NASAHA
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Kuporomoka kwa maadili katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake 

Na H. Sulayman 

Kuiga utamaduni na maadili ya kimagharibi:

Tabia ya kuthamini na kutukuza kila kifanywacho na Wazungu imekuwa ikikua siku baada ya siku. Umagharibi umeingia ndani ya nyumba zetu kupitia katika milango ya vyombo vya habari. Utamaduni wa kuadhimisha siku ya wapendanao(Valentine day) na siku ya wajinga (fools day) ni ushahidi tosha wa uvamizi huo haramu. 

Kiislamu ni ibada kujifunza na kuiga kila chenye kuleta faida kwa jamii, na ni dhambi kubwa mtu kuiga chenye kuleta hasara na kuisababishia jamii madhara. Anasema Mtume Muhamad( s.a.w.): "Usiwe mpenda kuiga wa kila kitu, ukasema miminiko na watu, wakifanya mema au mabaya niko nao tu. Isipokuwa uwe nao watapokuwa wanatenda mema na yenye faida kwa jamii, na uwe mbali nao pindi wakitenda maovu (ya kuihilikishajamii)". Hadithi hii inatoa msimamo ambao kila mwanadamu mwenye akili timamu anapaswa awe nao;afanye au aige jambo kwa sababu ya uzuri wake na faida yake kwa jamii. Na hii inatupelekea kuamini kuwa hekima ya Uislamu kuwaelekeza wafuasi wake kutafuta elimu japo sehemu ya mbali kama Uchina, ni kutaka watu wafanye utafiti wa mambo mazuri yenye faida kwa watu kisha wayaeneze mazuri hayo. Anasisitiza Allah Mafhumu (concept) hii kwa kusema: "Kwa nini halitoki kundi miongoni mwao(yaani Waislamu wa Taifa fulani) kwenda kujielimisha vema katika dini ili waje kuwaelekeza wenzao na kuwaonya baada ya kurejea makwao, iliwapate kujitahidharisha na mabaya" 9:122. Mwanafalsafa Mashuhuri wa Kiislamu Al-Ghazali amesema katika kitabu chake "Ihyaa ulumiddini" kuwa mtu kusafiri kwa ajili ya kujifunza mambo muhimu yenye kuleta faida katika jamii ni "WAJIB" kwa maana kama kuna mtawala wa Kiislamu basi atawalazimisha baadhi ya watu waenda kutafuta taaluma au fani muhimu katika jamii ile. 

Yako mambo mengi mabaya ambayo yameigwa na Watanzania wengi, wakubwa kwa wadogo, japokuwa vijana ndio walioathirika zaidi na wimbi hili la Umagharibi. Taifa hii kwa bahati mbaya imechangia katika kuharibika maadili sawia ya vijana wetu. Kunyoa Panki, kusokota au kusuka nywele kijana wa kiume, kuvuta na kubugia madawa ya kulevya yote haya ni miongoni mwa mabaya wanayoyaiga vijana wetu. Sitaki kuelezea zaidi hivi vitendo ambavyo athari yake ni kubwa lakini kwa idadi kidogo ndogo ukilinganisha na maadili mengine mabaya ya Kimagharibi ambayo yanaosha akili za jamii nzima, kwa lengo la kuwafanya watu wadharau dini na tamaduni zao wafuate matamaniyo na tamaduni za Kimagharibi. Kwa mfano" Bid'a (Fabrication) ya siku ya wajinga (Fool's day). Hii ni tabia mbaya, japokuwa utaambiwa kudanganya mara moja kwa mwaka, kwa ajili ya kujifurahisha siyo vibaya! La ajabu ni kuwa tabia hii inalindwa na sheria zote za Kimataifa. Kwa maana huwezi kumshitaki mtu kwa kuwa kusema uongo, kama atafanya hivyo tarehe moja mwezi wa nne kila mwaka kabla ya saa nne asubuhi. Tabia hii ni sawa na ile ya Wayahudi waliodhania kuwa waweza kumdanganya MwenyeziMungu kwa kutega nyavu zao za kuvulia samaki siku ya Ijumaa na usiku wa kuamkia Jumamosi na kuweza kuwanasa samaki waliokuwa wakizagaa ovyo siku ya Jumamosi siku ambayo waliharamishiwa kuvua!! (Rejea Quran 7:163-166). Hebu tujiulize uzuri na uhalali wa tabia kama hii. Ni watu wangapi duniani wameathirika au kufariki dunia kutokana na mshituko kwa habari mbaya za uongo walizoletewa kwa jina la fool's dayu!. Pesa ngapi, muda na nguvu zilizoteketea au kupotea kwa kuuendeleza upuuzi huu!! Watu waishio mabondeni hapa jijini walijikuta wakipoteza muda na nauli zao kwa kwenda hadi kwenye ofisi ya mkuu wa Mkoa tarehe1/4 kufuatia tangazo lililosikika katika kituo kimoja binafsi cha radio, kuwa watu hao wangepewa viwanja vipya pamoja na misaada mingine!! 

Uislamu unapinga vikali tabia hii na unakemea uongo hata ule wa kumdanganya mtoto njoo nikupe pipi au andazi. Mtume Muhammad s.a.w. alinuna siku moja alipomsikia mtu mmoja akimuita mwanawe (mtoto) njoo nikupe tende,lakini bahati nzuri yule mtu alikuwa na kipande cha tende mkononi. Hapo Mtume akasema laiti ungelikuwa huna kipande hicho ukamdanganya mtoto, basi ungeliandikwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa wewe ni mwongo -kuashiria kuwa angeliandikiwa dhambi. Kisha Mtume s.a.w. akatoa mwongozo kwa kusema: "Semeni(ongeeni)ukweli mtupu hata katika mizaha yenu". Na "Jihadharini na kusema uongo, hakika uongo humpelekea mtu katika maasi, na maasi humpeleka mtu motoni. Hakika mwanadamu huendelea kujizoesha na kusema uongo (mara kwa mara) kwa kila dogo na kubwa mpaka akafikia kuandikwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa fulani ni mwongo". Kuandika huko ni ishara ya kupewa cheti cha kumpeleka jahannam. 

Katika hali ya kawaida ni watu wangapi wameshasalimika na tabia hii? Je vijana wetu vijiweni, mashuleni na hata nyumbani wanapewa mwongozo wa kujenga tabia ya ukweli au ya udanganyifu. Vipi na nini tunawaeleza juu ya siku ya wajinga, nani nani mjinga, mwongo au mkweli aliyedanganywa!! Haya ni maswali muhimu ya kutafutiwa majibu. Hebu fikiria hali ya mtoto aliyedanganywa na mwalimu wake darasani siku ya tarehe 1/4 (siku ya wajinga)kisha mwalimu huyo akapigiwa makofi na mtoto kuzomewa. Sijuia ni taswira gani watatoka nayo watoto! Kwa nini mwalimu asizingatie maelekezoya Mwalimu mkongwe wa Kiingereza Herbert Spencer (19543, P.314)alipomshauri mwalimu ambaye ni mlezi kuwa afanye chini juu kumuelekeza mwanafunzi wake namna ya kupambanua baya katika zuri kwa kumfanya alishangilia na kulipenda zuri, kwa sababu kizuri hupendwa na wenye akili sawia, wakati kibaya huchukiwa na kuwafanya watu wasinyae wakisikiapo na kukiona. 

Tusihadaike na usemi wa hao Wazungu kuwa kuna uongo mweupe (white lie). Sijui mweusi ni upi!! Kama uitwao uongo mweupe hauna madhara basi usiitwe hivyo bali uitwe "ukweli", maana uongo kama neno lilivyo ni mbaya unaostahiki kukemewa na watu wote, vyombo vyote vya habari na dini zote. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumekata mizizi ya fitina. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu

Mbukuzi anguruma Chuo Kikuu:
Wasomi mnatakiwa kukomesha dhuluma

Kuelekea uchaguzi mkuu 2000:
CUF yaiteka Dar

Maalim Seif afunguliwa mashitaka

‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi

MPASHO NASAHA
WE THIO LAFKIYANGU TEENA!

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani

WAZO  LA  WIKI
Ajenda mpachiko

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake

Kalamu ya Mwandishi
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake

Makala
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5):
Wananchi mjiandae kulinda kura

HABARI ZA KIMATAIFA

Riwaya
Kisasi cha mauti -2

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Kajumulo atishia kuwanyang’anya Kibadeni Simba
  • Kipukuswa kufuata nyayo za ‘Mgosi’ Hazali
  • Hazali sio Yanga ni Simba ‘kindakindaki’

  • Madadi azionya timu za Ligi Kuu
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita