AN-NUUR 
Na.182 Ramadhan 1419, Januari 1 - 7, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MASHAIRI
 

Hawa ni watu waovu 

Wapo wenye ushupavu, wa kuyapamba maovu, 
Maneno ya upumbavu, yawatoa kama povu, 
Mema wayapa makovu, yaonekane mabovu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Wapo wenye Bongo kavu, wasiona kwa upevu, 
Walokosa hata wivu, wa kuiga zile mbivu, 
Watumia zao mbavu, kuhubiri sera mbovu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Wapo wenye ulemavu, wa kupuzia maovu, 
Pombe wageuza ndovu, eti yatoa “uchovu”, 
Kutwa wanazoza mbovu, wajisifu kwa maovu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Wapo wenye dhana mbovu, wanaotudhani ni wachovu, 
Wajenga hoja lemavu, tufate yao maovu, 
Eti kondom wokovu, mekalia kuti kavu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Wapo wale wenye nguvu, watumiao mabavu, 
Watunyonya zetu nguvu, na kutuita wavivu, 
Wamependeza mashavu, sisi zachomoka mbavu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Wapo wategao nyavu, kuwanasa wenye ndevu, 
Nguo zao ‘mbovumbovu’, wavaa kwa ulegevu, 
Mwendo wao wa ‘uvivu’, wajifanya watulivu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Nasikia maumivu, kwa kuzagaa maovu, 
Sipati uvumilivu, kuyameza mabavu, 
Wayabebao maovu, wafuata upotevu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Kiko mesema kwa nguvu, kuyakemea maovu, 
Kiko kalamu i kavu, imeshakuwa chakavu, 
Kiko meishiwa nguvu, najisikia mchovu, 
Hawa ni watu waovu, tusidhani ni werevu. 

Idd S. Kikong’ona 



Tusitiri Ya-Latifu 

Ya-Lilahi Ya-Satari, tusitiri Ya-Latifu, 
Tupe nyoyo za swaburi, penye miswiba na khofu, 
Duniani tupe kheri, na akhera makundufu, 
Kila baya na machafu, twepushiye Ya-Allahu. 

Twaani mwako tudumu, twakuomba Ya-Jalali, 
Swala zetu na swaumu, twaomba uzikubali, 
Ria na kila haramu, ututenge navyo mbali, 
Adhabu ndogo na kali, twepushiye Ya-Allahu. 

Tupe mema duniani, na akhera tupe mema, 
Usitutiye motoni, twakuomba Ya-Karima, 
Utuingize peponi, pamwe na wajao wema, 
Shetani na zake njama, twepushiye Ya-Allahu. 

Twaubata ya nasuha, majaaliwa ya kheri, 
Tutende yaloswahiha, uyapendayo Kahari, 
Kesho nyumba ya furaha, twingize tusitakhari, 
Dunia yenye ghururi, twepushiye Ya-Allahu. 

Na dini ya Islamu, iliyo dini ya kweli, 
Na Mtumeo mwangamu, Muhammadi Rasuli, 
Zimuendee salamu, Yeye na yake ahali, 
Kila jambo la batili, twepushiye Ya-Allahu. 

Wa Swalatu wa Salamu, zende kwa tumwa Nabiya, 
Uwapandishe makamu, Yeye na yake dhuriya, 
Jamii ya Islamu, wafuasi wote piya, 
Kesho mahali pabaya, twepushiye Ya-Allahu. 

(Mshairi - Bora), 
Amiri A.S. Andanenga (Sauti ya Kiza), 
S.L.P. 4775, Kinondoni - Shamba, 
Dar es Salaam. 



Ndoa ya mkeka (jibu) 

Hujambo nakusalimu, ndugu Zabibu I. Ng’onda, 
Na wote nawasalimu, Mwadui pia Mpanda, 
Swali lako muhimu, kuuliza umependa, 
Kazi kwao walimu, sasa wakaze mikanda, 
Ndoa hii ya mkeka, siyo ndoa si chochote. 

Watu wakutwa kizini, mnaitia balozi, 
Mwalimu haraka ndani, leo mambo yako wazi, 
Pia Sheikh karibuni, kushuhudia uzinzi, 
Jambo hili la kihuni, linanitoa machozi, 
Siyo ndoa si chochote, mwahalalisha zinaa. 

Usiku mwafunga ndoa, asubuhi ni talaka, 
Ndoa mwazitia doa, ama kweli mmechoka, 
Ati sasa mambo poa, ndoa imekamilika, 
Lo! Mnacheza na ndoa, bure mnakusanyika, 
Si ndoa ni upuuzi, kushangilia uzinzi. 

Ndoa huanza uchumba, wazazi wakafahamu, 
Sharia yake Muumba, hiyo na iwe muhimu, 
Wajitenge na umwamba, wa maficho kutuhumu, 
Mwisho mama naye baba, kuridhika ni muhimu, 
Ndoa hii ya kuwinda, ni upagani mtupu. 

Mwijilisti B.E. Dettu, 
S.D.A Kerege - Bagamoyo, 
c/o S.L.P. 60474, 
DAR ES SALAAM. 



Ndoa ya mkeka (jibu) 

Swali umeulizia, la ndoa ya mkekani, 
Kama hiyo ni sheria, imo ndani vitabuni, 
Au madhehebu pia, yanatambuwa udani, 
Mzinifu hataowa, ila mzinifu mwenza. 

Wengi hawana ridhaa, kwa kuupenda uhuni, 
Ndoa hii inafaa, kutokomeza ugoni, 
Majibu nakupatia, kwa ufupi wa maoni, 
Mzinifu hataowa, ila mzinifu mwenza. 

Zinaa sio sheria, aya zimo vitabuni, 
Tangu vilio tangulia, na ndani ya Qur’ani, 
Vipi unasuasua, maneno ya kitabuni, 
Mzinifu hataowa, ila mizinifu mwenza. 

Zabibu nakuambia, mzinifu maluuni, 
Tena ukifuatilia, hatufai mtaani, 
Wanawake huchukuwa, bila kuwa shariani, 
Mzinifu hataowa, ila mzinifu mwenza. 

Mashaka nakuondoa, kwa jibu la hapa chini, 
Ya mkeka nayo ndoa, sio ya dhehebu gani, 
Mungu ametuambia, ndoa ya huyo mzini, 
Mzinifu hataowa, ila mzinifu mwenza. 

Tamati natamatia, mzinifu tumlaani, 
Nawasubiri Mashia, waje wakupe undani, 
Kama utanibishia, uandike gazetini, 
Mzinifu hataowa, ila mzinifu mwenza. 

Zuberi Mohammed Mwinyi (Amir) 
P.O. Box 61428, 
DAR ES SALAAM. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma

Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha

Matokeo ya Darasa la Saba yacheleweshwa kusherehekea sikukuu ya Krismasi: Wananchi wahoji je, nchi hii ina dini moja tu?

Njaa yaikumba Kilwa

Dondoo za Saikolojia
Na. Abu Halima Sachangwa

Kona ya Wacha Mungu
Mavuno yangu yasiwe...

Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana huyoo!
Na Sompo wa Kahambwe

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897)

Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Imetayarishwa na Africa Muslims Agency

Marekani ni mtetezi au adui wa haki?: Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Na Abu Salim

Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Na Habiba Swedi, Arusha

Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an

Ijue  Madrasa Hudaa Arusha

Wazazi waaswa kutoshabikia maovu

Mzee maarufu afariki Moro

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? (jibu) 
Na Ally Said

Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani?

Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Na Habiba Swedi

Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar

Baada ya kuvunjiwa nyumba, kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Na Q. Mtaita

Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile

Sayansi na Teknolojia 
[Kuunganisha Kompyuta kwa Kutumia Modem

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Saumu na lishe ya mama anayenyonyesha] 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita