AN-NUUR 
Na.187 Shawwal 1419, Februari 5 - 11 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Hijab ivaliwe shuleni
 
  • Ijumaa masomo mwisho saa 6 - Serikali
  • Wakuu wa shule watakaokiuka kuchukuliwa hatua
SERIKALI imesisitiza na kutilia nguvu kauli ya Mh. Rais Benjamin William Mkapa kwamba dini zote zinaheshimiwa na hakuna mtu atakayeonewa kwa ajili ya dini yake. Kwa hiyo imekariri agizo lake la kuwaruhusu wanafunzi wa kike Waislamu wavae hijab wakiwa shuleni/vyuoni. Aidha imekariri agizo lake kwamba shughuli za masomo zikome saa 6 hadi saa 8 mchana ili kuwapa fursa wanafunzi Waislamu kwenda kuswali. 

Akiongea Bungeni mwanzoni mwa wiki hii Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya amesema kwamba serikali imekwisha toa agizo kwamba pasiwepo masomo kati ya saa 6 na saa 8 mchana siku ya Ijumaa. 

Aidha, amesema ruksa ya kuvaa hijabu mashuleni ipo pale pale ili mradi tu kitambaa cha hijabu hiyo kifanane na kile cha sare ya shule. 

Mh. Profesa Kapuya amewataka Waislamu wasitoe malalamiko ya jumla jumla, bali waisaidie serikali kwa kuwaripoti kwake (serikalini) wale wakuu wa shule ambo wanakiuka maagizo hayo mawili ya serikali ili wachukuliwe hatua. 

Maelezo hayo ya serikali yanafuatia malalamiko yaliyowasilishwa Bungeni na Mbunge wa Kigamboni Mh. Kitwana Kondo. 

Malalamiko hayo yanatokana na kilio cha wanafunzi Waislamu mashuleni na vyuoni kwamba wamekuwa wakinyimwa haki zao za kidini, mfano ratiba ya masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yamekuwa yakiendelea hadi saa saba mchana siku ya Ijumaa. Pamoja na wanafunzi kuilalamikia sana ratiba hiyo, uongozi wa chuo hicho umeonyesha kutokujali. 

Hata hivyo, huko nyuma hata kabla ya siku ya Jumamosi kufanywa siku ya mapumziko, wanafunzi Wasabato walikataa kusoma au kufanya mtihani siku ya Jumamosi na kilio chao kikasikilizwa. 

Baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakidai kwamba wao hawajapewa waraka wowote unaohusu maagizo hayo mawili. 

Mfano hata baada ya kauli ya Serikali Bungeni juzi Mwalimu Matmbo wa shule ya Msingi Tabata alimzuia mwanafunzi Hasina Abdallah wa darasa la tano kuingia darasani kwa vile kavaa hijab. 

Suala hilo lilipofikishwa kwa mkuu wa shule Msaidizi alidai kuwa wao hawafanyi kazi kwa hotuba za Waziri. Wanachodai ni waraka ambao alidai haupo. 

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. L. Baishe hakuwepo kulizungumzia suala hilo. Hadi tunakwenda mitamboni mwanafunzi Asina alikuwa hajaruhusiwa kuingia shuleni hapo na hijab yake. 


Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais

WAISLAMU mjini Dodoma wametahadharisha juu ya watu wenye hisia na fikra za kibaguzi kwamba wasipotibiwa maradhi hayo wataiangamiza nchi. 

Wamesema; "Watu hao kama walivyokuwa makaburu wa Afrika ya Kusini wanadhani wao na vizazi vyao ndio wenye haki na kila jema la nchi hii na wengine wasio wa dini yao ni wapagazi tu". 

Maoni hayo yametolewa na Waislamu mbalimbali waliohojiwa na Mwandishi wa Habari hizi katika Msikiti wa Nunge, Masjid Manyema na Masjid Qubah mjini Dodoma. 

Maoni hayo yanafuatia taarifa zilizozagaa mjini hapa kwamba baadhi ya watu wakubwa serikalini na baadhi ya Wabunge wanamlaumu Rais kichinichini kufuatia hatua yake ya kuyapokea malalamiko ya Waislamu na kuahidi kuyafanyia kazi. Wakubwa wengi wa serikali na Wabunge hivi sasa wapo Dodoma kuhudhuria kikao cha Bunge. 

