|
|
|
Umoja wa Mataifa upo upande gani? KWA muda mrefu Marekani imekuwa ikijenga hoja ya vitendo vyake vya kuvamia nchi za watu kuwa vinatokana na msimamo wake wa sera za kutetea demokrasia na haki za binadamu ulimwenguni. Kwa kutumia hoja hiyo imejipa kazi ya kuwa "polisi" wa kimataifa. Lakini vitendo vyake vingi vinaonekana kuwa upolisi wake umekuwa wa kujipangia madaraka ya kuamua nani mhalifu na achukuliwe hatua gani, bila ya kusubiri maelekezo ya wakubwa wake. Katika mazingira yetu, Marekani ilibidi kuusikiliza Umoja wa Mataifa. Lakini sivyo ilivyofanya kuhusu Iraq. Marekani ilijiamulia kuivamia Iraq kwa niaba ya Umoja huo kabla ya Umoja huo kutoa amri ya kufanya walichokifanya Iraq. Lakini kitendo cha Marekani dhidi ya Iraq kinaonesha kuwa nchi hyo haina sifa ya kuwa mtetezi bali ni dhalimu wa haki za binadamu na adui hususan kwa Waislamu. Mara tu baada ya kuanza mashambulizi yao Iraq hivi karibuni Marekani iliwahi kutamka kabla ya kufuta kauli yake hiyo kwamba ingelisitisha mashambulizi hayo kwa kuheshimu mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waliyatamka maneno hayo utadhani ilikuwa halali kuua na kuharibu mali za watu katika miezi isiyokuwa ya Ramadhani. Matamashi hayo bila shaka waliyatoa kwa kujua kwamba mabomu yao yalikuwa yakiwaua Waislamu ambao ni zaidi ya asilimia 90 nchini Iraq. Marekani walitamka vile pengine kwa kujua kwamba Waislamu na watu wema ulimwenguni kote wangelishangaa wao kuwaua watoto wa wenzao katika kipindi ambacho Marekani yenyewe walikuwa wakiwaandalia watoto wao zawadi nzuri - nzuri za Krismasi. Na kwa hakika inaelekea sitisho lao la kuishambulia Iraq baada ya kusahihisha kauli yao ya awali na kusisitiza kuwa wasingejali kuendeleza mashambulizi ndani ya mwezi wa Ramadhani, sitisho hilo lilifanywa ili kutoa nafasi kwa wanajeshi wake ambao wengi wao ni Wakristo, wapate kusherehekea sikukuu ya Krismasi. Mtu mwenye sura mbili; moja ya kuua watoto wa wenzie katika kipindi adhimu cha imani ya dini yao, na nyingine ile ya kuwanunulia wanae zawadi nzuri-nzuri za Krismasi na kuwaombea maisha marefu, hawezi kuwa mtetezi wa haki za binadamu. Sifa ya binadamu hutokana na vitendo vyake. Kama ilivyo kwa anaekufuru huitwa Kafiri, anayedhulumu haki ya kuishi binadamu wenzie, ni dhalimu na anastahiki kuitwa hivyo. Lakini mtu anaweza akajiuliza, vipi mtu kama huyu (Marekani) anaweza akatamba na kujigamba kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu licha ya vitendo vyake hivyo vya kidhalimu na watu wakamshangilia? Hali hiyo inawezakana kuwepo kutokana na kustawi kwa unafiki katika mazingira yetu ya jamii ikiwemo na ile inayoitwa Jumuiya ya Kimataifa. Wamo watu katika jamii wanaojiita waumini wa dini lakini huutizama kwa mfano, Uislamu kama klabu shindani katika kombe la dunia. Hawa hushangilia kuuliwa kwa Muislamu sawa na wale wanaoshangilia klabu pinzani inapopoteza mchezaji wake wa kutumainiwa katika mashindano. Kila anapouliwa Muislamu, watu hawa huwa wa kwanza kujitokeza na kwenda huko na huko wakijenga hoja ya kuhalalisha mauaji yale kiasi cha kumshangilia na kumsifu dhalimu. Mifano hiyo ni mingi hapa kwetu. Hawa ndiyo watu wanaommiminia sifa asizostahiki Marekani na kumuita mtetezi wa haki za binadamu kila anapodhulumu roho za binadamu wenzake. Kuhusu suala la Iraq, Marekani iliivamia nchi hiyo kwa kisingizio cha kuilazimisha itekeleze azimio Na. 687 la Umoja wa Mataifa, ambalo linaitaka Iraq