NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Tahariri 
 
 

Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari 

KATIBA ya nchi katika nchi yoyote ya kidemokrasia, ni mali ya wananchi na hivyo ni wananchi pekee ndiyo wenye haki ya kubadili katiba ya nchi yao.

Ni hivyo basi, katiba ya Zanzibar ni mali ya Wazanzibari na si vinginevyo, ni Wazanzibari pekee wenye haki ya kuibadili katiba ya nchi yao, na yeyote asiye Mzanzibari bila kujali yeye ni Mheshimiwa au la, yeye ni Profesa au mwanasiasa, yeye ni Kadinali, Askofu au Sheikh, hana haki hiyo.

Aidha, katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari wote na kamwe si ya chama tawala cha CCM, hivyo si sahihi suala la mabadiliko ya kabla ya nchi hiyo yakafanywa ni agenda ya kujadiliwa na kuamuliwa na wana-CCM tu.

Azma ya Wazanzibari kuifanyia marekebisho katiba ya nchi yao tayari imeleta sakata la aina yake ambapo mambo matatu yamejitokeza.

Jambo la kwanza, ni kuwepo kwa kundi ambalo limeonesha kuwa na donge dhidi ya Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour.

Jambo la pili, ni kuwepo kwa kundi la watu wasiopenda kuona Zanzibar kuwa ni nchi, hawataki kuitambua kuwa Zanzibar iliingia katika muungano mwaka 1964 ikiwa ni nchi kamili, na kwamba iliingia kwa makubaliano na siyo kutekwa na kubaki na mamlaka ya mwisho juu ya masuala fulani chini ya serikali yake.

Jambo la tatu, wapo watu ambao wameonesha chuki za kidini dhidi ya Zanzibar nchi yenye Waislamu wengi na ambayo kwa muda mrefu imekuwa ni kitovu cha elimu ya dini ya Kiislamu kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na nje ya hapo. Wamejitokeza Maaskofu kuwashutumu Wazanzibari kutaka kuifanyia marekebisho katiba yao. Aidha zipo habari kuwa baadhi ya Masheikh walifuatwa na viongozi waliomo katika serikali ya Muungano (ambao wao wanatoka Zanzibar) ili walizungumzie suala hilo lakini Masheikh hao walikataa kwa vile shutuma dhidi ya suala hilo tayari kwa wananchi wengi limeonekana lina sura ya udini dhidi ya Uislamu.

Lakini baya zaidi katika kadhia hii ya mapendekezo ya kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar ili kuondoa kifungu kinachoweka ukomo kwa mtu kuongoza katika nafasi ya Urais ni propaganda na uzushi mwingi uliojitokeza.

Uzushi huu umekuwa ukitolewa na baadhi ya watu waliochangia dhidi ya haja ya marekebisho hayo, na kisha uzushi huo 'ukapokewa' na baadhi ya vyombo vya habari.

Wapo waliokuwa wakisema kuwa kadhia hii inamhusu Dk. Salmin kung'ang'ania kugombea kwa kipindi cha tatu baada ya kuwa ameiongoza Zanzibar kwa vipindi viwili wakati katiba ya Zanzibar inamkataza.

Propaganda hii iliandaliwa makusudi kumshambulia Dk. Salmin kama vile tayari amekwishaivunja katiba kwa kwenda kinyume na vifungu vinavyomtaka mtu aongoze kwa vipindi viwili tu.

Ukweli ni kwamba, kwanza Dk Salmin mwenyewe hajatamka kuwa anakusudia kugombea Urais wa Zanzibar mwaka huu. Pili, hata kama wananchi wa Zanzibar wanamtaka Dk Salmin agombee, basi hawajamtaka Rais wao huyo agombee tena kwa hali ya katiba ilivyo hivi sasa, ndiyo maana Wazanzibari wametaka kurekebisha katiba yao hiyo kwanza.

Propaganda hii ni mbaya sana, kwa vile hailengi kuwaelimisha Watanzania badala yake inajenga chuki dhidi ya Mtanzania fulani au kikundi fulani cha Watanzania.

Wakati ukweli wa jambo hili ni kwamba kulikuwepo na pendekezo la wananchi kutaka kuibadilisha katiba ili hata kama Dk Salmin atataka kugombea, aweze kufanya hivyo baada ya katiba hiyo kurekebishwa na ikawa inamruhusu.

Propaganda hizi ambazo kwa bahati mbaya zimeonesha 'kupokewa' hata na baadhi ya viongozi wa upinzani, zimewadhalilisha baadhi ya wananchi ambao wanaunga mkono vyama vya upinzani. Hii ni kwa sababu imekuwa ikiripotiwa kwamba "hata wapinzani wanasema kama katiba itarekebishwa kumruhusu Dk Salmin kugombea tena Urais basi atakuwa sultani".

Kwa hoja hiyo mtu anaweza akadhania kwamba viongozi wa vyama vyote vya upinzani wanamuona Dk Salmin ni mshindi tu kila atakaposimama katika kila uchaguzi. Tunasema hivi kwa sababu kama Dk. Salmin anataka kuongoza tena hawezi kufanya hivyo pasipo kuingia katika uchaguzi wa kidemokrasia na kisha akasubiri ridhaa ya wananchi watakaopiga kura. SULTANI HAPATIKANI KWA KUPIGIWA KURA. 

Sasa viongozi hawa hawaoni kwamba wanatoa sura mbaya ya msimamo wao mbele ya wananchi kuhusu suala la Zanzibar. Upo uwezekano kwamba wananchi waliopo kambi ya upinzani wamejizatiti kuwachagua viongozi wao kutoka kutoka upinzani na kumuangusha Dk. Salmin na chama chake cha CCM, Je, hapa Dk. Salmin ataupata pataje huo usultani?

Baya zaidi katika propaganda hizo na kwamba wanaoshabikia kadhia hii ya Zanzibar wanataka waonekane ni wananchi wazalendo, wapenda demokrasia na wenye uchungu mkubwa na nchi yetu, Tanzania. Ikiwa kuibadilisha Katiba ya Zanzibar ni kumuwezesha Dk. Salmin licha ya ugumu wote huo tulitangulia kuutaja, basi katika mabadiliko ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marekebisho hayo ya 13 ya Katiba yetu yamebadili kifungu kinachosema atakayechaguliwa kuwa Rais lazima apate idadi ya kura zinazozidi asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa kwa maana hiyo.

Kwa mfano, chini ya kifungu hicho kilichokuwepo wakisimama wagombea kumi na wa juu akapata kura 30 katika mia, anayemfuatia akapata 25 katika mia, na waliosalia wote wakagawana kura zote zilizobaki kwa idadi ya chini ya kura 25 kwa mia kila mgombea, basi huyu aliyeoongoza kwa kupata kura 30 kwa mia hatokuwa mshindi. Hii ni kwa sababu mgombea huyu, kwanza, hakupata zaidi ya asilimia 50 ya kuwa zilizopigwa, na pili atakuwa amepingwa na kura 70 katika mia. Katika hali hii jambo ambalo lingefanyika ni kurudiwa kwa uchaguzi kati ya mgombea huyu na yule aliyepata kura 25 katika mia ili wananchi watoe uamuzi wao baina ya wagombea hao wawili.

Ni dhahiri kuwa katika hali hiyo, kitu kinachojitokeza zaidi ni kwamba, ikiwa yule mgombea aliyeongoza ni kutoka chama tawala, katika marudio upo uwezekano mkubwa kwa wananchi wote kutoka upinzani kumpa kura zao yule mgombea wa pili ambaye atakuwa ni kutoka upinzani. Hivyo huyu wa upinzani atashinda kwa asilimia 70!

Ni wazi kwamba njia nyepesi kwa chama tawala kuliepuka hilo kujihakikishia ushindi ni kuibadili katiba kwa kuondoa kifungu kinacholazimisha mshindi apate zaidi ya asilimia 50, na badala yake kuweka kifungu kinachoruhusu ushindi wa kura 30 dhidi ya wagombea 9 waliogawana kura 70. Je, hii siyo njia nyingine ya mtu kujipa usultani japo kwa kipindi kimoja?! Je, wananchi hawa 'wapenda demokrasia' hawakuliona hilo ambalo linaweza kuwanyima haki wapiga kura 70 ambao hawakumtaka huyo aliyepata kura 30?!

Mpaka leo hii wananchi hawajaelezwa saabu za msingi ni kwanini kifungu kile kimeondolewa na sasa kimepitishwa kifungu kitakachomhakikishia mtu usultani japo wa kipindi kimoja cha Urais.

'Wazalendo' hawa wanapata wapi uso wa kumzushia zogo Dk. Salmin kwa jambo ambalo mwenyewe hajalitolea tamko kuwa anataka usultani wakati wanaufumbia macho usultani huu unaoweza kupatikana kutokana na mabadiliko ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?!

Jambo la kusikitisha ni kwamba propaganda hizi zimekuwa zikizoa kila aina ya uzushi kutilia mkazo hoja hizo potofu dhidi ya Dk. Salmin, Zanzibar na wananchi wake. Imetolewa mifano ambayo kimsingi haiendani na hali ilivyo Zanzibar.

Hivi karibuni tulifikiwa na habari za serikali ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kushindwa katika kura ya maoni kupitisha marekebisho iliyoyakusudia.Wazushi wa propaganda dhidi ya Dk. Salmin waliyachukua matokeo ya kura ya maoni ya Zimbabwe na kuyafanya 'ubeti muhimu katika nyimbo' zao dhidi ya azma ya Wazanzibari kubadili katiba yao.

Bahati mbaya kwa kufanya hivyo wameweza hata kuupotosha ukweli wa kile kilichotakiwa na Rais Mugabe na pia kile kilichopelekea serikali ya Rais Mugabe kushindwa katika kura hiyo.

Kulifananisha suala la Zimbabwe na hili la Zanzibar na hadaa kwa wananchi kwa sababu hili la Zanzibar halijapigiwa kura ya maoni kama lile la Zimbabwe.Ikiwa ni hivyo basi na suala hili la Zanzibar lirudishwe kwa wananchi likapigiwa kura ya maoni, hapo ndipo ukweli utakapoonekana. Basi ni kwa nini 'wazalendo' hawa wanaogopa kushauri kura ya maoni Zanzibar.

Zaidi ya hayo mbona haifafanuliwi kuwa waliyoyapinga mapendekezo ya serikali ya Rais Mugabe ni Wazungu ambao ndio kwa mara ya kwanza katika Zimbabwe huru walijitokeza kwa wingi kupiga kura na pia wakawa wamewapa pesa wafanyakazi wao Waafrika wapige kura ya hapana kuyapinga marekebisho yale kwa vile waliyaona yana athari kwao.

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k


  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE 
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita