|
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000 |
|
|
|
|
|
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake NA MAALIM BASSALEH JUZI, Jumatatu, Aprili 3, 2000, huko mjini Cairo, Misri, ulifanyika mkutano wa kwanza wa aina yake, tokea bara la Afrika lipate uhuru wake, baina ya Mawaziri wa nchi za nje wa nchi 15 zinazounda Jumui ya ya Ulaya (EU) pamoja na viongozi wa nchi 52, wanachama wa umoja wa nchi huru za Afrika (OAU). Ingawa mkutanohuo ulilenga kuzungumzia mambo mbalimbali, lakini lengo kuu lilikuwa ni kujaribu kuanzisha ukurasa mpya wa uhusiano na mashirikiano bina ya nchi za pande mbili hizo, ili kujaribu kufuta uhasama uliopo baina ya pande mbili hizo, uliosababishwa na athari za ukoloni. Aidha, nchi za Ulaya zimedai kuwa miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kutafuta njia ya kuisaidia Afrika kiuchumi kwa kauli ya Bwana Christ Pattern, ambaye ni Kamishna wa Mambo ya nje wa Jumuiya ya Ulaya (EU) amesema kuwa Jumuiya yake inataka kuona kuwa bara la Afrika linashiriki kikamilifu katika kuchangia uchumi wa dunia. Inaonekana, hilo la pili ndilo hasa, lililopelekea takriban viongozi wengi wa Afrika waliohudhuria mkutano huo wawe na matumaini kuwa Jumui ya Ulaya ingetangaza rasmi azma yake yakutaka kuzifutia nchi za Afrika madeni yake. Lakini wapi! viongozi wa nchi za Afrika wamerudi mikono mitupu. Ahadi ya kufutiwa madeni yao haikutolewa. Badala yake wameambiwa kabla ya kupewa ahadi ya kufutiwa madeni hayo viongozi wa nchi za Afrika wahakikishe kuwa wanaendesha utawala wa sheria katika nchi zao, wanaendeleza demokrasia, wanaheshimu haki za binadamu pamoja na kuepusha nchi zao kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kauli hiyo inaudhi, na hasa inapokuwa yule anayeambiwa hivyo ni mtu huru anayejitawala mwenyewe. Ni sawa na kutaka kuingilia mambo ya nchi isiyo kuhusu. Ndiyo maana Dkt. Salim Ahmed Salim, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha kwanza alisema kwa hasira, kuwa hakuna mtu yeyote awezaye kuifundisha Afrika demokrasia. Kwa mtazamo wa ghafla, nikweli nchi za Ulaya hazina haki ya kuzifundisha nchi huru za Afrika juu ya vipi ziendeshe tawala zao, na hasa ukitilia maanani kuwa nchi hizo hizo ndizo, huko nyuma, zilikuwa zikiongoza nchi hizi kimabavu pamoja na kuvunja haki za binadamu, wakati bara hili la Afrika lilipokuwa chini ya uwatala wao. Lakini kwa mtazamo wa ndani tutaona kuwa nchi za Ulaya, ingawa ndizo zinazoweza kubebeshwa lawama za kulikandamiza bara la Afrika, kiuchumi na kimaendeleo, wakati bara hili lilipokuwa katika utawala wao wa Kikoloni, juu ya hivyo, nchi hizo za Ulaya bado zina kila sababu ya kuzikosoa au kuzielekeza nchi za Afrika juu ya kuendesha utawala bora kwa raia wake. Kuna sababu nyingi za kufanya hivyo. Sababu ya kwanza kubwa ni kuwa wakati nchi za Afrika zilipokuwa zikidai uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa nchi hizo za Ulaya viongozi wa nchi za Afrika walikuwa wakidai kuwa wanataka kumrejeshea Mwafrika uhuru na utu wake; lakini tokea Afrika ijikomboe, mambo katika nchi nyingi za bara hili yamekuwa mbaya zaidi kuliko hata katika zile zama za Kikoloni! Kwa nini basi Wakoloni hao wa zamani wasituseme na kutukosoa? Wachilia mbali kuzungumzia habari za maendeleo ya kiuchumi tokea bara hiki lilipojinasua kutoka katika kucha za ukoloni, nchi nyingi za Afrika zimejikuta zikijiingiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, visivyokwisha, vinavyoendelea kuua maelfu ya Waafrika wasiokuwa na hatia yoyote. Ni vita vinavyoendeshwa na baadhi ya viongozi wa nchi hizo wenye uchu wa kubakia madarakani na kuendeleza tawala za kidhalimu, kwa gharama yoyote ile. Viongozi hao huwa hawajali maslahi ya nchi zao au watu wao. Raia wanalipuliwa na mabomu yakufukiwa ardhini na kulemazwa viungo vya miili yao, watoto wachanga wanakabiliwa na maradhi ya utapia mlo kwa kukosa lishebora, na wanawake pamoja na vikongwe wanateseka kwa njaa, maradhi na kukosa amani na utulivu katika maisha yao. Idadi ya Waafrika waliouawa, kujeruhiwa na kulemazwa baada ya uhuru, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, barani Afrika, ni kubwa zaidi kuliko hata ile idadi ya wale walioathirika namna hiyo katika kile kipindi chote cha ukoloni! Kwa nini iwe hivyo? Huo uhuru tulio udai Waafrika, kutoka kwa Wakoloni utakuwa na maana gani kwetu, ikiwa maana ya kujitawala ni kuhatarisha uhai wa watu wetu? Kwa nini basi Wakoloni, ambazo ndizo hizo nchi za Ulaya, tunazoziomba zitufutie madeni, wasililaumu bara hili pamoja na viongozi wake? Sababu ya pili kubwa inayozipa haki nchi za Ulaya kuzikosoa nchi za Afrika na kuzielekeza jinsi ya kuendesha tawala zao ni ile ya kuwa nchi hizo ndizo zilizozikopesha nchi za Afrika hayo madeni ambayo nchi za Afrika leo zinaomba yafutwe. Ingawa fedha hizo, zilitolewa kama mikopo kwa ajili ya kuinua uchumi na kuleta maendelo katika sekta za kilimo, viwanda, elimu na afya, lakini nyingi ya fedha hizo zilitumika kinyume na makusudio yake. Viongozi wengi wa nchi za Afrika walizifuja fedha hizo katika kujijengea ngome kuhami tawala zao kwa kuunda majeshi makubwa, ambayo baadaye ndiyo yanayogeuka kuwa tishio kwa usalama na uhuru wa wale wale raia wanaohitaji kulindwa na majeshi hayo. Baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika, bila ya kujali shida za wananchi wao wanaowaongoza wamekuwa wakilifuja pato la nchi pamoja na fedha za misaada na mikopo zinazotolewa kwa nchi zao, kwa kujinunulia majumba ya kifahari nchi za nje, vyombo vya anasa kama ndege na magari ya kifahari, pamoja na kujifungulia akaunti za fedha za kigeni katika mabenki ya nchi za nje. Hivi karibuni, huko Nigeria, mke wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Sami Abacha, alikamatwa na mabegi zaidi ya ishirini yaliyojaa fedha za kigeni ambayo alitaka kuyapeleka nchi za nje. Alizipata wapi fedha zote hizo? Juu ya hivyo wanapotokea wananchi kukosoa ulafi wa viongozi wao hadharani husakamwa na rungu la dola. Ni tokoea kumalizika kwa vita baridi baina ya nchi za Magharibi na Mashariki ndiyo nchi za Afrika zikaanza kunusa harufu ya demokrasia. Ni nchi za Ulaya Magharibi ambazo nyingi ndizo hizo zinazounda hiyo Jumui ya ya Ulaya(EU) ndizo zilizozilazimisha nchi za Afrika zianzishe mfumo wa vyama vingi na kuachana na mfumo wa ukiritimba wa chama kimoja. Kwa nini basi Afrika isifundishwe Demokrasia? Ingawa nchi nyingi za Afrika zimekubali kufuata mfumo wa vyama vingi, lakini nyingi zimefanya hivyo kwa shingo upande tu. Zimekubali ili zipate kuendelea kupata misaada kutoka katika nchi hizo za Ulaya. Laiti nchi za Afrika zingalikuwa zinauwezo wa asilimia mia kwa mia, kujitegemea wenyewe, basi tawala nyingi za Kiafrika zingaliendeshwa kwa misingi ya kibabe babe na kidikteta; kwa sababu pangalikuwa hapana wa kuzikemea! Lakini mfumo wa utawala ulimwenguni unageuka kidogo kidogo. Dunia inaanza kuwa kama kijiji kimoja tu. Hakuna anayethubutu kusema jambo lake halimhusu mwenziwe. Wenzetu wa Ulaya wamekwisha liona hilo. Wameelewa kuwa shida na taabu wanayopata watu wa nchi moja ulimwenguni inayotokana na utawala mbaya wa viongozi wake inaisababishia jumuiya ya kimataifa hasara ya hali na mali katika kusaidia kuwaendeleza watu wa nchi husika shida na taabu zao hizo. Kwa hivyo, nchi za Ulaya zimeamua kuipasha Afrika ziboreshe tawala zao zijali maslahi ya nchi zao na watu wao. Kwa mfano, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza Bw. Robert Cork, alipokutana na Rais William Mkapa wa Tanzania katika Hoteli ya Sheraton, huko Cairo, Misri, katika kipindi cha mapumziko, alitaka kujua kama nia ya serikali ya Tanzania ya kupunguza bajeti ya uchaguzi mkuu ujao si mkakati wa makusudi wa kutaka kuvibana na kuvidhoofisha vyama vya upinzani? Rais Mkapa alimjibu kuwa Tanzania imebidi ipunguze bajeti ya uchaguzi si kwa nia mbaya yoyote dhidi ya kambi ya upinzani bali kutokana na ufinyu wa bajeti ya nchi yenyewe. Na akamwambia kuwa Tanzania iko tayari kupokea misaada kutoka kwa wafadhili watakaojitokeza kufanya hivyo. Na akawashukuru wale waliokwishaanza kusaidia. Rais Mkapa alisema kuwa serikali yake itahakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru na wa haki. Ili kumhakikishia hayo alimwambia Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uingereza kuwa serikali ya Tanzania itawaalika wachunguzi wa kimataifa waje wenyewe kufuatilia uchaguzi huo jinsi unavyoendeshwa. Huu niushahidi tosha, kuwa katika ulimwengu wa leo, hakuna nchi inayoweza kujitenga na nyingine, na hasa ikiwa nchi hiyo ni ile isiyoweza kujitegemea yenyewe kiuchumi, kama Tanzania ilivyo. Vipi basi viongozi wetu wa kitaifa wanaoyaelewa vizuri hayo wasisaidie katika kuhakikisha kuwa visiwa vya Zanzibar vinatekeleza vile vifungu vya mkataba wa mwafaka vilivyosimamiwa na Jumuiya ya kimataifa ili kuleta, mazingira mazuri kabla ya uchaguzi mkuu ujao, ambao siyo kwamba unahitaji mshindi tu, bali unatakiwa ukubalike na Jumuiya ya kimataifa kuwa ni uchaguzi huru na wa haki? |
YALIYOMO
Tahariri
Mbukuzi
anguruma Chuo Kikuu:
Kuelekea
uchaguzi mkuu 2000:
Maalim Seif afunguliwa mashitaka ‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
Lishe
Madadi azionya timu za Ligi Kuu |
|
|
|
|