kuruhusu wakaguzi wa silaha kali kuipekua nchi hiyo na kuziangamiza silaha hizo. Lakini Iraq imekuwa ikiuruhusu ujumbe wa Umoja wa Mataifa upatao zaidi ya watu ya 30 kuikagua nchi hiyo kwa kipindi cha miaka minane. Na katiak kipindi hicho watalaamu hao wa Umoja wa Mataifa ambao wengi wao ni Wamarekani, wamekuwa wakiipekua nchi nzima bila kuona wanachotafuta. Kile kinachodaiwa ukaidi wa Iraq katika kuruhusu tume hiyo kufanya kazi yake ni maswali ambayo Iraq, Umoja wa Mataifa na Marekani ambayo inaelekea kujipa madaraka ya kuwa msimamizi wa Umoja huo. Maswali ambayo wote wameshindwa kuyajibu. Maswali yenyewe ni je, wakaguzi wale ni watalaam kweli wenye uwezo wa kukiona hicho wanachokitafuta? Kama ni watalaam mbona kwa muda wa miaka hiyo na baada ya kupekuwa kila eneo la nchi bado hawaamini macho yao kuwa hakipo wanachokitafuta? Na swali jingine ambalo watalaam hao wamekuwa wakiulizwa ni je, maeneo gani ya Iraq ambayo wao wanadhani hawajayapekua ili wapelekwe wapate kukamilisha upekuzi wao? Wasiwasi wa Iraq na watu wengi wenye kufikiri vyema ni kuwa Umoja huo na hasa Marekani imeshindwa kuona chochote lakini inaendelea kujenga kisingizio cha kutafuta vita ili ipate kuipiga mabomu nchi hiyo na kuwakandamiza wananchi wake chini ya utawala - ukoloni wa Marekani. Iraq wanayo haki ya kuwa na wasiwasi huo. Kwa sababu azimio hilo 687 la Umoja wa Mataifa limetaja haja ya kuondoa silaha kali katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Lakini Umoja huo haujaunda tume ya kwenda kuchunguza silaha hizo Uyahudi ambako imekuwa ikijilimbikizia silaha za Atomic na nyuklia kuanzia mwaka 1948. Katika suala hili la Iraq na suala zima la amani ya eneo ya Mashariki ya Kati, Umoja wa Mataifa kwa kuiachia Marekani kuwa msimamizi mshiriki wa mambo yanayohusu usalama wa eneo hilo, tayari imejipa sura ya ubaguzi dhidi ya Wapelestina na Waarabu kwa ujumla. Umoja huo unaonekana zaidi sasa kuwa upo chini ya Marekani na kuendesha masuala ya eneo hilo kwa manufaa ya Uyahudi. Kwa mfano maazimio kadhaa ambayo yalipitishwa na Umoja wa Mataifa kuitaka Uyahudi iachie maeneo ya Wapalestina na Waarabu ambayo inayakalia hayajatekelezwa. Lakini Umoja huo umekuwa butu. Hatuzioni jazba zake dhidi ya Iraq ilipoivamia Kuwait kuwa na mfano wowote wa msimamo wake wa upole na ubutu kwa Uyahudi inapovamia na kuuwa wananchi wa Lebanon. Mwaka 1982 Uyahudi ilifanya uvamizi mkubwa Lebanon, jeshi lake likauwa maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina waliokuwa katika makambi ya Sabra na Shatila katika eneo la Beirut. Lakini hapakuwepo na hatua zilizochukuliwa kama zile dhidi ya Iraq ilipoivamia Kuwait. Mwaka 1981 Uyahudi ilituma nduge zake na kuteketeza mtambo wa kinu cha kutengeneza nguvu za nishati Iraq. Kisingizio cha Mayahudi kilikuwa kuteketeza mtambo wa nyuklia. Shirika la Kimataifa la nguvu za nishati (International Atomic Energy Agency) lilichunguza madai hayo ya Uyahudi na kugundua kuwa ni uongo. Ilikichunguza kiwanda hicho na kuthibitisha kuwa hakikuwa chenye madhara yoyote. Lakini si Umoja wa Mataifa wala Marekani iliyochukuwa hatua yoyote dhidi ya Uyahudi kwa kitendo chao cha kuvamia Iraq na kuharibu mtambo wake wa nguvu za nishati. Mwaka 1973 Uyahudi ilituma ndege zake za kivita kwenda kuipiga ndege ya kiraia ya Libya iliyokuwa ikipita katika anga za Sinai, Misri na kuua raia wasafiri 111. Lakini hakuna jazba yoyote iliyofanywa au kuoneshwa na Umoja wa Mataifa kama inavyoonyesha kuhusu Libya kwa kuiwekea vikwazo nchi hiyo kutokana na tuhuma tu za eti raia zake waliitungua ndege ya Marekani katika anga za Lokerby Scotland mwaka 1987. Aibu kubwa kwa Umoja wa Mataifa ni pale Marekani inapovamia, kuua na kuharibu mali kisha ikawa si lolote si chochote! Meli ya kivita ya Kimarekani iitwayo "New Jersey" iliivurumishia Lebanon, kuua raia na kuharibu mali. Ikaamuliwa Kamanda wake akamatwe na kupelekwa mahakamani Lebanon. Marekani haikumtoa. Jazba za Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya kwa tuhuma za Lokerby hazikuonekana kwa Marekani. Marekani pia iliwahi kugoma kutekeleza uamuzi wa mahakama ya Kimataifa (Court of Justice) ambayo ni chombo cha Umoja wa Mataifa na haikuwa chochote. Uamuzi huo uliitaka Marekani iilipe fidia Nicaragua kutokana na uvamizi wake na kuharibu bandari ya Nicaragua kwa mabomu. Marekani inaweza ikakurupuka kwa kisingizio chochote kile na kuivamia nchi, kuua watu wake na kuharibu mali, kisha ikawa basi. Kitendo chake cha kuivamia Sudan pasipo ushahidi wa sababu kisha ikaangamiza kiwanda cha madawa cha nchi hiyo mara tu baada ya balozi zake kupigwa mabomu Tanzania na Kenya Agosti 1998, si cha kwanza. Mwaka 1986 Marekani ilituma ndege zake za kivita kuipiga Libya kwa kisingizio kuwa ilihusika na ulipuaji wa ukumbi wa Disko Ujerumani ambako mwanajeshi wa Marekani aliuawa. Katika shambulio hilo, raia 400 wa Libya waliuawa katika miji ya Tripoli na Benghazi, kati yao 104 watoto, 85 wanawake, 33 vilema na 41 wazee. Hatimaye ilikuja kugundulika kwa mujibu wa mtaalam wa sheria za kimataifa, Profesa Richard Falk wa chuo kikuu cha Princiton Marekani kuwa Libya hawakuhusika na kulipuliwa kwa ukumbi ule wa Disko. Ni dhahiri upo uadui wa Marekani dhidi ya haki za binadamu au Waislamu katika sura zao za Uarabu au Uswahili. Pamoja na wale wenye kujitokeza kutetea kikweli kweli haki za binadamu ulimwenguni. Ni jambo la kusikitisha kuwa katika ufisadi unaofanywa na Marekani, Umoja wa Mataifa unakubali kujitokeza kwa mashinikizo yasiyokuwa na msingi mbele ya wadhulumiwa. Mfano wa kusikitisha ni kuhusu azimio la Umoja huo Na. 661 ambalo liliiwekea vikwazo vya kiuchumi Iraq ili kuwalazimisha kutoka Kuwait. Lakini tangu Iraq itoke Kuwait Februari 1992 hadi leo Baraza la Usalama limekuwa ikijizungusha katika kuiondolea vikwazo nchi hiyo. Yote hayo yanafanywa kwa kuiridhisha Marekani ambayo haina huruma kwa
maisha na roho za wananchi wa Iraq. Na yanafanywa zaidi ili kuwafurahisha
Wayahudi na wlae wanaowatizama Waislamu kama wachezaji hodari wa klabu
pinzani.
|
YALIYOMO
Tahariri Kingunge, kweli upo uonevu na dhulma Wananchi wahoji kuhusu polisi aliyeua Arusha Dondoo za Saikolojia
Kona ya Wacha Mungu
Jicho la Uzalendo: Bhabhoo! Muungwana
huyoo!
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) Mafunzo kuhusu funga ya Ramadhani
Marekani ni mtetezi au adui wa haki?:
Umoja wa Mataifa upo upande gani?
Dawa ya ukimwi ni mwenendo mwema
Mwalimu Maif: Mwanamke aliyetumia maisha yake kufundisha Qur'an Wazazi waaswa kutoshabikia maovu Je, hivi tuendelee kushika amri za
Mungu tena? (jibu)
Mapinduzi, Muungano kwa manufaa ya nani? Fufueni EAMWS - Sheikh Amana
Msiitupie lawama serikali - Dk. Omar Baada ya kuvunjiwa nyumba,
kuchomewa vyakula na Serikali: Nzasa sasa wafuturu Maembe
Acheni mifumo mibovu, fuateni Qur'an - Sheikh Kilemile Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|