NASAHA
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
USHAURI NASAHA 
 
 

Matitizo ya ajira, Nini kifanyike? 

NA KHADIJA IDD

KUMEKUWA na malalamiko mengi juu ya ukosefu wa ajira katika jamii yetu siku hizi. Hata hivyo, malalamiko haya huishia katika kuwaelekeza hao wasio na ajira kujiajiri. Kwa upande mwingine kuna watu wengi ambao wamekosa kazi na wengine kuacha kazi kutokana na kukosekana kwa taarifa muafaka za kumfanya asiye na kazi aipate na aliye nayo aitunze.
 

MARA nyingi huwa ni jambo lisiloshangaza kuona vijana wengi wamehitimu masomo na hawaelewi wafanye nini huku wakidai kuwa wanataka kuwa wanasosholojia, madaktari au mwanasayansi. Vijana hawa na wengine wanahitaji ushauri NASAHA ambao utawasaidia katika kuchagua kazi waipendayo na wanayotarajia kuifanya, kujiandaa na kazi waliyoichagua, kuipata kazi hiyo na hatimaye kuendelea katika kazi hiyo. 

Ili vijana hawa waweze kupita salama na kwa mafanikio katika ngazi hizo hapo juu inawabidi wajue wanapenda kazi gani na wawaoneshe wazazi au walezi wao kuwa aina gani ya kazi wangependa kuifanya. Kwa mfano, kuna wale wanaopenda kazi za kutoa huduma kwa jamii kama vile kufundisha, uanasheria, uganga, uuguzi n.k. au wale wanaopenda kazi za nje kama vile kilimo, uvuvi, uwindaji n.k. 

Katika kuonesha kuwa wanapenda kufanya kazi gani, walezi au washauri wanatakiwa wawe na ufahamu wa kutosha juu ya kazi iliyotajwa na kijana na mambo aliyotaja kuyapenda kwani wakati mwingine mtoto anaweza kupenda kazi fulani ambayo inafanywa na baba au mama yake. Kuoanisha kazi anayopenda na mambo anayoyapendelea ni muhimu kwani kukiwepo na mgongano baina yake, kijana anaweza kujikuta anachukia kufanyakazi fulani baada ya miezi michache. 

Kabla ya kuchagua kazi fulani kijana anatakiwa ajue mgawanyiko wake. Mshauri au mzazi amsaidie mtoto wake ili apate fursa ya kufahamu mgawanyiko wa kazi ili waweze kufanya uamuzi. Kwa mfano mtu anaweza kusema kuwa anapenda kuwa mwandishi. Ni vuzuri basiakisaidiwa ajue kuwa kuna waandishi wa habari, wa vitabu, n.k. au anayependa kuwa daktari asaidiwe kuelimishwa kuwa daktari wa meno, wa watoto, wa mifupa, wa magonjwa ya wanawake n.k. 

Ushauri NASAHA ni muhimu pia kwa watu hawa kutokana na matatizo ya kuadimika kwa ajira. Hali hii husababisha ushindani wa kupata wafanyakazi wenye juhudi na ujuzi. Katika hali kama hii nafasi chache zilizopo zitajazwa na wale wanaonesha kuwa na sifa zinazotakiwa. Hivyo kijana anaposaidiwa kujiandaa na kazi fulani aliyoichagua anaandaliwa ili aweze kushindana na wengine wachache wenye sifa hizo, na anapopata kazi ushauri NASAHA unamsaidia ili aweze kudumu kwenye kazi yake na hivyo kuepukana na tatizo la kuhama hama kutoka kazi moja kwenda nyingine. 

Ili aweze kudumu na kazi yake ipasavyo, anahitajika kufahamu masharti ya kazi hiyo, na mazingira atayofanyia kazi, mishahara na mafao mengine, jinsi ya kupanda daraja na cheo, mikataba n.k. kwa kuyafahamu haya yote kabla ya kuanza kazi kijana atakuwa na taarifa zote kabla na hivyo ataepukana na tatizo la kuingia kazini akiwa hajui la kufanya. Utaratibu huu pia utapunguza au kuondoa kabisa tatizo la kuchoshwa na kazi muda mfupi baada ya kuianza. 

Vilevile mshauri NASAHA na mzazi au mlezi, wanakuwa na jukumu la kutafuta taarifa muhimu kuhusu ajira na kazi kutoka sehemu mbalimbali kama vile magazetini, katika majarida au kutoka katika makampuni ya ajira. Taarifa hizi zitawasaidia katika kuwashauri vijana wao juu ya kazi hizo na namna ya kutatua matatizo kazini, jambo ambalo litawasaidia wadumu na kazi zao. Pamoja na kufanya hili, kufuatilia maendeleo yao kazini, kuangalia mafanikio na matatizo yao na kuyajadili pamoja ni njia bora itayosaidia vijana hawa kudumu na kazi yao huku wakiendelea kuwa na juhudi kama walivyokuwa hapo mwanzo. 
Juu


MAKALA
 
 

MAREKEBISHO YA KATIBA YA ZANZIBAR
Mgogoro wa kisera ndani ya CCM usigeuzwe kuwa ni wa kitaifa 

NA RAJAB KANYAMA

DEMOKRASIA ni kinyume cha udikteta, nchi inayoongozwa kidikteta ni ile ambayo kiongozi wake mkuu au kikundi cha watu wachache huhodhi mamlaka na madaraka yote ndani ya nchi. Kwa kupitia mfumo waliyoundaa kwa katiba walizoandika wenyewe, ili matakwa yao yageuzwe na kufanywa kuwa ndio sheria.
 

MADIKTETA hawana tabia ya kuwajibika kwa wananchi na wala hawapendi kuongozwa na matakwa ya wananchi. 

Viongozi au serikali za aina hii huwa hazitoi nafasi kwa wananchi kuhoji matendo na maamuzi wanayopitisha, na wakati wote hubuni mbinu mbali mbali, pamoja na kutumia vibaraka ambao tayari walikwisha pandikizwa sehemu kadhaa muhimu ili kuwekea vizuizi. Haki za msingi za wananchi, kama vile uhuru wa maoni, uhuru wa kuchaguliwa kuwa kiongozi na hata uhuru wa kujumuika, kupokea na kutoa habari. 

Mayowe yaliyopamba vyombo vya habari siku za karibuni, hususan magazeti kuanzia tarehe 20 ya mwezi wa Januari 2000, baada ya Askofu Mkuu, Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, Polycayo Kadinali Pengo kukemea nia iliyojitokeza ya kutaka kufanya marekebisho katika katiba ya Zanzibar, ili kuongeza vipindi vya urais wa Zanzibar kutoka vivuli na kuwa zaidi, ni ya kumshangaza kila mtu mwenye akili timamu. 

Inatisha zaidi kuona kwamba ni baada ya kauli ya Baba Askofu ndio na walalamikaji wengine wakajitokeza kwa wingi, kama vile watu waliokuwa wanasubiri amri ya kufanya hivyo. 

Jaji Joseph Sinde Warioba akajitokeza na akasema yake, hatujatulia vizuri tarehe 24 ya mwezi wa Januari, wabunge 45 wa Chama Cha Mapinduzi nao wakafuata nyayo, na tarehe 4 (nne) Februari idadi ya wabunge ikaongezeka na kuwa 52 wote wakiwa ni Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi upande wa Tanganyika na wao wakarudia yale yale ya baba Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. 

Wanataaluma hao hawakutaka kubaki nyuma, wakaandaa mdahalo wa wanasheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kurudia yale yale ya marekebisho ya Katiba ya Zanzibar na kwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba Zanzibar sio nchi, isipokuwa ni sawa na mkoa tu. 

Hapo mtandao ukawa umekamilisha kazi yake. 

Sasa wananchi nao wanahoji hiki kitendawili, hivi ni kweli kwamba hata wanasheria wa Chuo Kikuu nao pia hawaelewi kuwa moja ya kanuni muhimu za Demokrasia ni kuhakikisha kwamba vitendo vya viongozi wa kijamii katika nafasi yoyote ile kinatakiwa kudhihirisha matakwa ya wananchi na sio yale matakwa wanayoyataka wao? Na kwamba Demokrasia ya kweli ni pamoja na kuvumiliana katika maoni tofauti ya kisiasa na kwamba maoni ya kisiasa ya wananchi ni lazima yasikilizwe na haki zao za msingi kuheshimiwa? 

Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba Dk. Salmin Amour hajawahi kutamka kuwa katiba ya Zanzibar ifanyiwe marekebisho ili agombee Urais kwa kipindi cha tatu na wala hajatamka kuwa anataka kugombea tena nafasi hiyo. 

Hizi jazba na mayowe ya baba Askofu na wanamtandao wengine zinasababishwa na nini? 

Kwa nini vyombo vya habari navyo badala ya kutekeleza lile jukumu adhimu la kuelimisha jamii kuhusu ukweli wa mambo yanayowahusu kama taifa, wao wanatilia mkazo utoaji wa taarifa tu za matukio hata kama matukio hayo hayana manufaa yeyote ndani ya jamii? Au tuseme na wao ni sehemu ya mtandao na kwa hivyo wanafanya ile kazi waliyotumwa ya kuwachanganya wananchi fikra ili wasielekeze fikra hizo katika marekebisho ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni ya hatari zaidi kuliko hayo ya tafsiri tu ya kifungu cha katiba ya Zanzibar kinachohusu vipindi vya Urais Zanzibar? 

Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kwamba mayowe tunayoyasikia kutoka kwa wanamtandaona wabunge wa chama cha mapinduzi wa Tanganyika ni kiini macho tu katika harakati za kufikia lengo lililojificha gizani. 

Ukweli uko wazi, kiini cha tatizo hili la sasa kuhusu Zanzibar na katiba yao ni ukiukwaji uliofanywa makusudi, wa kutokutekeleza vizuri vifungu vitatu muhimu vya mkataba wa muungano wa mwaka 1964. 

1. Kutokutekelezwa kwa kifungu namba (m)(b) kilichotaka kuwepo na taasisi za makamu wawili wa Rais ambapo mmoja kati yao aliye mkazi wa Zanzibar ndio anakuwa kiongozi wa Serikali ya Zanzibar na msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa kazi za kiserikali kwa upande wa Zanzibar. 

2. Kutokutekelezwa kwa kifungu namba (vii)(b) kilichomtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kukubaliana na Makamu wa Rais ambaye ni kiongozi wa Serikali ya Zanzibar, kuitisha baraza la kutunga katiba likiwa na wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar katika kipindi cha mwaka mmoja tokea kuanza kwa muungano kwa madhumuni ya kutafakari mapendekezo ya tume ya katiba na kupitisha katiba ya Jamhuri ya Muungano 

3. Kutokutekelezwa kwa kifungu namba (viii) kilichotaka mkataba wa muungano kuthibitishwa kwa kutungiwa sheria na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri la Jamhuri ya watu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Baraza lake la Mawaziri na mkataba kupitishwa na kuundwa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kwa kufuata masharti yaliyokubaliwa. 

Bunge la Tanganyika lilitunga sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Namba 22 ya 1964, Baraza la Mapinduzi la Jamuhuri ya watu wa Zanzibar kwa kushirikiana na baraza lake la mawazi halikutunga sheria iliyotakiwa. 

Hii ndio hali halisi ya muungano wetu, japokuwa tulizotaja hapo juu ni baadhi ya dosari nyingi zilizopo. 

Mtu au kikundi cha watu kinapozuka na kuanza kupiga mayowe kuhusu katiba ya Zanzibar au uhusiano uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tanganyika au na Zanzibar bila ya kuzingatia ukweli tuliotaja na bila ya kutumia vikao halali vya Chma Cha Mapinduzi mtu huyo ni mchochezi na anayepaswa kuchukuliwa hatua kali. 

Huu si wakati wa kuendelea kukwepa ukweli, watu wa kulaumiwa katika hali hii ya kisiasa tuliyonayo sasa ni wale waliochangia au kusababisha kuwepo kwa hali hii ya utata kati ya katiba ya nchi na sera za chama, hali inayoonyesha jinsi dhamira zinazodaiwa kuwa ndizo zilizozaa muungano zilivyokuwa za bandia. 

Nidhahiri sasa kuwa waasisi wa muungano tunaotakiwa kuulinda kwa gharama zozote kama ulivyo, kila mmoja alikuwa na sababu nyingine za ziada zilizomfanya aukubali muungano tofuati na ile iliyotajwa ya kudumisha udugu wa asili uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar. 

Hali tuliyokuwa nayo ya mfumo wa chama kimoja cha siasa wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza, haikuruhusu wala haikutoa fursa kwa wananchi kuweza kufahamu ukweli au jambo lolote kuhusu muungano, ilikuwa ni mwiko wa kisiasa kuutaja muungano kwa kuudodosa. 

Mambo yaliyowapata wananchi wenzetu waliokuwa viongozi wa juu kabisa katika serikali ya Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe na Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuonyesha dalili tu za kutaka dosari zilizojitokeza katika muungano wetu ziondoshwe, sote tunazijua. 

Watanaznia wote tukalazimishwa kukumbatia bomu lililokwisha washwa utambi huku hatufahamu ni lini litalipuka. 

Mwaka 1992 Mheshimiwa Jaji, sasa ni Mstaafu Francis Nyalali alieleza wazi katika ripoti yake kuwa muundo wa Serikali mbili una matatizo mwengi, muundo muafaka ni wa serikali tatu. Vigogo walipokutana Chimwaga wakasema hapana, Jaji Kisanga nae amerudia yale yale katika ripoti yake ya hivi karibuni, nae pia ameambiwa hapana sera za Chama Cha Mapinduzi hazibadiliki. 

Kwa vile haya ni kwa maslahi ya wanamtandao hatujasikia malalamiko kutoka kwa Baba Askofu wala midahalo ya kisheria. 

Inashangaza leo kusikia mtu akisema kuwa upo uwezekano wa usultani kurudishwa Zanzibar wanataka kurekebisha katiba yao ili kumuwezesha rais wa Zanzibar, wanaemchagua kwa kura zao, kuwa na vipindi zaidi ya viwili. 

Matamshi ya aina hii ni ya watu waliofilisika kifikra ambao wanadhani wananchi wote ni wajinga. 

Katika mkutano, Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika Dodoma, chama kilipitsha azimio kwamba suala la Urais wa Zanzibar na katiba likajadiliwe katika vikao vya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar. 

Wananchi wanahoji ni lini Kadinali, Pengo, wanasheria wa Chuo Kikuu na Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi wa Tanganyika walipewa mamlaka ya kutengua maamuzi ya mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? 

Na kama si hivyo, hizi chuki za wazi zinazoonyeshwa dhidi ya wananchi wa Zanzibar na Rais wao sababu yake nini? Haya mayowe tunayoyasikia kila kukicha ni kwa niaba na maslahi ya nani? Na kama watadai kuwa wanatumia haki yao ya msingi kama raia katika kutoa maoni kuhusu mambo ya nchi, ni lini wananchi wa Zanzibar - walinyang'anywa haki hiyo ili wasiwe na uwezo wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi yao, pale wanapoona inafaa. 

Ni kawaida ya wakati kuwa ndio muamuzi wa kweli na huu ni wakati wa ukweli na uwazi, kwa hivyo ni wakati muafaka kuachana na tabia mbaya tunayotaka kurithi ya kuendesha nchi kwa ngonjera, Propaganda za magazeti na vitisho. 

Viongozi waache hofu. Kinachotakiwa kufanywa ni kuilea demokrasia inayoanza kukua kwa faida na maendeleo ya nchi yetu. 

Tusiogope mizimu, maana yenyewe haina uwezo wa kudhuru walio na uhai. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Mkataba wa Muungano wa 1964 usifanywe siri

Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF

Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili

Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano

Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia

Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji

Makala 
Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Hassan Mussa Takrima  katika maadhimisho ya miaka 23 ya CCM 

MAKALA
Uhuru na ukombozi

MAKALA
Suala la Dk. Salmin kubadili katiba:
Wasomi wafichua siri ya Muungano

Kalamu ya Mwandishi
Wazanzibari unganeni 

Makala
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 2

USHAURI NASAHA
Matitizo ya ajira, Nini kifanyike?

MAKALA
Mgogoro wa kisera ndani ya CCM usigeuzwe kuwa ni wa kitaifa

HABARI ZA KIMATAIFA 

  • Wachechnya wapania kuidhibiti upya Grozny
  • Wanaoacha umalaya wagawiwa fedha Zamfara
  • n.k

  • Riwaya
    Ndoto ya ajabu

    LISHE 
    Umuhimu wa mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Ligi Kuu sasa kuchezwa kwa makundi
  • Simba kuipa Prisons mazoezi leo 

  • Michuano ya soka Mataifa ya Afrika


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita