AN-NUUR 
Na.185 Shawwal 1419, Januari 29 - Februari 4 , 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Parole kwa mbinde!
 

HATUA ya serikali kuzivunja bodi za Parole zilizoundwa kwa kuzingatia udini na kuunda bodi mpya zinazodaiwa kuwa na uwiano mzuri katika jamii inathibitisha madai ya siku nyingi ya Waislamu kuhusu udini unaoendeshwa na watendaji wakuu wa serikali. Hatua hii imeacha masomo kadhaa kwa Waislamu, Wakristo, serikali yenyewe na Watanzania wengine kwa ujumla. 

Na Saidi Rajab

Kwa Waislamu, tumejifunza falsafa ya msemo mkongwe wa Waingereza: He who asks for nothing gets exactly what he asks for nothing. (Usipoomba kitu hupewi kitu). Kelele za Waislamu kwenye vyombo vya habari leo zimesaidia angalau kuifanya serikali ione haya na itengue uteuzi wa bodi za Parole zilizojazwa Mapadre na Maaskofu bila ya kuzingatia uwakilishi wa Waislamu. 

Mazoea ya udini ya watendaji wakuu wa serikali yamewafanya waone kila jambo la kitaifa ni haki ya Wakristo. Kama Waislamu wasingelalamika, kweli serikali ingekiri hadharani kwamba kulikuwa na uwiano mbaya katika bodi zile? Waislamu msichoke kupigania haki zenu na kufichua dhulma mnazofanyiwa. 

Kuna maeneo mengine mengi tu Waislamu wananyanyaswa na kubaguliwa mbali na Parole. Katika elimu, mgawanyo wa madaraka, haki za kuabudu na mahakama. Kwa kutaja chache tu. Kuundwa kwa bodi mpya za Parole ni kielelezo cha ukweli wa madai ya Waislamu kuhusu udini unaoendeshwa na serikali. Vipi serikali isiyo na dini iunde bodi kidini? 

Waislamu msijali ububu wa serikali katika kuondoa dhulma dhidi yenu. Anayevaa kiatu ndiyo anayejua wapi kinabana. Hatuwezi kumtegemea mtu yeyote aseme kwa niaba yetu. Ni nyie wenyewe. 

Kuna baadhi ya Wakristo, Wachungaji na taasisi zao ambao ni maalumu kwa kudharau, kukejeli na kuponda madai ya Waislamu kwa serikali yao. Kuna wengine wameshathubutu kusema kwamba kudumaa kielimu kwa Waislamu kunatokana na kuendekeza mno pilau! Kuna Mwinjilisti mmoja alishawahi kuandika "Waislamu na Wakristo siyo wakewenza" yaani kila alilopendelewa Mkristo siyo lazima na Muislamu apate! 

Hawa wote ni wana propaganda wa Kanisa na wananufaika na mfumo dhalimu wa kidini uliopo nchini. Ndiyo maana wanapiga vita vya kipropaganda na kisaikolojia ili kudhoofisha ukweli wa madai na hoja za Waislamu.  

Walimshutumu Rais alipovunja bodi za Parole kwa sababu bodi zile zilikuwa kwa manufaa yao binafsi siyo taifa. Hawakuona hata hekima ya Mheshimiwa Rais kuzikataa bodi zile kwa jinsi walivyo na chuki na Waislamu. 

Hawatoi hoja zenye mashiko wala ushahidi mzito, bali ni porojo, chuki na ukereketwa tu. Kwa mfano Waislamu wanatumia sana historia ya mapambano ya uhuru, ahadi za Mwalimu Nyerere na kitabu cha Padre John Sivalon kuthibitisha dhulma na udini uliopo ndani ya serikali yetu. Lakini Wakristo na watendaji wakuu wa serikali hawatoi majibu ya hoja za Waislamu wala hawakiri kama kuna hali ya namna hiyo. Wanaruka ruka tu.  

Hata siku moja hutoona Wakristo wala viongozi wa serikali wakitumia kitabu cha Sivalon kujibu hoja za Waislamu. Wanakwepa. Kitabu chenyewe ni cha kwao na wao ndiyo waliokichapisha ili kutathmini mafanikio ya siasa za udini walizozianzisha nchini. Leo kitabu hiki hawakirejei kabisa! Kimekuwa mama mkwe wao! Kwa nini? Kinathibitisha madai ya Waislamu na kinaweka wazi dhulma za Kanisa dhidi ya Waislamu kupitia serikali. 

Kwa hiyo, Wakristo wajifunze kuwa madai ya Waislamu ni halali na yana mashiko. Si vyema kuwadharau, kuwakejeli na kuwaita majina yasiyofaa. 

Serikali inapaswa ielewe kwamba haki ya mtu haipotei. Ni suala la muda tu. Huwezi kudanganya watuwote kwa wakati wote. Bila shaka hatua ya Rais kuzivunja bodi za awali ilizingatia hilo. Rais aliona vipi bodi hizo zitafanya kazi yake kwa jamii wakati sehemu kubwa ya jamii haikushirikishwa katika muundo wa bodi hizo? Huko ni kupalilia mgogoro ambao utailipua nchi siku za usoni. Akachukua uamuzi wa busara wa kuzivunjilia mbali na kuagiza ziundwe upya. 

Kazi nzuri! Lakini Mh. Rais udini hauko katika Parole peke yake. Upo katika maeneo mengi na nyeti zaidi kuliko Parole. Je, huko hakuhitaji hatua madhubuti kama hizi? Au kilio cha Waislamu bado haujakisikia kama ilivyokuwa kwa Parole? 

Somo lililopo ni kwamba serikali isisubiri mpaka Waislamu walalamike. Ni jukumu la serikali kutambua haki za msingi za raia wake na kuwapatia bila kinyongo. Kwanini mpaka iwe kwa mbinde! Mambo hayo yanawafanya Waisalmu wakose kabisa imani na serikali yao.  

Madai ya Waislamu siyo Parole peke yake. Waislamu wanadai waliouwa Mwembechai wafikishwe mahakamani, waliowadhalilisha wanawake magerezani wachukuliwe hatua za kisheria, mtoto Chuki Athumani akatibiwe nje ya nchi, polisi na vyombo vya dola viache kunyanyasa Waislamu na kadhalika.  

Kama hili la Parole limeonekana baya; mengine kulikoni? Au siyo madai halali? Basi tambueni kama siyo halali tuache kudai. Kukaa kimya na kutia pamba masikioni siyo dawa yake. Historia ina tabia ya kujirudia kusahihisha makosa na kudhihirisha dhulma dhidi ya wanyonge. Hatudhani kama watawala wa nchi yetu watapenda kukumbukwa kwa ubaya na Watanzania. 

Kuundwa kwa bodi mpya za Parole kunategemewa kuwafumbua macho Watanzania wengine wenye taasubi ya kukebehi na kupuuza madai ya Waislamu. Angalau wajifunze kwamba Waislamu wana kitu, hoja na ushahidi mzito. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Kama hakuna haki watu watachukua sheria mkononi 

Kupokelewa kwa malalamiko ya Waislamu: Masheikh wasubiri ukweli wa Mkapa 

Afariki baada ya kutokwa damu nyingi: Yadaiwa hakuwa na sh. 4,000 

Nyumba ya Wakfu iliyoporwa yarejeshwa 

Kamanda Gewe atakiwa amkamate Daniel 

Sheikh awasambaratisha walevi Liwale 

Msikiti wavamiwa na kuvunjwa milango, madirisha 

Mjue Usama bin Ladin -2 

Msikiti wa Mwinyimkuu wafanya sensa 

Njaa hakuna, tunategemea kula silaha 

Parole kwa mbinde! 

Mabaraza yawatetee Waislamu - Sheikh Bafadhil 

Hali ya Uislamu Lukulunge, Kongwa inatisha 

Waislamu Kondoa waagizwa kuyatunza magazeti ya ANNUUR 

I.P.C yatakiwa kujitangaza 

Kutoka magazeti ya zamani 

Sabato ni ya Waisraeli, Mungu alikwishaiondoa 
Na Muhibu Said 

Waislamu wachoma moto nguruwe 

Tume ya kubadili Katiba Kenya: Waislamu kuwakilishwa 

Waislamu Msonge waomba wanusuriwe 

Sayansi na Teknolojia 
[PELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! – (2)] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na Lishe 
[Mwongozo wa mlo wa kila siku] 
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita