|
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
Kujiunga na OIC ni kwa maslahi ya taifa Ndugu Mhariri, NI MIAKA sasa imepita ambapo kimekuwepo kilio cha Waislamu kutaka Taifa letu kujiunga na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislam, yaani OIC (organization of Islamic Countries). Suala hili ni mojawapo ya madai wa Waislamu kwa Serikali kuhusu kunyimwa haki zao. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikipuuza kilio chao likiwemo suala hili. Imekuwa ikisisitizwa kwamba, endapo Tanzania itajiunga na uanachama huu, upo uwezekano mkubwa kwa raia wake kunufaika kutokana na kupata misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya kuendeshea miradi ya maendeleo, na hivyo kuweza kupunguza makali ya maisha yanayotokana na umaskini "wa kujitakia", uliokithiri. Serikali imelipuuzia suala hili kutokana na sababu zisizokuwa za msingi. Mojawapo likiwa ni hofu eti ya udini. Yaani kwamba huenda kujiunga na uanachama kutaifanya Tanzania kueleweka nchi ya Kiislam. Hivi karibuni, Kardinali Pengo, kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki nchini, alitoa changamoto kwa Waislamu kuthibitisha kama suala la uanachama OIC lina maslahi ya kitaifa. Jibu ni kwamba Tanzania kujiunga na kuwa mwanachama wa OIC lina maslahi kwa Taifa. Hii ni kutokana na ushahidi tunaoupata kutoka nchi jirani ya Uganda. Uganda, pamoja na kwamba si Taifa rasmi la Kiislamu, liliamua kujiunga OIC kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Taifa hilo. Kutokana na uanachama wake, wauzaji wa bidhaa nje (exporters) wa Uganda, bila kujali udini wao, wameweza kunufaika kutokana na kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu sana, inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB). Kwa hiyo, haliwezi kuwa jambo la ajabu kwa Uganda kupiga hatua muhimu ya kimaendeleo ya kujiongezea pato la fedha za kigeni, wakati ambapo jirani yao Tanzania anahaha kutafuta mikopo ambayo ina masharti magumu na pia kushindwa kuwasaidia mitaji wauzaji bidhaa nje. Ndiyo maana nchi sasa imekumbwa na mzigo wa ulipaji wa madeni katika fedha za kigeni ambazo nazo tunazihitaji kwa ajili ya maendeleo. Fedha hizo za ziada Uganda inazipata kupitia wauzaji wake wa bidhaa nje, kutokana na uanachama wa nchi hiyo katika OIC (rejea jarida la The Ugandan Export Bulletin, Vol. 8 No.2, May/August 1999, litolewalo na Ugandan Export Promotion and Development Board, UEPB). Hivyo, tunapenda kusisitiza tena kwamba suala la Tanzania kujiunga na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu, ni suala linalozingatia maslahi ya Taifa na wala sio kwamba lina maslahi ya kikundi cha watu, kama ambavyo imekuwa ikinadiwa siku zote kupitia baadhi ya vyombo vya habari. Mansour Mbamba,
BAKWATA si kibaraka wa dola Ndugu Mhariri, NIMESOMA katika toleo namba 033 kwenye Hoja Binafsi. Mtoa hoja anaeleza kuwa BAKWATA ni kibaraka wa dola (Serikali). Ninachotaka kuweka wazi ni kuwa endapo mtoa hoja anadhani hiyo ni muhimu aelewe kuwa wafanyakazi wa BAKWATA si wote ni vibaraka wa dola bali ni wachache tu katika jumuia hiyo kongwe waliyoundiwa Waislamu na kuwa kiini macho cha kuleta maendeleo na kusimamia maslahi ya Waislamu ndio vibaraka. Vibaraka hao wapo hapo kwa maslahi ya waliounda jumuiya hiyo ambayo iliundwa si kwa misingi ya Ucha-Mungu, bali kwa misingi ya kuwadhibiti na kuwatawala Waislamu. H.J. Ramadhani,
Hongera Kidato cha Kwanza Ndugu Mhariri, Nachukua fursa hii kuwapongeza wanafunzi waliobahatika kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu iwe katika shule za serikali au shule za binafsi. Waelewe kuwa nafasi waliyopata ni tunu kwani kuna wenzi wao hawajafanikiwa kufika hapo kutokana na sababu mbalimbali na hasa za kiuchumi na kitaaluma. Ni matarajio yetu kuwa watathamini tunu hiyo na si kwenda kwanza kujiingiza katika maadili yasiyofaa ikawa ni sababu ya kushindwa mitihani iliyo mbele yao na kuleta sifa mbaya katika kiwango cha familia na hadi jamii (shuleni). Fanyeni jihudi na maarifa ili mje kuwa zao bora lenye manufaa kwa jamii. Fatma Omar Juma,
Tuchangie redio kheri Ndugu Mhariri, Naomba unipatie fursa ya kutoa maoni yangu katika gazeti lako. Nimeona tangazo lililotolewa na Baraza Kuu katika gazeti lako la kuwataka Waislamu wachangia redio kheri. Mimi napenda kutoa wito kwa Waislamu kote nchini tutoe michango ili kufanikisha kuanzishwa kwa redio yetu. Hassan J. Hassan,
|
YALIYOMO |
|
|
|
|