|
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi Na Mwandishi Wetu CHAMA cha upinzani cha NCCR-Mageuzi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora kimewakataa wasimamizi wa uchaguzi mkuu ujao katika wilaya hiyo kutokana na madai kadhaa, likiwemo la kushindwa kusimamia uchaguzi wa serikali za vijiji na hivyo kufanya uchaguzi kutokuwa wa haki na huru. Katika barua ya Februari 8, yenye kumbukumbu nambari NCCR/NCG/Vol. I/975 ambayo chama hicho kimemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kusainiwa na Katibu wa Wilaya ya Nzega, Bw. Katoro Ramadhani, ambayo NASAHA ina nakala yake, chama hicho kimetaja majina ya wasimamizi hao kuwa ni Ndugu Jamari Gazembe ambye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na Ndugu Masili ambaye ni Katibu Tawala katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Nzega. "Mkurugenzi Mtendaji wilaya ameshindwa kabisa kusimamia uchaguzi wa serikali za vijiji, hivyo kufanya uchaguzi kuwa na migogoro mingi na kufanya kuwa sio HURU NA HAKI. Hii inatokana na kwa yeye kutoa maamuzi kwa shinikizo la chama tawala... Mfano hai ni kitongoji cha Nyasa Mpya kata ya Nzega mjini na katika kijiji cha Ifumba kata ya Lusu ambapo wapinzani tulishinda lakini yeye kwa shinikizo alibatilisha matokeo", kinasomeka kifungu A(1) cha barua hiyo. Aidha, kifungu B(1) kinasomeka, "Katibu tawala wilaya ya Nzega yeye kama Mwenyekiti wa Kamati ya rufaa ya wilaya amekuwa akishirikiana na Mkurugenzi kutoa maamuzi yao kwa kuegemea chama tawala". Kifungu B(2) nacho kinasomeka, "Maamuzi mengi aliyokuwa akiyatoa yeye na kamati yake yalikuwa ya jazba, hayakufuata sheria, taratibu na maelekezo. Hii imejionesha katika rufaa nyingi zilizopelekwa mbele yao kam avile rufaa ya Nyasa Mpya na kijiji cha Nzega Mashariki, Ifumba na vingine vingi". Pamoja na mambo mengine yaliyoorodheshwa katika barua hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Nzega, pia barua hiyo inamtaka Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua hatua mapema ili kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba wasihusishwe kama wasimamizi. Wakati huo huo ule mkutano Mkuu wa Taifa wa uchaguzi wa Chama cha NCCR-Mageuzi uliokuwa ufanyike siku ya Jumatatu Februari 21, umeahirishwa mpaka Machi 4, kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Vijana wa chama hicho, Bw. Joseph Selasini alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu katika ofisi za chama hicho zilizopo Ilala hapa jijini. Sababu zilizotolewa za kuahirishwa kwa mkutano huo ni kutokana na mikoa mitano kati ya ishirini kushindwa kuhudhuria mkutano huo kulikosababishwa na kushindwa kumaliza chaguzi ndani ya mikoa hiyo. Sababu nyingine ni chama makao makuu kukosa pesa za kuendesha mkutano huo wa uchaguzi, japokuwa haikuelezwa wazi kwanini wajumbe waliitwa huku ikiwa inajulikana wazi kuwa fedha hakuna. Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walioongea na mwandishi wetu walisema kuwa wameridhishwa na sababu iliyotolewa na uongozi wa juu ya kuahirishwa kwa mkutano. "Sababu ni za msingi, kumbuka kuwa kuna watu ambao kwa nafasi ya ushiriki ni wagombea nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao wako kwenye mikoa hiyo, hivyo kuwanyima nafasi ni kuvuruga demokrasia", alisema Bwana Ahmed Khalid ambaye ni mjumbe kutoka mkoa wa Tabora. |
YALIYOMO
Tahariri:
‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali' Suala la Mwembechai lazua mtafaruku Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi MPASHO
NASAHA
Habari
za ndani
Ushauri
Nasaha
MAKALA
WAZO
LA WIKI
Makala
ya Kimataifa
Kalamu
ya Mwandishi
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|