|
|
Kufuatia
mauaji holela ya raia wasio na hatia:
Aidha, wametaka kujua ni taratibu gani zinachukuliwa ili kuilipa fidia familia ya marehemu. Wamesema kwamba Bw. Dossa Salim asifanywe muhanga aliyetolewa roho yake bila ya sababu yeyote ya haki au ya kisheria. Kwa hiyo, serikali inawajibika kuilipa fidia familia ya marehemu. Dukuduku hilo la wananchi limekuja kufuatia ukimya uliofuatia toka kuuliwa kwa Bw. Dossa Salim. Bw. Dossa Salim aliuliwa na askari kwa kupigwa risasi kichwani (kisogoni) na kutokea usoni. Wakiongea na mwandishi wa habari hizi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Arusha, wananchi walikielezea kitendo hicho kama cha kizembe na kinyama kwani hakikutarajiwa kwa Polisi kufyatua risasi ovyo mbele ya raia bila kujali. Bw. Ahmad Lesika wa Msikiti wa Bondeni akitoa maoni yake juu ya tendo hili la kinyama alisema kwamba, familia ya Bw. Dossa imepokonywa mlezi na muangalizi wake kwa uzembe na utendaji mbovu wa kazi wa vyombo vya Dola. Na kuongeza kwamba ni lazima Dola iwalipe fidia mke na watoto wa marehemu. Alisema kwamba, fidia vyovyote itakavyokuwa haiwezi kuwa badala ya roho ya mtu, lakini ni lazima serikali iwajibike kuwapa kiliwazo waathirika. Naye Bw. Jamal Lubuva wa Ngaranaro alisema kwamba, serikali ina kawaida ya kujifanya bubu na kiziwi watendaji wake wanapowahujumu wananchi. Matokeo yake watendaji hao wanazidi kuwa vichwa maji na wananchi kuzidi kukosa imani na serikali yao. Alitoa mifano kadhaa ambapo ama polisi waliua au kuwajeruhi wananchi bila sababu zozote za msingi na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao. Katika hali hiyo, amesema kwamba wananchi hulazimika kujenga dhana ya kuonewa na kudhulumiwa na serikali yao. Kwa upande mwingine amesema vitendo vya kinyama vinavyofanywa na polisi dhidi ya wananchi vitazidi kuongezeka kama hakuna hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya polisi wazembe. Naye Abu Islamu amewataka Waislamu wa Arusha na wa nchi nzima; kwamba pamoja na kuisaidia familia ya Bw. Dossa kupata riziki yao hasa katika mwezi huu wa Ramadhani, lakini pia wasaidie familia hiyo kudai haki yao ya kulipwa fidia. Bw. Abu Islam amewataka Waislamu wa Arusha kuwa madhali wamejitolea kuisaidia familia yake katika mwezi huu wa Ramadhani basi waunde Kamati ya kudai haki ya fidia ya marehemu ili mke na watoto alioacha marehemu wapate uhakika kuendesha maisha yao. Bw. Dossa Salim mkazi wa Matejoro alipigwa risasi na kufa hapo hapo na askari aliyekuwa akimkimbiza mahabusu aliyetoroka akiwa chini ya ulinzi. Baada ya kifo chake maiti yake ilichukuliwa na polisi na kuhifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru ambapo mazishi yake yalifanyika kesho yake. Mke wa marehemu Bi. Zena Said ameeleza kuwa marehemu mumewe alikuwa akipita njia katika eneo la karibu na mahakama ya mwanzo Makoromboso ambapo askari alifyatua risasi ovyo akizielekeza alikokimbilia mahabusu. Bi. Zena alisema kuwa risasi moja ilimpata mumewe kichwani akaanguka chini kifudifudi damu nyingi zikimtoka. Alisema kuwa alimwangukia mumewe hata hivyo askari wakamtoa kwa nguvu wakamwacha pale huku wakiondoka na maiti ya mumewe. Marehemu Dossa Salim ameacha mjane na watoto saba na wa mwisho wao akingali ananyonya. Tendo hili la mauaji ya raia limetokea siku chache tu tangu kufanyika kwa kikao cha maafisa wa polisi huko Zanzibar ambako viongozi wa juu serikalini waliasa juu ya uadilifu wa askari wanapokuwa kazini ili kujenga imani kwa raia. |
YALIYOMO
Tahariri Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha Dondoo za Saikolojia
Kona ya Wacha Mungu
Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana
huyoo!
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Marekani ni mtetezi au adui wa haki?:
Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an Wazazi waaswa kutoshabikia maovu Je, hivi tuendelee kushika amri za
Mungu tena? (jibu)
Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani? Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar Baada ya kuvunjiwa nyumba,
kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|