NASAHA
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Habari za Ndani
 
 

Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia 

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO 

WANAWAKE wa Kiislamu wametakiwa kupinga kile kilichodaiwa kuwa ni unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao vinaofanywa na baadhi ya watu na hata taasisi mbalimbali hapa nchini.

Wito huo umetolewa katika semina iliyoandaliwa na jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (MSASUA) Morogoro, hivi karibuni, kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya jamii ya Kiislamu hapa nchini. 

Wakichangia katika mada juu ya Uislamu na Ukombozi wa mwanamke katika jamii, kina mama kadhaa walidai kuwa matatizo mbalimbali yanayowakabili katika jamii hayatokani na kanuni au mwenendo wowote wa dini yao. 

Kinyume chake, walieleza kina mama hao, Uislamu kama dini, umemkomboa mwanamke; na kwamba matatizo yanayowapata yanatokana na unyanyaswaji wa kijinsia ambao wakati mwingine hufanyiwa hata na waume zao wenye tabia ya kuasi mafundisho ya dini yao. 

Akifafanua juu ya hilo, mama mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana, alisema: "Mwenyezi Mungu amekataza kuwabadilishia watu ukoo wao.... Lakini inasikitisha kuona kuwa waume wa Kiislamu nao wanaiga mila zisizokuwa za Kiislamu kwa kutaka wake zao waitwe kwa ubini wa baba za waume zao", alisema mama huyo na kuongoza, "huu kwa kweli ni unyanyasaji wa kijinsia, kwa nini mwanamke alazimike kutumia jina la ukoo wa mumewe?" 

Wakitoa mifano kadhaa ya jinsi wanavyonyanyaswa kijinsia na waume wa Kiislamu kinyume cha mafundisho ya dini yao, walieleza kuwa imekuwa ni jambo la kawaida katika familia nyingi za Waislamu hapa nchini kuona mwanamke anaachika na kisha kutupwa nje ya nyumba pasipo kujali au kufuata sheria za Eda zinazolinda haki ya mwanamke anapoachika. 

Kuhusu masuala hayo ya Eda ilielezwa pia unyanyaswaji wa mwanamke wa Kiislamu upo hata pale anapofiwa na mumewe ambapo ndugu wa mume hupuuza sheria hii ya Mwenyenzi Mungu inayohitaji mfiwa (mfano) kuwekwa eda kwa kipindi cha miezi minne chini ya familia ya marehemu mumuwe. 

Awali, akiwakilisha mada hiyo, Bwana. Hashim Hemed ambaye ni mwalimu wa shule ya Sekondari alisema kuwa unyanyaswaji mwingine unaowakuta wanawake wa Kiislamu ni ule unaotokana na mfumo wa fikra potofu uliopo katika jamii yetu ambao ni chimbuko la ulimbukeni wa kuiga mila na tamaduni za nchi za kigeni. 

Akifafanua juu ya hilo Bi Fathiya alisema kuwa utamaduni wa kigeni hasa wa Kimagharibi una mtazamo mwanamke kama kipodozi na wakati mwingine hutumiwa kupumbaza fikra za wanaume wapotofu kama ambavyo bangi au madawa mengine ya kulevya yanavyotumiwa kuwapumbaza walevi. 

Akitolea mfano, mwalimu Hashim alieleza jinsi matangazo mbalimbali ya biashara yanavyopambwa na picha za wanawake waliomo katika mavazi yanayo waonyesha wakiwa katika hali ya nusu uchi. 

Akiwakilisha mada yake Mwalimu Hashim alieleza kushangazwa kwake na wanawake kutumika katika matangazo ambayo hayahusiani na mazingira yao kama vile masuala ya mapishi, mavazi, malezi na kadhalika. Mwalimu Hashim alihoji, kama huu si unyanyaswaji wa kijinsia, mbona hatuoni wanaume wengi kutumika katika matangazo ya aina hiyo. 

Akitoa mchango wake katika mada hiyo, mwanafunzi mmoja wa shahada ya kwanza katika Chuo hicho Bi. Fathiya Ali, alisema kuwa wanawake wa Kiislamu wamekuwa wakidhulumiwa haki zao za ajira kutokana na mitazamo potofu ya kutaka kumtathmini mwanamke kwa sura yake, "usafiri" (miguu yake) na kadhalika. Hivyo, alieleza Bi Fathiya, wanawake wa Kiislamu ambao huvaa Jijab hudhulumiwa haki yake ya kupata ajira kwa kuwa si rahisi kuiona miguu yake. "Unyanyasaji huu wa kijinsia lazima upigwe vita, na ni wajibu wetu wanawake wa Kiislamu kushikamana kupinga unyanyasaji huo", alimaliza Bi. Fathiya. 

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Kiislamu (TAMPRO) Ustadhi Pazi aliwataka wanawake wa Kiislamu kusimama kidete katika masuala yote yanayowahusu. Alisema, "mtetezi bora wa haki za wanawake ni mwanamke mwenyewe; wanaume ni wasimamizi wema na wenye uwezo wa kufanikisha pale ambapo wanawake wameamua kuweka msimamo." 


Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji:
Chanzo ni uzembe wa makada wa CCM 

Na Mwandishi Wetu

IMEDAIWA kuwa chanzo cha CCM kukata rufaa kupinga matokeo ya chaguzi za serikali za mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana ulitokana na uzembe wa makada wa chama hicho ambao hawakuwa na uwezo wa kuhawamasisha wananchi kukipigia kura chama hicho.

Madai hayo yametolewa na baadhi ya wananchi wa kata mbalimbali za wilaya ya Kisarawe ambao waliongea na mwandishi wa habari hizi. 

Wakisisitiza kauli yao hiyo, wananchi hao walionesha nakala ya barua kutoka kwa Katibu wa CCM wilaya ya Kisarawe kwenda kwa Makatibu Kata wa Wilaya hiyo ikiwaelekeza makatibu hao kupinga matokeo ya chaguzi hizo. 

Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo ilitumwa kwa Makatibu kata wa CCM wa kata za Masaki, Kibuta, Manerumango na Marumbo, iliwataka Makatibu hao kukata rufaa kupinga matokeo ya chaguzi hizo katika maeneo waliyoshindwa ili kupata fursa ya kugombea tena "ili kurejesha heshima ya CCM". 

Sehemu ya barua hiyo ya tarehe 2 Desemba mwaka jana yenye kumbukumbu Na. CCM/KS/KC/1999/83 inaeleza: "Mnatakiwa kufanya kila jitihada ili kurejesha heshima ya CCM, kwanza mkate rufaa kwa msimamizi wa uchaguzi". 

Ikisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya hivyo barua hiyo pia iliwaeleza makatibu hao wa CCM tatizo lililowafanya washindwe katika uchaguzi huo: "Tatizo kubwa linaloonekana hapa ni kwamba hamkuwapitia watu kwenda kupiga kura. Pia wanawake hawakutumika vema na wazee". 

Mwandishi wa habari hizi aliwasiliana na Katibu wa CCM Kisarawe ili azungumzie juu ya barua hiyo. Katibu huyo alithibitisha kuwepo kwa barua hiyo na alipoulizwa kama tatizo la kutokupigiwa kura za ushindi ni sababu ya kukata rufaa, alieleza kuwa yeye haoni tatizo liko wapi na akaongeza kwa kusema:"lengo la chama cha siasa ni kushinda kwenye uchaguzi, hivyo ukishindwa unaangalia wapi palikuwa na matatizo. Hata wapinzani wanalalamika kwa kuwa hawataki kupoteza ushindi wao". 

Hata hivyo, wananchi mbalimbali wa maeneo ya kata hizo walipoulizwa kama hawakupiga kura kwa kuwa hawakupitiwa na makada wa CCM kwenda kupira kura, walionesha mshangao wa dai la kutokupitiwa na kusema kuwa wao siku ya uchaguzi walikwenda kupiga kura na kuwachagua wagombea wawatakao. 

Tangu chaguzi hizo kwisha wapinzani wamekuwa wakilalamika kwamba CCM hawakubali kushindwa na kwamba maeneo waliyoshinda wapinzani yamekuwa yakikatiwa rufaa pasipo sababu za msingi. 

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa John Malecela amekiri kuwa chama chake kimepoteza zaidi ya viti elfu mbili katika chaguzi za serikali za mitaa, vitongoji na vijiji. 

Hayo aliyasema katika sherehe za kuazimisha miaka 23 tangu kuzaliwa kwa CCM kutokana na muungano wa TANU na ASP. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Mkataba wa Muungano wa 1964 usifanywe siri

Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF

Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili

Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano

Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia

Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji

Makala 
Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Hassan Mussa Takrima  katika maadhimisho ya miaka 23 ya CCM 

MAKALA
Uhuru na ukombozi

MAKALA
Suala la Dk. Salmin kubadili katiba:
Wasomi wafichua siri ya Muungano

Kalamu ya Mwandishi
Wazanzibari unganeni 

Makala
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 2

USHAURI NASAHA
Matitizo ya ajira, Nini kifanyike?

MAKALA
Mgogoro wa kisera ndani ya CCM usigeuzwe kuwa ni wa kitaifa

HABARI ZA KIMATAIFA 

  • Wachechnya wapania kuidhibiti upya Grozny
  • Wanaoacha umalaya wagawiwa fedha Zamfara
  • n.k

  • Riwaya
    Ndoto ya ajabu

    LISHE 
    Umuhimu wa mafuta mwilini

    Barua/Maoni

    MASHAIRI

    MICHEZO

  • Ligi Kuu sasa kuchezwa kwa makundi
  • Simba kuipa Prisons mazoezi leo 

  • Michuano ya soka Mataifa ya Afrika


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita