AN-NUUR 
Na.187 Shawwal 1419, Februari 5 - 11 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Rais Mkapa atekeleze hadi yake kwa hadhari
 

Baadhi ya Mawaziri anaowategemea sio waadilifu 
 

J.R. Msuya, Moshi
 

AHADI ya Mheshimiwa Rais Ben Mkapa kwamba atashughulikia kilio cha siku nyingi cha Waislamu nchini juu ya kufanywa raia wa daraja la pili yapasa kupokewa kwa mikono miwili na wapenda amani wote nchini. 

Hakuna ubishi kwamba amani ni hazina kubwa inayopaswa kulindwa kwa gharama zozote zile. Hata hivyo ni makosa makubwa mno kufikiria kwamba amani yaweza kulindwa kwa ubabe, vitisho na hata kuua kama ambayo Watanzania tumefanywa kuamini. 

Wanasiasa wetu, ama kwa makusudi au kutokuelewa wamekuwa mstari wa mbele kuhubiri au kuimba amani na utulivu huku wakitoa mifano ya Burundi, Rwanda, Algeria, Bosnia na kwingineko ambaKo amani sasa imebakia msamiati. Hata hivyo ni nadra viongozi hao kubainisha sababu zinazopelekea vita katika nchi hizo kwa kuchelea kuumbuka kwani huenda maovu wanayofanya yakawa wazi. 

Ni wazi kuwa vita vinavyoendelea katika nchi zilizotajwa ni matokeo ya mifumo mibaya ya tabaka au kundi moja kuhodhi madaraka dhidi ya tabaka au kundi lingine. Na hii bila shaka imetokana na uongozi au utawala mbaya usiozingatia uadilifu. Vita ni matokeo ya kundi linalodhulumiwa kutaka kujichukulia haki yao baada ya njia za amani kushindwa kuwapa haki hiyo. 

Kwa mantiki hii, viongozi na wanasiasa wetu, kama kweli ni watu wanaoitakia nchi hii mema wangejisafisha kwanza na kujiuliza kama kweli wanatenda kazi zao kwa uadilifu. Mifano ya Burundi na Rwanda haiwasaidii wananchi, bali inatakiwa iwasaidie hao viongozi na wanasiasa watende uadilifu kwa kuwa kukosekana uadilifu ndio chanzo cha kuvurugika amani popote pale duniani. 

Vitisho vinavyoendeshwa na propaganda dhidi ya Uislamu si suluhisho na wala haliwezi kuwafunga Waislamu midomo katika kudai kile wanachoamini kuwa ni haki yao. Vitisho, propaganda na mauaji vinachochea chuki na hasira miongoni mwa raia na hii ndiyo itakayotupeleka Burundi au Rwanda. 

Ni amani na upendo gani huo unaotegemewa kama mtu ananyanyaswa na kusutwa kwa kuvaa kanzu au hijabu tu eti kwa misingi kwamba anaeneza hisia za siasa kali! Je, hatujui kwamba haya ndio yaliopo mashuleni? 

Tunategemea amani gani endapo watu hawaruhusiwi kuhubiri dini yao au kufanya mikutano kujadili maendeleo yao? Je, hiyo amani tunayoiimba itakuja vipi endapo mashirika yoyote yenye lengo la kusaidia Uislamu yanajengewa hoja na fitina kuwa ni ya kigaidi na yanajihusisha na uchochezi? Hii ni mifano michache tu lakini ni kweli Waislamu wamefanywa raia wa daraja la pili. 

Kuna hoja zilizokosa mashiko kwamba Waislamu wa Tanzania wameshindwa kupiga hatua kimaendeleo kutokana na sababu za kihistoria. 

Tunakubali kuwa ukoloni ulilipa Kanisa nafasi kubwa na kuukandamiza Uislamu. Na hakuna ubishi kuwa ndiyo maana mchango mkubwa katika kudai uhuru ulitolewa na Waislamu. 

Hata hivyo, tutakuwa hatujafanya haki kuulaumu ukoloni peke yake bila kuilamu serikali ya TANU na CCM ambayo imekaa madarakani kwa karibu miongo minne bila kurekebisha hali hiyo mbaya. 

Hali ya Uislamu Tanzania inayonisukuma kuandika makala hii na kuipokea kwa mikono ahadi ya Rais Mkapa. Hata hivyo, ningependa kumuomba Mheshimiwa Rais achukue hadhari katika kutekeleza ahadi hii. 

Sitaki kuamini kwamba ahadi ya Rais Benjamin Mkapa ni kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2000 na wala sifikirii kuwa ahadi hii ni propaganda za kisiasa. 

Hata hivyo, endapo Rais amedhamiria kweli kufanyia kazi matatizo ya Waislamu, badala ya kukutana na Baraza la Mawaziri tu, angeunda tume huru ambayo ingetafuta ukweli juu ya madai ya Waislamu. 

Aidha, angewawajibisha baadhi ya watendaji wake ambao moja kwa moja wameshiriki katika kuwadhalilisha na kuwanyanyasa Waislamu. Inawezekana kabisa kwamba Rais ni muadilifu na ana huruma na shida za Waislamu. 

Lakini hii haifanyi Mawaziri wake wote kuwa hivyo. Tunategemea Bw. Ali Ameir Mohammed atamshauri nini Rais Mkapa wakati yeye mwenyewe amehusika na suala la Mwembechai. Je, Bw. Ameir atashauri nini endapo alimshangaa Rais kwa kutengua uteuzi wa Bodi za Parole. 

Je, Waziri Nagu atamshauri nini kama waziri wa wanawake na watoto hakushughulishwa na kudhalilishwa kwa wanawake na watoto wa Kiislamu na askari polisi. 

Hii ni mifano michache tu lakini la msingi ni kwamba Mheshimiwa Rais Mkapa asingetegemea sana Baraza lake katika kutoa maamuzi kwani walio wengi hawana rekodi nzuri kwa maana ya kukosa uadilifu. 



Mashirika ya Dini yaelekeze misaada vijijini 

MASHIRIKA mengi ya dini kwa kiwango kikubwa yameelekeza huduma zao za jamii katika miji mikuu ya mikoa na kwa asilimia kubwa Dar es Salaam inaongoza kwa kupata misaada hiyo, wakati mwingine misaada hiyo huwa ni ziada kwa wahusika. Mwandishi KAWELE SAIDI wa Dodoma anatoa hoja binafsi kutokana na utafiti alioufanya wilayani Kondoa na Dodoma vijijini hivi karibuni. 

HUDUMA za jamii ni jambo la msingi sana kwa maisha ya kila siku ya mwanadamu, hasa katika kipindi hiki kigumu cha uchumi, mwelekeo wa kuelekeza huduma katika maeneo maalum hasa kwa mashirika ya dini (ya Kiislamu) yanafanya jamii nyingine kujisikia kama imetengwa na kuona hakuna umuhimu wa mashirika hayo kuwepo iwapo kweli lengo ni kusaidia Waislamu. 

Uislamu umeagiza sana na kutilia mkazo juu ya kusaidiana hasa kwa wale wenye uwezo kuelekeza misaada katika jamii isiyo na uwezo na ujira upatikanao kwa wale walengwa ni mkubwa sana mbele ya Allah (s.w.) kuliko kuelekeza sehemu ambayo misaada hiyo huonekana ni ziada tu. 

Tuchukue taarifa ambazo tunazozisoma kuwa Waislamu fulani wanafuturu embe, au mapapai, hivi karibuni huko Ulanga (Kijiji cha Mbugu) watu wanatembea zaidi ya kilomita 30 kutafuta maembe katika kijiji cha Ruaha kama mlo wa asubuhi, mchana na jioni, wakati huo huo angalia baadhi ya mashirika ya dini, watu binafsi walivyofuturisha na kutumia gharama kubwa sana za fedha hasa katika baadhi ya miji kama Dar es Salaam n.k. Chukulia misaada hiyo ingekwenda Nzasa, Kilwa, Ulanga, Handeni, Kondoa Waislamu wa sehemu hizo wangefarijika kwa kiasi gani? 

Kuiga jambo zuri si vibaya hata kama jamii hiyo watakuwa si wenzetu katika imani, lakini kizuri kinachofanywa lazima isifiwe, wao huduma za jamii zinatolewa kuanzia mijini hadi vijijini na wanazo takwimu sahihi na siyo ubabaishaji wa taarifa, wanawaelewa waumini wao, idadi yao, na matatizo yanayowahusu, shule, zahanati, vituo vya kulea watoto yatima, vituo vya ufundi (Vocational Training Centres) huduma zao zimetanda maeneo yote. 

Wilaya ya Kondoa asilimia kubwa ya wakazi wake ni Waislamu. Kila kijiji pana Msikiti au Misikiti sambamba na madrasa za dini, hawa hawa wanastahili kupongezwa kwani katika Tanzania bara wilaya ya Kondoa inaongoza kuwa na Waislamu wengi na wasomi wengi wa dini, ingawa hawasikiki sana katika ngazi kuu za uongozi katika taasisi za dini. 

Kwa kiwango kikubwa cha Waislamu wa Kondoa matatizo yao yanafanana, kuanzia Kondoa Mashariki, Kaskazini, Kusini na Magharibi, mingi ya Misikiti ni ya zamani sana na michakavu, haikusakafiwa, baadhi ya Misikiti imeezekwa kwa nyasi, Misikiti haina misala (majamvi), hakuna misahafu, hadi juzuu amma, walimu hawana uhakika wa posho kutokana na kazi wazifanyazo, nenda vijiji vya Dalai, Masange, Mauno, Mondo, Goima na Simba. 

Vingine ni Songolo, Hamai, Bukulu, Masawi na Berebera hali ni mbaya. Huduma nyingine za jamii kama shule za sekondari hakuna au kama zipo zinahesabika na hazizidi tano, zahanati hazina dawa, maji kwa mtu asiyeyazoea hawezi kuyanywa. 

Kwa mtazamo, watu hawa si kuwa wamekaa tu, wanajishughulisha sana, kwa mifugo, kilimo lakini hali zimefikia lazima wanahitaji msaada wa kila namna, hasa katika kuendeleza taasisi za dini kama Misikiti, madrasa, shule na huduma za afya. 

Hali hiyo, inafikia hata Dodoma Vijijini, mfano kijiji cha Veyula (Masjid Jihad) Msikiti hauna hata masahafu, au kama ipo imechanika vibaya. Mvua inaponyesha suala la kusali linakuwa ni la uvumulivu sana kwani Msikiti mzima unavuja. 

Pamoja na michango inayofanyika kila siku au kila Ijumaa bado hali ya gharama ya vitu inavyopanda husababisha fedha hizo zinapofikia kuhitajika kununua kifaa huwa hazitoshi kwani vifaa hivyo tayari huwa vimeshapanda bei. 

Ninatoa hoja binafsi kuwa taarifa zinazotolewa na waandishi wa gazeti la ANNUUR ziwe zinafuatiliwa ili misaada itolewe sambamba na sehemu husika na kwa walengwa. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Mauaji ya Mwembechai; Mh. Rais apewe kanda

Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri

Hijab ivaliwe shuleni

Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais

Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe  -   Manyema

Maoni yetu
Kauli ya Waziri Mkuu Bungeni: Tumsikilize nani?

DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA

Mjue Usama bin Ladin -3

Uislamu na Mazingira katika Umoja wa Mataifa
Na Dk.  Wahid

Barua ya wazi kwa Rais Mkapa

Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika Internet
Na. Zituzzaman Hoque

Kutoka magazeti ya zamzni

Rais Mkapa atekeleze hadi yake kwa hadhari
J.R. Msuya, Moshi

Mashirika ya Dini yaelekeze misaada vijijini
Na KAWELE  SAIDI 

Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma

Ni serikali ipi anayoiwakilisha Sumaye
Na Abu Salim

Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni

Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Na SALUM ALI 

Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro

Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel

Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina

Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti

Sayansi na Teknolojia 
[Jifunze ‘Kubana’ Majalada] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Chakula na Lishe 
[Ni hatari kuwaambia wananchi wasichague chakula] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita