|
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000 |
|
|
|
|
|
WE THIO LAFKI YANGU TEENA! Na Abu Halima Sa Changwa NILIRUDI nyumbani jioni baada ya mizunguuko yangu ya kimaisha. Kwa kawaida mwanangu mdogo, Halima, (jina la kitoto tunapenda kumwita Mima), hunikimbilia kwa shangwe kuja kunipokea, lakini siku ile nilishangaa alikuwa "kauchuna". Nikamuuliza: "Mima, vipi mwanangu?" Kimya! "Hujambo?" Kimya! Baada ya kumhojihoji ili kumdadisi nifahamu tatizo lilikuwa nini, alitoa maneno ya ukali akisema: "We thio lafki yangu teena!" Waliokuwepo waliangua kicheko na kusema tu, "Mima bwana!" Nilimuuliza kwa nini mimi sio rafiki yake, nikagundua sababu. Kumbe nilikuwa nimemfinya asubuhi kabla sijaenda kazini, kwa sababu alikuwa hataki kwenda shuleni (chekechea) eti kwa sababu alikuwa amechoka sana ile asubuhi. Nilichokifanya ni kutoa kafuko ambako ndani kalikuwa na vituvitu vya kutafuna, kama ilivyo kawaida nikirudi nyumbani. Nikasema: "Sawa kama mimi thio lafki yako". Mima alipoona kale kafuko akajua mna vitu. Akawa anatafuta suluhu. Akaja mbio huku akisema: "Thalamaleku, baba!" Waliokuwepo wakaangua kicheko tena. Bila ya kuwajali waliokuwa wakicheka, alisema: "Nilikuwa nadanganya tu baba, wewe ni lafki yangu". Kwa nini alifanya hivyo? Alijua kwamba uadui wake kwangu ungemkosesha maslahi, walau kwa kipindi kile kifupi cha neema. Wengi waliokuwepo waliangua kicheko tu, wakiishia kusema: "Mima bwana!...Watoto bwana!... blah...blah...blah! Lakini kwa watu wa fasihi kila tukio lina maanisho (implication) katika maisha, na vile vile kwa watu wa fasihi maisha yote ni tamthilia (drama), unaweza kuyafanyia uchambuzi. Nilikuwa nafikiria niandike nini kwenye Mpasho Nasaha wiki hii, lakini tukio lile dogo kwangu likawa na maanisho kubwa zaidi katika maisha yetu leo kuliko wale waliokuwa wakicheka tu walivyolichukulia. Mwezi uliopita kuna kigogo mmoja wa chama fulani alirudisha kadi ya chama chake na kurejea chama tawala. Nilipomuona kwenye luninga akirudisha kadi ya chama cha upinzani na kujiunga na chama tawala nikajiuliza, zile hasira zake kwa chama tawala wakati ule zilikuwa za kweli au ilikuwa ni ile ile "we thio lafki yangu teena!" Juzi tu kuna kigogo mwingine kaomba radhi kwa Rais, na ameacha upinzani. Huyu naye kanishangaza, maana alikuwa mkali huyo kama nini! Lakini kaomba radhi, na upinzani kwake basi. Sijui kuomba radhi imekuwa ni fasheni baada ya Papa Yohane Paulo kuanza. Nilijiuliza, huyu naye kaweka manyanga chini, tena bado kidogo tu siasa zianze, maana siasa za nchi hii ni karibu na uchaguzi. Sasa ule ukali ulikuwa ni ukali kweli au ni ile ile "we thio lafki yangu teena!". Sasa hivi kila kona unayokwenda watu wanalalamika hali ngumu, na jina wameipa, inaitwa "Ukapa". (Sijui neno hili linatokana na nini). Utamkuta mtu mimacho imemtoka: "Hatukubali. Ngoja elfu mbili inakuja. Huyu sasa basi. Mimi kura yangu kwa Chupaki tu safari hii. Eeh, ndio! Mffvyyyy! Kshxnz$!!! kabisa! Blah...blah...blah...!" Ukimkuta mtu utadhani mkali kweli, lakini ngoja vifuko vitolewe. Na safari hii nasikia hakuna ruzuku, kila chama na ujanja wake. Ona watu watakavyobadilika rangi. Angalia watu watakavyorudisha kadi na kuomba radhi. Cha kuchekesha, wengine ni mashehe na maaskofu. Wakati wa kaneema ka muda mfupi ndio waja huo. Ukiwa nje ya mchezo ndio unaufaidi. Miye sina chama lakini ninapo pa kupiga kura. Usiniulize wapi, kwa sababu wenye busara zao wameshatupa uhuru wa kuchagua tunapopapenda. Nauliza tu wale wanaojidai wana hasira, hasira hizo ni za kweli au ni zile zile za "We thio lafki yangu teeeeeena!" Vifuko vikitolewa tu, "Thalamaleku baba!" Haya, tutaona!
|
YALIYOMO
Tahariri
Mbukuzi
anguruma Chuo Kikuu:
Kuelekea
uchaguzi mkuu 2000:
Maalim Seif afunguliwa mashitaka ‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi MPASHO NASAHA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
Makala
MAKALA
Riwaya
Lishe
Madadi azionya timu za Ligi Kuu |
|
|
|
|