Kwa upande mwingine, wameeleza kuridhishwa kwao na hatua iliyofikiwa kwa serikali kuyapokea rasmi madai ya Waislamu na kuahidi kuyashughulikia. 

Waislamu wengi wamesema kwamba risala iliyosomwa mbele ya Mh. Rais ilikuwa nzuri. Aidha wamempongeza Mh. Rais Benjamin William Mkapa kwa kufungua historia mpya ya nchi.  

Wamesema kiongozi yeyote bora mwenye kujali maslahi ya muda mrefu ya nchi hawezi kuyapuuza malalamiko ya wananchi hata wakiwa wachache. 

Mzee mmoja maarufu katika masuala ya dini alisema; huko nyuma Marais waliotangulia waliyachukulia madai ya Waislamu kama madai ya wakorofi wachache ambao wakati mwingine waliitwa Siasa kali wanaotaka kuvuruga amani ya nchi. 

Aidha, wakati mwingine Waislamu waliodai haki zao za kidini ambazo tangu hapo zimetambuliwa na Katiba ya nchi, walidaiwa kuleta udini na propaganda kubwa ikapigwa kwa lengo la kuwatenga na jamii. Mzee huyo ambaye anamiliki biashara kubwa kubwa mjini Dodoma hakutaka jina lake litajwe gazetini amesema kwamba ukurasa huo sasa umefungwa. 

"Yale yaliyokuwa yakinasibishwa na uchochezi, siasa kali, ukorofi, uvurugaji wa amani, sasa yametambuliwa rasmi na Mh. Rais baada ya kuwasilishwa rasmi na Kamati rasmi iliyowakilisha Waislamu wote", alisema mzee huyo. 

Katika hali hiyo, mzee huyo amesema kwamba atashangaa sana kuwasikia tena wanasiasa na vyombo vya habari alivyoviita visivyojali maslahi ya nchi vikirejea tena propaganda za siasa kali. 

Kwa upande mwingine, akina mama Waislamu wameonya juu ya wanasiasa na watendaji serikalini wenye kujali maslahi yao binafsi ya muda mfupi hata kama athari yake italiangamiza taifa mbeleni. 

Wamesema hao hawataacha kunung’unika na kumlaumu Mh. Rais kwa umakini wake wa kuisoma na kuielewa hali halisi ya nchi.  

Pamoja na hayo wamesema kwamba hawakuridhishwa sana na majibu ya Mh. Rais. Wamesema majibu yale yaliwachoma roho kwani katika sura yake ya nje yalionekana siasa na "bembeleza toto". 

Akina mama hao wanaojiita "Bi Khadija Muslim Women Group" wamesema kwamba walilazimika kukutana baada ya hotuba ya Mh. Rais ili kuijadili. 

Maoni ya wengi yalikuwa kwamba majibu ya Mh. Rais yalilenga kuwapumbaza Waislamu. Egemeo lao kubwa lilikuwa kwamba kila kitu kinajulikana dhulma ipo wazi isiyohitaji kufanyiwa utafiti. 

Hata hivyo, baada ya mjadala mrefu wamesema kwamba waliridhika kwmba Mh. Rais kaonyesha nia njema na ni wajibu wao kumuunga mkono na kumsaidia katika ahadi yake ya kuyashughulikia matatizo ya Waislamu. 

Mwenyekiti wa umoja wa akina mama hao amesema wao msaada wao kwa Mh. Rais itakuwa kumpa ripoti yenye ushahidi madhubuti juu ya uonevu wanaofanyiwa Waislamu katika mkoa wa Dodoma. 

Hata hivyo, mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua uonevu gani wanaofanyiwa, Mwenyekiti huo hakutaka kueleza kwa madai kwamba si vyema kuvuja ripoti yao kwa vyombo vya habari kabla ya kumfikia Mh. Rais. 

Wamesema wataiandaa ripoti hiyo ikionyesha udhalimu wanaofanyiwa Waislamu katika mashule, makazini na masuala ya ardhi na kuiwasilisha kwa Kamati ya Alhaj Madabiba. 

Hata hivyo, katika mahojiano hayo Bi. Mwanahamisi Abdallah aligusia kwamba mabinti zao wamekuwa wakipigwa na kunyanyaswa mashuleni kwa kuvaa nguo za stara. Aidha, jumuiya zao zimekuwa zikinyimwa Tasjila pamoja na ardhi kwa visingizio na vikwazo mbalimbali. 

Bi. Mwanahamisi amesema kwamba wao hivi sasa wanakusanya na kuweka katika maandishi matukio mbalimbali yanayodhihirisha ubaguzi na unyanyasaji unaofanywa dhidi ya Waislamu nchini. 

Aidha, amewataka akina mama Waislamu kote nchini wafanye hivyo ili kumsaidia Mh. Rais kuondoa dhulma nchini na kujenga mazingira mapya yatakayodumisha amani ya nchi yetu. 

Kwa upande mwingine ameitaka kamati ya Alhaj Madabida kuwaeleza Waislamu ipo wapi ili kurahisisha mawasiliano. 



Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe - Manyema 
 
  • Waumini wasema dhulma imekithiri nchini
  • Waliohoji kuhusu nyumba za Wakfu Masjid Mwinyi wanyimwa dhamana na mahakama ya Kisutu
WIKI moja tu baada ya Waislamu kukamata mali ya Wakfu iliyoporwa na mtu mmoja anayejiita Daniel Zakaria, wadhamini wa Msikiti Manyema maarufu jijini nao wamesema hawako tayari kuruhusu viwanja vyao kuporwa na baadhi ya watu kwa mwavuli wa chama Tawala (CCM). 

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano wiki hii, wadhamini hao wamesema licha ya kuliendea suala hilo kwa hekima na kufuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na nyaraka zinazothibitisha umiliki halali wa viwanja nambari 4, 5, 6, 29, 30 - 31 kitalu 70 Kariakoo, wamesita kuanza ujenzi katika viwanja hivyo kutokana na kusumbuliwa na baadhi ya viongozi wa CCM na Tume ya Jiji. 

Akiongea kwa niaba ya wadhamini hao, Mweka Hazina wa Msikiti huo Bw. Said Hilal aliwaambia waandishi wa habari kwamba wameamua kuanza ujenzi mara moja na kwamba yule ambaye hataridhika na hatua hiyo aende mahakamani. 

"CCM hawana hati zozote zaidi ya barua ya Kamishna wa ardhi", alieleza Bw. Hilal huku akionyesha hati na barua kadhaa ilizonazo Msikiti Manyema ambazo baadhi yake zilitolewa nakala kwa waandishi. 

Akielezea historia fupi ya mgogoro wa viwanja hivyo, Bw. Hilal alisema mnamo mwaka 1980 CCM chini ya Uenyekiti wa Mwalimu Nyerere ilitoa pesa kuutaka Msikiti huo uviache viwanja hivyo ili mahali hapo pajengwe makao makuu ya chama hicho. 

Hata hivyo, wadhamini wa Msikiti wa Manyema walikataaa fidia hiyo kwa hoja kwamba Msikiti ni mali ya Mungu kwa hivyo wao wasingeweza kwa namna yoyote ile kupokea pesa hizo kwa niaba ya Mwenyezi Mungu ili mahali pawe pa chama hicho. 

Sheikh Hilal alisema baada ya CCM kuamua kuhamishia makao yake makuu Dodoma, katika hali ya kutatanisha viwanja hivyo vilimilikishwa kwa shirika la nyumba. 

Kutokana na hatua hiyo, wazee wa Manyema waliuona uongozi wa Shirika hilo na kuutaka uviache viwanja hivyo viendelee kuwa milki ya Msikiti. 

Bw. Hilal alieleza kwamba kwa muda wa miaka 10 tangu 1980 wazee hao walihangaika kufuatilia suala hilo hatimaye mwaka 1989 uongozi wa shirika la Nyumba uliamua kuvirejesha viwanja hivyo kwa Msikiti Manyema. 

Kuanzia mwaka huo (1989) Bw. Hilal aliwaeleza waandishi, wadhamini wa Msikiti huo walifuatilia hati miliki hadi ilipotolewa Machi 18, 1992. 

"Kuona hivyo, CCM ikamuendea Rais na kumtaka atengue milki hiyo, Rais alikubali", alieleza Bw. Hilal. 

Baada ya kupokea taarifa za utenguzi wa milki ya viwanja hivyo, wadhamini walikwenda kwa Rais na kutoa ufafanuzi hali iliyopelekea Rais kuahidi kulipeleka suala hilo mbele ya Kamati Kuu ya CCM kwa ajili ya uamuzi. 

Bw. Hilal alisema Kamati hiyo iliamua kwamba CCM ijiondoe kwenye mgogoro na Msikiti juu ya umiliki wa viwanja. 

Taarifa rasmi ya CCM kujitoa katika suala hilo ilijulishwa kwa Msikiti Manyema kupitia barua ya Rais Kumb. Na. SHC/L.50/143 ya Septemba 21, 1992 iliyosainiwa na Katibu wa Rais wakati huo Bw. Paul M. Rupia. 

Baada ya taarifa hiyo ya Mweka Hazina, mmoja wa wadhamini wa Msikiti huo, Sheikh Abubakar Mwilima alihoji ushupavu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Peter Kafanabo wa kupuuza maamuzi ya Kamati Kuu ya chama chake kuwa unatoka wapi. 

Wakati huo huo, waumini watatu walioripotiwa polisi kuhusiana na purukushani iliyotokea Masjid Mwinyi Ilala Jijini Dar es Salaam wamenyimwa dhamana na Mahakama ya Kisutu baada ya kusomewa shitaka lao Ijumaa iliyopita. 

Waislamu hao ni Bw. AbdulRahman Kileo mkazi wa Ubungo, Rajab Mmanga mkazi wa Kinondoni na mtu wa tatu ambaye gazeti hili halikufanikiwa kupata jina lake. 

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo kutokuelewana baina ya Imam wa Masjid Mwinyi na waumini hao kulikuja baada ya Bw. AbdulRahman Kileo kusimama kueleza jinsi Bw. Daniel Zakaria alivyofanikiwa kughushi nyaraka zilizopelekea kupora nyumba ya Wakf Na. 58 Gerezani Jijini Dar es Salaam. 

Nyumba hiyo ilitolewa Wakf kwa Waislamu na marehemu Hajat Aziza bint Omar ambapo Masjid Mwinyi ulikabidhiwa dhima ya usimamizi. 

Hata hivyo, ilielezwa Msikitini hapo kuwa hadi nyumba hiyo inakamatwa na Waislamu wakiongozwa na Bw. AbdulRahman Kileo juma moja lililopita, ilikuwa baa ambapo chupa za pombe na mipira ya zinaa ilizagaa vyumbani. 

Kufuatia kunyimwa dhamana kwa watuhumiwa hao, waumini kadhaa wa dini ya Kiislamu wameelezea wasiwasi walionao juu ya taasisi za usalama na utoaji wa haki hasa yanaposhughulikiwa masuala yanayohusu Waislamu. 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Mauaji ya Mwembechai; Mh. Rais apewe kanda

Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri

Hijab ivaliwe shuleni

Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais

Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe  -   Manyema

Maoni yetu
Kauli ya Waziri Mkuu Bungeni: Tumsikilize nani?

DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA

Mjue Usama bin Ladin -3

Uislamu na Mazingira katika Umoja wa Mataifa
Na Dk.  Wahid

Barua ya wazi kwa Rais Mkapa

Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika Internet
Na. Zituzzaman Hoque

Kutoka magazeti ya zamzni

Rais Mkapa atekeleze hadi yake kwa hadhari
J.R. Msuya, Moshi

Mashirika ya Dini yaelekeze misaada vijijini
Na KAWELE  SAIDI 

Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma

Ni serikali ipi anayoiwakilisha Sumaye
Na Abu Salim

Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni

Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Na SALUM ALI 

Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro

Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel

Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina

Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti

Sayansi na Teknolojia 
[Jifunze ‘Kubana’ Majalada] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Chakula na Lishe 
[Ni hatari kuwaambia wananchi wasichague chakula] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita