|
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000 |
|
|
|
|
|
Kwanini tunataka CCM ing'oke madarakani Na Mwijilisti Kamara Kusupa NI wakati ndio ulionilazimisha
kuandika mada hii ambayo nitaitoa katika mikupuo(series) na pia nitaitoa
kwa muda mrefu kwa kuwa sababu zenyewe ni nyingi. Imenipasa kuweka bayana
sababu zinazotufanya sisi Wanamageuzi wa kweli pamoja na wengine wasio
wanachama wa chama chochote lakini wanamapenzi mema kwa nchi yetu kutaka
CCM itoke madarakani ili nafasi yake ichukuliwe na chama kingine.
CCM ni tofuati kabisa na TANU Kwanza kabisa neno moja inabidi lieleweke wazi kwamba CCM hii iliyopo leo, ni tofauti kabisa na TANU iliyoleta uhuru kwa Watanganyika. TANU kilikuwa chama cha Wazalendo wakati CCM ni chama cha mamluki. Waanzilishi na wanachama wa TANU walitoa mali zao, walitoa sumni zao na wakati wao kwa manufaa ya taifa wakati ambapo CCM ya leo inatwaa mali za taifa kwa manufaa ya watu binafsi na wajanja wachache wenye nafasi. TANU kilikuwa chama cha ukombozi wakati CCM ni chama cha walaji. Kila aliyeko ndani ya CCM awe mkubwa au mdogo, yupo kwa ajili ya ulaji ikitokea bahati mbaya kwao kuwekwa benchi kama ilivyotokea kwa chama rafiki yake UNIP ya Zambia, basi CCM itaanza kukimbiwa kwanza na viongozi wake wakuu na hatimaye kada ya chini kabisa. Umoja na mshikamano wao unashikiliwa na dola, kama watanyang'anywa nguvu za dola watasambaratika baada ya muda mfupi sana. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanaoiongoza CCM kwa sasa hawana historia yoyote ya harakati za ukombozi wa Taifa hili. Waliojitoa mhanga kupigania uhuru wa nchi hii, wengi wao wamewekwa kando na wengine tunapata kujua habari za mchango wao mkubwa baada ya wao kufa kwani hapo ndipo inapopatikana nafasi na wasaa wa kueleza historia ya marehemu na mambo makubwa aliyoyafanya enzi za uhai wake. Mfano hai ni mzee Zuberi Mtemvu, hakuna aliyetaraji kwamba pamoja na mchango wake mkubwa katika TANU, na katika kuleta uhuru wa nchi hii CCM ingemhesabu kuwa si kitu hadi siku ya kifo chake kiasi kwamba washindwe hata rambirambi za chama, kweli sasa naamini kwamba "CCM ina wenyewe." Hao wanaojiita wenyewe, wanajijua walikotoka, wanajijua jinsi walivyojipanga na jinsi walivyojiweka madarakani kinyume na matakwa ya wana wa nchi hii. Neno moja lililowazi ni hili, hao wanaojiita wenyewe, hawakutokana na TANU wala sio uzao wa hao walioanzisha TANU hawa ni uzao wa nyoka. Lengo na madhumuni ya TANU vimetelekezwa Mojawapo ya lengo na madhumuni ya TANU ni kuwatayarisha Watanganyika ili wawe na uwezo wa kujitawala. Uhuru uliokuwa ukipiganiwa na TANU si kuondoa ngozi nyeupe tu, bali ni kuondoa uonezi, dhuluma na ukandamizaji wa aina zote, na baada ya kuyaondoa maovu haya wananchi wawe na uwezo wa kuendesha nchi yao chini ya utawala wa haki. Anayetaka kuhakikisha haya, ajitwalie andiko au "document" yoyote yaTANU aone kilicho andikwa humo,ni wazi atagundua 'spirit' ya ukombozi. Ukombozi kamili unaojidhihirisha katika maisha ya siku kwa siku ya wananchi, kama watu wana uwezo wa kuendesha nchi yao bila ya mashinikizo kutoka nje basi hao wamejikomboa lakini kinyume cha hivyo ni ukoloni wa aina yake. Kwa hivi sasa mambo yako kinyume kabisa na matumaini waliyokuwa nayo wapigania uhuru wa nchi yetu. Kwanza nchi haiko huru badala yake wananchi tunalazimishwa kufanya tusiyo yataka na wanaotulazimisha siyo hao wanao tutawala bali ni watu walio nje ya mipaka ya nchi yetu isipokuwa hayo masharti yao na lazima zao wanazipitishia kwa watawala wetu tuliowachangua kwa kura zetu * Mpaka sasa tunalazimishwa kulipa kodi ili kulipa madeni na siyo kwa ajili ya maendeleo yetu. * Tunalazimishwa kuchangia huduma za jamii (baada ya kulipa kodi) wakati huduma hizo aidha hazipo au zinatolewa katika uduni wa kutisha. * Tunalazimishwa kila mmoja kubeba msalaba wake mwenyewe na hao wanao tuhubiria sera za kubeba msalaba hawasemi wazi mwisho wa safari yetu ni lini na wapi na itakuwaje, maana historia ya msalaba inaonesha wazi kwamba kila aliyeubeba aliishia kusulubiwa na kuuawa kikatili. Sasa sijui kama watawala wetu nao wamekusudia wananchi baada ya safari ndefu ya kubeba msalaba tutundikwe juu yake na tufie msalabani? * Tunalazimishwa kuuza kila kitu na mbaya zaidi kuwauzia wageni tena kwa bei wanayo itaka wao wanunuzi. Kupitia lazima hiyo NBC imeuzwa, mahoteli ya kitalii yameuzwa, mbuga za wanyama wetu zimeuzwa, nama shirika yetu yote yameuzwa. * Tumebaki hatuna kitu. Hatuna fedha, hatuna kazi wala tumaini la watoto wetu kufanya kazi za staha kwenye hivyo viwanda na makampuni tuliyouzia wageni. * Tunalazimishwa kuuza bandari yetu, mwisho wa yote mtu asije kushangaa akifika pale bandarini akaambiwa ya kwamba geti namba fulani ni kuwaajili ya Wazungu tu, na geti namba fulani ndilo lililotengwa kwa ajili ya Waafrika na weusi, maana huko kwenye mbuga za wanyama tayari Wazungu walionunua wanasema hawataki kuona mwenyeji. Tunalazimishwa kupunguza thamani ya sarafu kila kukicha, madhara yote ya kuanguka kwa thamani ya shilingi yetu hawabebi watawala wala matajiri bali wanabeba maskini. Huu ndio ambao wao CCM wanauita msalaba, kisha wanathubutu kusema bila haya kwamba "kila mmoja abebe msalaba wake mwenyewe." Wakati sisi walalahoi tunatwishwa msalaba wa dhiki, umaskini, na njaa, wao CCM ndio kwanza wananunua magari ya kifahari, na kujenga mahekalu kana kwamba wana mashindano ya nani zaidi. Je, ni kwa haki ipi ya ziada waliyo nayo hadi kutufanyia yote haya? Ukweli ni kwamba hawana haki yoyote ya ziada wala uwezo wowote wa ziada isipokuwa kinachosababisha tufanyiwe yote haya ni upole wetu, uungwana wetu, na utuwema wetu. Katika sehemu fulani ya maandiko ya TANU, ilitamkwa kwamba tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumenyonywa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tupuuzwe, tunyonywe na kunyanyaswa. * Sasa tunataka mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena,wala tusipuuzwe tena. Haya yaliandikwa kutokana na hali halisi ya watu waliochoshwa na Ukoloni kwa hiyo waliamua kwa dhati kwamba wanataka mabadiliko ya kuwaondolea unyonge wao ili wasipuuzwe tena. Nadhani waligundua kwamba unyonge wao ndio mchawi wao. Lakini sasa uonezi wa watawala wa leo umezidi hata ule wa Mkoloni. Watawala wetu wanatupuuza hata kuliko Wakoloni walivyotupuuza, watawala wetu hawatusikilizi, hawatujali wala hawaogopi kuudhi umma. Je ni kitu gani kinachowapa kiburi na jeuri ya kutufanyia haya yote? Mwaka huu ukiwa mwaka wa uchaguzi serikali ya CCM inabomoa nyumba za watu, vibanda vya watu vya biashara pasipo hofu kwamba watu wakiudhika watainyima CCM kura, ni wazi kwamba hawategemei kura za wananchi bali tumaini lao li katika hizo njia zao za kijambazi za kujipatia ushindi. Siku hizi limekuwa neno la kawaida kwa vijana wetu kufungwa mashati na Polisi, na kuongozwa msururu sawa na msururu wa yule mfanyibiashara maarufu wa watumwa Bwana Tip Tip. Kosa lao nini? Eti ni wazurulaji, hawana kazi wala vitambulisho. Mtu akiuliza ni vitambulisho vya aina gani ambavyo Polisi wanataka vijana wetu wawe navyo? maana serikali ya CCM haijatoa vitambulisho vya taifa kama vile jirani zetu wa Zambia na Kenya, ambavyo vinaitwa "National Identity Card". Hizi kadi za taifa ndizo ambazo raia hujitambulisha nazo hata wakati wa kuandikisha wapiga kura. Licha ya kilio cha muda mrefu kwamba Watanzania tutengenezewe vitambulisho vya Taifa kwa manufaa ya watu na utaifa wetu, lakini bado watawala wamepuuza kilio hicho na matokeo yake sasa mgeni anayejua Kiswahili hana tofauti na mzawa. Wakati mwingine wageni wananeemeka zaidi nchini Tanzania kuliko katika nchi zao walikotoka wakati huo huo Mtanzania na hasa Mwafrika asilia ananyanyasika kana kwamba yuko katika nchi hii kwa bahati mbaya. Je mateso yote haya yataondoka lini? Jibu ni kwamba mateso yetu yataondoka na utawala uliopo, bila ya kuundoa utawala wa sasa wa CCM, mateso hayataondoka. Inabidi CCM itoke na mateso yake, itoke na taabu zake, itoke na rushwa yake, itoke na uonezi wake, naam itoke na ushetani wake. Imefika wakati wa kusema CCM mmetupuuza kiasi cha kutosha sasa hatutaki kupuuzwa tena, tunataka mageuzi. Umefika wakati wa kusema tumekuwa na umaskini kwa kiasi cha kutosha sasa tunataka chama kingine cha kututoa toka kwenye umaskini uliopo hadi kwenye neema kama vile TANU ilivyotutoa kwenye Ukoloni hadi uhuru. Inaendelea wiki ijayo "MPENDE MSIPENDE, MTAKE MSITAKE NI LAZIMA NITASHINDA." |
YALIYOMO
Tahariri
Mbukuzi
anguruma Chuo Kikuu:
Kuelekea
uchaguzi mkuu 2000:
Maalim Seif afunguliwa mashitaka ‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
Lishe
Madadi azionya timu za Ligi Kuu |
|
|
|
|