|
|
| Msiitupie
lawama serikali - Dk. Omar
Asema kaeni nayo
kama kuna tatizo
MAKAMU wa Rais Dk. Omar Ali Juma amewataka Waislamu kukaa pamoja na serikali kila wanapohisi kuna tatizo lolote lililojitokeza kati yao na serikali yao. Dk. Omar amesema kwamba kubaki pembeni na kuanza kuitupia lawama serikali sio njia sahihi ya kutatua matatizo. Makamu wa Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Shirika la Kimataifa la Kidini iliyofanyika jijini hivi karibuni alisema kwamba asingependa kusikia Waislamu wananung’unika. Na hivyo akawahimiza kuwa karibu na kuongea na serikali yao. Naye Waziri wa Elimu na Utamaduni Profesa Juma Athumani Kapuya amewalaumu Waislamu kwa tabia ya kuanzisha mataasisi yenye malengo mazuri bila ya kuwepo utekelezaji. Alhaj Kapuya alisema kuwa tatizo hilo linatokana na ubinafsi wa wengi wanaoanzisha taasisi hizo bila kujali mwelekeo mzima wa Uislamu na Waislamu katika karne hii ya 21 ya sayansi na teknolojia. "Nakumbuka niliposema kule Bagamoyo kwa nia njema kwamba Waislamu wana agenda gani katika karne hii ya 21 nikaeleweka vibaya", alisema Profesa Kapuya na kuwataka Waislamu wazingatie kuwa matatizo yanayomgusa Muislamu mwenzao pia yawaguse na wao bila kubagua. Sherehe hizo za uzinduzi wa Shirika hilo lijulikanalo kama Muslim
World Congress ziliandamana na vijana wa Kiislamu kutoka Dar es Salaam
na visiwani Zanzibar kuhifadhi Qur’an tukufu ambapo zawadi mbalimbali zikiwemo
fedha taslimu zilitolewa kwa washindi.
Baada ya kuvunjiwa nyumba, kuchomewa vyakula na Serikali.. Nzasa sasa wafuturu Maembe WANANCHI wa Nzasa katika wilaya ya Ilala jijini wanakabiliwa na hali ngumu katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani kutokana na ukosefu wa futari na daku. Hayo yameelezwa na Bw. Khamis Issa Ulende alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni. Akizungumza kwa masikitiko makubwa, Bw. Khamis amesema kwamba matatizo wanayoyapata katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani yametokana na kitendo cha serikali kuwachomea nyumba zao pamoja na akiba zao za vyakula. Bw. Khamis ambaye ni miongoni mwa viongozi wanaoshughulikia masuala ya wana Nzasa walio chomewa nyumba zao. Amesema anawaomba watu binafsi na mashirika kuwapatia vyakula ili kuwarahisishia ugumu wanaokumbana nao hasa katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani. Amesema kutokana na hali ngumu inayowakabili, inafikia mtu kufuturu kwa embe daku embe na kesho yake kuendelea kufunga hivyo hivyo. Wakati huo huo, Waislamu wanaoishi Nzasa ambao ni katika wale waliochomewa nyumba zao wanaweza kukosa sehemu ya kuswalia kutokana na Msikiti wao kukosa paa. Bw. Khamis Issa akiongea kwa niaba ya wenzake amewataka Waislamu sehemu mbalimbali nchini kuwasaidia ili waweze kupata mabati ya kuezekea Msikiti wao huo. Wananchi wa kijiji cha Nzasa walichomewa nyumba zao mwanzoni mwa mwezi
Oktoba mwaka jana na kuwafanya wakose sehemu ya kuishi na kulazimika kuhama
katika eneo hilo.
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur’an - Sheikh Kilemile IMEELEZWA kuwa lengo kuu la kuteremshwa Qur’an tukufu ulimwenguni ni kuja kuleta mabadiliko dhidi ya mifumo ambayo wanadamu wameamua kuibuni ili iwaongoze katika maisha yao ya kila siku hapa duniani. Aidha, Waislamu wamepewa changamoto kwamba lau wangeliifanya Qur’an kuwa ndio mwongozo wa maisha yao ya kila siku wasingekuwa katika hali ya unyonge inayowakabili hivi leo. Hayo yalisemwa na Sheikh maarufu nchini, Sheikh Suleimani Amrani Kilemile alipokuwa akitoa Wa’adhi wa fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhani katika sherehe za uzinduzi wa shirika la Kiislamu la Kimataifa la World Muslim Congress tawi la Tanzania Musabaqa wa kuhifadhi Qur’an tukufu zilizofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam. Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Makkah, nchini Saudi Arabia lilizinduliwa Jumapili ya Desemba 27, mwaka jana, mbele ya halaiki ya Waislamu wa Jijini Dar es Salaam na mikoani na Makamu wa Rais, Dk Omar Ali Juma. Akinukuu mara zote katika kila nukta ya maelezo yake aya za Qur’an tukufu zilizo katika sura tofauti zinazotilia mkazo mada yake, Sheikh Kilemile alisema jambo kubwa ambalo Waislamu wanapaswa kulikumbuka katika mwezi huu mkutufu wa Ramadhani ni kushuka kwa Qur’an ndnai ya mwezi huu ambayo alisema imeteremshwa na Allah (s.w.) ili kuja kuleta mabadiliko ya taratibu za maisha ambazo watu wameamua kujitungia. Sheikh Kilemile alisema hali ya Waislamu leo kuwa nyuma kimaendeleo katika nyanja zote za maisha kamwe haitokani na kuifuata kwao Qur’an tukufu kama wanavyoeneza propaganda hio maadui wa Uislamu. Lakini alisema chanzo kikuu cha kuwepo kwa hali hiyo kinatokana na makosa ya kutokuifanya Qur’an isiyokuwa na shaka ndaniyake kuwa ndio mwongozo wa maisha yao ya kila siku. "Ndugu Waislamu, tatizo kubwa hapa tumeifanya Qur’an kuwa ni kitabu cha kusoma basi na siyo kwamba ni mwongozo wetu wa maisha. Inatakiwa pia tuifanyie kazi ili kutoa matunda yake", alisema Sheikh Kilemile. Aidha, Sheikh Kilemile aliwakumbusha Waislamu umuhimu wa kuitumia fursa hii ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuzidisha kutenda mambo ya kheri kwani alisema fadhila nyingine za mwezi huu ni Waislamu kuwa karibu zaidi ya Allah (s.w.) ambapo Muislamu kufanya faradhi moja ndani ya mwezi huu huandikiwa kama mtu aliyefanya faradhi sabini na sunna moja kama faradhi moja. |
YALIYOMO
Tahariri Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha Dondoo za Saikolojia
Kona ya Wacha Mungu
Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana
huyoo!
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Marekani ni mtetezi au adui wa haki?:
Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an Wazazi waaswa kutoshabikia maovu Je, hivi tuendelee kushika amri za
Mungu tena? (jibu)
Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani? Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar Baada ya kuvunjiwa nyumba,
kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|