|
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni NA Y. KIJUKUU HATUNA budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana tena Jumatano nyingine tukiyajadili yale yale yanayotuhusu yenye kulenga kuiokoa jamii yetu isije angamia wakati tupo wenye uwezo wa kukemea hata kama hawayatilii maanani. Katika siku chache za hivi karibuni, tumejionea kwa macho yetu kupitia vyombo vya habari kuwa wanafunzi wa Kiislamu katika Shule za Sekondari nchini wananyanyashwa. Pamoja na manyanyaso yote hayo, baya zaidi lililozuka sasa ni walimu kuwatolea vitisho wanafunzi tena si vitisho vya kawaida bali ni vitisho vya kikachero, vitisho ambavyo historia ndiyo inayohukumu kuwa viliwamaliza wanasiasa wengi waliopita kabla yetu. Vitisho vilivyotolewa na waalimu wa Kisutu Sekondari dhidi ya wanafunzi wa Kiislamu ni dhahiri kuwa vilikuwa na mlengo wa kikachero na sio kitaaluma, kitendo ambacho ni kinyume kabisa na taaluma yao. Nijuavyo mimi, taaluma ya Ualimu inamruhusu Mwalimu kutoa motisha kwa mwanafunzi. Motisha huo huweza kuwa chanya au hasi. Motisha chanya ambao mwalimu anatakiwa ampe mwanafunzi ni kama vile zawadi. Hii hutolewa mwanafunzi muhusika anapofanya vizuri, kwa mfano kufaulu mtihani. Motisha hasi ni kama vile kumchapa mwanafunzi viboko au adhabu nyingine yoyote ile iwe ya kimwili au ya kisaikolojia. Hii ndiyo miongoni mwa taaluma ya mwalimu yeyote yule aliyeiva mafunzoni. Kinyume na hapo uwalimu wa mwalimu muhusika utakuwa na kasoro ambazo wizara husika itashindwa kumvumilia. Ni jambo la kushangaza kusikia mwalimu au waalimu wakitoa adhabu ya kuwahoji mwanafunzi kwa kosa lisilo wazi, tena ni kinyume na taaluma yao hasa pale wanapoingilia kazi ya jeshi la polisi kwa kuhoji kwa vitisho. Nanukuu baadhi ya maswali na hoja za waalimu hao wa Kisutu kwa wanafunzi wa Kiislamu "Hebu semeni, Chuki anakaa wapi? Baba yake alikufa vipi, anakaa mtaa gani. Maadhimisho ya waliokufa Mwembechai yatahutubiwa na nani? Mbukuzi au Ponda? DAMUSSA inajulikana wizarani? Tunawaambia DAMUSSA si nzuri kwenu, kila mmoja aeleze mtaa na nambari ya nyumba anayoishi pamoja na mzazi au mlezi wake anayeishi nae. Semeni ukweli kwani msije kutulaumu huko tutakako wapeleka".Mwisho wa kunukuu. Kutokana na maswali na maelezo hayo ya walimu haihitaji kwenda shule au kupekuwa vitabu na kamusi mbalimbali ili kutambua maswali hayo kama siyo ya polisi basi yalikuwa ni ya kikachero na yana mlengo wa kisiasa ambayo muhusika asipokuwa makini katika kuyajibu huenda yakamuathiri kwa kiasi kikubwa. Inafikia mahali, mtu mwenye akili timamu ni lazima ajiulize maswali mengi kama vile, "hivi lengo hasa la waalimu hawa ni lipi? Kwa nini wafanye hivi? Kama suala ni DAMUSSA, hivi Y.C.S.ambayo ni jumuiya maarufu ya Kikristo mashuleni hawaitambui pia? Na kama suala ni maadhimisho ya waliouawa Mwembechai, je wanafunzi hawa yanawahusu nini wakati kamati ya maandilizi ipo? Haiyumkiniki kuwa huenda walimu wahusika wakawa sasa wameamua kuicha taaluma waliyoisomea na kwa makusudi wameamua kuwa vibaraka wa dola ili kufanya ukachero ambao dola inaona kwa kuwatumia wataalam hao waliopewa jukumu la kuilea jamii ya wanafunzi, itafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ewe mwalimu, chonde ndugu yangu wewe tayari ni mpishi wa tabia na mwenendo wa vijana ili jamii inufaike. Kazi hiyo umeipenda na umeichagua mwenyewe. Hivyo kama unaona upolisi unakufaa kuliko ualimu basi acha chaki uende C.C.P. ili urudi ukiwa na gwanda la polisi ufanye shughuli ya ushushushu ambayo sasa unaipenda. Wakuu wa shule, ninyi ndiyo mliopewa jukumu la kuangalia mwendo mzima wa shule zenu. Hivyo tambueni kuwa ninyi ni wachunga na mtaulizwa juu ya mlichokichunga. Kufumbia macho walimu wanaopenda ukachero hata kama ninyi hamuhusiki, jamii itawahusisha kwani ninyi ndiyo vinara wa mashule hayo. Hebu mkuu wa shule ya Kisutu angalia, tangu habari hizo ziandikwe gazetini wanafunzi wako wahusika wanakosa sala ndani ya shule yao, wanashutumiwa vikali eti kwa nini wamepeleka mambo hayo gazetini wakati walimu hawana uhakika kuwa wao ndiyo waliopeleka habari hizo gazetini. Huenda sasa wanafunzi wahusika na wazazi wao hawalali kwa kufikiria hatma yao kwani wao ni wakubwa na wanatambua kuwa akumulikae mchana usiku atakuchoma. Si jambo la busara kwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ambayo ndiyo mhimili wa waalimu hao hukaa kimya hali ikijua jinsi ukachero dhidi ya wananfunzi wa Kiislamu ambao kwa kweli hawana kosa kusoma katika shule za serikali kwani wao ni sehemu ya jamii ya Watanzania. Kuvaa hijabu kwao kusiwe kigezo cha wao kuonekana kuwa ni watu hatari, siyo tu ndani bali hata nje ya shule zao. Ileweke na jamii kuwa mgawanyo wa kazi ni muhimu katika jamii yoyote ile. Tabibu awe tabibu tu na asiende kuwa mhasibu, rubani awe rubani tu na asiende kutibu, hivyo hata mwalimu ni bora akawa mwalimu tu na aepuke upolisi. Mwanasiasa asipeleke siasa mashuleni bali awangoje wanafunzi majukwaani, kamwe pasitokee mtu kupeleka ukachero katika mashule kwani kufanya hivyo ni kuharibu jamii kisaikolojia. |
YALIYOMO
Tahariri:
‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali' Suala la Mwembechai lazua mtafaruku Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi MPASHO
NASAHA
Habari
za ndani
Ushauri
Nasaha
MAKALA
WAZO
LA WIKI
Makala
ya Kimataifa
Kalamu
ya Mwandishi
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|