NASAHA
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
'CUF tumejiandaa kuchukua serikali'
  • Mwinjilisti ahoji mbona vibaka wa kodi hawachomwi moto 
  • Asema udini ni propaganda, CCM inaogopa upinzani 


Na Rajab Nkawa 

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mheshimiwa Wilfred Lwekatare amesema kuwa chama chake kimejiandaa vyema katika kuhakikisha kuwa kinashinda uchaguzi ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu ili kuchukua serikali kwa lengo la kuwaondolea umaskini wa kutisha unaowakabili wananchi.

Mheshimiwa Lwekatare aliyasema hayo katika Uwanja wa shule ya msingi Magomeni Februari 20, mwaka huu, alipokuwa akiwahutubia mamia ya wananchi wa wilaya ya Kinondoni katika mkutano uliandaliwa na chama chake wilayani humo. 

Alisema kuwa wanajua kwamba kuongoza nchi si jambo la ushabiki na jepesi kama vile wengine wanavyoota kuingia Ikulu na wengine kung'ang'ania madaraka, ilhali wamekwisha shindwa kuiongoza nchi kuleta maendeleo. 

"Tunajua kuwa kuongoza serikali si jambo la lelemama, inabidi kupanga vyema safu yako, kwani Ikulu si lile jengo moja tu, kama wengine wanavyofikiria. Ikulu ni kutoka Mtwara mpaka Kagera", alisema Naibu Katibu Mkuu huyo na kuongeza, "sisi (CUF) tumekwisha jijenga na kujiandaa vyema katika ngazi zote, kutoka chini mpaka juu". 

Akiongelea yale yaliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitisha mswada ambao pamoja na mambo mengine unataka mgombea Urais atangazwe mshindi hata kama amepata chini ya asilimia hamsini ya kura zilizopigwa, Mheshimiwa Lwekatare amesema kuwa huko ni kutapatapa kwani wamekwisha gundua kuwa wananchi hawawataki. Na akaongeza kuwa wao walipolipinga jambo hilo si kwamba walikuwa wanaiogopa CCM, bali jambo hilo lnaweza kuwagawa wananchi. 

"Kitendo cha Rais kupita kwa kura chini ya asilimia hamsini ni kuua utaifa wetu uliopo. Vyama vitaanza siasa za kimajimbo, vitatilia mkazo maeneo yale tu ambayo wanayoweza kupata kura za ushindi na kusahau kabisa kuleta maendeleo katika yale maeneo ambayo hawakupigiwa kura", alisema Mheshimiwa Lwekatare. 

Aliendelea kusisitiza kuwa hakuna muundo wowote ule wa mfumo wa kijamii ambao umeweza kudumu kwa muda wote na hasa mfumo ukiwa ni wenye kudhulumu haki za wananchi, hivyo akasema, "CCM lazima wajue kuwa nao wataondoka tu, jambo hili halina mjadala. Wananchi wamekwisha choka". 

Naye Mshauri wa mambo ya siasa wa chama hicho Mwinjilisti Kamara Kusupa, akizungumza katika mkutano huo wa hadhara aliwaambia wananchi kuwa propaganda zinazoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) eti kuwa chama chake cha CUF kina udini ni kutapatapa kwa chama hicho kwani kimekwisha kugundua kuwa CUF ni kikwazo kikubwa kwao kuendelea kubaki madarakani. 

Akasema kuwa kama udini ni kuwako watu wenye dini moja katika nyadhifa za juu mbona hawasemi kuwa CCM nacho ni chama cha udini, ambapo sehemu kubwa ya viongozi wake wa juu ni Wakristo na kuhoji, "Au udini umekuwa pale tu viongozi wa juu wanapokuwa Waislamu". 

Mwinjilisti Kusupa alisema kuwa nchi inaendeshwa kwa sheria mbovu zisizothamini haki za raia kwa kuwapa mamlaka polisi ya kuwakamata vijana na kuwafungulia mashitaka bila mpangilio kwa visingizio mbalimbali ikiwemo uzurulaji. Matokeo yake, alisema ni magereza kujaa na hatimaye kufurika wafungwa. "Haya ni matokeo ya sera mbovu", alimaliza Mheshimiwa Kusupa. 

Aidha, Mheshimiwa Kusupa aliwataka wananchi waoneshe hasira zao kwa vibaka waliko serikalini wenye kuiba mamilioni ya shilingi badala ya kuwaua na kuwachoma moto walalahoi wenzao wanaokwapua muhogo kwa ugumu wa maisha na njaa na akasema kuwa wizi huo lazima hufichwa na wananchi katika njia mbalimbali. 

"Wizi unaofanyika katika serikali hulipwa na wananchi kufidia pengo la bajeti ambalo serikali imejipangia, ama kwa kuongeza kodi za bidhaa na bei kuwa juu au kukosa huduma muhimu za jamii, kama huduma za hospitali", alisema Mshauri huyo wa CUF. 

Aidha, katika mkutano huo ilielezwa kuwa chama hicho cha CUF katika wilaya hiyo ya Kinondoni kinaendelea na kesi katika mahakama ya rufaa ikiwa ni hatua iliyofikiwa katika kupinga hatua ya kunyang'anywa ushindi wa viti sita vya uenyeviti wa serikali za mitaa. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Katiba ya Zanzibar ni ya Wazanzibari

‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali'

Suala la Mwembechai lazua mtafaruku

Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi

MPASHO NASAHA
Ulimbukeni wa siku ya Valentino

Habari za ndani
NCCR-Mageuzi wamkataa Msimamizi wa Uchaguzi

Ushauri Nasaha
Nafasi ya familia katika makuzi ya mtoto

MAKALA
CCM imepindua nini?

WAZO  LA  WIKI
Vitisho vya kikachero visihamishiwe mashuleni

Makala ya Kimataifa
Mtazamo wa maadui wa Uislamu juu ya Uislamu

Kalamu ya Mwandishi
Katiba irekebishwe, lakini kwa maslahi ya wananchi

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO -2
Vita dhidi ya demokra

HABARI ZA KIMATAIFA

  • Clinton kusaidia  amani Burundi
  • Nigeria yaazimia kuwa taifa la Kiislamu
  • n.k

  • Riwaya 
    Ndoto ya mafanikio - 2

    LISHE
    Madhara ya mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Makoye, Mapunda wateta Dar 
  • Tino, Katolila, Omar 'wautwaa' ukocha 
  • Tuna mashaka na Shungu - Yanga

  •  

     
     
     

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita