AN-NUUR 
Na.182 Ramadhan 1419, Januari 1 - 7, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Saumu na lishe ya mama anayenyonyesha

Na Mujahid Mwinyimvua

KATIKA makala yetu ya chakula na lishe ya wiki iliyopita tulijifunza saumu na lishe ya mama mjamzito. Makala hiyo ni mfululizo wa masomo maalumu ya chakula na lishe kwa wasomaji wetu Waislamu wanaoendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika kuendeleza lengo hilo, makala ya juma hili inatazama saumu na lishe ya mama anayenyonyesha. 

Tulijifunza katika makala ya wiki iliyopita kuwa mama aliyekwishajifungua (anayenyonyesha au la) wanaruhusiwa na sheria ya dini ya Kiislamu kuahirisha funga zao. Kwa maneno mengine wanaruhusiwa kula mwezi wa Ramadhani na watawajibika kulipia siku zao wakati hali zao zitakapokuwa za kawaida. Hata kama zitakutana Ramadhani mbili kama sababu ya kutokufunga bado ipo atazilipia siku za mbele. 

Baadhi ya kina mama wa Kiislamu wamekuwa wakisita kuitumia ruhusa hiyo (ya kuahirisha kufunga) kwa hoja dhaifu. 

Kwa mfano, wapo kina mama wa Kiislamu (wenye mimba hata za miezi minane) ambao wanafunga kwa hoja kuwa hawawezi kulipia katika siku ambazo hakuna wengine wanaofunga. 

Sheria ya dini ya Kiislamu imewapa kinamama wenye mimba na wanaonyonyesha (na Waislamu wenye nyudhuru nyingine) uhuru wa kufunga au kuahirisha funga kwa hoja kwamba watazame afya za watoto wao (wanaonyonya au wale walio tumboni). 

Kwa hiyo, kudai kuwa ukiahirisha saumu itakuwa tabu wakati wa kuilipa kwa sababu hakuna watu wengi watakaokuwa wanafunga kama ilivyo wakati wa mwezi wa Ramadhani ni makosa. 

Sambamba na hoja hiyo, swala la kuathirika kiafya kwa mama mjamzito (au anayenyonyesha) na mtoto wake aliyetumboni (au aliyekwisha zaliwa) tunaweza kulilinganisha na mvuta sigara au anayekunywa pombe. 

Mvuta sigara au mnywa pombe si rahisi mwanzoni kuona anavyoathirika na na ndiyo maana wapo wanaodai kuwa mbona afya zao ni sawa au bora zaidi ya wale wasiovuta sigara au kunywa pombe! 

Lakini kadiri siku zinavyokwenda inafikia mahali mvutaji sigara au mnywaji pombe anaona athari mbaya ya "kazi" yake ya uvutaji au ulevi. 

Halikadhalika, mama mjamzito au anayenyonyesha anaweza kuiona athari ya yeye kufunga katika mwili wake au kwa mtoto. 

Kwa mfano, mama mjamzito au yule anayenyonyesha asipopata lishe ya kutosha (hata kwa masaa kumi na nne au zaidi kidogo kama ilivyo katika funga) anaweza kuathiri ukuaji wa mtoto kiakili. 

Athari kama hiyo mama hawezi kuiona kwa macho yake. Kwa hiyo, ushauri wa watalaamu wa afya, tiba na lishe lazima uheshimiwe. 

Baada ya utangulizi huo, ni vyema sasa tukarudi katika kiini cha makala yetu ya wiki hii. 

Lishe bora ya mama baada ya kujifungua ni jambo la muhimu sana. Hii ni kwa sababu mama huyo anahitaji kurekebisha mwili na hali yake ya lishe iliyoathirika wakati wa ujauzito. 

Zaidi ya hayo, hali nzuri ya lishe ya mama itauwezesha mwili wake kujilinda na maradhi na vile vile mwili kuweza kutoa maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto wake mchanga. 

Baada ya kujifungua mama anahitaji kula vyakula vya mchanganyiko. Vyakula hivyo ni: Vyakula vya kujenga mwili kwa mfano, nyama, samaki, maharage, kunde, njegere, choroko, dengu, mbaazi, n.k. 

Vyakula vingine ni vile vya kutia nguvu na joto mwilini kama vile mahindi, mtama, uwele, ulezi, mpunga, ngano, ndizi za kupika, viazi, mihogo, asali, mafuta, n.k. 

Pia kundi lingine la vyakula ni vile vya kulinda mwili kwa mfano matunda na mboga za majani za aina mbalimbali. 

Mama anayenyonyesha anahitaji mlo wa mchanganyiko tuliouona hapo juu. Lazima apate milo ya aina hiyo mara nne au zaidi kwa siku. Pia ale chakula zaidi ya kile anachokula siku za kawaida. 

Ni matarajio yangu kuwa baada ya maelezo ya hapo juu, hikma ya sheria ya dini ya Kiislamu ya kuwaruhusu kina mama wanaonyonyesha kuahirisha saumu zao iko wazi. Hivyo basi, na tuipokee. 

 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri 
Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma

Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha

Matokeo ya Darasa la Saba yacheleweshwa kusherehekea sikukuu ya Krismasi: Wananchi wahoji je, nchi hii ina dini moja tu?

Njaa yaikumba Kilwa

Dondoo za Saikolojia
Na. Abu Halima Sachangwa

Kona ya Wacha Mungu
Mavuno yangu yasiwe...

Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana huyoo!
Na Sompo wa Kahambwe

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897)

Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Imetayarishwa na Africa Muslims Agency

Marekani ni mtetezi au adui wa haki?: Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Na Abu Salim

Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Na Habiba Swedi, Arusha

Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an

Ijue  Madrasa Hudaa Arusha

Wazazi waaswa kutoshabikia maovu

Mzee maarufu afariki Moro

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? (jibu) 
Na Ally Said

Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani?

Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Na Habiba Swedi

Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar

Baada ya kuvunjiwa nyumba, kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Na Q. Mtaita

Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile

Sayansi na Teknolojia 
[Kuunganisha Kompyuta kwa Kutumia Modem

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Saumu na lishe ya mama anayenyonyesha] 
  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita