|
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
S.L.P. 72045, Simu: 761753, Dar es Salaam
Mkataba wa Muungano wa 1964 usifanywe siri
INAFAHAMIKA vizuri sana kwamba waungwana hawagombani barabarani, bali hurudi nyumbani kwao ambako kuna wazee. Wazee hawa, kwa umri wao na kwa kuwajua vizuri hao wenye kugombana, huweza kuzimaliza tofauti za hao wenye kugombana. Hapo haki huwa imetendeka na aibu imehifadhika. Katika wiki za hivi karibuni, kumeibuka wimbi la mashambulizi ya maneno dhidi ya Wazanzibari juu ya azma yao ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi yao kumuwezesha Mzanzibari kuongoza visiwa hivyo kwa zaidi ya vipindi viwili iwapo wananchi watamchagua. Mashambulizi hayo yametolewa na watu wenye hadhi na nafasi tofauti Tanzania Bara, wakiwemo Wabunge kadhaa wa CCM, wanasiasa, wanasheria, kiongozi wa kidini na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu serikalini. Wote hawa wamekuwa wakitumia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara kutoa maoni na hisia zao. Hoja kubwa ya kundi hili ni kuwa Wazanzibari hawawezi kufanya hivyo bila ridhaa ya serikali ya Muungano. Wanaoshambuliwa - Zanzibar - nao wameanza kujibu 'mapigo', wamekuwa wakiwaambia hao wachokozi wao kwamba wao wanayo mamlaka ya kuifanyia marekebisho katiba yao wakati wowote na katika namna yoyote kwa maslahi ya nchi yao, na kwamba hakuna yeyote asiye Mzanzibari "mwenye sauti" juu ya hilo. Mpambano huu unakaribia kufanana na watu wanaogombana barabarani. Kwa vile yaelekea kuna utata wa mamlaka ya Zanzibar baada ya Muugano, ni vema ikiwa makundi hayo mawili yakarudi kwenye makubaliano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Huko ndiko nyumbani, na tunaamini tofauti zilizopo zitaondoka. Hivyo tunaungana na wale wote ambao wamekuwa wakitoa maoni kuwa sasa ule mkataba wa makubaliano ya 1964 yaliyounda Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar utolewe hadharani. Tunaonavyo sisi, wale wanaowapinga Wazanzibari kuifanyia marekebisho katiba ya nchi yao wamekuwa wakitumia hoja za hisia zaidi kuliko hali halisi. Aidha, wamekuwa wakitumia 'majina na nasaha' za waasisi wa Muungano, badala ya ni vipi ilikubaliwa Muungano huo uwepo. Waasisi hao wa Muungano, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika wakati huo, na marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, walitia saini mkataba wa makubaliano wa kuziunganisha nchi mbili hizo wakijua fika kwamba siku moja wao hawatakuwepo (na hata majinamizi yao) kuweza kuulizwa juu ya nini na vipi walikubaliana. Hivyo basi badala ya kukazana kuwaambia Watanzania kuwa "huu ndio usia wa Mwalimu" ni bora kurejea kwenye huo mkataba. Ni jambo baya sana mtu kuongea fikra zake halafu akazinasibisha na mtu aliyekufa. Kufanya hivyo ni kumzulia hayati huyo. Watu warejee kwenye makubaliano. Washiriki katika mpambano huo wanatakiwa kuelewa kwamba mazingira yamebadilika: leo ni tofauti sana na mwaka 1964. Watanzania pia wanahitaji mabadiliko ili kuendana na hali halisi ya leo sio ile ya 1964. Hata hivyo mabadiliko yoyote huwa hayaanzi hewani, lazima kuwepo na mahala pa kuanzia, mahala hapo ni huo mkataba wa makubaliano ya Muungano. Ndio sababu tunasema kuwa tunaungana na wale wote wanaotaka mkataba huo utolewe ili ieleweke ni nini kilikubaliwa na kupitishwa. Hivi ni kweli Zanzibar ilipoteza mamlaka yake? Mwanasiasa mmoja mkongwe nchini aliwahi kueleza kuwa mwenye kutaka kujua mamlaka ya Zanzibar akumbuke sababu za kuwepo kwa balozi mbili za Ujerumani, ile ya Ujerumani Mashariki (GDR) na ile ya Ujerumani Magharibi (FRG). Kutokana na kuwepo kwa vita baridi ulimwenguni, Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi hazikuweza kuwa na balozi zake katika nchi moja. Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Nyerere alitaka ubalozi wa Ujerumani Magharibi uliokokuwepo Tanganyika uendelee kuwepo Tanzania na kwamba ubalozi wa Ujerumani Mashariki ulokuwepo Zanzibar ufungwe. Aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Marehemu Sheikh Karume alikataa katakata na aliyekuwa Rais wa Muungano Hayati Mwalimu Nyerere hakuweza kuamuru vinginevyo. Hivyo ubalozi wa Ujerumani Mashariki ukasalia, na kwa mara ya kwanza katika historia ya mataifa hayo mawili ya Ulaya, Ujerumani Magharibi na Ujerumani Mashariki zikawa na balozi zake katika nchi moja. Jambo jingine alilowahi kulisema mwanasiasa huyo, ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali katika serikali zote mbili ni kwamba, katika mkataba wa makubaliano ya muungano ilikubaliwa kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatumia kwa muda katiba ya iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika. Lakini baadaye, katika namna isiyojulikana kwa watu wengine, Mwalimu Nyerere 'aliihalalisha' katiba ile ya Jamhuri ya Tanganyika kuwa ndiyo ya Muungano. Kitendo hiki tayari kiliyakiuka makubaliano ya Muungano. Baada ya Muungano, watumishi wa serikali ya iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika wakachukuliwa moja kwa moja kufanya kazi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano, na hata katika maeneo ambayo Zanzibar haikuhusika, bado watumishi hao walijulikana kuwa ni watumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano! Ajabu kubwa hii! Lipo suala lingine. Katika miaka ya 1970 uchumi wa Tanzania Bara uliporomoka sana. Hali hii ilipelekea kushuka thamani kwa shilingi ya Tanzania. Kwa vile sarafu hiyo hiyo ndiyo inayotumika Zanzibar, uchumi wa visiwa hivyo nao uliathirika kwa matatizo yasiyo ya kwake. Kadhalika lipo suala la Rais wa Zanzibar 'kupokonywa' wadhifa wake wa Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliokubaliwa kuwa nao katika makubaliano ya Muungano wa 1964. Kwa mnasaba masuala yote hayo hapo juu na mengineyo, Wazanzibari wanayo haki ya kuwa na hofu kwamba ni kweli zipo juhudi za kuimeza Zanzibar. Tuonavyo sisi mambo hayo yakiachwa hivi hivi na hizi chokochoko zilizoanza dhidi ya Wazanzibari na katiba ya nchi yao zikaendelea, basi siku si nyingi tutajikuta pabaya. Hata hivyo dawa haipo mbali, turudi "majumbani" tukaupekue mkataba wa makubaliano ya Muungano na bila shaka huu ndio utakuwa 'hakimu'. Wanaojinadi kwamba wanamuenzi hayati Mwalimu Nyerere, sisi tunaamini, hawawezi kufanya hivyo bila kufuata kile ambacho hayati Mwalimu alikitilia saini yake kwamba amekikubali. Wakati ni huu, TUUANGALIE MKATABA WA MAKUBALIANO YA MUUNGANO WA JAMHURI YA TANGANYIKA NA JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR WA MWAKA 1964. |
YALIYOMO
Tahariri:
Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
USHAURI
NASAHA
MAKALA
LISHE
|
|
|
|
|