AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha
 
  • Qur’an, miswala, jeneza vyachomwa moto
  • Mkuu wa wilaya adai ni wahuni
KATIKA hali isiyo ya kawaida Desemba 26, 1998 watu waliodaiwa kuwa ni waumini wa Kikristo waliuvamia Msikiti wakati Waislamu walipokuwa wanaendelea na swala ya tarawehe ndani ya Msikiti huo. 

Tukio hilo lilitokea katika Masjid Nuru ulioko kata ya Bazirayombo kata ya Chato wilayani Biharamulo. 

Kadhia hiyo ilifuatia baada ya kundi hilo kupiga disko kwa sauti ya juu kiasi ambacho Waislamu hawakuweza kusikilizana katika swala. 

Waumini wa Msikiti huo waliamua kwenda kwa wanaopiga disko hilo ndani ya ukumbi uliopo katika nyumba ya wageni (Guest House) iliyoko jirani na Msikiti huo na kuwaomba wapunguze sauti kama sio kuzima kabisa, kwani ibada yao haifanyiki kwa utulivu unaotakiwa. 

Mpiga disko aliyejulikana kwa jina la Abdallah Omar aliamua kupunguza sauti ya muziki huo jambo ambalo washabiki (wachezaji) hawakuwa tayari na hilo wakaamua kuwafuata Waislamu ili kujua ni kwanini waharibiwe starehe zao kwa masuala ya ibada (swala). 

Kabla ya kufika Msikitini walikutana na kundi la Waislamu waliokwenda kuwaomba wapunguze sauti ya muziki. Ndipo mzozo mkali ulipoanza na kurushiana makonde na bakora jambo ambalo liliwafanya waumini (Waislamu) kukimbia kwa vile walikuwa wachache kuliko kundi jingine. 

Kundi hilo halikuishia hapo lilikwenda moja kwa moja Msikitini na kuvamia milango na madirisha wakaivunja vunja. Aidha, misahafu (Qur’an), miswala pamoja na jeneza viliteketezwa kwa moto kabisa. 

Mwandishi wa habari hizi alipoongea na Mkuu wa wilaya kuhusiana na kadhia hii; mkuu huyo alionyesha kutokuwa tayari kulizungumzia japo analifahamu vizuri badala yake alitakakujua ni nani aliyefikisha taarifa hizi gazetini. 

Hata hivyo, aliamua kulizungumzia ambapo alidai kuwa hili si suala la kidini bali suala la kijamii kwani mpiga disko ni Muislamu. 

Amesema kwamba vyanzo vyake vya habari vyaonyesha kwamba kundi fulani lililojiita la Kikristo lilimuomba Bwana Abdallah ambaye ni mfanyabiashara aonyeshe kanda za Kikristo siku ya Krismasi ambazo zingeonyesha historia ya Yesu Kristo. 

Wakati Bwana Abdallah anangojea watazamaji wajae ndani ya ukumbi aliweka kanda za muziki kuwaburudisha watu ambao tayari walishaingia ukumbini tayari kwa maonyesho ya sinema (picha) zilizokusudiwa. Muziki huo ukawa ndio chanzo cha vurugu hizo. 

Aidha, Mkuu wa wilaya alisema kwamba analiita suala la kijamii lililowahusisha vijana wa kihuni kwa sababu wale waliotoka Msikitini hawakuingilia mlango wa mbele kama kawaida bali walitumia mlango wa nyuma jambo ambalo si la kawaida. Si hivyo tu, bali waliingia na bakora tayari kwa mapambano. 

Kundi la pili nalo ni la kihuni kwa sababu hapakuwa na uhusiano kati ya Msikiti na watu waliwafuata kuzima disko lao. La msingi wangepambana nao kisha baada ya kuona wamekimbia wangeendelea na starehe zao. 

"Kwa hiyo, ndugu mwandishi hilo ni suala la kijamii na wala si la kidini", alimalizia sehemu hiyo. 

Hata hivyo; Mkuu huyo wa wilaya alisema bada ya yeye kupata taarifa hizo akiwa mkutanoni Bukoba mjini alilazimika kwenda haraka baada ya mkutano huo ili kushughulikia suala hilo. 

Aliongeza kusema kuwa alikwenda eneo la tukio na kukutanisha pande zote mbili (Wakristo na Waislamu) kwa lengo la kusuluhisha mgogoro huo na si kusikiliza kesi. 

"Kwa bahati nzuri ndugu Mwandishi tulikubaliana kwamba suala hilo ni la wahuni na hivyo lisiendelee zaidi ya hapo na wala asilitoe yeyote katika vyombo vya habari kwani lingeleta sura mbaya katika jamii ", alimalizia Mkuu wa Wilaya. 

 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi 

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa 

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000 

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa 

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel 

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale 

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha 

Mjue Usama bin Ladin -2 

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa 

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha 

Parole kwa mbinde! 

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil 

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha 

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR 

I.P.C yatakiwa kujitangaza 

Kutoka magazeti ya zamani 

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa 
Na Muhibu Said 

Waislamu wachoma moto nguruwe 

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa 

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe 

Sayansi na Teknolojia 
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na Lishe 
[Mwongozo wa mlo wa kila siku] 
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita