NASAHA
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Mashairi


Kiswahili kitumike

Hodi Mhariri hodi, nipange japo pembeni,
Kueleza lisobudi, humu mwako NASAHANI,
Na tusiwe wakaidi, kwa kujivuna nchini,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Katika kufundishia, sekondari na vyuoni,
Miaka inaishia, maendeleo ni duni,
Hadhi tunajishushia, kwa kuiga lugha ngeni,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Wahusika msikie, kasumba iondoweni,
Hebu natuangalie, wenzetu kule Japani,
Korea tushuhudie, kwa hakika wamewini,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Kiingereza ni somo, kifundishwe darasani,
Kifaransa kiwemo, kisikose ratibani,
Haya kwetu msukumo, shime tuyaendeeni,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Tazama Uarabuni, Kiarabu namba wani,
Kwa kila alo mgeni, hukisoma kwa yakini,
Yahudi hakosekani, na hata Wamarekani,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Nchinyingi hujifunza, hii lugha ya nyumbani,
Na tena wameshaanza, kukiweka redioni,
Fanya utafiti kwanza, sauti Ujerumani,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Histori Fizikia, yote hayashindikani,
Biologia kemia, hayapati upinzani,
Msamiati tungia, ili iwe kitabuni,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Basi tunangoja nini, ikiwa tunaamini,
Na vipi tukawa duni, Waafrika barani,
Tazama ulimwenguni, chachu kwao ni kubuni,
Kiswahili kitumike, katika kufundishia.

Kadi tama nakomea, wenyedhima fikirini,
Hatua tutajongea, hatutakuwa wa chini,
Thama tajiongezea, furaha kwetu nyoyoni,
Kiswahili kitumike, katikakufundishia.

Rajab Said (Rasaki),
S.L.P. 90329, 
Dar es Salaam.


KIKO KARIBU NASAHA

Naanziliza Karima, alo mwema asilani,
Rabbi mwingi wa huruma, msifika Rahmani,
Illah Mola Karima, Mola uso na kifani,
Karibu utamadadi, Idd bun Kikong’ona.

NASAHA Arobaini, toleo lake yakini,
Ndipo nilipobaini, ametufika mgeni,
Kijukuu kasaini, Jushaka na Hanzuruni,
Karibu utamadadi, Idd bun Kikong’ona.

Fani inayumba yumba, kwa kutokuwa na nyenzo,
Watunzi waliotamba, wanaacha zao nyenzo,
Sijui kilowakumba, wayakumbuke ya mwanzo,
Karibu utamadadi, Idd bun Kikong’ona.

Karibu usife moyo, NASAHA yafurahiya,
Watumi walo na moyo, ni haramu kwao “Riya”,
Chuki umbea na choyo, Mola hakuwajaliya,
Karibu utamadadi, Idd bun kikong’ona.

Ilobaki yetu Rai, ni kumuomba Jalia,
Tuzidi jaa imani, NASAHA kutumikia,
Lisomwe kila mahali, gazeti lizidikua,
Karibu utamadadi, Idd bun kikong’ona.

Sitopenda kuchosheni, kalamu naweka chini,
Idd usikae chini, NASAHA ujisaini,
Utupe nyingi imani, tumaini la moyoni,
Karibu utamadadi, Idd bun kikong’ona.

Binti Swaleh “Shangazi lao”, 
Kinondoni.


Kiko karibu NASAHA

Uje kinara wa tungo, tupange mashambulizi,
Uchemshe zetu bongo, tuwatwange hawa wezi,
Ingawa wana kinyongo, ukweli uweke wazi,
Kiko karibu NASAHA, tushambulie kwa zamu.

Y. Kijukuu, Mkuranga 
Nasaha 22/03/2000

‘Labbaika’ (Jibu)

“Labbaika” naitika, “Labbaika” Kijukuu,
Kiko nimekwishafika, nakita wangu mguu,
NASAHA nimeibuka, naleta  ujumbe huu,
“Labbaika” Kijukuu, Joka tulichane chane.

Sogea tushikamane, nyoka tumjie juu,
Visu tumchanechane, asiipate nafuu,
Mbavu zake ziachane, nguvuze tuzime vuu,
“Labbaika” Kijukuu, Joka tulichanechane.

Tuanze lake jalala, tukichome kichuguu,
Kichaka anapolala, nduli mwana jokakuu,
Tena asije tawala, kitini akawa juu,
Labbaika!! Kijukuu, Joka tulichanechane.

Moto tuwashe NASAHA, wa kuni hadi vifuu,
Joka lipate karaha, lijitupe “puu” “puu”,
Ateseke majeraha, macho aone bluu,
Labbaika Kijukuu, Jola tulichanechane.

Sie tulo Wamachinga, na wauza vitunguu,
Makuli wenye matenga, washusha mizigo juu,
Nduli tumle mapanga, atoweke mwaka huu,
Labbaika!! Kijukuu, Joka tulichanechane.

Na sie wapiga debe, wapandisha zege juu,
Nyoka tusimpe shibe, atule hadi miguu,
Gundi kinywa tumzibe, akome anune nuu!
Labbaika!! Kijukuu, Joka tulichanechane.

Idd Kikong'ona,
Morogoro.


Hilo ni tunda gani? (Swali)

Tunda hilo adilishi, kwa walao ni kidhishi,
Tunda hilo elimishi, kwa walao hawabishi,
Tunda hilo waidhishi, kwa walao maandishi,
Tunda hilo tamanishi, kwa walao halichoshi,
Tunda hilo kiamshi, kwa walao ni tumishi,
Tunda hilo ni ridhishi, kwa walao kusudishi,
Tunda hilo tunda gani, nilinenalo mtunzi?

Almas H. Shemdoe “Tunda la Matumaini”,
Kigogo, Dar es Salaam. 
(NASAHA NA. 041 29 Machi 2000)

Hilo ni tunda gani? (Jibu)

Hodi hodi Mhariri, Jushaka hodi nabisha,
Shairi langu hariri, Nasahani kuchapisha,
Kurasani navinjari, jawabu kuwajulisha,
Sana msije fikiri, fumbo likawachokesha,
Tunda si tunda dhahiri, hilo ninabainisha,
Nasahani ni mahiri, tunda nawafahamisha,
Alinenalo mtunzi, “Tunda la Matumaini.”

Kwa walao maandishi, “Tunda la Matumaini”.
Kwa walao ni kidhishi, “Tunda la Matumaini”,
Kwa walao halichoshi, “Tunda la Matumaini”,
Kwa walao ni tumishi, “Tunda la Matumaini”,
Kwa walao hawabishi, “Tunda la Matumaini”, 
Kwa walao ni ridhishi, “Tunda la Matumaini”,
“Tunda la Matumaini”, ndilo wanena mtunzi.

Tunda halitoki Bara, Lushoto, tena jeusi!
Tunda halina kipara, sikimbilie Masasi,
Tunda halina papara, mambo yake si ya wasi,
Tunda machoni lang’ara, si chungwa wala nanasi,
Tunda halina madhara, si chawa wala papasi,
Tunda lina fani bora, mashairi limepasi,
“Tunda la Matumaini”, ndilo wanena mtunzi.

Tunda kweli elimishi, jamii laelimisha,
Tunda kweli adilishi, jamii laadilisha,
Tunda kweli amkishi, walolala laamsha,
Tunda kweli ni ridhishi, ujumbe laufikisha,
Tunda kweli tamanishi, kuiga latamanisha,
Tunda kweli waidhishi, jamii lawaidhisha,
“Tunda la Matumaini”, ndilo wanena mtunzi.

Juma S. Katanga (Jushaka),
“Sugu la Mashairi -Tanzania”,
Mapumzikoni -Chanika.



Nifanyeje walimwengu? (Swali)

Siasa niliingia, CCM namba wani,
Mawazo yalinijia, itanitoa shidani,
Lakini najijutia, dhiki hadi mlangoni,
Nambieni walimwengu, la kufanya silioni.

Kunambi S. Kilongola “Bichwa sugu”,
S.L.P. 61018, 
Dar es Salaam, 
Safarini Msanga Ngwengele -Kisarawe.

Kigwanda achana nacho (Jibu)

Naanza kwa taratibu, kuingia kurasani,
Kunambi pokea jibu, huko huko safarini,
Na pole kwa maswaibu, yalokukuta mtani,
Cha kufanya toka sasa, ni haki kupigania.

Maisha kwako magumu, wanao wakulilia,
Sababu waifahamu, na chanzo unakijua,
Chama kushika hatamu, sasa nakupasulia,
Haraka jitenge nao, wa vikadi vya kijani.

Bichwa Sugu’ chonde chonde, Usijinyonge mtani,
Maisha yasikushinde, ukaja hama mjini,
CCM usipende, “wazandiki” nambawani,
Chakufanya tokasasa, ni haki kupigania.

Chama ulichoingia, si chama cha kisiasa,
Ingawa ulisifia, na mwisho ukatuasa,
Lakini nakuapia, hakina njema siasa,
Bichwa sugu pole sana, kuwa kwako CCM.

Dhiki inayokukuta, Kunambi umeitaka,
CUF ilikufuata,tahadhari ikaweka,
Hawa watu wakipita, kwetu dhiki itafika,
Kama kigwanda unacho, cha kijani kiondoe.

Lipumba alishasema, mwana wa chui ni chui,
Kwa maneno ya hekima, kuonesha hatufai,
Lakini “Ukalizima”, sasa hivi uko hoi!
Kama kigwanda unacho, cha kijani kiondoe.

Beti saba maridadi, mwisho wa “Mtaaluma’,
Dhiki ilivyoshadidi, sisi wote yatuuma,
Hata Zalia Saidi, hili pia atasema,
Cha kufanya ‘Bichwa Sugu’, kigwanda ukiondoe.

MTAGALUKA RASHIDI (Mtaaluma),
S.L.P. 16380, Dar es Salaam. 



Kiswahili lugha yangu

Kiswahili lugha yangu, Kiswahili nima yangu
Kiswahili pambo langu, Kiswahili neno langu,
Kiswahili nembo yangu, lugha kwa Taifa langu,
Kiswahili lugha yangu, nakipenda Kiswahili.

Almas H. Shemdoe “Tunda la Matumaini”,
(NASAHA NA. 041  29 Machi 2000)
 

Kiswahili lugha yangu (Wito)

Kila asili ni mali, na tena ni afadhali,
Keshaiumba jalali, na kuipatia hali,
Kisha akaifadhili, na kuifanya asili,
Kiswahili wakipenda, kila asili ni mali.

Kiswahili ni asili, na tena kina fasili,
Nyenginewe sijidhili, kuzipatia asili,
Kiswa-nglishi” si fadhili, ni kujitia dhalili,
Kiswahili ni asili, kila asili ni mali.

Kiswahili Afirika, ndicho kilichosifika,
Lugha ilokubalika, wahenga walikipika,
Cha sasa mevurugika, asili ishakitoka,
Kiswahili ni asili, kila asili ni mali.

Kiswahili cha asili, chenye mizizi asili,
Kile kino mihimili, ya lafudhi za asili,
Kishapoteza asili, cha sasa sio asili,
Turudi kwenye asili, kila asili ni mali.
 

Juma S. Katanga (Jushaka),
“Sugu la Mashairi -Tanzania”,
Mapumzikoni -Chanika.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu

Mbukuzi anguruma Chuo Kikuu:
Wasomi mnatakiwa kukomesha dhuluma

Kuelekea uchaguzi mkuu 2000:
CUF yaiteka Dar

Maalim Seif afunguliwa mashitaka

‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi

MPASHO NASAHA
WE THIO LAFKIYANGU TEENA!

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani

WAZO  LA  WIKI
Ajenda mpachiko

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake

Kalamu ya Mwandishi
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake

Makala
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5):
Wananchi mjiandae kulinda kura

HABARI ZA KIMATAIFA

Riwaya
Kisasi cha mauti -2

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Kajumulo atishia kuwanyang’anya Kibadeni Simba
  • Kipukuswa kufuata nyayo za ‘Mgosi’ Hazali
  • Hazali sio Yanga ni Simba ‘kindakindaki’

  • Madadi azionya timu za Ligi Kuu
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita