|
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Tangu lini BAKWATA ikaikataa CCM? Ndugu Mhariri NAOMBA nafasi japo kidogo nitoe maoni yangu ili yawasaidie wapenda amani wenzangu. Katika gazeti moja litokalo mchana kila siku kwa lugha ya Kiswahili la Februari 22, 2000 kulikuwa na habari iliyosomeka "BAKWATA hamkana Sheikh Ponda". Katika habari hizo imeandikwa kuwa "Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limesema kwamba kauli ya kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao unamhusu Sheikh Ponda Issa Ponda na kundi lake". Gazeti hilo linaendelea kuripoti: Afisa Habari wa BAKWATA, Abbas Kihemba amesema tangu mwanzo Baraza hilo limekuwa na msimamo tofauti na kikundi cha Sheikh Ponda na kusisitiza kuwa mpango wa kuinyima kura CCM hauwahusu wanaoikubali BAKWATA aliodai ni wengi", lilimaliza. Gazeti hilo linasema kuwa: "Wakati BAKWATA inapinga msimamo huo, kiongzi wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi ameunga mkono na kuwaambia Waislamu hawapendwi na watawala". Ukizingatia hoja alizozitoa Sheikh Ponda na majibu ya BAKWATA, hupati tabu kuelewa BAKWATA. Na itakuwa ajabu BAKWATA kuikataa CCM. Zaidi ya hayo, BAKWATA iliundwa na serikali ya TANU (CCM mzazi wake) mwaka 1968 baada ya kuvunjwa kwa jumuiya zilizoundwa na Waislamu wenyewe (EAMWS, Maulid Committee na BAKWATA ikarithishwa mali nyingi za Waislamu. Hata hivyo, tangu wakati huo, mchango wa BAKWATA kwa Waislamu ni msiba mtupu. Kwa mfano kila mwaka shule zake za sekondari zinazongoza kwa kufelisha. Haya ndiyo yaliyotarajiwa na serikali ya CCM. Kwa hiyo katu BAKWATA haitamkataa mwasisi wake (CCM) badala yake itawakana Waislamu mfano wa Sheikh Ponda. Juma Digelo,
TAMWA wanatetea haki na kusahau maadili Ndugu Mhariri NIKIWA msomaji mzuri wa gazeti lako naomba unipe nafasi ili nizungumze na dada zetu wa TAMWA, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake lakini wamesahau kulinda maadili yetu kama binadamu tena Waafrika. Lazima TAMWA wafahamu kuwa kuna tofauti kubwa kati ya mila za kizungu na za Kiafrika. Kwa Wazungu kutembea na kimini au kichupi ni jambo la kawaida, tena nyuma nzima yaani baba, mama na watoto wanaweza kuvaa vichupi tu wakaenda pwani kuogelea au kupunga upepo, lakini sio kwa Waafrika huo utakuwa ni ushenzi. Kwa kifupi ni kuwa Wazungu ni wafu katika upande wa maadili. Sasa siku hizi mfumuko wa viguo vya kishenzi vyenye kubana mpaka vikaonesha ramani ya kila sehemu ya mwili wa mwanamke achilia mbali vimini vyenye kuishia juu ya mapaja na nyepesi na angavu (strasparent) zenye kuonesha rangi za nguo za ndani, imekuwa ndio fasheni. Hali inatisha pale unapomuona mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari anakwenda 'tuition' kavaa viguo vya aina hii, na hawa wanatoka ama kwa wazazi au kwa walezi wao. Je, wazazi wanawafundisha nini watoto hawa? Au kutembea uchi ndio maendeleo kw akuwa Wazungu wanafanya hivyo? Fika kwenye vyuo vya elimu ya juu, kama Chuo Kikuu au IFM ukaone mabinti wanavyotembea uchi wakiwa katika shughuli zao za kila siku. Hawa ndio wasomi tunaowategemea watajiunga na TAMWA ili kumtetea mwanamke. Atatetea nini kama si haki ya mwanamke kuvaa suruali kama mwanaume. Pengine kama wangeweza wangelalama kuwa Mungu kawanyima haki kwa kutowafanya waume nao wabebe mimba. Ili muradi tu hawawezi kudai kitu cha maana kama hivyo ndivyo walivyo. Maofisini nako kunatisha, wafanyakazi wa kike wanavaa nguo za usiku wanazoziona kwenye michezo ya kuigiza ya Kizungu kupitia televisheni. Utamkuta sekretari wa bosi yupo nusu uchi, halafu analaumiwa bosi akimtaka amkidhie haja yake ya kimwili au akimbaka wakati yeye ndiye aliyeamshwa hisia zake. Nawakumbusheni TAMWA kuwa ninyi muwe mstari wa mbele na msijisahau. Kwani wakati serikali imekwishashindwa kutimiza majukumu yake ninyi ndio wakombozi oekee mliobaki lakini lazima muwe na mtizamo sahihi. Msicheze ngoma msiyoijua ya kudai haki za kipuuzi mkasahau mambo ya msingi. Seleman Kindamba,
Kesi zasimama kwa ukosefu wa karatasi Ndugu Mhariri KATIKA serikali awamu ya tatu tumeshuhudia mengi yanayogonga kichwa. Moja ya hayo ni serikali kujigamba kuwa inakusanya mabilioni ya shilingi kila mwezi. Lakini huduma za jamii zinaendelea kudidimia kadiri serikali inavyozidi kupata mapato zaidi. Kwa mfano, hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imesimamisha kusikiliza kesi kwa muda wa miezi mitatu sasa kutokana na ukosefu wa karatasi za kuandikia mwenendo wa uendeshaji wa kesi. Vyombo hivyo pia vilimnukuu Hakimu wa mahakama hiyo aliyesema: "Kwa sasa hali ni mbaya, serikali haina pesa. Tulishaeleza tatizo hili lakini hatujapatiwa". Nchi yetu ni moja kati ya nchi zinazotoza kodi kubwa duniani. Sasa hayo mabilioni ya shilingi mbona hayatumiki kuondoa kero za wananchi? Kwa vile wakubwa wanabadili magari mara kwa mara, sisi raia tunahisi kuwa pesa za kodi zinawanufaisha viongozi tu. Tafadhali rekebisheni hali hii. Malema Magesa,
TLP vipi, kulikoni? Ndugu Mhariri NIKIWA miongoni mwa wasomaji wako nipe nafasi niweze kuwauliza ndugu zangu wa chama cha upinzani cha TLP kwa vipi wanafanyakazi ya CCM. Yaliyopita huko nyuma kwenye chaguzi zote zilizopita tunayaelewa fika, tulikosa umoja wa kuiondoa CCM. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa tathmini ya chaguzi ndogo za ubunge za Ubungo na Temeke CCM walipata si zaidi ya asilimia thelathini na tano. Ina maana kuwa wapinzani walishinda kwa kupata asilimia zaidi ya sitini. Lakini kura zao zilitawanyika na hatimaye CCM kushinda. Hivyo basi wananchi tunataka kuwepo kwa muungano wa vyama hivi kwenye uchaguzi mkuu ujao. Hao waliokwisha anza kuonesha njia tusiwabeze bali tuwasaidie na tuungane nao. Lengo la kwanz aliwe ni kuing'oa CCM madarakani. Sasa ninaposikia kauli za kutatanisha toka kwa viongozi wa TLP nazidi kuchanganyikiwa na kuzidi kuamini kuwa kwli wapo kwa ajili ya upinzani au kusindikiza CCM kuingia Ikulu. Kauli ya Mheshimiwa Mrema kuwa yeye anamtaji wa kura milioni moja na laki nane na kwamba hao wanaotaka kuungana wamuunge mkono yeye hayaeleweki. Kwanini aongelee jukwaani na asiwafuate kuwaambia hiyo nia yake. Kama anachotaka yeye ni kuwa Rais tu basi hamna lingine basi hapa kuna ubinafsi. Mwenyekiti wa TLP Tanga naye anasema muungano uliotangazwa na UDP, CHADEMA na CUF una misingi ya ukabila. Huyu naye ndiyo kabisa sijui katumwa au si mpinzani? Kama imetokea kuwa viongozi wa juu wa vyama hivyo vyote wanatoka mikoa ya kati hiyo ni bahati tu mbona Bwana Kimaro hatuhoji kwanini wafadhili wengi na karibu wote wa NCCR enzi za Mrema na kwa sasa TLP ni Wachagga hivyo chama hicho ni cha ukabila. Dalili ya mvua ni mawingu, nakuhadharisheni wananchi, kwani mti bora huzaa matunda na mti mbaya huza miiba. Sisi sote tuwe wenye kusubiri. Zabron Chacha,
Mikoa ya Pwani amkeni, CCM ndio mchawi wetu Ndugu Mhariri NAOMBA unipe nafasi kwenye gazeti lako kuwakumbusha wakazi wenzangu wa mikoa ya Pwani kwamba pamoja na kujipendekeza kwa kukipa ushindi ktokana na kura zetu Chama Cha Mapinduzi bado kimeshindwa kutuletea maendeleo. Profesa Lipumba alishangaa iweje maembe yaoze Kisarawe halafu jinsi ya embe iagizwe toka Arabuni. Au iweje pamoja na ukweli kuwa watu wa pwani ni wavuvi wazuri kutokana na sababu za kijiografia, lakini serikali ishindwe hata kujenga kiwanda cha kusindika minofu ya samaki. Au pale alipotueleza kuwa serikali kama ingeamua kujenga barabara ya Kibiti-Lindi ingeweza isipokuwa haitaki tu, na akatoa data kuwa wakati gharama za ujenzi ni dola milioni mia moja, misaada inayopata serikali toka kwa wafadhili ni dola milioni mia nane kwa mwaka. Wananchi wa mikoa ya pwani hasa Lindi na Mtwara mnasubiri nini tena, au mnafikiri kuna Mtume ataletwa labda huyo mtamuamini, hapana, haya tunayoelezwa na mtaalamu huyu lazima tuyafanyie kazi. Lazima tushirikiane naye kuindoa serikali ya CCM madarakani, halafu tuangalie maendeleo. Zubeda Ismail,
|
YALIYOMO
Tahariri:
‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali' Suala la Mwembechai lazua mtafaruku Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi MPASHO
NASAHA
Habari
za ndani
Ushauri
Nasaha
MAKALA
WAZO
LA WIKI
Makala
ya Kimataifa
Kalamu
ya Mwandishi
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|