|
|
|
MAKAMU wa Rais Mh. Dk. Omar Ali Juma katika nasaha zake siku ya Idd - el - Fitr hivi karibuni alilaani vikali vitendo vya mauaji na kusisitiza kwamba hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kumuua mwenzake kwa sababu yoyote ile. Mh. Makamu wa Rais aligusia nukta hiyo wakati akionyesha uovu na kukemea vitendo vya utoaji mimba na kutupa watoto. Ni dhahiri kwamba kama kutoa mimba ya kiumbe ambacho hakijazaliwa, ni jambo ovu, basi ni uovu zaidi kumuua mtu aliyemzima bila ya haki. Tunasema bila ya haki kwani wakati mwingine sheria ya nchi/dini yaweza kuruhusu kuuliwa kwa mtu kama adhabu ya kosa hilo. Hivi sasa nchini kwetu miongoni mwa makosa ambayo yakithibiti mahakamani mtu aweza kuhukumiwa kifo ni pamoja na kuua kwa kukusudia (murder), makosa mengine yote hata yale mabaya zaidi kama ubakaji, ujambazi, uharamia n.k. adhabu kali hutolewa kama vile vifungo virefu, kuchapwa viboko n.k. lakini si kifo. Katika kuheshimu na kulinda uhai wa watu na kuhakikisha kwamba hauchezewi ovyo pale ambapo mtu ameua bila ya kukusudia (Manslaughter) basi adhabu kali pia yaweza kutolewa. Yaweza kuwa kifungo cha muda mrefu au hata maisha. Na hata katika mahakama kesi ikshakuwa ni ya mauaji aghalabu huchukua muda mrefu ambapo mtuhumiwa hata kama atakuja kuachiwa baadaye lakini atalazimika kukaa rumande muda mrefu. Pengine kesi pekee duniani ya mauaji ambayo iliendeshwa kwa muda mfupi zaidi na mtuhumiwa kuonekana hana hatia ni ile iliyotokea Tanzania mwaka 1996. Katika kesi hiyo kijana wa Kiislamu aliuliwa. Mtuhumiwa alikamatwa, licha ya kupelekwa mahakamani ndani ya Pajero na Mobitel mkononi, uchunguzi wa tukio hilo uliendeshwa kwa kasi ya mwanga na mtuhumiwa kuachiwa katika kipindi kisichozidi masaa 72. Pamoja na hayo, lakini angalau vyombo vya dola vilimfikisha mtuhumiwa mahakamani na hukumu ikatoka huko kwamba hana hatia. Iwe hukumu hiyo ilifuata sheria na haki si hoja kwa hapa. Lakini angalau imetambuliwa kwamba yule aliyeuliwa alikuwa mtu, ila tu muuaji hakupatikana. Zipo nchi duniani ambapo Rais ana madaraka ya hali ya juu sana na anaweza hata kutoa amri mtu auliwe bila ya haki kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa. Madikteta wengi duniani wamefanya hivyo na wameendelea kufanya hivyo. Kina Bokasa, Hitler, Mussolin, Makaburu wa Afrika Kusini n.k. ni mfano wa watu wa aina hiyo. Lakini haina maana kwamba udikteta wao wa kutokuthamini kwao uhai wa wengine kunaondoa kweli ile thamani na haki ya kuishi ya raia wake. Ndio maana yale mamlaka na maguvu ya kisiasa na kijeshi aliyo nayo yakishamtoka, raia huja juu kutaka kumshtaki na kumuadhibu kwa makosa aliyoyatenda. Leo ingewezekana watu wangeifufua mifupa ya Hitler wakaichoma moto kuonyesha hisia zao juu ya uovu alioufanya. Wananchi wa Chile ndani ya Chile na nje wanaandamana kutaka Rais wao wa zamani Pinochet afikishwe mahakamani. Yote hii ni kuonyesha kwamba uhai wa mtu ni kitu cha thamani kubwa isiyokadirika na damu ikishamwagwa kisasi hakiwezi kuondoka kwa kufukia damu ya muhanga kwa mchanga kama ilivyofanywa pale Mwembechai. Katiba na sheria za nchi zinadai Tume huru iundwe kuchunguza tukio lile na wahusika wafikishwe mahakamani. Na hatudhani kufanyika kwa haya kunahitajika kwanza utafiti wa kisayansi kupitia kamati ya Alhaj Madabida na mjadala kati ya Mh. Rais Mkapa na Baraza la Mawaziri. Watu wameuliwa, kanda zipo zikionyesha mtoa amri akisema "piga yule" mpigaji anaonekana akimpiga Muislamu kwa kulenga shabaha, anaamriwa tena kuongeza anaongeza, kijana wa Kiislamu anaanguka anapigapiga miguu mithili ya mbuzi aliyechinjwa akaachiwa, anakata roho na kutupwa ndani ya gari la polisi kama mzoga na damu yake kufukiwa kwa mchanga. Hatujui uchunguzi gani wa kisayansi Mh. Rais Benjamin William Mkapa anangojea ufanyike juu ya tukio hili. Hatuoni uchunguzi zaidi ya kuunda tume huru mara moja itueleze sheria gani iliwaruhusu wakuu wa serikali na vyombo vyake kuitikia kilio cha Paroko Lwambano na kuua Waislamu. Tume hiyo ndiyo itatueleza kamanda yule aliruhusiwa na kifungu gani cha sheria za polisi na zile za nchi kwa ujumla kutoa amri ya kuwalenga watu risasi kama wao ni ngiri mwitu. Kama tulivyosema katika maoni yetu ya huko nyuma katika gazeti hili, yawezekana taarifa za kamanda huyo "piga yule" wala jinsi damu ya kijana yule wa Kiislamu iliyofukiwa kwa mchanga hazijafika kwa Rais Mkapa. Pengine kama hatua yake ya wali, Kamati ya Alhaj Madabida ianze kwa kumpelekea Mh. Rais mkanda wa mauaji hayo ya Mwembechai. Kisasi cha damu hakiondoki kwa propaganda wala kwa kufukia damu ya aliyetolewa muhanga kwa mchanga. Hatutaki historia yetu iandae wajukuu watakao kuja watafute kina Pinochet waliowaua babu zao. |
YALIYOMO
Tahari
Matokeo ya mitihani darasa la saba serikali ieleze: Je, Waislamu ni taahira au kuna agenda ya siri Wenye siasa za kikaburu wasimyumbishe Rais Hatuko tayari kuruhusu viwanja viporwe - Manyema Maoni yetu
DONDOO ZA KISAIKOLOJIA: PEDOPHILIA Uislamu na Mazingira katika
Umoja wa Mataifa
Barua za Mtume (s.a.w.) za Jihad katika
Internet
Rais Mkapa atekeleze hadi yake
kwa hadhari
Mashirika ya Dini yaelekeze
misaada vijijini
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni Dodoma Ni serikali ipi anayoiwakilisha
Sumaye
Sehemu ya maelezo ya Waziri Mkuu bw. Frederick Sumaye bungeni Zanzibar ni nchi au mkoa?.
Sheikh Bafadhil aamuru kusimamishwa shughuli za African Muslim Agency Moro Vijana Arusha njooni mnione - Alhaj Mollel Waislamu Korelo wazama kwenye ushirikina Waislamu Hanang’ wajenga Msikiti Sayansi na Teknolojia
Chakula na Lishe
|