NASAHA
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF
  • Yasema misaada haitumiki ipasavyo 
  • Yawataka wananchi wa kusini 'wasiikumbatie' CCM 


Na Rajab Nkawa 

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa barabara ya Kibiti-Lindi inawezekana kujengwa na hivyo kumaliza kero hiyo ya muda mrefu kwa wananchi wa mikoa ya kusini, iwapo Serikali itakuwa na nia na kuipa kipaumbele, lakini hivi sasa Serikali haina mpango wa kuijenga barabara hiyo.

Profesa Lipumba aliyasema hayo katika ukumbi wa Starlight uliopo jijini Februari 3, mwaka huu, alipokuwa akiwahutubia wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara waishio Dar es Salaam kufuatia ziara yake ya mikoa hiyo aliyoifanya hivi karibuni. 

Alisema kuwa tatizo kubwa linaloikabili Serikali yetu ni kushindwa kuwahakikishia wananchi na wafadhili juu ya matumizi ya pesa zinazotolewa kama misaada ambazo kiasi kikubwa huishia kwenye kuwanufaisha wajanja wachache, na kutowafikia walengwa jambo ambalo limewafanya wafadhili kuzuia misaada ya maendeleo. 

"Ikiwa serikali ya itawahakikishia wananchi na wafadhili kwamba pesa za msaada zitatumika kujenga barabara na hazitayeyuka kujengea mahekalu basi barabara ya Kibiti-Lindi itajengwa", alisema mtaalamu huyo wa uchumi. 

Mwenyekiti huyo wa CUF Taifa alishangaa kuwa pamoja na Tanzania kuwa ni mingoni mwa nchi zinazopokea misaada mingi toka kwa wafadhili, misaada hiyo imekuwa haitumiki ipasavyo. 

"Gharama za kutengeza barabara ya lami kutoka Kibiti mpaka Lindi ya haizidi dola za Kimarekani milioni mia moja. Serikali inapata misaada kati ya dola za Kimarekani milioni mia saba na mia nane kila mwaka... kama kuna nia ya kujenga barabara na kama tunahakikisha kwamba pesa zitakazotolewa zitatumika kujenga barabara basi itajengwa", alisisitiza Profesa Lipumba. 

Aidha Mheshimiwa Lipumba alizungumzia ardhi nzuri yenye rutuba iliyoko katika mikoa hiyo ambayo kama ingetumika vyema ingeinua uchumi wa mikoa hiyo na pia uchumi wa Tanzania kwa ujumla. Amesema kuwa kilimo kinapokua ndipo viwanda vinapoweza kuanzishwa. 


Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J'pili 

  • Wawakilishi toka mikoani waanza kuwasili 
  • Wasema waliouawa hawakuwa wahuni 


Na Mwandishi Wetu 

WAISLAMU nchini, Jumapili ijayo wanatarajia kujumuika jijini Dar es Salaam katika Khitma ya kuwaombea Waislamu wenzao waliouawa na serikali katika mauaji ya Mwembechai yaliyotokea Februari 13, mwaka juzi.

Taarifa iliyotolewa na kamati ya maandalizi iliyo chini ya Halmashauri Kuu ya Waislamu imeeleza kwamba khitma hiyo itafanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Februari 13 kuanzia saa 10 jioni. 

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa mbali na Waislamu waliouawa katika mauaji yale ya Februari 1998, Khitma hiyo pia itawajumuisha Masheikh na Waislamu wengine "waliotangulia" (ambao tayari wamekwisha kufa). 

Aidha taarifa zaidi zimeeleza kuwa makundi ya Waislamu toka mikoani yameanza kuwasili Jijini kushiriki katika khitma hiyo kuwakumbuka na kuwaombea dua ndugu zao Waislamu waliouawa katika tukio ambalo Waislamu wamekuwa wakilieleza kama ni "kilele cha dhuluma ya Serikali ya Tanzania dhidi ya Waislamu." 

Katika mauaji hayo, Polisi waliwaua Waislamu wawili kwa kuwalenga na kuwafyatulia risasi Waislamu waliokusanyika kupinga kitendo cha polisi kumkamata Mhadhiri mmoja wa Kiislamu ili kuzuia muhadhara usifanyike msikitini hapo. 

Aidha, katika tukio hilo Waislamu wengine kadhaa walikamatwa na kuwekwa rumande ambapo Muislamu mmoja alifariki akiwa mikononi mwa polisi, na hivyo kufanya idadi ya waliokufa katika tukio hilo la kwanza la aina yake nchini kufikia watatu. 

Taarifa zaidi zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa baadhi ya misikiti hapa jijini tayari imekamilisha maandalizi ya kuwapokea Waislamu toka mikoani, na kwamba baadhi ya wajumbe toka mikoani wameanza wasili. 

Bwana Omari Shila kutoka Shinyanga alizungumza na NASAHA ambapo alieleza kuwa Waislamu zaidi kutoka Shinyanga wanatarajiwa jijini kwa vile msiba ule wa Mwembechai ulikuwa ni Waislamu wote. 

".....watu wengi wamejiandaa kuja katika khitma ya wenzetu hao waliokufa shahidi (wakipigania dini ya Mwenyezi Mungu) .... Na wala halikuwa jambo la watu wachache, au wahuni, au wakorofi kama ilivyotangaza serikali", alisema Bwana Shila. 

Tangu kutokea kwa mauaji hayo kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya Waislamu na Serikali ambapo Waislamu wanaitaka Serikali kuunda tume huru kuchunguza mauaji hayo lakini Serikali imekuwa ikipinga jambo hilo kwa maelezo kuwa "kilichotokea Mwembechai kinafahamika" na hivyo hakuna haja ya kuunda tume. 

Mwezi Desemba mwaka jana Rais Benjamin Mkapa aliwaambia Waislamu, katika barua yake aliyomwandikia Katibu wa Halmashauri Kuu ya Waislamu, Saleh al-Miskry, kuwa serikali haioni haja ya kuunda tume. 

Baada ya majibu hayo ya Rais Mkapa, Waislamu walikutana na kutoa tamko la pamoja kuwa hawatakaa chini mpaka wauaji wa ndugu zao wafikishwe mahakamani. 


Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano

Na Mwandishi Wetu 

KUFUATIA harakati za Wabunge na Wasomi wa Tanzania Bara kupinga azma ya wananchi wa Zanzibar kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo, wananchi hao wa Zanzibar wamesema sasa wanataka kuuona mkataba (wa makubaliano) wa Muungano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Serikali Jamhuri ya watu wa Zanzibar uliofanyika mwaka 1964 ambapo ilizaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wamesema, baada ya kuyasikia maoni ya wasomi, wanasheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadhi ya wananchi kwamba Zanzibar ni sawa na mkoa na kwamba Rais wake ni sawa na Mkuu wa Mkioa wa Dar es Salaam, Bw. Yusuf Makamba, sasa wanataka kuuona mkataba huo ili waone kama Zanzibar ilitajwa kuwa itakuwa mkoa wa Tanzania. 

Aidha wamesema kwamba wanataka kuona iwapo katika mkataba huo kulikuwa na makubaliano ya muungano wa nchi huru mbili au ilikuwa ni hadaa kwa nchi moja kuidhulumu nyingine. 

Wananchi hao ambao wengi wao ni vijana walisema iwapo itagundulika kuwa mkataba huo ulikuwa ni wa hadaa tu, basi muungano huo utakuwa ni batili. 

Wamesema wanavyotambua wao Zanzibar ni nchi yao iliyokombolewa na babu zao toka kwa Wakoloni wa Kiingereza na Kiarabu, sasa ikiwa baba zao waliingizwa katika mkataba wenye hadaa na hivyo Zanzibar kuporwa, basi wanaona ni jukumu lao hivi sasa kuikomboa Zanzibar kutoka katika ukoloni mamboleo wa Bara. 

"Bwana Mwandishi, ninyi mmezoea kuandika kuwa vijana ni taifa la kesho, lakini hapa Zanzibar sisi vijana ni taifa la leo... tunataka tuuone mkataba..... 1964 nilikuwa sijazaliwa. Tukigundua kuwa kulikuwa na hadaa, basi tutaikomboa Zanzibar; na huu ndio msimamo wa vijana wote wa Unguja na Pemba", alisema kijana Ali Machano (23) wa Michenzani. 

Mwananchi mwingine aliyekuwa safarini Dar es Salaam kutoka Zanzibar ameeleza kuwa huu ndio wakati wa kuirejesha hadhi ya Zanzibar na kwamba hilo ni jukumu la kila Mzanzibari bila kujali yeye ni mwanachama wa chama gani cha siasa. 

Mwananchi huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Nassor na kwamba ni Mwenyekiti wa Tawi moja la Chama cha Wananchi (CUF) Kisiwani Pemba, amesema kitendo cha kumlinganisha Rais wa Zanzibar na Mkuu wa Mkoa wa Tanzania Bara ni katika kufikia azma ya Tanzania Bara kuimeza Zanzibar. 

"Sisi(CUF) tulikwisha liona jambo hili (la kumezwa Zanzibar) ndio maana walipoleta mabadiliko ya 11 ya katiba, ili kumuondolea madaraka Rais wa Zanzibar katika serikoliya Muungano sisi (CUF) tulifungua kesi mahakamani kupinga dhuluma hiyo dhidi ya Wazanzibar", alisema Bwana Nassor. 

Kwa mujibu wa makubaliano ya awali ya muungano yaliyotiwa saini na Hayati Mwalimu Nyerere na Marehemu Sheikh Karume, ilisemwa kwamba Rais wa Bara atakuwa Rais wa Muungano wakati Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wake. Kadhalika kwa nafasi yake hiyo ya Umakamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar alikuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Muungano ambalo mawaziri wake wote hushika nafasi hizo kwa ajili ya Tanzania Bara. 

"Sasa hivi hakuna mtetezi wa interests (maslahi) za nchi yetu (Zanzibar)....." amesema Bw. Nassor. 

"Mimi ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba hawa wenzetu (CCM-Zanzibar) sasa wameliona hili na wamejiunga nasi", alisema Bw. Nassor na kuongeza kuwa anaona ajabu kwa nini viongozi wa CUF "wamepiga kimya" kuhusu suala hili muhimu ambalo ni la kitaifa na si la kichama. 

Bi Mtumwa Suleiman anasema siku zote Bara imekuwa ikiiburuza Zanzibar na amewataka Wazanzibar wawe kitu kimoja "kuinusuru" Zanzibar. 

"Mimi siku zote nimekuwa nikimpinga Salmin (Rais wa Zanzibar) lakini katika hili Wallahi nipo pamoja naye....(Bara) hawawezi kutushurutisha (kutulazimisha) wanayotaka wao; na sasa wana-CCM wote na wana-CUF wote na kila Mzanizbar lazima tuungane tuinusuru (tuihami isipotee)nchi yetu", amesema Bi Mtumwa ambaye aliliambia NASAHA kuwa aliwahi kufanya kazi ya Ualimu wa "Skuli" mpaka alipostaafu mwaka 1989. 

"Tatizo kubwa lililopo hapa", anaeleza Bi Mtumwa, "ni hawa viongozi wa serikali ya Muungano....hawataki kutuonesha wazi wazi hayo makubaliano ya Muungano. 

Anasema hali hiyo ya usiri wa Serikali ya Muungano huwa inawafanya Wazanzibar "kutia shaka" iwapo kweli Marehemu Sheikh Karume alisaini mkataba ule wa muungano, na kwamba kama aliusaini, basi huo aliousaini huenda siyo huo unaofuatwa hivi sasa. Hivyo alisisitiza kwamba mkataba huo uwekwe bayana kama ulivyo sainiwa mwaka 1964. 

Mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mama Maryam (27) ametoa wito kwa vijana wote wa Zanzibar kuungana kudai mkataba wa muungano wa 1964 utolewe hadharani. 

Wiki iliyopita msemaji wa Ikulu ya Zanzibar, Hafidh Ali, alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kelele za wabunge wa bara kupinga marekebisho ya katiba ya Zanzibar ni chuki dhidi ya Zanzibar. 

Hafidh amesema anashangaza na wabunge hao kupinga marekebisho ya Katiba ya Zanzibar wakati wao wenyewe wanajiandaa kifanyia marekebisho katiba ya muungano. 

Aidha Msemaji huyo wa Ikulu ya Zanzibar aliungana na aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bw. Wolfgang Dourado, kudai kwamba marekebisho ya katiba ya 11 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yalikiuka makubaliano ya muungano kwa kumnyang'anya umakamu wa rais wa Jamhuri ya muungano, na wakashangaa ni vipi ja,mbo hili halijahojiwa na hao wabunge wa muungano amabo sasa wanaipigia kelele Zanzibar kuizuia isbadilishe katiba yake bila ridhaa ya serikali ya muungano. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Mkataba wa Muungano wa 1964 usifanywe siri

Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF

Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili

Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano

Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia

Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji

Makala 
Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Hassan Mussa Takrima  katika maadhimisho ya miaka 23 ya CCM 

MAKALA
Uhuru na ukombozi

MAKALA
Suala la Dk. Salmin kubadili katiba:
Wasomi wafichua siri ya Muungano

Kalamu ya Mwandishi
Wazanzibari unganeni 

Makala
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 2

USHAURI NASAHA
Matitizo ya ajira, Nini kifanyike?

MAKALA
Mgogoro wa kisera ndani ya CCM usigeuzwe kuwa ni wa kitaifa

HABARI ZA KIMATAIFA 

  • Wachechnya wapania kuidhibiti upya Grozny
  • Wanaoacha umalaya wagawiwa fedha Zamfara
  • n.k

  • Riwaya
    Ndoto ya ajabu

    LISHE 
    Umuhimu wa mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Ligi Kuu sasa kuchezwa kwa makundi
  • Simba kuipa Prisons mazoezi leo 

  • Michuano ya soka Mataifa ya Afrika


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita