|
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Hassan Mussa Takrima katika maadhimisho ya miaka 23 ya CCM MHESHIMIWA Makamu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, pia ukiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bara la Mapinduzi, waheshimiwa viongozi wote wa chama na serikali na mama Salma.Kwanza nadhani akina mama simnajua kwamba Kamandoo kafuatana na mlezi mkuu? Mnajua hamjui? Basi hebu nione basi kama kweli mnajua...Sawa kwa hiyo mnajua kuwa na mama Salma yupo. Inabidi nitoe shukrani zangu za dhati kwa wananchi wote mliohudhuria hapa, napenda kumshukuru ndugu Nashad kwa msaada wake, lakini kwa kweli kazi niliopewa hapa muda ni mfupi tunahitaji Komandoo atuambie maneno.Mimi nitasema kwa ufupi tu kwamba, dalali wa nchi hii ya Zanzibar keshapatikana tangu sitini na nne Mzee Karume, hatutaki madalali wa nchi hii tena, Zanzibar isichuuzwe. La kwanza, Watu kama wana mambo yao basi Zanzibar isifanywe ndiyo ngazi ya kwenda huko kwenye mambo yao. Kama mna yenu basi mfanye wenyewe lakini msiiguseguse Zanzibar ikawa ndiyo ngazi yakutaka yenu. La tatu, Mwanaadamu kama hana fadhila kwa Mungu kwa kuwa hamuoni, basi hata kwa binadamu wenziwe? Usimsahau aliyekugawia maji ukanywa ulipokuwa na kiu. Haiwezekani leo mtu kakutoa unapapatika unakufa, watu walikuwapo wamehangaika wewe ukaja ukachomolewa tu na wananchi wakakuambia kaa hapo, leo unajidai ubwabwa wa shingo? Unajidai ubwabwa wa shingo leo? Hutambui unakotoka? Ubinadamu gani huu, tunasema basi wengine muwe wabinadamu, mnakotoka tunakujueni, wananchi wakawaokota, msiwasahau wananchi. Haya wakiwaacha wananchi mtakwenda wapi? Mtamlaumu nani? Na kama kitu chenyewe ni Kamando, huyu kawekwa na watu huyu bwana!! Sasa kama kawekwa na watu, na pengine na wewe kama unataka siungoje watu wakupe, kama hawakupi usibabaike. Na kama unadoweadowea ukibwatabwata tu utapewa kweli? La nne, Wale Wabunge wajijue kwamba ni wabunge wa chama, sasa nazungumzia wale wabunge wa CCM, ni wabunge wa Chama cha Mapinduzi, kina utaratibu wake wa kujadili mambo. Sasa tena leo ilikuwaje. Hivi Chama Cha Mapinduzi kikikaa kitako kikakuambia tuambie wee, utapepesa macho tu. Lakini sasa unataka nini, wakati kuna utaratibu, tungoje utaratibu. La tano, Zanzibar bwana ilipochanganywa ikawa Muungano, wengine wanafikiri hazikuwa nchi, hizi zilikuwa nchi! Zanzibar ina chama chake wakati huo AfroShiraz, na Tanganyika ilikuwa na chama chake TANU. Kiserikali ndiyo ukapatikana muungano wakati wa Mzee Karume, kichama tukapata chama wakati wa Mzee Jumbe. Lakini ni kwa ridhaa ya watu, tumeulizana humu hivi. Je, hili.... Au mmesahau, labda wale wengine waliokuwa wanafanya madudu tu yasiyofahamika hata utaratibu hayana. La sita, Nawaambia nyie watu, hawa watu wanakusudia kuichochea nchi hii iwe na vurugu, hasa wale vijana tunasema, hatutaki vurugu, vijana msibabaike uzi uleule. Nchi hii imekombolewa haitoki kwa hila au vitendo vyovyote. Sasa hizi njia za ujanja ujanja huu hizi, tatizo nini Kamandoo... he he! Masikini mnamuonea lakini mnajua kumuonea kwenyewe Wa-laah wanamuogopa! Wanamuogopa! Wale wanaosema sijui meno kwa meno wanamuogopa komandoo. Na wale wanaochukua maneno kwa kuiponda serikali, sijui msifanye hivi
Kamandoo kasema nini habari ya kubadilisha katiba. Katiba si inabadilishwa
na watu na kwanini wasibadilishe wenyewe! Na kweli ni viroja si mara nne
hii?! Sasa ikibadilishwa, mbona hakutokeza mtu hapa mnabadilisha, kwanini
mnabadilisha, ibadilishwe leo! Wanamuogopa! Sasa kama inabadilishwa simungoje.
Yeye mwenyewe maskini wala hajasema kitu. Mie nna hakika hapo alipo hivi
tukimzungumza yeye huku anaona wanasema mwenyewe nipo. Mheshimiwa Rais
utafanyaje watu wanakupenda. Kwanini wasiseme? Watasema na waliopo walio
wanachukiwa watachukiwa watapasuka, lakini Kamandoo yumo atazungumzwa naye
atazungumza kama akipata nafasi yale ambayo anahisi busara kwa ajili ya
maendeleo ya nchi yetu sisi. Watu wasibadilishe katiba... kwa sababu ya
nini? Komandoo, mtamuona hivo hivo.
Suala la Dk. Salmin kubadili katiba:
WAKIJADILI hatua zinazodaiwa maandalizi ya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar na kesi ya uhaini ya wanachama na viongozi wa CUF, wasomi na wanasheria wa Chuo Kikuu Dar es Salaam walidai kwamba Zanzibar si nchi yenye utawala kamili, hivyo Rais wake hawezi kupinduliwa. Madai haya ya wasomi tena wanasheria yameamsha hisia za watu wote bila kujali itikadi za kisiasa na kuzusha mjadala mkali pande zote za muungano kuhusu hadhi ya Zanzibar na Rais wake. Kauli hizi za wasomi zimefichua siri iliyotunzwa na viongozi wa TANU (sasa CCM Tanzania Bara) ya kuimeza Zanzibar na kuwa mkoa wa 21 wa Tanganyika. Mwandishi OTHMANI MUHUNZI anaelezea zaidi. MARA nyingi imekuwa ikisemwa kwamba sababu ya muungano wa Tanzanyika na Zanzibar ni mahusiano ya siku nyingi ya watu wa nchi hizi mbili kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Lakini ukweli ni kwamba kuna sababu muhimu na ya msingi ambayo haiwekwi wazi nayo ni kwamba uhuru kamili wa Zanzibar yaani ZANZIBAR SOVEREIGNITY haukumpendeza aliyeasisi fikra za muungano marehemu Mwalimu Nyerere. Kwani siku nyingi hata kabla ya uhuru wa Tanganyika Nyerere aliwahi kuweka wazi hisia zake za kuihofia Zanzibar katika utawala wa Tanganyika hasa pale aliposema wazi kabisa kwamba, "If I could tow that Island (Zanzibar) out in the middle of the Indian Ocean..... I'd dot it..... It is very vulnerable to outside influences. I fear it will be a big headache for me (Tazama Prof. G.M. FIMBO "constitutional making and Courts in Tanzania). Uk. 5. Tafsiri yake ni kwamba Nyerere kama angeweza kukitupa Kisiwa cha Zanzibar katika bahari ya Hindi angefanya hivyo kwa sababu Zanzibar haina ulinzi imara hivyo ni rahisi kushawishiwa na mataifa ya nje. Na kuhatarisha kile kinachoonekana kuua sera zake za kuitawala Tanganyika kwa jinsi anavyopenda. Ni katika hali hiyo Nyerere ambaye sasa anaitwa Mwanasiasa wa karne wa ulimwengu!, aliona ni vyema aandae fikra za kuunganisha Zanzibar na Tanganyika na kuwa nchi moja, akitumia zaidi ukaribu wa Zanzibar na Tanganyika, mwingiliano wa utamaduni, lugha na uhusiano wa ASP na TANU kuwa ndizo sababu kuu za kuunganisha Zanzibar na Tanganyika. Lakini ukweli ni kwamba Nyerere alimshawishi Karume kuunganisha Tanganyika na Zanzibar ili kuifunika Zanzibar isiweze kuwa na uwezo wa kuwa na mahusiano na nchi za nje bila ya kupata ridhaa ya serikali ya muungano, (ambazo kimsingi ni Serikali ya Tanganyika). Hata ukitazama muundo wenyewe na muungano utagundua kwamba unaifanya Tanganyika kuwa nchi kuu na Zanzibar kuwa chini ya Tanganyika kupitia serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ndiye Rais wa Tanganyika ndiye mkuu wa nchi ikiwemo Zanzibar na ndiye kiongozi mkuu wa viongozi wote akiwemo Rais wa Zanzibar, na pia ndiye Amir jeshi mkuu wa majeshi yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar. Ni kwa sababu hizi basi Mwalimu Nyerere ilibidi awe mkali kwa mtu yeyote atakaye hoji mfumo wa serikali mbili. Itakumbukwa kwamba Nyerere alilisambaratisha kundi maarufu la Wabunge wa CCM (GSS) lililotaka mfumo wa serikali tatu mwaka 1992, kwa hoja kwamba mfumo wa serikali mbili ni sera ya CCM na anayehoji hilo basi kwanza atoke CCM. Nyerere alikuwa ni mtu wa mahesabu siku zote kwa sababu aliona kwa kuleta serikali tatu kutafanya Tanganyika iwe na serikali yake. Matokeo yake ni kwamba Tanganyika itakuwa na hadhi sawa na Zanzibar jambo ambalo litaifanya Zanzibar kuwa kama nchi huru isiyo chini ya Tanganyika bali chini ya serikali ya muungano ambayo itabidi iwe na udhibiti ulio na uwiano sawa kati ya Zanzibar na Tanganyika. Hivyo mpango wa kuitawala Zanzibar kupitia serikali ya Muungano inayodhibitiwa zaidi na Tanganyika usiwezekane au kuwa mgumu. Lakini huenda wanasheria wale wa Chuo Kikuu wakawa sahihi na kauli zao. Kwa sababu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa tarehe 26.4.1964 uliunda nchi moja iliyoitwa. "Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo tarehe 11.12.1964 jina hili lilibasilishwa kuwa sheria namba 61 ya 1964 na kuwa "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania." Ni siku hii hii mkataba wa Muungano kati ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar ulipitishwa naBunge la Jamhuriya Tanganyika na Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kupitishwa (Act No. 22/1964 Cap 557). Katika Mkataba wa Muungano Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na ile ya watu wa Zanzibar zilikubaliana kuunda serikali moja kamili ya Jamhuri (SOVEREIGN REPUBLIC). Kwa hiyo kwa mkataba huu hakutakiwa kuwe na nchi kamili "Sovereign state" inayoitwa Zanzibar wala Tanganyika bali kuwe na "Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" ambavyo ndivyo "Sovereign Republic" au "Sovereign State" inayotambuliwa na mkataba wa muungano. Ikumbukwe kwamba mambo yote haya yalifanywa kwa haraka sana chini ya kipindi cha miezi minane (8) wakati ambao Zanzibar hata haijakaa sawa baada ya mapinduzi ya mwaka huo yaliyoiweka madarakani serikali ya mapinduzi, ilihali wenzao wa serikali ya Tanganyika walikuwa tayari wana miaka mitatu (3) ya uhuru hivyo walishajiandaa kiutendaji ndio maana hata mkataba wa muungano uliweza kuiweka juu Tanganyika na Zanzibar kuwa chini na kutimiza mpango wa Hayati Nyerere. Watu wanaotaka Zanzibar itambuliwe kama mkoa wa Tanzania walikuwa na kiu ya muda mrefu ya kuimwaga siri hii ya Muungano wa Tanzania, lakini inawezekana walikuwa wanamhofia Nyerere, kwa sababu kama suala la watu kushitakiwa kwa uhaini Zanzibar hii si mara ya kwanza na pia kesi hii ina zaidi ya miaka miwili siku zote hizo mbona hawakuwahi kutamka kuwa Salmin au Rais wa Zanzibar hawezi kupinduliwa kwa sababu serikali yake ni sawa na ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam? Wasomi hao wameingilia mwenendo mzima wa kesi iliyoko mahakamani na pengine kuathiri maamuzi mazima ya kesi. Kwa kumalizia ningependa kuwaonya Wazanzibari hasa wa CCM waache kujadili hoja hiyo ya wanasheria kwa jazba kwa kudhani kuwa wanasheria wamelenga kumdhalilisha Dk. Salmin bila ya kutazama hoja yenyewe na kuilinganisha na mfumo wenyewe wa muungano hadhi ya Zanzibar hasa linapokuja suala la mahusiano ya Zanzibar na nchi za nje katika kuinua uchumi wake kama vile kujiunga na OIC na uanzishwaji wa Bandari huru. Alamsiki,
Wazanzibari unganeni NA MAALIM BASSALEH MALUMBANO yanayoendelea kwa karibu wiki tatu sasa, baina ya wasomi na baadhi ya viongozi wa CCM, Bara, kwa upande mmoja na viongozi wa CCM, Visiwani, kwa upande wa pili, juu ya azma yaserikali ya Zanzibar kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar ingawa yanaonekana kama kwamba yamelengwa katika kumzuia Dkta. Salmin Amour, asijiongezee kipindi kingine cha urais, baada ya kumalizika muda wake lakini kwa kweli shutuma hizo, kama mtu atazizingatia kwa makini, ataona zimelengwa zaidi kuuhujumu uhuru wa Zanzibar pamoja na Wazanzibari kwa jumla! Inaonekana kuna mkakati maalumu wa kuimeza Zanzibar na kuigeuza kuwa kama ni mkoa tu wa Tanzania Bara. Mojawapo wa mbinu nyingi zinazotumiwa kufanikisha hilo ni kuwagawa Wazanzibari wasiwe na sauti moja, katika kupigania maslahi ya Visiwa vyao. Kabla ya Mapinduzi ya 1964 Wazanzibari waligawiwa kwa misingi ya kikabila. Ulipokuja mfumo wa vyama vingi wakagawiwa katika Upemba na Uunguja, CCM kikawa ni chama cha Waunguja na CUF cha Wapemba! Baadaye tukaambiwa kuna CUF ya Visiwani na CUF ya Bara. Hivi sasa tayari tunachorewa sura kuwa kuna tofauti baina ya CCM ya Visiwan na CCM yaBara. Mambo yangaliishia hapo kungelikuwa na afadhali lakini wapi! Hivi sasa tayari vyombo vya habari vya Bara viko mbioni kuonesha kuwa ndani ya CCM yenyewe huko Zanzibar kuna mgawanyiko, baina ya wale wanaomwunga mkono Dkt. Salmin na wale wanaodaiwa kumpinga. Katika kudhihirisha hilo gazeti moja maarufu la lugha ya Kiswahili linalotoka, kila siku, katika toleo lake la jana, Jumanne tarehe 08-02-2000, limeandika habari kuwa wanamaskani wa maskani mbili za CCM za Mwembe Kisonge na Kachorora eti wamepigana Zanzibar, wale wa Mwembe Kisonge wakitaka Dkt. Salmin aongezewe kipindi kingine cha urais wakati wale wa Kachorara wakipinga! Mpaka lini Wazanzibari watakubali kugawiwa. Kwa nini viongozi wetu wa kisiasa badala ya kuweka maslahi ya Zanzibar mbele, wao wanaweka mbele maslahi yao au maslahi ya vyama vyao? Inafaa Wazanzibari wakaelewa kuwa huu si wakati mwafaka wa kupingana wenyewe kwa wenyewe. Huu si wakati wa kutazama maslahi ya mtu binafsi wala chama! Ni wakati wa kutazama maslahi ya Zanzibar na mustakabali wa Wanzanizbari. Swali la Rias wa Zanzibar aongoze kwa vipindi vingapi si swali la muungano. Ni swali linalowahusu Wazanzibari wenyewe. Ni swali linalowahusu wale wenye haki ya kumpigia kura Rais huyo. Ni hao tu walio na haki ya kusema wanataka Rais wao awaongeze kwa vipindi vingapi! Wala haina maana kwamba madamu katiba ya Muungano imeweka vipindi viwili tu kwa Rais wa Muungano basi na Rais wa Zanzibar lazima naye aongoze kwa vipindi viwili tu. Hao wasomi na wanasiasa wa Bara wanaomshinikiza Dkt. Salmin asiibadilishe katiba ya Zanzibar wanaitazama Zanzibar kama ni mkoa tu wa Tanzania Bara. Katiba ya Zanzibar inasimamia yale mambo yanayohusu Zanzibar tu kwa hivyo, serikali ya Zanzibar ina mamlaka kamili ya kuibadilisha katiba ya Zanzibar katika yale mambo yanayohusu Zanzibar bila ya kuomba kibali kutoka serikali ya Muungano. Kinachohitajika ni kuwa mabadiliko kama hayo lazima yaungwe mkono na zaidi ya theluthi mbili za wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi. Na hata katiba ya Muungano, Serikali ya Muungano haiwezi kuifanyia marekebisho katiba hiyo mpaka ipatikane ridhaa ya theluthi mbili ya wabunge wa Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar. Ikikosekana idadi hiyo kutoka upande wowote wa muungano katiba hiyo haiwezi kufanyiwa marekebisho. Lakini tunasikia kuwa eti kuna kifungu kingine kinachotoa ruhusa kubadilishwa kwa katiba ya muungano kama theluthi mbili ya wabunge wote, kutoka Bara na Visiwani, kwa pamoja wataunga mkono marekebisho hayo. Kama kweli kipo kipengele hicho hatuoni kuwa kipengele kama hicho kitakuwa kinapingana na kile kipengele cha kwanza? Vipi basi katiba moja iwe na ibara mbili zenye kupinzana. Kama hicho kipengele cha pili kiko tokea awali basi inaonesha katiba yenyewe ina utata! La! Ikiwa kipengele hicho kilikuja kuingizwa baadaye jee wabunge wa Zanzibar vipi walitoa aridhaa zao? Hivi sasa kuna madai kwamba baadhi ya viongozi wa Zanzibar wanataka kuona kuwa Rais wa Zanzibar anarejeshewa hadhi yake ya kuwa ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama kweli kuna madai ya aina, hiyo mbona Maalim Seif Shariff Hamadi aliwahi kutoa madai ya aina hiyo akapuuzwa? Au kwa vile alikuwa ni kiongozi wa CUF basi hata kama atasema jambo lenye maslahi na visiwa vya Zanzibar hatasikilizwa? Mara nyingi Wanzanzibari wamekuwa wakishughulikia mambo madogo madogo na kuacha yale mambo ya msingi. Al-Hajj Aboud Jumbe Mwinyi alilazimishwa ajiuzulu uongozi kwa kudai serikali tatu. Na baadhi ya Wazanzibari walisherehekea kufukuzwa kweke. Lakini Rais wa Zanzibar, aliyechaguliwa na Wazanzibari kwa kura anakuja kuondoshwa madarakani na kikao cha CCM cha NEC chenye wajumbe kiasi cha 200 tu! Niajabu! Wazanzibari hawalioni hilo. Lakini kama tukiangalia yule mwasisi wa Muungano Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume vipi alikuwa akiendesha mambo ya muungano ni dhahiri kuwa yeye alikusudia muungano wa serikali tatu. Al-Haj Jumbe katika kitabu chake alichokiita "The Partnership" ameeleza kuwa baada ya Muungano wa 1964 kulitokea kadhia ambayo nusura iuvunje muungano. Ilikuwa ni kuhusu kuwa na uhusiano wa serikali mbili Serikali ya Shirikisho la Ujerumani ambayo kwa wakati huo ikijulikana kama Ujerumani ya Magharibi na Jamhuri ya kidemokrasiya Kijerumani, ambayo ilikuwa ikijulikana kama Ujerumani ya Mashariki. Katika zama hizo nchi yenye uhusiano wa kibalozi na Ujerumani Magharibi haiwezi kuwa na uhusiano na Ujerumani ya Mashariki. Tanganyika tayari ilikuwa ina uhusiano na Ujerumani ya Magharibi. Lakini Zanzibar baada ya Mapinduzi ilianzisha uhusiano na Ujerumani ya Mashariki. Ujerumani ya Magharibi ikaitaka Tanzania, baada ya Muungano, Zanzibar ivunje uhusiano wake na Ujerumani ya Mashariki. Mzee Karume akamwambia Hayati Mwalimu Nyerere kuwa jambo hilo haliwezekani kabisa. Basi Zanzibar ikaendelea na uhusiano wake na Ujerumani ya Mashariki na Tanzania ikaendelea kuwa na uhusiano na Ujerumani ya Magharibi. Kama Zanzibar haina mamlaka yake wenyewe, katika yale mambo yasiyohusu muungano mbona ina Baraza lake la kutunga sheria na pia ina Rais. Jee? Rais huyo hana mamlaka yo yote? Ndani nchi yake? Mbona jamani mnatupa kitendawili? Kuna wengine wanadai kuwa hawawezi kudai serikali tatu eti kwa kuwa sera ya CCM ni serikali mbili tu. Lakini tumekwisha sikia baadhi ya viongozi wa CCM û Bara wakisema kuwa sera ya CCM ni Serikali mbili kuendea serikali moja. Jee! Wazanzibari wanalichukulia vipi swali hilo? Wanataka iwepo serikali moja tu? Na kwanza tokea lini katiba ya nchi ikafuata sera ya chama fulani? Na hasa katika mfumo wa vyama vingi kama huu tulio nao sasa. Tuseme kila chama kitakachoingia madarakani kitabadilisha katiba ya nchi kwa ajili ya maslahi ya chama hicho na siyo kwa maslahi ya nchi na wananchi wake? Umefika wakati Wazanzibar waache jazba, waache ubinafsi na waungane katika kupigania maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano. Hakuna anayepinga muungano lakini tunapinga kuburuzwa Zanzibar. Kama Wazanzibari hawataungana na kuwa kitu kimoja katika kupigania maslahi ya Zanzibar kuna hatari siku moja wakaikuta Zanzibar ina Mkuu wa Mkoa badala ya Rais kwa sababu tunaambiwa sera ya CCM ni serikali mbili kuendea serikali moja! |
YALIYOMO
Tahariri:
Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
USHAURI
NASAHA
MAKALA
LISHE
Michuano ya soka Mataifa ya Afrika |
|
|
|
|