenye misikiti hiyo – Allah (s.w.)

Na Waislamu wa "Mji Mpya wa Kaole", wametosheka kujiita "Mamwinyi" bila kujali uchafu unaofanywa na Wazungu (watalii) katika nyumba hizo za Allah (s.w.).

Halikadhalika masheikh na waalimu wa Bwagamoyo, wanaendelea kubishana katika mambo ambayo hayawezi kuondosha dhulma zinazofanywa katika misikiti hiyo, na wanazofanyiwa Waislamu, bali baadhi yao wanashiriki kuudhulumu Uislamu na Waislamu wa Bwagamoyo na Tanzania kwa jumla.

Katika utafiti niliofanya, hakuna Waislamu wa hapa waliofika hapo Kaole kuchunguza habari zilizotolewa na Ndugulile. Ni jambo la kushukuru mno kwa Allah (s.w.) aliyewawezesha maamiri wa tabligh ambao walifika hapo na kuswali rakaa mbili za kuamkia msikiti (Tahiyyatul Masjid) katika kila msikiti, na kumtaka mtunzaji wa magofu hayo (Muislamu) aswali swala tano na ajiepushe na vivutio vya shetani.

Inasemekana lipo fungu maalum linalotolewa na serikali kwa wanaohusika na magofu. Kwa mfano kanisa Katoliki Bagamoyo wanapewa fungu hilo kila watalii wanapotembelea hapo kanisani. Kwa hiyo sisi tulipaswa tupewe fungu hilo kila watalii wanapotembelea misikiti hiyo. Pia ipo kampuni inayoshughulika na ukarabati wa magofu, kama Waislamu wangefuatilia misikiti hiyo ingekarabatiwa kama lilivyokarabatiwa kanisa Katoliki jengo la kanisa lilipo katika eneo la magofu ya Kaole na majengo mengi ya hapa Bwagamoyo.

Katika toleo la AN-NUUR Na. 118 ukurasa wa 5, Bwsana Abdul Rahiim Mussa wa Singida alisema kwamba wao wako karne ya 18 kwa sababu hawana huduma muhimu kama elimu, barabara, maji, afya n.k. shule ni 16 tu. Sisi wa Bwagamoyo tuko karne ya 16 kwa sababu ya hayo na zaidi ya hayo. Tunashule 4 tu za sekondari, na saba za msingi ambazo hazitoshelezi.

Kipo chuo cha sanaa ambacho pamoja na mambo mengine, hujihusisha sana kufundisha kucheza ngoma, kwaya, Tamithilia n.k. Vitu ambavyo ni kinyume na maadili ya Wabwagamoyo.

Kipo chuo cha Utafiti wa zao la Minazi – Chambezi. Walichofanikiwa ni kuua minazi yetu ya asili (mirefu) na kupanda ya kigeni (mifupi) ambayo haipatani na hali ya hewa ya hapa. Watu wengi wamepata hasara mfano ni Zinga Farm na Zabarelo. Hivi sasa chuo hicho ni wasambazaji wakubwa wa pombe ya mnazi hapa Bwagamoyo na Dar es Salaam.

Kipo chuo cha uongozi wa elimu – Mantep. Wanaonufaika ni wageni na wengi ni Wakristo.

Kipo chuo cha Maendeleo ya Uvuvi – Mbegani. Kinafundisha uvuvi, utengenezaji boti n.k. Wanacnhi walio karibu na chuo hicho ambao takribani wengi ni wavuvi bado wanavulia ngalawa, mitumbwi, mashua n.k. Hawana ujuzi wa kutengeneza chombo cha uhakika katika shughuli zao.

Pia hairuhusiwi kuvua samaki katika bahari ya Bwagamoyo umbali wa k.m. 5 toka ufukweni, kwa kuwa wameuziwa wenye mahoteli ili waoge Wazungu (watalii).

Samaki aina ya kamba ambao ni zao kubwa la biashara, haturuhusiwi kuvua kwa kuwa kibali chake kina vikwazo vingi badala yake wanavua wageni.

Eneo kubwa la bonde la Mto Ruvu wamepewa wageni ili waendeshe kilimo cha umwagiliaji jambo ambalo akifanya mzawa ataambiwa anaharibu mazingira (vyanzo vya maji).

Barabara zote nne (ya kutokea Msata, Kongowe, Sadani na Dar es Salaam) ni mbaya mno. Kwa hali hiyo ya sasa, safari ya hapa mpaka Dar es Salaam ni masaa 4, wakati kama barabara hiyo ingekuwa na ubovu unaofanana na barabara ya Kawawa Jijini Dar es Salaam inayotaka kuvunjwa na kutengenezwa upya, safari yake ingekuwa ni saa 1.30 tu.

Kuna kiwanja cha ndege - Zinga kinachomilikiwa na Pink Shark Hotel. Hatukatai maendeleo, lakini ni haki yetu kuhoji maendeleo hayo ni kwa manufaa ya nani na yana lengo gani? Kwanini kiwanja hicho kiwe mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya (Boma) mahali ambapo hapana kituo cha Polisi, Uhamiaji n.k. Je, serikali itadhibiti vipi nyara zetu? Au watazuia vipi hatari itakayoingizwa nchini? Je, serikali itakusanya vipi ushuru? Walikuwa wanatumia helikopta na sasa wanatumia kiwanja hicho.

Mwaka huu maulidi ya Kitaifa yatasomwa hapa Bwagamoyo. Si kwamba tunapendwa sana, bali ni furaha ya BAKWATA kwa kufungua tawi Bwagamoyo. Al Marhumu Sheikh Mohammed Ramiya na mwanawe Sheikh Yahya Mohammed Ramiya walisimama kidete kuipinga BAKWATA tangu ilipoanzishwa.

Kila mwaka walikuwa wanafanya maulid kubwa kinyume na ile ya BAKWATA katika uwanja wa Zawiya 

Baadaye msimamo huo ulikiukwa na kuikaribisha BAKWATA Bwagamoyo.

Tunadhani kuwa "ugeni mkubwa’ utakaohudhuria maulidi hayo makubwa, yatalipa "Kura ya veto" BAKWATA dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Hapo nyuma liliwafanyia fitina Waislamu wa Masjid Siraaj Al Muniir - Majani Mapana wakakamatwa eti sababu waliswali mwanzo Idi ya Mfunguo Mosi kabla ya BAKWATA.

Mfunguo Tatu waliswali tena Idi mwanzo kabla ya BAKWATA wakamkamata Sheikh Ramadhani Mwagize (China) kisha wakamuunganisha na kesi ya Mwembechai. Alishiriki vipi katika vurugu wakati yeye anaishi hapa Bwagamoyo na vurugu zimetokea Dar es Salaam? Tunataka maelezo Waislamu wa Bwagamoyo!

Msikiti Mkubwa wa Ijumaa wa Kihistoria (gofu) umefungwa na eneo la msikiti linalopakana na Bahari ya Hindi amepewa Mfadhili aliyejenga msikiti mpya kama shukrani.

Je, kero hizi Mbunge wetu Mhe. Ramiya hazijui mpaka anagombea hoja binafsi ya "Kadhi"? Je, Kadhi akiwepo ataondosha zinaa. Ulevi, ushirikina wa Bwagamoyo? Atatengeneza barabara na hospitali za Bwagamoyo? Atazuia Misikiti ya Kaole isijengwe Hoteli ya Kitalii?

Je, Maulidi ya mwaka huu yatakemea dhulma hizo na nyinginezo wanazofanyiwa Waislamu au yata Kuwa kichocheo cha kuwakamata tena Waislamu wa Bwagamoyo na Tanzania kwa jumla?

Mwisho nawaomba wananchi wote wa Bwagamoyo tudai utekelezaji wa ahadi alizoahidi Mheshimiwa Ramiya wakati wa kampeni za uchaguzi
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu:Tusianze kuulizana tena shida yenu nini 

Agizo la Rais Mkapa lapuuzwa:Wazee wa miaka 80 wateseka Gerezani

Wanawake wasema hawatarudi nyuma mpaka dhulma iondoke

Serikali kuzuia mahubiri ya Waislamu, kuvamia Msikiti, kukamata, kudhalilisha na kuua Wananchi ni kuvunja Katiba na Sheria za Nchi

Kujua lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah
Na Sadick M. Sadick"

Serikali isidhani kuwa Waislamu wa Tanzania wamelala usingizi

Intifada ndio jibu (2)
Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Kusema ukweli ni sehemu ya uadilifu
A.S. Chachika

Mafumbo ya imani yabakie ndani ya Makanisa
Na J. Hussein

Majibu kwa Kamara Kusupa

Tamko la Wanawake wa Kiislamu mkoa wa Morogoro kuhusu kadhia ya Mwembechai

Asiye na elimu kwa mujibu wa Biblia
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa

TAMTA yaadhimisha miaka 36
Na Masoud Mohamed Said, Tanga

Muumini aliyeachiwa aeleza jinsi Waislamu wanavyoteswa Segerea
Na Muhibu Said

Wakwama kujenga msikiti kwa miaka 30

Habari za Madrasa

Barua 

Mashairi 

Lishe : Mtoto anyonye maziwa ya mama miaka miwili 
Na Dk. Ali. A. Mzige
  

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita