|
Mashairi
Wapemba ni watu gani?
1. Twambieni CCM, Wapembe ni watu gani,
Mmeishusha nidhamu, kuwatangaza wageni,
Kumbe wao Wazaramo, walohamia zamani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
2. Pemba mahali hadhimu, kapabariki Manani,
Pana mazao muhimu, tele tele mashambani,
Nayo matunda matamu, vile vile yapo ndani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
3. Mmanyema yupo humu, kahamia kisiwani,
Mnyamwezi mfahamu, yupo Pemba vijijini,
Kabila zote za humu, wapo huko visiwani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
4. Mwenyekiti CCM, Mkapa hana makini,
Wapemba kuwalaumu, kupenda CUF kwa nini,
Wameshindwa majukumu, wote tupo adhabuni,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
5. Zanzibar si adimu, wapo pia visiwani,
Hatuwezi kulaumu, ndugu zetu kwa yakini,
Makanisa yamo humu, kuabudu zao dini,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
6. Pemba ipo CCM, Wameweka watu gani,
Vipi mwaiweka sumu, watu hatuelewani,
Wenzetu wa CCM, mnatuweka kizani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
7. Miaka mingi imedumu, nchi imerudi chini,
Viongozi wote bomu, wananchi tambueni,
Kwakuigawa sehemu, ndugu zetu visiwani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
8. Sote tunakufahamu, atokako Salmini,
Omari Juma Makamu, ametoka nchi gani?
Amevua umhumu, ili akae kitini,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
9. Wahindi tunao humu, wapo Dodoma bungeni,
Hakuna atoshutumu, CCM “baniani”,
Waarabu kem kem, mwawabagua kwa nini?
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
10. Tunajua mahalumu, wapo tokea zamani,
Kwani twawafahamu, kuwa wao si wageni,
Bure mnakituhumu, eti kwamba cha udini,
CCM twambieni, Wapemba
ni watu gani?
11. Naiachia kalamu, taratibu NASAHANI,
Kina Cheyo muadhamu,
na Bob Bin Makani,
Lipumba mtaalam, wa
uchumi duniani,
CCM twambieni, Wapemba ni watu gani?
MTAGALUKA RASHID (Mtaaluma),
S.L.P. 16380, Dar es Salaam.
Siku ya Mwembechai
Siku ya MWEMBECHAI, Rabi yatuhuzunisha,
Hai fai fai fai, Rabi kutoadhimisha,
Dini yetu yatudai, wewe uliyepitisha,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
MWEMBE CHAI twaishika, wenzetu kuwakumbuka,
Damu iliyomwagika, ni vigumu kututoka,
Virungu nikikumbuka, mateke tukapigika,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Tarehe kumi na tatu, mwezi wa pili kumbuka,
Ilisikika MITUTU, wenzetu wakipigika,
Salehe twamkumbuka, Chuki nae asumbuka,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Si utu utu hakika, Mkapa hili kubisha,
Ya Makamba kuyashika, WAHUNI kutuvumisha,
Atatulipa Rabuka, kwake twajisalimisha,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
MWEMBE CHAI Tanzania, ni kubwa historia,
Kwamba tuliangamia, Islamu Tanzania,
TUME kamwe nawambia, sitoi hata fidia,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Kumbe sasa tunajua, ya kuwa mwatubaguwa,
Fundisho hili twajua, MWEMBECHAI yalokuwa,
Tu duni kwenu majua, mbwa juu amekuwa,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Damu damu pote damu, jamani ya hudhunisha,
Damu ya Waislamu, Mwembechai imeisha,
Katiba mwaidhulumu, HAKI kutoipitisha,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Mola nina nyingi hofu, ya CHAI yote kunena,
Hali yangu nidhaifu, wao wana nyingi zana,
Mimi kwao kuwa mfu, kwao ni rahisi sana,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
Rabi wa baba ADAMU, Nuhu na Ibrahimu,
Musa NA Issa Mwalimu, na wote Waislamu,
Rabi hao wasalimu, wambie kwako twadumu,
Piga yule piga yule, sauti ilisikika.
Tamati sasa nafika, sasa ninahitimisha,
Ni wapi sasa kufika,
Mwembechai kufikisha,
Sipaoni kwa hakika, juu tumeshafikisha,
Piga yule piga yule, muaji alisikika.
A.H. SHEMDOE, Dar es Saaam.
Fani yangu mashairi
1. Kwa jina lako Ghafuri, Muumba wetu Jalali,
Moyoni ninafahari, hadi leo kuvinjari,
Mimi ni Haji Bakari, mahili wa mashairi,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
2. Fani yangu mashairi, naipenda siyo siri,
Hata ukitafasiri, hilo utalibashiri,
Watu walinitabiri, kabla sijatunga hili,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
3. Sasa nikijivinjari, mahala penye wakali,
Kati ya wale wakali, kumi bora numerali,
Moja nisipohimili, nitashika namba mbili,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
4. Mi nilianza zamani, kuipenda hii fani,
Ila “wahenga” jamani, walinitoa manani,
Niliwekwa lawamani, na kunitoa thamani,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
5. Walinena hadharani, ni makida mchezoni,
Eti wenye hii fani, ni wakongwe wa zamani,
Nasema yaondosheni, mawazo ya kizamani,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
6. Nimefanya juu chini, kuhamasisha mijini,
Na hata huko swekani, kupitia NASAHANI,
Nasema “nasi tupeni”, uhuru wa hii fani,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
7. Vijana wengi nchini, waipenda hii fani,
Hebu leo tazameni, “vijana ndani ya fani”,
Wameingia fanini, juhudi zangu juweni,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
8. Wameingia fanini, juhudi zangu jamani,
Wengi wapo mashuleni, Fatma na miongoni,
Ukitaka kuamini, muangalia Mwapwani,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri.
9. Msanii chipukizi, Yusuphu kapata dozi,
Mariam Mkombozi, naye nilimpa dozi,
Wameshamaliza kozi, hawa sasa kazi kazi,
Fani yangu mashairi, nayapenda siyo siri,
10. Nakaribia mwishoni, kalamu naweka chini,
Malenga tuokoeni, vijana humu nchini,
Malenga wa kizamani”, simimbi zenu acheni,
Fani yangu mashairi, nayapenda
siyo siri.
Haji Bakari Nganenga na Ndukanagaye,
S.L.P. 20378, Dar es Salaam.
Dhulma tumeichoka
1. Naanza kwa jina lako, Mola uliyetukuka,
Twaomba rehma zako, ili tupate ongoka,
Rabbi sisi waja wako, Radhizo zahitajika,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
2. Sasa twawafahamisha, dhulma tumeichoka,
Twawambia yatutosha, yale yaliyotufika,
Japo mnayakanusha, kweli haitofichika,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
3. Ujumbe tunautoa, kwenu nyinyi wahusika,
Amri mnaotoa, madaraka mmeshika,
Hamna mnachotoa, tunazidi kudhikika,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
4. Udini umeenea, ubaguzi wafanyika,
Viongozi mwachekea, Isilamu nyanyasika,
Hamtaki kutetea, haki yetu mwafutika,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
5. Kwanza urongo acheni, maovu kutupachika,
Islamu si wahuni, kama mlivyoandika,
Kaeni mkibaini, mtakuja kuumbuka,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
6. Katiba ya kazi gani, iwapo mliandika,
Mnachokifanya nini, kuonewa tumechoka,
Na jueni kwa yakini, tutakapo tutafika,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
7. Kaeni mkitambua, na bado hatujachoka,
Haki tutaichukua, wakati utapofika,
Nanyi hili mwatambua, mtakuja fedheheka,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
8. Tamati namalizia, kwa uwezo wa Rabuka,
Kheri tatuingizia, kuomba hatutochoka,
Nuru tatuangazia, Ye siri yatafichuka,
Dhulma tumeichoka, ubaguzi nao pia.
Rahma Abdulrahmaan,
Dar es Salaam.
Siyo kinga ya Ukimwi
1. Mola kateremsha, Gonjwa hili la ajabu,
Waganga wamechemsha, wameshindwa kuutibu,
Mbinu zote zimekwisha, kila dawa mejaribu,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
2. Kondomu sio imara, hilo wengi wanakiri,
Labda kwa biashara, kidogo nitakubali,
Lakini sio sitara, gonjwa kulikabili,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
3. Mfano ni Amerika, na pia Uingereza,
Kondomu zinakotoka, ndiko watengeneza,
Huko gonjwa lasifika, wengi lawaangamiza,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
4. Vijana tuwe makini, katu tusijidanganye,
Waume nawanandani, viziwitusijifanye,
Wanetu tuwaonyeni, uwasharati, tuwakanye,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
5. Eti “tumia salama, ukimwi hutoupata”,
Tamko linaniuma, na moyo unanikita,
Mbele ya Baba na Mama, fedheha inatupata,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
6. Utani msidhanie, haya niyasemayo,
Kondomu tuziachie, sio kinga ifaayo,
Zinaa sijifanyie, hilo ndio zingatia,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
7. Hapa ninatia nanga, beti saba namaliza,
Watu tusiwe wajinga, ucha Mungu kupuuza,
Kondomu kamwe si kinga, bali gonjwa mwaeneza,
Kondomu sizihafiki, kuwa kinga ya ukimwi.
Mtagaluka Rashid (Mtaaluma),
S.L.P. 16380,
Dar es Salaam.
Ndoa muhimu
1. Mhariri saidia, ninaionya jamii,
Zisizo njema tabia, waache kuchekelea,
Na hasa wewe Zakia, wapumbazwa na Dunia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
2. Wengi waliokataa, kuolewa wajutia,
Walijiona ‘staa’, na maringo kujitia,
Zama wamesha zubaa, wamebakia kulia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
3. Ni “nusu ya dini” ndoa, vizuri kufurahia,
Dhambi unaziambaa, thawabu kukumbatia,
Vigezo vya kuolea, mtume katwelezea,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
4. Si kitu cha kukawia, bali cha kukimbilia,
“MSAUD” nawambia, “TAMUSSA” “DAMUSSA” PIA,
Kichelewa tajikwaa, majonzi kujatutia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
5. Nimekaa metulia, huku nimejinamia,
Uamuzi kanijia, niseme kuwazindua,
Ugali mboga dagaa, Mola ndie ajalia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
6. Chagueni walomea, vizuri wakatulia,
Sio warukaji njia, Hancha ninakataa,
Sifa tajivurugia, si Dodoma sio Daa,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
7. Kwanini mwajipangia, mahari iliyopea,
Watu wakajishindia, zinaa kujifanyia,
Kweli tutaangamia, tusipolifikiria,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
8. Vema si kupendelea, “matirio” Bi Zakia,
Dini ukaiachia, ujinga kujitapia,
Siku ikijatimia, nini utamuambia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani na Akhera.
9. Beti tisa naishia, witiri nimezoea,
Salamu nawatumia, Issa, Asha na Safia,
“Allah” akitujalia, chuoni natazamia,
Ni jambo muhimu ndoa, Duniani
na Akhera.
Hancha, A.S. (Mujadilu),
S.L.P. 2036, Dodoma.
|
YALIYOMO
Tahariri:
Mkataba
wa Muungano wa 1964 usifanywe siri
Serikali
inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF
Waislamu
kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili
Wazanzibar
sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano
Wanawake
wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia
Rufaa
za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji
Makala
Hotuba
ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Hassan Mussa Takrima katika
maadhimisho ya miaka 23 ya CCM
MAKALA
Uhuru
na ukombozi
MAKALA
Suala
la Dk. Salmin kubadili katiba:
Wasomi
wafichua siri ya Muungano
Kalamu
ya Mwandishi
Wazanzibari
unganeni
Makala
UPINZANI
OCTOBA 2000 - 2
USHAURI
NASAHA
Matitizo
ya ajira, Nini kifanyike?
MAKALA
Mgogoro
wa kisera ndani ya CCM usigeuzwe kuwa ni wa kitaifa
HABARI
ZA KIMATAIFA
Wachechnya
wapania kuidhibiti upya Grozny
Wanaoacha
umalaya wagawiwa fedha Zamfara
n.k
Riwaya
Ndoto
ya ajabu
LISHE
Umuhimu
wa mafuta mwilini
Barua/Maoni
MASHAIRI
MICHEZO
Ligi Kuu
sasa kuchezwa kwa makundi
Simba
kuipa Prisons mazoezi leo
Michuano
ya soka Mataifa ya Afrika |