AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil

MABARAZA yote yanayodai yapo kwa ajili ya Waislamu nchini hayawatumikii Waislamu na badala yake watu waliokuwemo humo wapo kwa ajili ya kutunisha matumbo yao na kuwatelekeza Waislamu. 

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa Baraza la Iddi mjini hapa na Sheikh wa Mkoa wa Morogoro na mjumbe wa kamati ya Ulamaa wa Taifa Sheikh Omar Mohammed Bafadhil, Baraza la Iddi lililofanyika katika Msikiti mkuu wa Boma. 

"Leo Baraza gani linatetea Waislamu wa Tanzania ebu niambieni ndugu zangu Waislamu, hakuna kwani mabaraza yote yapo kwa ajili ya kunufaisha matumbo ya watu na hayana msaada wowote kwa Waislamu wa Tanzania", amesema Sheikh Omar na kuongeza kuwa katika Bakwata kuna watu wachache wenye msimamo lakini hawawezi kufurukuta. 

Sheikh huyo akilikosoa baraza lake amesema kama Bakwata ipo inaangalia matatizo ya Waislamu na haiyapatii ufumbuzi, bora liundwe baraza jipya na Bakwata lifutwe au lijengwe upya. 

Ameendelea kusema kuwa Bakwata kama litabaki katika hali hiyo hakuna Waislamu wa Tanzania watakachokipata. Alidai kuwa Baraza limeshindwa kuwaandaa Waislamu hususan katika suala zima la elimu ambapo shule zote za Bakwata nchini maendeleo yake ni mabaya. 

Ameongeza kuwa wanataka Waislamu wenyewe na wawe kitu kimoja ambapo amesema hiyo itasaidia kudai haki zao kikatiba. 

Aidha, Sheikh Omar amemwagiza Sheikh wa wilaya ya Morogoro Mohammed Kairo kupiga marufuku semina zote zinazofanywa na Waislamu bila ya kupitia kwake. 

"Kuna watu Sheikh kupitia mgongo wako wanafanya semina ambazo zingine zinakuwa hazina malengo mazuri na Uislamu na hivyo kukuchafulia sifa ya wilaya yako. Nasema mimi kama Ulamaa wa Taifa sintopenda kuona mkoa wa Morogoro unaharibiwa na watu wachache kwa kigezo cha fedha hivyo lazima semina zidhibitiwe nimewachemsha Bakwata taifa sembuse watu hawa wadogo", amesema Sheikh Bafadhil. 

Pia Sheikh Bafadhil ametoa changamoto kwa Waislamu wenye uchungu na maovu yanayofanywa katika dini yao na kupuuzwa na Bakwata kufanya juhudi ya kuingia katika baraza hilo badala ya kulikataa na kulidharau. 

"Mpaka sasa hivi baraza la Waislamu Tanzania ni Bakwata mpende msipende na dawa si kulivunja Bakwata bali ni kulirekebisha kwa mtu kutoa maoni yao kwa baraza hilo na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi", alisema Sheikh Bafadhil. 

Vile vile Sheikh Bafadhil ametoa agizo kwa Waislamu wote nchini kutokubali kutoa viwanja vya Misikiti kama wafadhili wenye masharti kwa madai kuwa masharti hayo ndiyo yanayozua migogoro na migongamno ya Waislamu nchini. 

"Ndugu zangu Waislamu msikubali kuwapa ramani na hati wafadhili wanaotaka kuwajengea Misikiti bali muwaambie wawajengee na pasiwepo masharti ya kuwekewa Imamu na mambo mengineyo ambayo ndiyo chanzo cha migogoro. 

Ameendelea kusema kuwa Waislamu wote wanatakiwa wapendane, waondoe kibri, kudharauliana na tofauti za utaifa, rangi pamoja na ukabila vitu ambavyo amedai vinaondoa mshikamano na umoja wa Waislamu na unakiuka mwenendo wa Mtume (s.a.w.). 

Pia amewataka Waislamu wawe karibu na watu wasio Waislamu huenda kukaa nao karibu na kwa wema watu hao wakawa Waislamu. 


Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha
 

Waenda mazikoni kwa ngoma 

HALI ya Uislamu katika kijiji cha Lukulunge ambacho kipo kilomita 10 kutoka makao makuu ya tarafa ya Mvuha katika mkoa wa Morogoro ni ya kutisha ambapo Waislamu wa huko bado wanaendelea na utamaduni wa kuzika kwa ngoma maarufu kwa jina la "kipazi" au "upazi". 

Akizungumza na gazeti hili kijijini hapo, Sheikh wa umoja wa Waislamu wa kijiji cha Lukulunge na Tulo Sheikh Mohammed Mtali amesema yeye alifika kijijini hapo miaka ishirini iliyopita na kuwakuta Waislamu wa huko wakizikana kwa ngoma maarufu kwa jina la "upazi" ndipo alipolazimika kuanzisha madrasa mwaka 1970. 

Sheikh Mtali amesema kwamba alijihidi kuondoa hali hiyo kijijini hapo lakini baadhi ya Masheikh aliowakuta kijijini hapo walikuwa kikwazo na walikuwa mstari wa mbele katika mambo maovu kama ya unywaji pombe hali iliyopelekea Waislamu wa hapo kutomsikiliza Sheikh yeyote anayefika kijijini hapo. 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni umegundua kuwa kijiji hicho kina zaidi ya asilimia 99 ya Waislamu ambapo kina vilabu vya pombe (sehemu za kunywea pombe) vinne ambapo wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani vilikuwa vikiendelea kufanya kazi kama kawaida, 

Hata hivyo, Waislamu wachache wakishirikiana na Sheikh wao Mohammed Mtali, Mzee Ally Masea, Ramadhani Mapuyanga, Mzee Ally Madai pamoja na Mzee Sefu Kisogo walishirikiana na kufanikiwa kiwanja cha kujenga Msikiti. 

Waislamu hao waliendelea na juhudi zao na kufanikiwa kufyatua matofali ya tope na kuyachoma tayari kwa ujenzi wa Msikiti wa kijiji chao cha Lukulunge. 

Jitihada za Waislamu hao ziligonga mwamba mwaka 1992 baada ya serikali ya kijiji ikiwa chini ya kamati ya ujenzi ya kijiji iliyoongozwa na Athumani Manyundo wakawawekea shinikizo Waislamu hao na kuyachukua matofali hayo na kwenda kujenga shule na hivyo kukwamisha ujenzi wa Msikiti mpaka sasa. 

Kukosekana Msikiti kijijini hapo kumesababisha matatizo makubwa kwa Waislamu ambapo hakuna Ijumaa na kusababisha Waislamu wachache kwenda kuswali katika vijiji vingine vya mbali. 

Kutokana na juhudi za Sheikh Mtali wameweza kujenga msikiti mdogo ambao una uwezo wa kuchukua watu kumi (10) kwa mara moja. 

"Bwana mdogo naomba Waislamu kwa uwezo wao wote mahali popote waweze kutusaidia ili Waislamu wa hapa waweze kuondokana na mila zinazopingana na Uislamu baada ya madrasa yetu kufa", amesema Sheikh Mtali huku akizidi kuhimiza Waislamu kwenda kijijini Lukulunge ili kuinusuru dini ambayo inadidimia. 

Ameongeza kwa kutoa wito kwa wazaliwa wote wa kijiji cha Lukulunge popote walipo kuelekeza nguvu zao kijijini hapo. 

Wakati huo huo, kijiji cha Kongwa kilichopo tarafa ya Mvuha mkoani hapa bado kina msiba mkubwa kufuatia Waislamu wa eneo hilo kutokuwa na mwongozo sahihi wa dini yao ambapo kwa kiwango kikubwa kumechangiwa na watu waliofika kijijini hapo kujiita "Masheikh" na kuangukia katika vitendo vinavyokwenda kinyume na dini ya Kiislamu. 

Kijiji hicho ambacho kilianzisha madrasa mwaka 1978 ikiwa chini ya Sheikh Kibwana Omar Dege, haikuweza kudumu kwa muda mrefu baada ya wanafunzi na Waislamu wa hapo kumshuhudia Sheikh wao huyo akichanganya mambo ya mila katika mazishi ya Kiislamu, akiwacheza ngoma watoto wake pamoja na kupika pombe, hali iliyopelekea wanafunzi wote wa madrasa kumkimbia. 

"Mimi mwenyewe nilikuwa mmoja wa wanafunzi wa Sheikh huyo, lakini nikakata tamaa ya kusoma kwake kutokana na vitendo vyake", amesema mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Kibwana Bw. Omar Kisungura wakati akiongea na gazeti hili hivi karibuni kijijini Kongwa. 

Waislamu hao wamesema kuwa katika mazishi kuna kitu wanakiita "kumuli" hiki mtu anapokufa hukatwa kipande cha sanda, mkeka (mchakavu) pamoja na shilingi 20, ambapo Sheikh anapoingia kaburini baada ya kumlaza maiti hutoa hadharani kipande cha sanda huku akiwa amekifunga fundo na kusema kwa sauti "jamani kimuli hiki!". 

Wameendelea kusema kuwa kisha Sheikh hukikabidhi "kimuli", shilingi 20 pamoja na kipande kikukuu cha mkeka kwa watani pamoja na ndugu wa marehemu. 

"Kwa kufanya hivyo, tayari Sheikh ameshatoa ruksa kwa ndugu wa marehemu kwenda pamoja na vitu hivyo (kimuli) kwa waganga wa ramli ili kujua nini kilichomuua marehemu", amesema Bw. Ally Chanzi ambaye ni Imamu kijijini hapo. 

Aidha, uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa mpaka hivi sasa kuna koo bado zinaendelea na mazishi ya kimila ikiwa ni pamoja na kinamama kuimba pamoja na kucheza ngoma kwenye mazishi. 

Imamu wa Msikiti wa Kongwa Ustadh Ally Chanzi amesema hali ya Uislamu kijijini hapo inatisha na amewaomba Waislamu popote walipo kufika kijijini hapo kuwatoa mchanga wa macho Waislamu wa huko. 

"Sisi tumeishia juzuu tu elimu yetu ni ndogo Masheikh nao ndiyo hivyo wamekuwa wakihalalisha ndoa za "kinyumba" hali ambayo inaonekana kama ndiyo utamaduni wa Kiislamu", amesema Imamu huyo na kusisitiza kwamba walimu, Maustadh na Masheikh kutoridhika na hali ya Uislamu iliopo mijini bali waende vijijini ambapo kama kweli wana imani na dini yao wanaweza kububujikwa na machozi. 

Nako kijijiini Tulo tarafa ya Mvuha Waislamu ambao hawakuwapeleka watoto wao madrasa na wao wenyewe kuacha kuswali watatengwa kwenye mazishi pamoja na shughuli zote za Kiislamu. 

Agizo hilo limetolewa na Imamu wa Msikiti wa Tulo Mvuha Sheikh Kambi Kongwa katika hotuba ya sala ya Ijumaa hivi karibuni. 

"Tunabembelezana kila siku, lakini kila siku Misikiti na Madrasa ndiyo inazidi kuwa tupu, hivyo umefika wakati sasa wa anayejitenga na matendo ya Uislamu kutengwa", amesema Imamu huyo. 

Naye Sheikh Mohammed Mtali wa kijiji cha Lukulunge ambaye alikuwepo kijijini hapo kwa sala ya Ijumaa aliunga mkono hoja ya Imamu Kambi na kuongeza kusema kuwa mwezi wa Ramadhani umekwisha hivyo yeyote atakayerudi katika machafu ambayo aliyaacha mwezi wa Ramadhani basi mtu huyo afahamu kuwa swaumu yake haijfaa kitu. 



Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR 

MRATIBU Mkuu wa Ujenzi; Da’awah na Mawasiliano; Ustadh Rashid Salum Futa amewaagiza Waislamu wa kijiji cha Hamai tarafa ya Goima wilaya ya Kondoa kutoyasokotea tumbaku au kuyafungia bidhaa magazeti ya ANNUUR badala yake wayatunze kwa kuwa na kumbukumbu nayo. 

Ustadh Futa ameyasema hayo alipokuwa akigawa nakala za zamani bure kwa Waislamu wa Hamai na Songolo wilayani Kondoa hivi karibuni. 

Ustadh Futa aliwaambia Waislamu kwamba katika magazeti hayo mna maneno ya Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume (s.a.w) hivyo yasitumike kinyume na kusudio lake. Aliwaambia Waislamu kuwa yule atakayemaliza kulisoma alihifadhi au ampe mwenziwe alisome vile vile. 

Ustadh Futa alisema kuwa mbali na mafunzo ya dini yaliyomo ndani ya gazeti hilo, pia mna mambo mengi ya kujifunza na kuzingatia yahusuyo jamii kwa ujumla. 

Pia Waislamu wa vijiji hivyo (Hamai, Songolo) wana tafakari miundo mbinu ya kuhuisha Uislamu na kuanzisha kongamano litakalowakusanya Waislamu wote wake kwa waume, na kushirikisha vijiji zaidi ya sita. 

Wakati huo huo, Mratibu wa jengo la Masjid Dalai, Da’awah na mawasiliano, Ustadh Rashid Ramadhani amewaomba Waislamu kuelekeza sadaka zao katika kuziinua taasisi za elimu hususani madrasa za Qur’an (dini). 

Ustadh Ramadhani alitoa wito huo pale alipotembelewa na mwandishi wa habari hizi ambaye alitaka kujua maendeleo ya elimu na shughuli za Da’awah hapo kijijini Dalai wilaya ya Kondoa. 

Ustadh Ramadhani alisema pamoja na kupata maendeleo mazuri katika sekta ya elimu ya dini; kupatikana kwa walimu wawili, Ustadh Karim Hassan na Hassan Mussa Bariwan; pia kuongezeka kwa wanafunzi hadi kufikia 540, watoto wakiwa 350 na watu wazima 100, bado katika sekta yao ya elimu wanakabiliwa na matatizo kama vile mishahara ya walimu, vitabu na madawati. 

Aidha, alisema upanuzi wa haraka unahitajika kwa jengo la madrasati Aliyu Al-Islamiya ambayo ilianzishwa Nov. 17, 1998, jengo hilo limekuwa dogo na husababisha wanafunzi kujibana au kusoma kwa zamu, hali ambayo huzorotesha mtandao mzima wa elimu. 

Pia Waislamu wa Dalai wilayani kondoa wametoa shukrani zao za dhati kwa Bw. Athuman Tajwa (Ya Rabi Salama) kuwa mfadhili na mfuatiliaji wa shughuli za ujenzi wa Msikiti. 

Aidha, Ustadh Ramadhani amemshukuru Alhaj Ismail Dawood (Victory Bookshop) kwa kuwa karibu na Waislamu wa Dalai. Kijiji cha Dalai ni miongoni mwa vijiji vilivyoathirika sana kiuchumi kufuatia ukame uliotanda mkoani Dodoma. 


I.P.C yatakiwa kujitangaza

WAISLAMU wa Manispaa ya Arusha, wametoa changamoto kwa uongozi wa kituo cha kutangaza Uislamu tawi la Arusha (Islamic Propagation Centre - I.P.C.) kukitangaza kituo hicho ili shughuli zake zieleweke kwa jamii nzima ya Kiislamu. 

Changamoto hiyo imetolewa na Waislamu hao katika moja ya mikutano iliyoitishwa na uongozi wa I.P.C. mkoa kujadili maendeleo ya ujenzi wa shule ya msingi ya Kiislamu Mudio mkoani Kilimanjaro uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Madina mjini hapa. 

Katika kutekeleza kazi ya kuitangaza I.P.C. uongozi huo umeshauriwa kuandaa utaratibu wa mihadhara ambapo sera za kituo hicho zitanadiwa na hivyo kuwafanya Waislamu wengi kukielewa kituo hicho kinafanya nini. 

Akisisitiza hoja hiyo, Mzee Kisukari alisema kwamba baada ya I.P.C. na sera kufahamika ni wazi Waislamu wengi watajitokeza kuchangia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na kituo hicho ambayo alisema ni mizuri inayomtanabahisha mwanadamu kuliendea lengo kuu na la pekee la kuumbwa kwake. 

Aidha, I.P.C imeshauriwa pia kujitangaza nje ya nchi ili hata Waislamu walioko huko waweze kuchangia maendeleo ya dini yao yanayofanyika hapa nchini. 

Awali, katika taarifa yake fupi ya ufunguzi katika mkutano huo, Mwenyekiti wa I.P.C mkoa wa Arusha Dk. A.S. Ijani alifahamisha juu ya hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa shule ya msingi Mudio na kwamba bado fedha zaidi zinahitajika ili mradi huo ukamilike. 

Dk. Ijani alizidi kuufahamisha mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Ustadh Jabir Koosa ambaye ni Amir mkoa wa Kilimanjaro kuwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza A (AI) ya madarasa matatu mapema mwaka jana, katika awamu ya IB inahitajika kujengwa jengo la utawala lenye vyumba vinane. Jumla ya gharama za vifaa vinavyohitajika pamoja na ufundi ni shilingi 4,184,500. 

Waislamu wa Arusha katika mkutano huo waliazimia kuchangia shule ya Mudio kwa kila mmoja kutoa kiasi awezacho kila mwezi, kuandaa visanduku vya kuweka katika sehemu mbalimbali za biashara, kubuni na kuandaa miradi mbalimbali ya kuendeleza shule ili kuweza kulipa mishahara, kununua vifaa vya kitaalamu na mambo mengine. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi 

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa 

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000 

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa 

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel 

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale 

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha 

Mjue Usama bin Ladin -2 

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa 

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha 

Parole kwa mbinde! 

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil 

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha 

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR 

I.P.C yatakiwa kujitangaza 

Kutoka magazeti ya zamani 

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa 
Na Muhibu Said 

Waislamu wachoma moto nguruwe 

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa 

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe 

Sayansi na Teknolojia 
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na Lishe 
[Mwongozo wa mlo wa kila siku] 
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita