NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar
CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

Na Mwandishi Wetu 

IMEELEZWA kwamba matokeo ya kikao cha kamati maalumu ya CCM Zanzibar kilichoitishwa kufuatilia kuzuka kwa mvutano kati ya CCM Bara na Wazanzibar juu ya azma ya Wazanzibar kuifanyia marekebisho katiba ya nchi yao ili kuondoa ukomo wa vipindi vya mtu kushika wadhifa wa Urais wa Zanzibar yametoa dalili za ushindi kwa wananchi wa Zanzibar.

Aidha imeendelea kuelezwa kuwa mazingira ya kisiasa na kijamii yaliyotanda Tanzania kwa ujumla yanaweka Wazanzibar katika nafasi nzuri kuweza kufanya kile walichokusudia ingawa wanaweza kucheleweshwa. 

Hayo yameelezwa na wachunguzi wa masuala ya kisiasa na kijamii kufuatia kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo maalumu ya CCM kilichochukua jumla ya siku nne ambapo kwa mujibu wa kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Bw. Musa 

Hassan Takrima, CCM-Zanzibar imeunga mkono kwa kauli moja mapendekezo hayo ya marekebisho ya katiba. 

Taarifa zilizopatikana toka Zanzibar zimeeleza kuwa wana-CCM-Zanzibar kabla ya kikao hicho "walielimishana sawasawa" kiasi cha kuweza kuingia katika kikao hicho wakiwa na msimamo wa pamoja. 

"Kauli yetu ni moja, alhamdulillah, masuala ya Zanzibar ni ya Wanzibar tu na hili (marekebisho ya katiba) ni letu (Wazanzibar) peke yetu...suala hili si la Muungano, na wasioelewa warudi kwenye makubaliano ya Muungano", alisema Mwana-CCM-Zanzibar aliyekuwa mjumbe wa kikao hicho mara baada ya kikao kumalizika. 

Kikao hicho cha Zanzibar ambacho pia kilihudhuriwa na wajumbe toka CCM-Bara kwa mujibu wa nafasi zao katika CCM na serikali ya Muungano, kilimalizika Alhamisi iliyopita ambapo ilitolewa taarifa kuwa suala hilo litapelekwa katika kamati kuu ya CCM (CC) Februari 24 kabla ya kufikishwa Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala inayotarajiwa kukutana kwa siku mbili, kuanzia Jumamosi Febrauri 26 mjini Dodoma. 

Hata hivyo vikao hivyo viwili havitarajiwi kuweza kuwapokonya Wazanzibar kile walichokiazimia. Wana-CCM Zanzibar wametamka kuwa wanachofuata Dodoma ni maoni tu ya Chama Cha Mapinduzi na wala sio ruhusa ya kuubadili katiba ya nchi yao. 

"Tumekubaliana kimsingi kwamba tutakwenda Dodoma kupata maoni ya chama chetu (CCM) juu ya namna ya kuufanyia marekebisho, lakini siyo kwamba tunaenda kutafuta idhini ya kurekebisha katiba", alisema Bw. Takrima. 

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wameendelea kueleza kuwa mbali na msimamo uliooneshwa na wajumbe wa CCM-Zanzibar jambo lingine linaloweza kuwapa ushundi Wazanzibar ni kuwepo kwa kamati la wana-CCM-Bara ambao wangependelea Zanzibar inakuwa na sauti juu ya mambo yake ili nao baadaye wawe na sababu ya kudai serikali ya Tanganyika. 

"Suala la Tanganyika halikufa kama alivyotaka Hayati Mwalimu Nyerere, na katika suala hili la Zanzibar, lazima wapo wana-CCM Bara watetezi wa Tanganyika ambao wataitumia opportunity (fursa)hii", amesema mwanadiplomasia mmoja mstaafu ambaye hakutaka jina lake litajwe. 

Wachunguzi hao wa masuala ya kisiasa na kijamii wameendelea kuchambua kuwa vikao vya CC na NEC vitakuwa na wakati mgumu kuleta 'suluhu' kati yakuzuia marekebisho hayo ya katiba na hatari ya Wana-CCM, Zanzibar kujitenga na CCM Taifa na hiyo kuhatarisha matarajio ya chama hicho kurejea madarakani baada ya uchaguzi mkuu ujao, baadaye Oktoba mwaka huu. 

"Nchi hii ni ya kidemokrasia, na mtu anayo haki ya kujiunga na chama chochote, na juu ya hilo kura ya mtu ni siri na mwanachama wa CCM halazimiki kumpigia kura mgombea wa CCM. Hivyo wana-CCM 

Zanzibar wakibanwa katika suala hili la katiba wanaweza kuamua kuikomoa CCM, alisema mwananchi mmoja ambaye ni mwalimu wa sayansi ya siasa. 

Uchunguzi wa gazeti hili haujaweza kufahamu ni mikakati gani waliyonayo Wana-CCM Zanzibar kuizuia CCM Taifa isiwazidi nguvu lakini taarifa zilizopatikana toka Zanzibar ni kwamba Wazanzibar wameahidi kwamba yaliyomtokea Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Alhaj Aboud Jumbe na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa wakati huo Bw. Ramadhani Haji Faki hayatokei tena. 

"Safari hii tumejizatiti, tumeyagundua makosa yetu na tayari tumejirekebisha, wakati wa Mzee Jumbe tulichelewa kidogo lakini mwaka huu tumewatangulia mbali...." Alisema kiongozi mmoja wa CCM Zanzibar alipoongea kwa njia ya simu na gazeti hili. 

Alhaji Aboud Jumbe alilazimishwa kujiuzulu na kikao cha NEC chini ya uwenyekiti wa Mwalimu Nyerere wadhifa zote alizokuwa nazo katika serikali ya Muungano, serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Chama Cha Mapinduzi baadaye kutoka makubaliano ya muungano yatazamwe ili kuona kuwa mambo si tofauti na ilivyokuwa imekubaliwa. 

Aidha wananchi wengine wa Zanzibar wamedai kuwa wanashangazwa na jinsi suala hili la katiba ya Zanzibar linavyogeuzwa kuwa ni suala la CCM badala ya wazanzibar.Wamesema kama suala ni Dk. Salmin, CCM ingeweza kumzuia Dk. Salmin asigombea tena kwa kutompitisha katika vikao vyake. 

Kama ni hoja ya kubadili katiba, CCM watuachie Wazanzibar, walileta kwetu tupige kura ya maoni, na kama ni kutaka Salmin asigombea tena, basi wasimpitishe kwenye hiyo NEC yao", alisema Bwana Khamis wa Unguja aliyedai kuwa ni mwanachama wa CUF. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k

  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita