|
Na. 036 Jumatano Februari 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
CCM imepindua nini?
NA MWINJILISTI KAMARA KUSUPA KATIKA mfululizo wa makala hizi zinazohusu mada kuu ya maendeleo ya wananchi, sasa tunalazimika kuingia katika ukurasa mwingine unaoihusu CCM. Inatulazimu kuiangalia CCM kwasababu ndiyo chama tawala, na kwa kuwa tumeona jinsi utawala wa nchi unavyoathiri maisha na maendeleo ya watu, basi mada yoyote inayohusu utawala na maendelo ya nchi au maendeleo ya watu,haiwezi kukamilika pasipo kuigusa CCM. Tutaanza na hatua ya kwanza ya kuiangalia dhana ya mapinduzi na kile ambacho CCM imepindua. HAKUNA ubishi kwamba CCM ndiyo chama tawala kimerithi utawala kutoka kwa TANU ambayo nayo iliachiwa utawala na mkoloni. Mkoloni (Mjerumani na Mwingereza) ameitawala nchi yetu kwa miaka 75, na katika kipindi hicho ameleta maendeleo ambayo hayakuwako kabla yake. Mkoloni amejenga reli, mashule, mahospitali, na njia nyinginezo za mwasiliano kama simu, redio. n.k. Kwa upande wa uchumi mkoloni alianzisha miradi mikubwa ya kilimo kama vile mashamba ya mkonge ambayo yalitoa ajira kwa watu wengi sana. Mkoloni alikuwa mwaninifu kwa kodi za wananchi. Kile kidogo kilichotolewa kwa ajili ya maendeleo kilifanya kazi ya maendeleo, tofauti na CCM ambayo inakusanya kodi ya maendeleo, lakini maendeleo hayaonekani. Barabara nyingi zinazounganisha kijiji na kijiji hazipitiki. Shule nyingi hasa za msingi zimechakaa kiasi kwamba madarasa yenye uchakavu wa namna hiyo hayatoi elimu bali yanaua elimu. Hospitali na zahanati nyingi ziko taabani, huduma za fya zimekufa kabisa. Kwa kifupi misingi ya maendeleo imebomolewa unahitajika ufufuo wa miundo mbinu (infrastructure) kwa maana ya kufufua kilimo kilichokufa, elimu iliyokufa, njia za mawasiliano zilizoharibika, masoko yaliyokufa na utawala wenye maadili ambao ulipinduliwa taratibu sana kiasi kwamba mtu hawezi kugundua utawala huo ulipinduliwa tarehe ngapi na lini ulipokoma hadi kuanza kwa utawala mpya wa wizi, rushwa na kudhulumiana. Mapinduzi ya CCM CCM inajiita Chama Cha Mapinduzi sawa, lakini imepindua nini? Kule Zanzibar, wana-CCM wanayo haki ya kujiita CCM kwasababu walipindua utawala wa Sultani na hadi leo nchi yao inaongozwa na Baraza la Mapinduzi. Huku Tanganyika CCM wamempindua nani? Jibu ni kwamba CCM kupitia idara yao ya propaganda wamefanikiwa kupindua "akili" za watu nakuzitia giza ilizione mambo tofauti na uhalisi wake. Ndiyo maana kuna watu walifikia hatua ya kusema bila haya kwamba"CCM ndiyo Baba, CCM ndiyo mama." Watu wa jinsi hii wanaumwa pasipo wao wenyewe kujijua, wamerogwa na propaganda za CCM kiasi kwamba wanafana kabisa na mgonjwa wa homa ambaye anaweza kukazana kusema anaona baridi (huku akitetemeka) wakati wengine wote wanaona joto kali na kujificha kwenye vivuli. CCM imepindua fikra za watu na kuziharibu fikra za wale walioyakataa mapinduzi yake. Kila mara mwananchi alipoimbishwa kwamba "zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa CCM", na kuitikia zidumu!!! Papo hapo walikuwa na maana ya zidumae daima fikra za wengine wote wasiokuwa mwenyekiti wa CCM. Wakati wakiendelea kudumisha fikra za mtawala pia waliendelea "kudumisha" fikra zao kama watawaliwa. Naam wakafikia mahala ambapo fikra za watawaliwa na bongo zao zikawa sawa na nati iliyoingia kutu. Kila alichokitaka mtawala, na kila alichokiwaza ama kukisema kikawa ndiyo sahihi. Pale alipopotoka, upotofu ukawa ndio sahihi, pale alipoonea, uonezi ukawa ndio uko sahihi, na pale alipoharibu, uharibifu ukaenziwa na kutukuzwa maana nani angeweza kuwa kinyume kisha akawa salama na wengine wakamwelewa? Watu wakageuzwa kuwa washabiki wa kitu wasichokijua na wakati huo huo akili zao zikiwa zimehasiwa. Kilichofanyika hapa ni mapinduzi ya akili tu, watu wamelishwa kasumba na kasumba hiyo imepata nguvu vichwani mwao na mioyoni mwao hadi kuwawezesha kukubali mambo yasiyo kubalika. Kukubali kwamba mtawala ndiye mwenye haki kwa kuwa tu anakaliakiti na mtawaliwa hana haki ya kumkatalia lolote, kumpinga ama kumng'oa mtawala madarakani pale anapowaudhi watawaliwa. Utii unaokwenda sambamba na woga huo ni ushetani. Kuupindua utawala wa kichifu Mapinduzi yalianzia kwa machifu. Uchifu hakikuwa cheo tu, bali uchifu ulikuwa ni taasisi ya kulinda haki na maslahi ya watu katika ujumla wao. Pamoja na shughuli za utawala uchifu ulishughulika na morali za watu, na morali za nchi, mila na desturi, kulinda maadili na kutunza historia. Ndiyo maana usingeweza kumkuta chifu mzembe asiyetimiza wajibu wake hadi watu wafikie hatua yakutaka kumfukuza kazi, kumuondosha kwenye nafasi yake na kumweka mtu mwingine. Kulindwa kwa mambo haya muhimu ingawa hayashikiki wala hayakamatiki lakini yalikuwa muhimu kuiwezesha jamii husika kujua inatoka wapi, inakwenda wapi na wapi ilipojikwaa ama kuteleza hatimaye kujirekebisha. Lakini TANU kwa kuhofia upinzani, na kuuchukia upinzani, baada ya kupiga marufuku mfumo wa vyama vingi ikaiingilia taasisi ya uchifu, ikakomesha uchifu kwa kuhofia kwamba uchifu na machifu wanaweza kuwa kipingamizi kwa serikali kuu kupitisha mambo yake hadi kwa wananchi. Watawala walijua kwamba wamekusudia kuifanya nchi kuwa na utawalawa kiimla na kwamba machifu hawatakubali kupokea mambo yasiyotakiwa kwa niaba ya serikali kuu na kuwalazimisha watu wao kuyafanya, kwa hiyo njia pekee iliyosalia kwao ikawa ni kuuvunja uchifu, na kwa maana halisi kuupindua utawala wa kichifu na kuusimika utawala wa kichama. Makada wa chama wakachukua naafasi za machifu ingawaje makada hao walivaa kofia zingine za kiserikali. Wakati fulani mkuu wa mkoa alikuwa ndiye katibu wa chama wa mkoa, mkuu wa wilaya akawa katibu wa chama wa Wilaya na watu wakapendelea zaidi kumwita "katibu" badala ya DC. Chama kikashika hatamu zote za utawala, na kwa tafsiri nyingine Serikali ikawa inapokea maelekezo ya chama katika shughuli zake za siku kwa siku za utawala badala ya serikali hiyo kuelekezwa na sheria. Serikali badala ya kuendeshwa "kisheria", ikaendeshwa "kichama", (the civil service was politicized) hapo ndipo siasa ilipoanza kutawala kila kitu, nakujiinua juu ya yote. Kwakuwa siasa yenyewe ilikuwa ni fikra basi fikra za hao wanaotawala ndio zikawa ju! Juu! Juu zaidi. Fikra zikawa juu ya taaluma na zaidi ya haki. Watawala ingawaje walijipa nafasi ya juu kiasi hicho katika maisha ya watu, bado hawakufaulu kuziba pengo liliochwa wazi na machifu. Hawakuwa na huruma kama ya machifu, ya kiuhurumia nchi yao na watu wao au chochote chema kilichokuwa katika nchi. Hawakuwa na udugu wowote na hao wanaotawaliwa na kwahiyo hawakuwa na uchungu wowote na maendeleo ya maeneo waliyokuwa wanatawala. Kikubwa walichokiona wao ni kutukuzwa,kusifiwa, kuenziwa na kuabudiwa kwasababu tu ya hayo madaraka yao. Kupindua vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Kijamii. Mapinduzi ya chama hayakuishia hapo tu kwa machifu bali yaliziandama na kuzisakama taasisi zingine ili tu kuhakikisha kwamba wao watawala wanatawala pasipo kupingwa kwa lolote wanalotaka lifanyike. Wakavunja vyama huru vya wafanyakazi kama vile Tanganyika Federation of Labour (TFL) (TRAU) na kuunda chama cha kutetea maslahi ya serikali miongoni mwa wafanyakazi yaani NUTA.Wakavunja vyama vya ushirika, wakavunja taasisi za kidini kama vile East Africa Muslim Welfare (EAMWS). Yote hii ilikuwa ni kikiri kakara za kuua upinzani ili watawala waweze kuifikia nafasi yao waliyoikusudia ya Umungu mtu. Haya yalikuwa ni mapinduzi ya kuupindua utawala wa asili ndani ya taasisi hizo huru ambao uliheshimu uhuru na haki za binafsi, na kuusimika utawala mpya ambao kipaumbele chake ni kudumisha maslahi ya serikali kwanza ndipo na mengine yafuate baadaye. Taasisi zinapogeuka kuwa mtumishi wa serikali ni kiyama. Kuipindua elimu ya "uraia" na kuleta elimu ya "siasa". Mapinduzi ya watawala hayakuishia kwenye taasisi peke yake, bali walikwenda mbali zaidi, kwanza waligundua kwamba wasomi ni kipingamizi kikubwa sana katika ujenzi wa dola ya kiimla kwahiyo wakaendesha propaganda ya kuuponda usomi kwa kuufanya usomi liwe ni zao la ukoloni na kwamba wasomi wanaosimamia "ethics" waonekane ni mamluki mbele ya jamii iliyokusudia kuishi maisha mapya ya uhuru. Kwanza wasomi wakaenguliwa kwenye nafasi kama za ubunge, na ujumbe wa NEC au kamati kuu ya chama tawala. Wasomi wachache waliobahatika kushika nafasi hizo, ni wale tuambao walikubali kuzivua taaluma zao na ujuzi wao kuuweka pembeni, kisha kujivika kasumba ya chama ndipo walipopokelewa na kuitwa "mwenzetu", "ndugu yetu" n.k. Huko majeshini, polisi, magereza wasomi kwa makusudi, kabisa wakawekwa chini ya watu mbumbumbu ili wanyanyasike hadi kuuona usomi ni kama hatia ama jeshini si mahali pao. Wakati wakiendelea kuwasulubu wasomi walioelimishwa na mkoloni papohapo wakaleta mapinduzi kwenye sekta ya elimu, mapinduzi ambayo yalikusudia kuua kabisa ubora wa elimu na kumwezesha mwananchi kuwa na elimu duni(japokuwa atahitimu katika vyuo) ili aweze kutawalika kirahisi. Kwanza wakataifisha shule zote zilizokuwa zinaendeshwa na taasisi zisizo za kiserikali na kufanya utoaji elimu kugeuka kuwa jukumu la kiserikali peke yake. Serikali badala ya kujenga shule zake kwa kutumia kodi za wananchi na rasilimali za nchi,ikakimbilia kunyang'anya shule za binafsi na kupiga marufuku usajili wake kwasababu ilihofia kwamba endapo yenyewe serikali itatoa elimu sambamba na wengine, itakaribisha "challenge" kiasi kwamba ubora wa elimu na uduni wa elimu ungekuwa dhahiri kwa watu wote. Kwahiyo wakawapiga stopu wengine wote, na kujivika jukumu la kusomesha kila mtoto wa Kitanzania. Mbaya zaidi elimu waliyoamua kuitoa haikufanana kabisa na elimu aliyoleta mkoloni. Wiki ijayo 'kuipindua sheria na haki'. |
YALIYOMO
Tahariri:
‘CUF tumejiandaa kuchukua serikali' Suala la Mwembechai lazua mtafaruku Mabadiliko ya katiba ya Zanzibar: CCM Z'bar ina nafasi ya ushindi MPASHO
NASAHA
Habari
za ndani
Ushauri
Nasaha
MAKALA
WAZO
LA WIKI
Makala
ya Kimataifa
Kalamu
ya Mwandishi
MAKALA
Riwaya Ndoto ya mafanikio - 2 LISHE
|
|
|
|
|