NASAHA
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5)
Wananchi mjiandae kulinda kura 


VUGUVUGU la wananchi kujiunga kwa wingi na Chama cha Wananchi (CUF) limeanza kuwatia kiwewe viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake, kiasi cha kuwafanya viongozi wa Serikali kuzihama ofisi zao na kuhamia mikoani kwenda kupiga porojo kama walivyozoea kwa lengo la kuwalaza usingizi wapiga kura na kuwapa matumaini ya bandia. Mwandishi RAJAB KANYAMA anaendelea zaidi katika sehemu hii ya tano.
 

MKUTANO mkubwa wa hadhara uliofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) siku ya Jumapili katika Viwanja vya Jangwani, ilikuwa ni changamoto ya kutosha kwa Chama Cha Mapinduzi, kwamba sasa ni kweli wananchi wameamua kuagana na chama tawala, ambacho kwa kipindi chote walichoshika hatamu, wameshindwa kuboresha maisha ya Watanzania walio wengi. 

Siku hizi, wananchi wanaojishughulisha kutumia bongo zao wanafahamu kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeishiwa hoja. 

Kabla ya hapo, kwa kutumia vyombo vya propaganda (Ulaghai) walikuwa wakijaribu kuwapumbaza wananchi kwa kuwadanganya eti chama cha CUF nichama cha kidini. 

Wananchi walipuuza maelezo hayo ya kilaghai kama ilivyostahili na kisha wananchi wakatoa ushahidi kuonesha kwamba, kama ni udini basi ukweli unafichwa. 

Wachunguzi wa mambo ya kijamii nchini wanakiri kwamba, CCM ni chama kilicho na dalili za wazi kabisa za kuonesha kuwa ni chama cha kidini zaidi kuliko chama chochote cha siasa hapa nchini. 

Safu ya viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi yote imejazwa na watu wa dini moja(Wakristo) ukiachilia mbali viongozi waandamizi wengine waliojaa katika taasisi za umma na serikalini ambao huchaguliwa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi anapokuwa amevaa ile kofia yake ya pili ya Urais wa Jamhuriya Muungano wa Tanzania. 

Baada ya hoja hiyo kuthibiti, siku hizi suala la kuwa CUF ni chama cha kidini limetoweka kutoka katika vyombo vya habari. 

Sasa uchaguzi mkuu unakaribia, wahafidhina na washirika wao, chama cha waandishi wa habari, wameanza uzushi wa aina nyingine, tamko la umwagaji wa damu. 

Jambo hili halitushangazi, maana inafahamika na watu wote wenye akili timamu kwamba ni kawaida kwa chama cha kisiasa au hata dhehebu la dini lililoishiwa na hoja kutokukata tamaa na kuendelea kushikilia ile imani yao kongwe kwamba unapoishiwa na hoja, tumia vitisho, na wakati mwingine hata kuna watu wasio na hatia na kisha wasingizie wapinzani. 

Lengo ni kuwatia hofu wananchi wasiendelee kuwaunga, mkono na hatimae kufanikiwa kuwang'oa madarakani. 

Mifano yahoja hii iko mingi, mauaji ya wananchi wasio na hatia yanayofanywa na majeshi ya Serikali nchini Algeria na kisha kuwasingizia wanamgambo wa Kiislamu wanaoitwa wenye msimamo mkali ni mmoja. 

Na huko SriLanka, mauaji yanayofanywa na majeshi ya Serikali husingiziwa wapiganaji wa Tamil Tigers, wanaotaka kujitenga ili kuanzisha taifa lao huru. 

Mwandishi yoyote makini, anapaswa kuelimisha jamii sababu za vurugu ndani ya nchi hizo ambazo ni kudhulumiwa kwa ushindi uliokuwa unaelekea kukiweka madarakani chama cha Islamic Salvation 

Front (FIS) nchini Algeria na lengo la kutaka kujitawala kwa wananchi wa Kitamil wanaonyanyaswa na serikali huko SriLanka. 

Haya ndiyo masuala ya kuzingatia katika matokeo yanayozikumba nchi hizo. 

Kutoa taarifa kinyume na ukweli huo, na kuendelea kuwalaumu wanaharakati wanaoendesha mapambano ili kurejesha haki wanayostahili ni kupotosha wananchi. 

Kwa wasanifu wa lugha kinachofanywa na wanaharakati hao ndio huitwa "jino kwa jino au pua kwa pua" na hii ni kwa sababu hata madhalimu huwa na mashabiki wao ambao kwa pamoja huendesha dhulma dhidi ya wananchi wengine. 

Katika kuendeleza ulaghai na uchochezi usio na maana, mwandishi mmoja, ndani ya gazeti moja la kila wiki la tarehe 30 Machi 2000 chini ya anuani "Bwana Lipumba, tumwage damu kukuingiza Ikulu? Ameandika "Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam, alisema kuwa endapo chama tawala, CCM kitaiba kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, basi damu itamwagike nchi hii." 

Katika sehemu nyingine mwandishi huyo ameandika "Hii ni kauli ya hatari na ya kutisha sana." 

Hawa ndio watu wanaojiita waandishi tulionao nchini, anaandika akionesha chuki ya wazi kwa muhusika, na kisha anathibitisha upeo finyu wa fikra alizonazo. 

Katika sehemu nyingine ya makala yake anadhihirisha hilo kwa kuandika "Hata kama CCM imeiba kura, kama ulivyo wasiwasi na hofu yake, si aende mahakamani adai haki yake?" 

Haki inayokusudiwa hapa ni ya kunyang'anywa ushindi kwa kuibiwa kura. 

Mwandishi hajui kwamba, ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 74 (12) haki hiyo imezuiliwa, kama inavyoeleza, "Hakuna mahakama yoyote (nchini) itakuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na tume ya uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake." 

Haifahamiki mwandishi wa makala hiyo alikuwa anakusudia mahakama ipi? 

Ni vema waandishi wa aina hii na wale wa Chama Cha Waandishi, wakafahamu kwamba wananchi wa karne ya ishirini na moja, si wale wa miaka ya sabini, waliokuwa wakiamini kila kilichokuwa kikisemwa na wanasiasa na kuandikwa katika magazeti na kutangazwa katika radio. 

Tangu lini mtu anaetoa tahadhari ili kusitisha dhulma aitwe kuwa ni mtu wa hatari na yule anayedhulumu haki za wananchi mchana kweupe ndiyo aitwe mdumisha amani? 

Mkutano wa Jangwani ambao mwandishi wa makala tuliyotaja, ameutaja ulifanyika siku ya Jumpaili tarehe 26.2.2000 na ulikusanya umati mkubwa wa watu ambao bado haujawahi kukusanywa na kiongozi yeyote wa kisiasa ndani ya nchi, tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 1995 kwa ajili ya kuzungumzia sera za chama chake. 

Siku iliyofuata, hakuna chombo chochote cha habari kilichoandika au kutoa habari za mkutano huo wa aina yake, jambo ambalo limewaamsha wananchi wengi sasa, na kuwafanya waelewe kuwa mtandao wa Chama Cha Mapinduzi umeenea mpaka ndani ya vyombo vya habari. 

Hatuelewi mwandishi wa makala tunayoijadili hapa, alikuwa wapi muda wote huo, mpaka anaibuka siku ya Alhamisi na makala ambayo hata kuijadili hapa ni kuipa hadhi isiyostahili? 

Tatizo la waandishi wengi siku hizi hapa nchini ni kiwango chao kidogo cha ufahamu wa lugha ya Kiswahili pamoja na dhana zinazokusudiwa kujengwa na misamiati inayotumiwa na wanaoifahamu lugha ya Kiswahili katika kiwango cha juu zaidi yao. 

Tamko "Endapo Chama Cha Mapinduzi kitaiba kura katika uchaguzi mkuu...." Ni dhana iliyowekewa sharti, sasa labda tumuulize mwandishi wa makala hiyo endapo Chama Cha Mapinduzi kitaiba kura, wananchi walioibiwa kura zao wachukue hatua gani? Tukizingatia kwamba njia ya kwenda mahakamani ndio hiyo ambayo tayari imefungwa na Ibara ya 74(12) tuliyotaja? 

Juu
 

YALIYOMO
 
 

Tahariri
Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu

Mbukuzi anguruma Chuo Kikuu:
Wasomi mnatakiwa kukomesha dhuluma

Kuelekea uchaguzi mkuu 2000:
CUF yaiteka Dar

Maalim Seif afunguliwa mashitaka

‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi

MPASHO NASAHA
WE THIO LAFKIYANGU TEENA!

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani

WAZO  LA  WIKI
Ajenda mpachiko

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake

Kalamu ya Mwandishi
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake

Makala
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5):
Wananchi mjiandae kulinda kura

HABARI ZA KIMATAIFA

Riwaya
Kisasi cha mauti -2

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Kajumulo atishia kuwanyang’anya Kibadeni Simba
  • Kipukuswa kufuata nyayo za ‘Mgosi’ Hazali
  • Hazali sio Yanga ni Simba ‘kindakindaki’

  • Madadi azionya timu za Ligi Kuu
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita