AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua
 
Wajibu wa wasomi katika ummah wa Kiislamu

Ndugu Mhariri 

MAKALA ya mwandishi wenu juu ya dhima ya wasomi Waislamu, yaliyopewa kichwa cha habari "wasomi wawajibike" ambayo yalichapishwa Desemba 18, 1998 haiwezi kupita bila kuungwa mkono. 

Maoni yangu, mwandishi amekusudia kuwahamasisha na kuwakumbusha wasomi wajibu wao wa asili katika umma wa Kiislamu. 

Pili amebainisha dhima ya Misikiti kama vituo muhimu kwa wasomi hao kutekelezea majukumu yao. Mwandishi ametumia mtindo wa kulaumu katika kufikisha ujumbe wake, japo lengo si kulaumu. 

Maarifa au Ilimu kama ilivyo kwa vipawa vingine alivyopewa mwanaadamu ni miliki ya Allah (s.w.) na waliopewa vipawa hivyo wasione kuwa ni mali yao binafsi bali ni amana na wao ni wadhamini tu wa kuichunga na kuifikisha amana hiyo kwa walengwa (Waislamu wenzao). 

Ili kufikia lengo hili, wasomi Waislamu wajizoeze kuwa na sifa hizi: "Hakika wanaoamini kweli ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa aya zake huwazidishia imani na wakamtegemea Mola wao tu basi; hawana kuamini mizimu, wala pango wala shetani wala makaburi wala mengineyo. Ambao wanasimamisha sala na wanatoa katika yale tuliyowapa. Hao ndio wanaoamini kwelikweli. Wao wana vyeo (vikubwa) kwa Mola wao na msamaha na riziki bora (kabisa huko akhera). (Qur’an 7:2-4) 

Aidha, mwandishi ametaka Misikiti iwe kitovu cha mambo ya Waislamu, ambamo watajadili uchumi, afya, elimu, siasa n.k. Hili ni wazo zuri na linafaa kuungwa mkono kwa nguvu zote. 

Lakini tatizo ni mazingira yanayoikabili Misikiti yetu ya Tanzania. Japokuwa Misikiti hii imejengwa na Waislamu, umilikaji wake umekuwa wa kiukoo au kikabila. Sadaka zitolewazo Misikitini zinawanufaisha wamiliki husika. Ruhusa pekee inayotolewa kwa Waislamu ni kuswali, kusoma khitma na kufanya tahalili kwa maiti. 

Ili kufikia muafaka katika kadhia hii ya wasomi na Misikiti, ni vyema wasomi wakajitambulisha kwa ndugu zao Waislamu katika Misikiti. Na wamiliki wa Misikiti wawaruhusu Waislamu wajiundie Shuraa ambazo zitakuwa na kamati mbalimbali kama vile afya, elimu, uchumi n.k. 

Ni katika muundo huu ndio wasomi wanaweza kutoa ushauri. Kabla ya kuliendea jambo lolote ni vema Waislamu wakapata ushauri kutoka kwa wataalamu (wasomi) husika. 

Napenda kumalizia kwa kauli hii ya Mwenyezi Mungu: "Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (zake)". (Qur’an 48:29) 

Shaaban S. Ngemba, 
P.O. Box 22305, 
Dar es Salaam. 


Hotuba ya Rais Mkapa

Ndugu Mhariri 

Nimeshangazwa sana na Rais Mkapa kusema hakuwa na taarifa yoyote kuhusu ukandamizwaji wa Waislamu kote nchini katika nyanja mbalimbali kama vile mauaji ya Mwembechai, mashuleni, vyuoni, maofisini na katika magereza ambao idadi kubwa ni hawa waliokomboa nchi kutoka kwa wakoloni. Hii ni kejeli kubwa. 

Leo ukienda mashuleni unakuta katika wanafunzi 1000, mia 200 ni akina Juma na waliobaki ni akina John pamoja na nyanja nyingine. 

Huu ndio ubaguzi wa dini ulaaniwe na kila mmoja wetu kote nchini pamoja na jumuiya za kimataifa. 

Shaaban R. Mghuna, 
Dar es Salaam. 



Ndoa za kuondoa nuksi Masheikh katazeni 

Ndugu Mhariri 

KUMEKUWA na ndoa za ajabu sana na zinazo muudhi Allah (s.w.) sasa hapa Tabora; sijui, pengine ndoa nyingi hapa Tabora zimekuwa si zenye kudumu kwa muda mrefu sana, sana siku 3 au wiki moja (siku saba), eti mwanamke baada tu ya kufunga ndoa siku tatu anarudi kwao, eti ametoa mkosi wa kutoolewa, inashangaza kuona wazazi na Masheikh wanachekelea, na pengine ni wao ndio wapangaji wa mipango hiyo ili atoe nuksi katika nyumba yao. 

Kumbukeni Masheikh mtakuja ulizwa ndoa hizo vipi zinakuwa hivyo, sijui mtajibu nini? 

Mtume (s.a.w.) anasema: "Talaka ni halali inayomchukiza Allah (s.w.)". Vipi wazazi mnakubali mtoto wenu anarudi vipi? 

Mfano mkubwa hapa Tabora ni kijana mmoja anaitwa Umayyah, ameoa kabla wiki moja ya Ramadhani, mkewe baada ya kukaa siku tatu tu, Bi Harusi akaondoka kwa mumewe na kutamba kwamba ametoa mkosi. Hii ni halali sasa? Kijana huyu atakimbilia wapi? Gharama zote atalipwa na nani? 

Na huko Akhera mtajibu nini? Wanawake acheni kufanya hivyo, Masheikh na nyinyi kemeeni sana suala hili, mbona mmekaa kimya tumechoshwa na vitendo hivyo. 

Alley Mselem, 
P.O. Box 138/524, 
Tabora. 


Serikali yetu inatuzamisha topeni
 

Ndugu Mhariri 

DHUMUNI langu hasa ni kutaka kuongelea kuhusu mmomonyoko wa maadili katika nchi yetu, ambapo serikali yetu imechangia kwa kuharibu malezi kwa vijana wetu. 

Kwa kuweka matangazo kila kona ya kuchochea zinaa, ulevi na matendo mengine mabaya katika jamii. Matokeo yake ni kupatikana vitendo vya ubakaji, utoaji mimba, uvutaji bangi na vitendo vingine kama hivyo, huku serikali ikijifanya kukemea, na baadhi ya viongozi kutuhamasisha kwa kutugawia kondom na kutusingizia urithi wa ulevi na "Grocery" kuwa nyingi kuzidi mashule. 

Mimi ninasema Tanzania haiwezi kuondokana na umasikini licha ya viongozi husika kupita kila kona wanahubiri kuondokana na umasikini huku viongozi hao hao wakituhubiria kurithi ulevi, zinaa kwa kutujazia "Grocery" na kutugawia kondom. 

Mimi nasema kuondokana na umasikini huku tumelewa, hatufanyi kazi sawa sawa. Umasikini utabaki pale pale na utajiri kwetu ni ndoto tupu. 

Murshidu Issa, 
P.O. Box 3418, 
Dodoma. 


Waislamu tuzinduke

Ndugu Mhariri 

IMEKUWA ni kawaida kwa Waislamu kusikiliza muziki ambao si fundisho la Uislamu, pamoja na kuangalia mikanda ya sinema ambazo hazina maana na faida yoyote katika Uislamu. 

Kwa mfano, kuna nyimbo za Kizaire (sasa Congo) waimbaji husikika wakisema Al-Hamdullillah, Ssalm alaykum n.k. 

Tukirudi kwenye sinema kuna baadhi ya sinema za Kihindi waigizaji husikika wakisema Laailahaillah, Bismillah n.k. 

Kwa hiyo hii ni kuutukana na kuudhalilisha Uislamu. 

Jicho la Allah (sw.) huwaangalia wale walioamini kwa hiyo tubadili msimamo, kama hatutaacha hayo maasi pamoja na mengine tujue tutaendelea na laana ya Allah (s.w). 

Kwa vile kukosa mvua na hata ikinyesha inakuwa ni adhabu na maadui wa Allah (s.w.) kuendelea kuuharibu mfumo wa maisha wa amani (dini ya Uislamu). 

Mwisho, Waislamu ninawaomba turudi kwa Allah (s.w.) na tuwe na ushirikiano. Qur’an Kariym 3:103. 

Ustadh Id Hamad, 
Bukoli - Bukoba. 



Viongozi wapenda haki hawatakiwi na serikali yaCCM Newala?  

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nitoe kilio chetu wananchi wa Newala na Tandahimba juu ya msiba mkubwa uliotupata hivi karibuni baada ya serikali kutangaza kupitia Radio yake ya taifa kutangazia umma wote ulimwenguni kunyanyaswa kwa viongozi wetu mashuhuri katika Halmashauri yetu ya Newala na Tandahimba kwa kosa la kutetea mali ya wananchi. Ni ajabu, ingawa ndivyo ilivyo hapa Newala. 

Kwa yeyote anayewafahamu viongozi hawa kwa sifa zao, jitihada na ukereketwa wao juu ya shughuli za maendeleo ya wananchi, hususan ukaribu wao (yaani mahusiano baina yao na wanaowaongoza na kwamba walikubali kupoteza muda wao daima kwa kushughulikia masuala ya jamii usiku na mchana. 

Ni ajabu kuona wanang’atuliwa kwenye chama na serikali yake kwa kisingizio cha "Kukiuka maadili ya chama" hivi ni kweli kusimamia maendeleo, mali ya umma, kutetea jamii ni kukiuka maadili ya CCM ndani ya chama hicho? 

Ndugu wananchi, ni nani asiyemtambua kifasaha na kiutendaji kazi Mwenyekiti wetu mkongwe Bw. Bakari Sefu Madiva, kwa huruma zake, kujituma kwake, juhudi zake, ukereketwa wake na kwamba hakuwa mwenye tamaa ya mali. Ni mara ngapi kama Mwenyekiti wa CCM wilaya ametumwa na wananchi kwenda taifani kuzungumza na taifa kwa niaba yetu wananchi wa Newala na kuweza kuleta mafanikio ambayo sina haja ya kuyataja, wenyewe ni mashahidi wa yote hayo. 

Ni nani asiyemtambua Diwani Liyembe R. Mnyauka (diwani kata ya Mnekachi) kwa jinsi alivyo mkereketwa wa maendeleo ya jamii? Ni mfanyakazi hodari, mzoefu tangu enzi za mkoloni yupo madarakani hadi leo hii, wananchi kwa kumwona hana dosari wakamchagua kuwa msemaji wao katika Halmashauri. Ni ajabu Diwani huyo kupachikwa kosa la kukiuka maadili. 

Jambo la kushangaza, serikali imewatoa viongozi hao wapatao 6 na kuleta visingizio, bila ya kutoa ufafanuzi ni maadili gani yemekiukwa, maana anayeiba mali ya umma, mzembe kazini n.k. hutajwa na kosa hilo na kuleta ufahamu kwa wananchi waliowachagua "kama wameleta uharibifu kadhaa, aidha mali kadhaa yenye thamani kadhaa wamepoteza" ndipo kichama baada ya kuchunguzwa na kupata ushahidi kamili wameng’olewa madarakani kisheria. Hivi ndivyo inavyotoka taarifa sahihi na yenye ukweli. Tunashangaa taarifa hii "butu" isiyo na maelezo. 

Kwa mantiki hiyo, sisi wananchi hapa wilayani na vijijini tuna shaka juu ya mlipuko huu. Kama kampeni hii imeandaliwa kwa makusudi ili kuboresha uovu wao ndani ya Halmashauri yetu, na kuleta mwanya mkubwa wa kuchagua viongozi wabovu ifikapo mwaka 2000, kwani kwote tunajuwa kuwa viongozi hawa ndiyo waliokuwa chachu katika Halmashauri yetu na mahala popote penye ubadhilifu wa mali ya umma. 

Wote tunakiri kwamba viongozi hawa hawana hatia na kwamba serikali kwa makusudi ilione hili ili warudishwe madarakani mapema iwezekanavyo la sivyo ni dhahiri kuwa, viongozi wakereketwa (wapenda haki) hatakiwi katika serikali ya CCM. 

Tahadhari kwa serikali iliyopo madarakani kuwa kutowarudisha madiwani hawa ni kusababisha vurugu katika zoezi nzima la uchaguzi mwaka 2000 kwani tumeshagundua hila zenu na kwamba haina maana wananchi kupoteza wakati wao bure wa kutafuta maisha kwa kufikiria nani kiongozi atakayewafaa na hatimaye akipatikana hufanyiwa kampeni ya kuondolewa kwa ajili ya maslahi ya walio wachache. Nasisitiza tena kuwa haina maana. 

Mwisho wa kilio hiki, naiomba serikali ngazi ya taifa, Rais na Waziri Mkuu walichukulie suala hili kwa mapana na marefu, kufikiria kilio chetu Newala ili viongozi hawa warejeshwe madarakani (uongozini). Kwa kufuata sera za chama hicho hicho cha CCM kinachotawala. 

Kwa kukumbusha ni kwamba: CCM inasema: Itafanya kazi ya kulinda uhuru na raia wake, na kwamba inapiga vita dhuluma, vitisho na upendeleo". Swali la kujiuliza ni hili, huko ndiko kulinda uhuru na raia wake? Je, hiyo siyo dhuluma na vitisho? 

Mpenda haki, 
Newala, Mtwara. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi 

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa 

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000 

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa 

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel 

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale 

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha 

Mjue Usama bin Ladin -2 

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa 

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha 

Parole kwa mbinde! 

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil 

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha 

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR 

I.P.C yatakiwa kujitangaza 

Kutoka magazeti ya zamani 

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa 
Na Muhibu Said 

Waislamu wachoma moto nguruwe 

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa 

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe 

Sayansi na Teknolojia 
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na Lishe 
[Mwongozo wa mlo wa kila siku] 
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita