NASAHA
Na. 042 Jumatano Aprili 5 - 11, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Tahariri
S.L.P. 72045, Simu: 0811 - 600145, Dar es Salaam

Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu 

Miongoni mwa vitu vibaya kabisa katika jamii ni dhuluma. Dhuluma ikiachwa iendelee kutendeka, jamii huangamia mara moja!

Wajibu wa kukomesha dhuluma katika jamii ni wa kila mmoja: anayedhulumu anatakiwa kuacha kudhulumu mara moja; anayedhulumiwa anatakiwa kumkabili anayemdhulumu akamuondolea uwezo au nafasi ya kuendelea kumdhulumu; na yule asiyedhulumu au kudhulumiwa huyo anatakiwa kuwasaidia wote wawili kukomesha dhuluma hiyo.

Hapa Tanzania imethibiti kwamba Waislamu wana tatizo, nalo ni dhuluma. Waislamu wanatendewa isivyo haki na inavyostahiki kwa raia wa nchi hii.

Katiba yetu haisemi wazi kuwadhulumu raia fulani kwa sababu ya dini yao lakini, inapotokea serikali, kwa kuzienzi sera za chama chake inaona ni halali kuwadhulumu raia wake; au inapotokea serikali kuwaachia watendaji wake kutenda kwa matashi ya imani zao za kidini na hivyo kuwadhulumu raia wengine, basi hapo anayewajibika ni serikali.

Mtu ukileta udini au ukabila au u-chama katika kutekeleza shughuli za serikali, basi ni sharti kwa serikali kuchukua hatua dhidi yake kwa kutokuwa mwadilifu. Jambo hilo ni muhimu kwa sababu hao wanaodhulumiwa siku zote wanatozwa kodi kwa ajili ya kuendeshea shughuli za serikali ili kuleta ustawi wa jamii. Ni kwa hoja hii ndio maana Waislamu wanaidai serikali ikomeshe dhuluma dhidi yao.

Mahali tulipofikia ni kuwa serikali haithubutu kuwaadabisha hao wasiowatendea haki Waislamu. Madhali serikali haiwaadabishi watendaji wake hao, dawa waliyoigundua Waislmu ni kuwachagua viongozi ambao Waislamu wenyewe wamethibitisha kuwa ni waadilifu bila kujali dini zao, kabila zao, rangi zao wala itikadi zao za kisiasa.

Hali ya kuwa kuna watendaji wa serikali hawataki kuwa waadilifu kwa sababu tu ya mapenzi kwa dini yao na pia chuki dhidi ya Uislamu, basi katika hali hiyo Waislamu watakuwa na haki ya kuwachagua viongozi waadilifu kutoka miongoni mwao. Lakini ni vema watendaji hao wa serikali wasiifikishe nchi yetu huko.

Tunapenda kutoa wito kwa Watanzania wote kwamba madhali kuna chama kinachoendelea kutekeleza mambo kwa siri dhidi ya Waislamu, basi chama hicho ama kidhibitiwe kwa kuwekwa katika mikono ya watu waadilifu au kitengwe kwa kunyimwa kura za kuiongoza nchi.

Kadhalika, madhali kuna watu ambao wameonekana kushindwa kuziweka nyuma imani zao kwa maslahi ya kitaifa basi Waislamu watalazimika kuangaliana wao kwa wao,au la, vinginevyo ikibidi wamwangalie asiye mwenzao basi uadilifu wake sharti ujulikane.

Pili tunatoa wito kwa Waislamu kwamba wakati vuguvugu la uchaguzi linapamba moto, tayari kuna minong'ono kuwa baadhi ya watu wameanza kuwafuata masheikh na viongozi wa taasisi za Kiislamu kutaka kuwarubuni kwa ahadi zisizoingia akilini.

Wapo wanaojitapa kwa kuahidi "tukiingia madarakani Waislamu mtajengewa Chuo Kikuu", "tukiingia madarakani Waislamu mtapata nafasi hizi...." Tunawatanabaisha Waislamu kwamba huu ni unafiki. Je ahadi za namna hiyo zisipotekelezwa, Waislamu mna nguvu gani ya kumlazimisha? Tunasema hivi kwa sababu hakuna mahakama wala kikao chochote kinachoweza kulazimisha utekelezaji wa ahadi za uchaguzi!

Isitoshe unafiki huu wa ahadi ni maarufu katika uchaguzi uliopita wa mwaka 1995. Tunawauliza Waislam: "Leo kiko wapi?!"

Kadhalika yapo makundi ambayo yameandaliwa kwa makusudi kuwayumbisha Waislamu. Makundi haya yanawaelekeza Waislamu katika vyama kwa lengo la kuzigawa kura zao na kuwayumbisha wasijue la kufanya. Hawa hawapo mbali na wale walioanzisha program kudai wananchi hawana elimu ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowafaa.

Watu hawa, ingawa ni Waislamu tena masheikh na ma-ustadh, lengo lao ni kuwayumbisha Waislamu wabaki wakitangatanga wasijue wa kumpigia kura. Hali hiyo inaweza kuwafanya Waislamu ama wazigawe au waziharibu kura zao na hivyo wakose kiongozi waliyemtaka.

Tunapenda kuwafahamisha Waislamu kwamba wajihadhari na mambo haya. Hao wanaotaka kuzigawa kura zenu na hivyo kuwakosesha kiongozi mnayeona anawafaa, ni vibaraka wanaolipwa au wanaowatumikia maadui zenu pasipo wao kujua.

Waislamu ni sawa na wananchi wengine,na wana elimu ya kutosha ya kumtambua mwadilifu na asiye mwadilifu,na nani wamchague, na hivyo hawahitaji maelekezo ya 'hamasa za papo kwa papo'.

Mwaka 1995 walikuja ma-ustadhi wa 'hamasa za papo kwa papo'. Siku ya Ijumaa walitamba katika mimbari huku wakipigiwa takbira kuwa ni watetezi wa Waislamu, lakini ma-ustadh hao hao Jumamosi walionekana wakimeremeta katika majukwaa ya vyama ambavyo vimekuwa vikiendesha uadui dhidi ya Waislamu!

Hivyo, chonde chonde Waislam, tayari watu wamechukua tenda za kuwayumbisha na kucheza na kura zenu.

Hata hivyo 'chombo hakijaenda mrama'. Madhali mmekwisha mtambua adui yenu, na silaha(kura) mnayo mkononi na siku ya kumshambulia adui imekwishatajwa (Oktoba), kilichobaki ni kudumu mkikumbushana kwamba mwaka huu dhuluma mwisho.

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Mnaodhulumiwa lindeni kura zenu

Mbukuzi anguruma Chuo Kikuu:
Wasomi mnatakiwa kukomesha dhuluma

Kuelekea uchaguzi mkuu 2000:
CUF yaiteka Dar

Maalim Seif afunguliwa mashitaka

‘Tume ya Keenja’ haikufanya ilichoagizwa - Wananchi

MPASHO NASAHA
WE THIO LAFKIYANGU TEENA!

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani

WAZO  LA  WIKI
Ajenda mpachiko

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake

Kalamu ya Mwandishi
Ulaya yaiambia Afrika iboreshe demokrasia kabla ya kufutiwa madeni yake

Makala
Wasifu wa marehemu Sheikh Said Sabiq

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (5):
Wananchi mjiandae kulinda kura

HABARI ZA KIMATAIFA

Riwaya
Kisasi cha mauti -2

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Kajumulo atishia kuwanyang’anya Kibadeni Simba
  • Kipukuswa kufuata nyayo za ‘Mgosi’ Hazali
  • Hazali sio Yanga ni Simba ‘kindakindaki’

  • Madadi azionya timu za Ligi Kuu
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita