|
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000 |
|
|
|
|
|
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq Na Dr. Yusuf Al-Qardhawy 27 FEBRUARI/2000 sawa na Jumapili 23 Dhul Qaada 1420H alifariki mwanazuoni mkubwa na Dala Sheikh Sayid Sabiq akiwa na umri wa miaka 85. Sheikh Sayyid Sabiq ni mmoja wa wanazuoni wa Azhar aliyemaliza masomo yake katika kitengo cha Sheria, na hali hiyo iliwaunganisha Waislamu na kuwaelimisha katika sheria. Baada ya hapo Sheikh Sayid Sabiq alikuwa mmoja wa wanaharakati tangu alipokuwa mwanafunzi akiwa karibu na wenziwe kama Abdul Muiz Abdul Satar na Sheikh Muhammad Al-Ghazali lakini hawa wawili walikuwa katika kitengo cha Usul Diin katika Chuo Kikuu cha Azhar. Sheikh Sayid Sabiq alijishughulisha zaidi na fiqh, tofauti na ndugu zake maduat wa Azhar, hili lilitokana zaidi na kuwa yeye alisoma mambo ya sheria. Alianza kuandika katika gazeti la kila wiki la ikhwana masuala ya Fiqh ya tohara akirejea vitabu vya Diin Al-Khalis cha Sheikh Mahmoud Al-Khatab al-Sabaky, mwanzilishi wa jumuia ya sharia ya Misri, kitabu chenye jumla ya juzuu tisa cha Fiqh ya ibadat na kitabu cha mughni cha Ibn Qudama na Zaad al-aad cha Ibn Al-Qayyim na vinginevyo. Sheikh Sayyid Sabiq alitumia njia ya uandishi wa aina yake ambayo ni kuacha kasumba(taasub) ya madhehebu, pia hakuwa na tabia ya kuwajeruhi watu au kuwaudhi watu mbalimbali na akitegemea dalili kutoka kwenye quran,suna na Ijmai. Sheikh huyu alifanya kazi zake kuwa nyepesi kwa kutokutumia maneno magumu na mazito ya kisheria ya ki-Fiqh. Alitumia lugha ambayo inakubalika na kufahamika na kila mmoja anayesoma. Pia Sheikh alikuwa hapandelei kutaja tofauti zilizopo katika mas-ala, ila pale penye ulazima wa kufanya hivyo. Na alitoa rai mbali mbali juu ya mas-ala na kutanguliza rai inayokubalika, na aliacha kutoa msimamo iwapo jambo lenyewe halikumbainikia zaidi na pale ambapo rai yake na dalili vililingana uzito basi aliona ni bora kuliacha jambo hilo kwa msomaji abebe jukumu la kuchagua msimamo anaouona unafaa zaidi au aende kumwuliza mwanachuoni mwingine. Tabia hii ilikuwa haijachukuliwa na mwandishi mwingine kabla yake. Kitabu chake maarufu cha Fiqh sunna alianza kukiandika juzuu ya kwanza mwaka 1365 (1945M). Hicho kilikuwa ni kitabu kidogo juu ya Fiqh ya tohara ambacho utangulizi wake uliandikwa na Imamu Hassan al-Banna na kuusifu usulubi wake wakuandika katika Fiqh na kusema kuwa ulikuwa ni mzuri wenye kuvutia na kumpendeza kila mtu. Katika utangulizi wake Sheikh Sabiq alisema kitabu hicho kimechukua dalili kutoka ndani ya quran, hadith Sahihi dalili zinazokubaliwa na umma. Na akaongeza kuwa kinamfaa kila muislamu. Kitabu cha Fiqh sunna kinatoa sura ya daawa kama alivyoifanya mtume Muhammad (s.a.w.) na kufungua milango ya ufahamu juu ya Allah na Mtume wake na kina uwezo wa kuwaunganisha Waislamu kwa kutumia sunna na kina uwezo wa kuondoa kasumba ya tofuati ya madhehebu na ni wazi ameeleza kuwa milango ya ijithadi bado ikowazi. Aliendelea kutoa vijitabu vidogovidogo kwa mara 14 na alipokamilisha vikatolewa katika vitabu vitatu. Ilimchukua miaka 20 kukamilisha kazi hiyo ambayo iliziba pengo ambalo lilikuwepo katika maktaba ya Kiislamu katika upande wa Fiqh. Fiqh sunna ya Sayyid Sabiq haihusiani na madhehebu yoyote kwasababu imechukua dalili zake moja kwa moja kutoka vianzo vikuu vya quran na sunna jambo ambalo lilikifanya kitabu hiki kuwa maarufu miongoni mwa wasomaji wa dini ya Kiislamu na kuona kama kitabu cha kurejea katika mas-ala mengi ya Kiislamu. Jinsi kilivyokuwa maarufu ndivyo kilivyouzika na kuchapishwa mara kadhaa kama kawaida ya vitabu vyote vinavyopendwa sana na wasomaji. Mimi, nimemjua Sheikh Sayyid Sabiq katika uandishi wake wa makala katika gazeti la kila juma la Kiislamu na nilifuatia habari za kwa ukaribu mara baada ya kutoa juzuu yake ya kwanza ya kitabu chake cha Fiqh sunna kwani alikamatwa kwa tuhuma za kutoa fatwa ya mauaji ya Al-Nagrashy Basha. Tuhuma hizo zilieleza kuwa Sheikh Sabiq alitoa fatwa hiyo kwa Abdul-Majib Hassan, auwawe Al-Nigrashy kwa sababu alifungia jumuiya ya Ikhwani isiendelee na shughuli zake. Kwa tuhuma hizo hapo juu, magazeti yalimpachika jina la 'Mufti wa damu'. Pamoja na hivyo mahakama ilimwachia huru kwa kukosa kupata hoja ya kumtia hatiani,lakini alikamatwa tena pamoja na wafuasi wengine wa jumuiya ya Kiislamu hapo mwaka 1949 ambapo alipelekwa mahabusu ya atuur. Akiwa katika mahabusu ya Atuur, katika chumba namba 12, nilikutana uso kwa uso na Sheikh Sabiq ambamo nami nilikuwa mahabusu. Katika chumba namba mbili cha gereza hilo ilikuwa ni selo ya Sheikh Muhammad Al-Ghazal ambaye alikuwa Imam wetu katika kifungo hicho. Katika wakati huo Sheikh Sayyid Sabiq alikuwa anaendesha darsa duara la Fiqh baada ya sala ya Al-fajiri na baada ya kumaliza watu wote tuliohudhuria darsa hilo tulisoma dua ya maathurat. Na baada ya hapo Sheikh Muhammad Al-Ghazali alifanya darsa la daawa. Tulipotoka katika gereza la Atuur, tuliandamana katika kikundi cha pamoja cha daawah, nami nilikuwa nikimtembelea mara kwa mara nyumbani kwake katika mtaa mdogo wa Suuq Al-Silah na hata alipohamia mtaa wa Garden City katika sehemu ambayo ilikuwa ikimilikiwa na mayahudi baada ya kuhamia Falastini. Nilifanya kazi na Sheikh alipokuwa mkurugenzi wa idara ya utamaduni katika wizara ya Waqfu wakati ambapo Sheikh Al-Ghazali akiwa mkurugenzi wa idara ya misikiti na Sheikh Al-Bahy Al-Khuly alikuwa mratibu wa mambo ya dini katika zama ambazo waziri alikuwa Sheikh Ahmad Hassan Al-Bakuury. Sheikh aliendelea katika idara hiyo hadi wakati Dk. Al-Bahya lipochukua uwaziri wa Waqfu na uhusiano wao ukabadilika ukawa mbaya. Mara wakati huo Al-Ghazali na Sayyid Sabiq walihamishiwa Al-Azhar na kuondolewa wizarani. Tabia ya Sayyid Sabiq ilikuwa ni mcheshi na mwenye kupenda masheikh, inakumbukwa kuwa wakati alipotuhumiwa kwa kutoa fatwa ya kuuwawa kwa Nagrashy, akiwa mahakamani aliulizwa kama anamfahamu (Muhammad Malik). Basi jawabu lake mahakamani llikuwa! 'Vipi nisimjue Imam wa Daru Al-Hijra Radhia Llah Anhu?" jawabu hilo liliwaudhi sana waandishi wa habari ambao walimpachika jina la'mufti wa damu.' Kwa ghadhabu wakasema, wewe habithi, sisi hatuulizi juu ya Imam Maliki tunakuuliza juu ya gaidi Malik? Na jawabu lake lilikuwa yeye ni msomaji wa Fiqh hivyo anawajua watu wa Fiqh hawajui magaidi. Na hili ni wazi kuwa tulipokuwa tumekamatwa maswali mengi alikuwa akitupiwa Sheikh Al-Ghazali lakini kila lilipotokea swali la Ki-Fiqh basi alilirusha kwa Sheikh Sayyid Sabiq ambaye aliyajibu kwa ufasa kwani yeye ndiye alikuwa Faqih wa Kiislamu. Zaidi ya Fiqh Sheikh Sabiq alikuwa amebobea katika uandishi wa vitabu vya akida na daawa na vitabu vinginevyo. Katika miaka ya mwisho ya umri wake Sheikh Sabiq alienda chuo kikuu cha Umul-Qura kufundisha. Chuo hicho ni maarufu kiko katika mji mtakatifu wa Makah na aliungana na wanazuoni wengi waliotokea au kusoma katika chuo cha Azhar. Sheikh alifundisha huko Makkah hadi mwaka 1998 Kutokana na juhudi zake za kufanya daawa,Sheikh Sayyid Sabiq alipata tuzo ya Malik Faisal katika uwanja wa Fiqh Al-Islamiya. Sheikh ameondoka duniani akiwa ametuachia elimu yenye manufaa na wanafunzi wema wanaomwombea maghfira na rehma. Mwenyezi Mungu amrehemu Sheikh wetu, Sayyid Sabiq na amkubali pamoja na swalihiin katika waja wake wema. INNA LILLAH WA INA ILAHYIRAAJIUN.
|
YALIYOMO
Tahariri
Mbukuzi
anguruma Chuo Kikuu:
Kuelekea
uchaguzi mkuu 2000:
Maalim Seif afunguliwa mashitaka ‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
Lishe
Madadi azionya timu za Ligi Kuu |
|
|
|
|