AN-NUUR 
Na.182 Ramadhan 1419, Januari 1 - 7, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
 
Na Habiba Swedi, Arusha

IKIWA imebakia takriban mwaka mmoja na siku kadhaa, akipenda Allah (s.w.) tutaingia katika karne ya 21, maarufu kwa jina la karne ya sayansi na teknolojia na dunia iko katika pilikapilika za maandalizi ya kuifikia karne hiyo. 

Hata hivyo, ndani ya pilikapilika hizo, kuna kitendawili ambacho kwa wanasayansi kimekuwa kigumu na majibu yanayotolewa ni ya ubabaishaji tu, ndipo Waislamu mkoani hapa wamejipatia mji wa kukitegua kitendawili hicho sambamba na hizo pilikapilika za kuingia karne ya 21. 

Wakiongea na AN-NUUR kwa nyakati tofauti mara tu baada ya kufanyika kwa sherehe za kuadhimisha siku ya ukimwi duniani, hapo Desemba Mosi, waumini hao wamedai kwa kujigamba kabisa kuwa dawa ya ukimwi wanayo Waislamu ndani ya kitabu chao cha Qur’an kadhalika katika sunna ya Mtume Muhammad (s.a.w.). 

Sheikh Issa Ally ambaye ni Sheikh wa Mtaa wa Daraja II alisema kuwa, Allah (s.w) aliposema katika Qur’an sura ya 17 kwamba "Msiikaribie zinaa" alikuwa anafahamu madhara yake kwa wanaadamu na kwamba hizi kampeni za kuutokomeza ukimwi hazitafanikiwa hadi pale wanaadamu watakaporejea kwa Mola wao. 

Naye Sheikh Athumani S. Chalaa pamoja na kusisitiza yaliyosemwa na Seikh Issa aliongeza kuwa pamoja na dunia kudai inaadhimisha siku ya ukimwi kila ifikapo Desemba Mosi ya kila mwaka, bado ukimwi utaendelea kuwepo na tena utaongezeka kwa kasi kubwa sana endapo wanaadamu hawatarejea kwa Mola wao kwa kuifuata Qur’an na sunna kwa vitendo. 

Aidha, alisema, kwa ufahamu wake, neno kuadhimisha ni kukumbuka katika namna ya kutukuza, hivyo akahoji katika kukumbuka janga la ukimwi kinachotukuzwa ni nini? 

Sheikh Athumani alizidi kufafanua kuwa katika kuadhimisha siku ya ukimwi duniani, hufanywa sherehe zinazoambatana na mambo mbalimbali kama vile kuonyesha filamu za walioathika na ukimwi, ngonjera, mashairi hata ngoma na dansi zikiimbwa na kuchezwa nyimbo zinazozungumzia jambo hilo. 

Hapo Sheikh Athumani alisema Mwenyezi Mungu (s.w.) anaangalia tu sherehe hizo zinazoonyesha kana kwamba linafurahiwa janga hilo. 

Sheikh huyo alidadisi ya kuwa kwanini wanaadamu hawahuzuniki na kuendesha kampeni za kumlilia Allah (s.w.) ili ipatikane nusra kutoka kwake na Qur’an ikafuatwa kimilifu? 

Akizungumzia suala la matumizi ya kondom, Ustadh Mohammed S. Kakima wa Unga Limited alisema kuwa hazizuii chochote zaidi ya wanaosisitiza matumizi yake kuwahamasisha waja kuzini. 

Alinukuu Qur’an kwa kusema kwamba sura ya 17 aya ya 32 Mwenyezi Mungu (s.w.) amesema "Wala msiikaribie zinaa, hakika hiyo (zinaa) ni uchafu na ni njia mbaya (kabisa)". 

Aliongeza pia kwamba zinaa inaleta mambo mengi mabaya, ndio sababu Allah (s.w.) ameikataza, lakini mwanaadamu anaona maneno ya Mola wake hayafai na badala yake akabuni njia ili aweze kuzini zaidi. 

Kwa pamoja Masheikh hao waliwataka Waislamu kuitangaza kwa sauti kubwa dawa hiyo (Qur’an na sunna) kama ndio dawa pekee ya kuzuia na kuponya ukimwi kwani wamesema Mwenyezi Mungu amesema katika Qur’an sura ya 17:82 :"Natumeiteremsha Qur’an (mafundisho yake ambayo ni) ponyo (poza la moyo) na Rehema kwa wanaoamini, wala hayawazidishii (mafundisho haya) madhalimu ila khasara". 

Kwa mujibu wa Masheikh hao, wale wasioamini maneno ya Mwenyezi Mungu ndio hao wanaouingiza umma huu bora katika matumizi ya vifaa visivyofaa (kondom) ili kuhalalisha uchafu na kubuni sherehe zinazowachanganya wanawake (pasipo stara) na wanaume kuufurahia ugonjwa badala ya kuhuzunika. 

Kadhalika, waliwataka viongozi wa dini hususan ya Kiislamu, kuamrisha mema na kukemea maovu na wawe pia kioo cha uadilifu kwa wafuasi wao katika kuipiga vita zinaa. 

Zinaa itakapokoma Masheikh hao walisisitiza kuwa walioambukizwa ugonjwa huo watakufa, na wale wote wenye virusi wataugua hatimaye kufariki, walioipa mgongo zinaa watanusurika na hapo ndipo ukimwi utakwisha na kubakia dunia yenye wacha Mungu. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma

Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha

Matokeo ya Darasa la Saba yacheleweshwa kusherehekea sikukuu ya Krismasi: Wananchi wahoji je, nchi hii ina dini moja tu?

Njaa yaikumba Kilwa

Dondoo za Saikolojia
Na. Abu Halima Sachangwa

Kona ya Wacha Mungu
Mavuno yangu yasiwe...

Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana huyoo!
Na Sompo wa Kahambwe

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897)

Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Imetayarishwa na Africa Muslims Agency

Marekani ni mtetezi au adui wa haki?: Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Na Abu Salim

Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Na Habiba Swedi, Arusha

Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an

Ijue  Madrasa Hudaa Arusha

Wazazi waaswa kutoshabikia maovu

Mzee maarufu afariki Moro

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? (jibu) 
Na Ally Said

Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani?

Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Na Habiba Swedi

Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar

Baada ya kuvunjiwa nyumba, kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Na Q. Mtaita

Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile

Sayansi na Teknolojia 
[Kuunganisha Kompyuta kwa Kutumia Modem

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Saumu na lishe ya mama anayenyonyesha] 
 


Baraza ya Wasomaji
(Kwa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu)

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita