|
Na. 034 Jumatano Februari 9 - 15, 2000 |
|
|
|
|
|
Uhuru na ukombozi
NA MWINJILISTI KAMARA KUSUPA HII ni sehemu ya tatu ya mada inayohusu katiba ya nchi yetu na athari
zake katika maisha ya siku kwa siku ya wananchi, kuanzia athari za kiuchumi
mpaka athari za kijamii. Katika makala zilizotangulia tuliona athari kuu
mbili zinazotokana na katiba ya mkoloni ambayo baadaye ilirithishwa kwa
viongozi wa TANU na watawala wa Tanganyika huru, ambao katika uhalisi wa
mambo waliendelea kutawala katika misingi ile ile ya mkoloni kwasababu
misingi hiyo haikufunuliwa ili kujenga misingi mipya inayoendana na mazingira
ya uhuru. Badala yake misingi ya kikoloni iliimarishwa kwa njia ya mabadiliko
ya mara kwa mara ya katiba ya nchi.
KIMSINGI katiba ya Tanzania imenyang'anya mwananchi uwezo wa kumdhibiti mtawala badala yake uwezo mwingi umerundi kwa kwenye taasisi ya utawala na kuwafanya watawala kumdhibiti mwananchi. Katika mazingira ya namna hiyo ambapo mwananchi ndiye anayedhibitiwa na mtawala, moja kwa moja mwananchi anafanana na kiungo kilichopooza kisichoweza kufanya kazi yake. Mwananchi hawezi kuwaondoa watawala wabaya wala viongozi wabovu kwenye nafasi zao hata pale anapobaini kwamba wamefanya mabaya mengi na yaliyokithiri. Kwasababu hana uwezo kikatiba, wala hana haki yoyote ya kisheria kuwagusa watu ambao hahusiki kwa namna yoyote na uteuzi wao. Watawala wa Tanzania wanaishi kama masihi kutoka kwa Mungu. Mwananchi hana haki kisheria ya kumkataa fulani asiwe mkuu wao wa mkoa, au mkuu wa Wilaya, ama Katibu tarafa wala Katibu Kata, kwasababu wote hawa wanateuliwa na kwahiyo wanawajibika kwa mwajiri wao yaani huyo anayewateua. Mwannchi hana "uhuru" wa kukataa neno lolote linalosemwa ama linalofanywa na mtawala hata kama neno hilo lingekuwa baya au bovu kiasi gani, kwasababu katiba ya nchi haimpi uhuru wa aina hiyo. Nasema wazi kwamba katiba yetu bado ina ukoloni kwasababu hairuhusu uhuru kama walionao akina Monica Lewinsky kule U.S.A., kwani tangu mwanzo watu hawakuutilia mkazo uhuru wa mtu binafsi ndani ya katiba badala yake walikazania uhuru wa Tanganyika kama Taifa wa kutotawaliwa na taifa jingine. Baada ya mkoloni kurudi kwao Ulaya wengi wakahesabu kazi ya kudai uhuru imekwisha. UKOLONI NDANI YA KATIBA Tafsiri ya ukoloni ni kitendo cha mtu kutoka mahali pengine na kwenda kumtawala au kusimika utawala wake kwa watu wengine pasipo ridhaa yao na kuwatumia hao wanaotawaliwa kwa manufaa ya huyo au hao wanaotawala. Tofauti kuu ya watawala wa nchi huru na Wakoloni ni ridhaa ya hao wanaotawaliwa, pamoja na uwezo wa hao wanaotawaliwa wa kuwaambia hapana hao wanaotawala. Pia watawaliwa inabidi wawe na uwezo wa kuwaondoa watawala madarakani na kuwaweka wengine madarakani kwa njia halali. Kinyume cha hivyo ni ukoloni. Chini ya ukoloni mtawaliwa hana haki ya kumbadilisha mtawala, wala kumkatalia lolote lile. Siku zote chini ya ukoloni anayetawaliwa analazimika kutii tu na kufanya lile analoamriwa. Kwa bahati mbaya katika Tanzania tumekuwa na uhuru wa Taifa tu kwakuwa hatutawaliwi na Taifa jingine lakini ndani ya hii nchi huru watu hawana uhuru. *Watu hawana uhuru wa kuyakataa mabaya ya mtawala. *Watu hawana huru wa kusema yale yasiyomfurahisha mtawala, bali siku zote watawala wanataka kusikia yale wanayoyapenda wao. Mtu akisema hayo asiyotaka kusikia yeye mtawala, hata kama mtu huyo atakuwa anasema kweli ataitwa mchochezi na rungu la dola litamwangukia. * Watu hawana uhuru wala haki ya kutofautiana na mtawala. Yeyote anayetofautiana na mtawala anaitwa mpinzani kwa lugha ya leo, lakini kwa lugha ya zamani aliitwa mhaini. Kwa utamaduni huu ndiyo maana watawala na hasa Rais ameonesha chuki za waziwazi dhidi ya wapinzani na kuwafanya wawe kama siyo raia wema. * Mwananchi anapokosa uhuru ndani ya nchi huru basi hawezi kuendelea hata kama nchi hiyo ingerundikiwa utajiri wote wa dunia. Hii ni kwasababu maendeleo ya mtu yanapatikana baada ya uhuru. Maendeleo ya nchi yanaletwa na watu walio huru, watu wasio na uhuru hawawezi kuviletea vijiji vyao maendeleo, wala majimbo yao, wala wilaya zao, wala mikoa yao au sehemu zao na taifa lao kwa ujumla. Sababu kuu inayofanya wasiendelee ni kwamba mipango yao ya maendeleo haipangwi na wao wananchi bali inapangwa na watawala wao. Wala vipaumbele au "priorities" zao haziamuliwi na wao wenyewe bali hao wanaowatawala. Wananchi wanapochukua nafasi ya mtumwa na watawala wanapochukua nafasi ya BWANA basi hapo hakuna mjadala wala mwafaka. Watumwa itabidi wakae na kuanglia tu BWANA wao ataamua nini na atafanya nini! Hii ina maana kwamba Bwana akiamua kipaumbele chake kiwe "ULEVI", na matanuzi, ama "anasa", basi hiyo ndiyo itakayokuwa sera ya kutekelezwa na wananchi katika ujumla wao. Watu na uchumi wao watalazimika kuutumikia ulevi, anasa na matanuzi ya wakubwa wao. HASIRA ZA WANANCHI DHIDI YA 'VIBAKA" NA WATAWALA WABAYA Mtu yeyote asiwadanganye kwamba yanaweza kupatikana maendeleo pasipo demokrasia ya kweli maana kinyume cha utawala wa kidemokrasi ni utawala wa kiimla na kidikteta. Wala mtu hawezi kudanganya kwamba "ukoloni" ni mbaya kuliko "Udikteta", kwani vyote ukoloni na udikteta ni ndugu moja, ni utawala ambao mwananchi hana maslahi yoyote bali anaishi kama chombo cha kunufaisha wengine. Inabidi hasira dhidi ya ukoloni sasa zielekezwe kwa tawala zote za kidikteta popote zilipo katika Afrika pasipo kujali madikteta hao wana rangi gani wana dini gani, au kabila gani wala jinsia gani! Hapa Dar es Salaam na sehemu zingine za nchi yetu wananchi wamejenga utamaduni wa kupiga wezi(vibaka) na hatimaye kuwachoma moto. Hii huitwa "mob justice", ingawa siamini kama kweli vibaka huwa wanatendewa haki kwa kuhukumiwa kifo kabla hata ya kujitetea na kusikilizwa. Leo hii mtu akikurupushwa kwa lugha ya mwizi! Mwizi! hata kama atakuwa amekwapua kipande cha muhogo kwasababu ya njaa, basi huyo atakabiliana na hasira za wananchi, atapigwa utadhani watu wanaua nyoka, na hatimaye atachomwa moto. Lakini watu hao hao wakisikia kwamba kuna mabilioni yametoweka kwenye Wizara au mashirika, hawasemi lolote wala hawafanyi lolote kwani huyo aliyeiba anahesabiwa kwamba ameitimiza kauli ya "Chukua chako Mapema." Je hata lini tutaendelea kupiga na kuchoma moto vibaka wanaoiba mihogo na kukwapua heleni za masikioni huku tukawaacha vibaka walioko madarakani wanaoiba mamilioni na mabilioni ya fedha zetu na utajiri wa nchi yetu? Huu ni mfano hai wa mwananchi aliyenyang'anywa uwezo(kikatiba) wa kumdhibiti mtawala. Najua wazi kwamba wananchi hawafurahii wizi wa mabilioni ya fedha zao bali wanachoshindwa kufanya kwa hao wezi wa mabilioni kama wanavyofanya kwa vibaka wa mihogo ni vazi la "utawala". Mtu anapogeuka kuwa mwizi huku akiwa bado amevaa vazi la mtawala basi huyo siyo rahisi kumchoma kwa tairi kama wawafanyiavyo vibaka wengine kwakuwa uhusiano wa kikatiba kati ya mtawala na matawaliwa bado ni ule ule (wa enzi za mkoloni) wa BWANA na MTUMWA. Watumwa hawana ujasiri wa kumnyooshea kidole BWANA wao hata angekuwa dhalimu kiasi gani. Haya ndiyo maisha halisi ya Bongo, na ndiyo yanayosababisha tuwe na vibaka wanaodumu madarakani kwa muda mrefu. Huko vijijini, mwanakijiji hawezi kumnyooshea kidole katibu kata na kumwambia wewe ni mwizi umetuibia kiasi kadhaa cha fedha zetu na mali zetu zingine kwani katibu kata anao uwezo wa kuchapa mtu viboko mbele ya wanawe na hilo likaonekana kama adhabu ya huruma toka kwa mtawala mwema vinginevyo, angeweza hata kumfunga. Huko wilayani mwananchi hana uwezo wa kumnyooshea mkuu wa wilaya, au mbunge au mkurugenzi wa maendeleo wa wilaya na kumwambia umetuibia fedha zetu za kuijenga shule, au barabara. Watawala wanaishi kama miungu ya wilaya, hawaguswi wala hawaelekezwi lolote badala yake hata itokeapo mkutano kati yao na wananchi basi wao watawala ndio wanakuwa na cha kusema kwa wananchi na siyo kusikiliza. Inakuwa kana kwamba mtu kuupata ukubwa basi amepata vyote, anakuwa ndiye mwenye akili kuliko watu anaowatawala na ndiye mwenye kujua hata kuliko wataalamu walio chini ya madaraka yake na pia anakuwa ni "mtakatifu na mwenye haki", kuliko wananchi wengine ndiyo maana hata akiiba haitwi mwizi. Vivyo hivyo mikoani na ngazi zingine za kitaifa kama uwaziri, ukatibu mkuu, na ukuu wa idara au shirika la umma, watawala wamejivika "Umungu mtu." Na hawataki nafasi hiyo ibadilike. Asili ya Umungu mtu katika vyeo vya Tanzania ni Katiba ya nchi (katiba ya Kikoloni) ambayo imempa madaraka ya ziada Rais wa nchi. Sasa kwakuwa hawa watendaji wanateuliwa na Rais, na wanawajibika kwa Rais tu siyo kwa wananchi na pia wanamwakilisha Rais kwenye maeneo yao na nafasi zao, basi nao hao wamerithi huo "Urais wa kifalme" au "Umungumtu." Katibu kata awapo kwenye kata yake ni Rais wa kata, Katibu Tarafa ni Rais wa Tarafa, Mkuu wa Wilaya ni Rais wa Wilaya, Wakati fulani mkuu wa wilaya fulani ambaye ni askari alitishia kumweka ndani mbunge wa upinzani nikashangaa uwezo huo kautoa wapi!, Mkuu wa mkoa ni Rais wa Mkoa n.k. Sasa mwananchi anapotawaliwa na watu wa aina hii walio kama masihi ambao hawezi kuwagusa, basi mwananchi wa leo hana tofauti na Mtanganyika aliyekuwa anatawaliwa na mkoloni ambaye alikuwa haguswi wala habadilishwi. KUPIGA KURA NA KUPIGISHWA KURA Ingawaje vinaweza kuwepo visingizio vya uchaguzi kama ishara au ushahidi wa kuwepo demokrasia katika nchi huru, ukweli ni kwamba demokrasi siyo watu kushiriki uchaguzi tu, bali ni pamoja na watu kuwa na uhuru wa kuchagua viongozi wawatakao na kuwaweka ama kuwaondoa madarakani. Pia demdokrasia inategemea utawala wa siku kwa siku katika maisha ya mwananchi. Kama mwananchi atachagua viongozi lakini akatawaliwa kidikteta huo ni "Ukoloni." Uchaguzi wowote unaofanywa katika jamii ya watu wasio na uhuru, huo siyo uchaguzi bali ni "upakuzi" wa madaraka. Watawala wanapakua madaraka. Katika Tanzania maeneo mengi hasa vijijini wananchi huwa hawapigi kura bali wanapigishwa kura. Mahala ambapo katibu kata akiwaita watu na kuwaagiza kwamba kura zao zote wampe mgombea wa CCM, nao watu wakaipokea hiyo kama amri na agizo la Serikali na wala wasijue kwamba hiyo ni kampeni, kumbe uwapi uhuru wa kuchagua? Kwaajili hiyo hatuwezi kutumainia zoezi la uchaguzi kama njia pekee ya kubadilisha serikali kwasababu tayari zoezi lenyewe limeingiliwa na udanganyifu mwingi hadi kupoteza maana. UHURU NA UKOMBOZI KWANZA KABLA YA MENGINE Kabla ya kupigania mengine yote ni lazima tuupiganie uhuru ili kukamilisha maana halisi ya uhuru. Nchi iwe huru kwa maana ya kutokutawaliwa na taifa jingine na pia mtu binafsi ndani ya nchi huru ni lazima awe huru kwelikweli. Uhuru kama tulio nao sasa ni wa bandia kwa sababu kundi la Warasimu wachache wamewakalia walio wengi na baya zaidi wanawanyonya watu hata kuzidi mkoloni alivyonyonya. Wanaibia watu kwa kiasi ambacho mkoloni hakuwaibia. Baya kuliko yote watawala hao wamejipa kinga ya kikatiba na kujiweka juu ya sheria kiasi kwamba wanaweza kuua na wasichukuliwe hatua yoyote kisheria na hata wahusika wanapolalamika juu ya mauaji hayo wanaitwa wahuni. Hapo hamkani si shwari tena. Inabidi harakatiza ukombozi ziinuke upya na kwa moto ule ule uliomung'oa mkoloni. Wiki ijayo UHURU WA PILI NA UKOMBOZIWA MWANANCHI
UPINZANI OCTOBA 2000 - 2 Na J. Hussein UKIONDOA chama cha wananchi-CUF, NCCR- MAGEUZI ndicho chama cha upinzani chenye idadi kubwa ya wabunge ndani ya bunge la jamhuri ya muungano. Hata hivyo tofauti na CUF ambayo wabunge wake wote ni kutoka visiwani, wabunge wote wa NCCR-MAGEUZI wanatokea katika majimbo ya bara. Kieneo na kwa idadi ya watu visiwani ni sehemu ndogo tu katika jamhuri ya muungano, hivyo basi kuna hisia kwa wananchi wa bara kuwa kila kilicho cha kibara- bara ni kikuu au muhimu kuliko kila kilicho cha kizanzibari-zanzibari. Hisia hizi ndizo zilizopelekea siku za nyuma kabla NCCR-MAGEUZI hakijakumbwa na mgogoro mkubwa uliokigawa katika makundi mawili yanayopingana , kiwe kinatajwa kama ndicho chama kikuu cha upinzani japokuwa kikanuni na kisheria CUF ndio waliokuwa na uongozi rasmi wa upinzani ndani ya bunge. MGOGORO ndani ya NCCR-MAGEUZI- sababu zake na matokeo yake ni vitu ambavyo vimezungumziwa na kuandikwa sana na vyombo vya habari kiasi kwamba huenda kila mtanzania mwenye angalao chembe ya shauku katika siasa za ndani ya nchi, yuko hadhiri navyo. Labda kwa kukumbusha kidogo tu ni kuwa mgawanyiko huu uliongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wakati huo (sasa ni mwenyekiti) Bwana Mabere Marando kwa upande mmoja, na aliyekuwa mwenyekiti wakati huo ( sasa amejiengua, kujiunga na kutwaa uenyekiti wa TLP ), Bwana Agustino Lyatonga Mrema kwa upande mwingine. Kimsingi, haieleweki hasa tofauti zao zilikuwa juu ya nini. Itakumbukwa tu kuwa muda si mrefu baada ya kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho kilichoketi kule Tanga na kuvurugika kufuatia jaribio la kamati kuu ya chama hicho kumvua Mrema uenyekiti wa chama, Bwana Marando na waliomuunga mkono katika hadhara walitoa tuhuma nzito dhidi ya Mrema. Miongoni mwa tuhuma hizi ni kuwa Mrema ni kiongozi mwenye upeo mdogo, asiyetaka ushauri, ambaye akili yake yote imejaa 'kwenda ikulu', mwenye tabia ya kudhalilisha wanachama wa kike kijinsia, na anayeongoza chama kidikteta. Bwana Mrema naye na wale waliomuunga mkono walimtuhumu Marando hadharani kwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nia ya kumwengua mwenyekiti ili aweze kutumia ruzuku ya chama toka serikalini apendavyo, kutumiwa na serikali kuvuruga upinzani kwa nia ya kuinufaisha CCM, kuwa hakuwa na haja na Mrema tena baada ya Mrema kumpandisha (Marando na wenzake) chati kisiasa n.k. Kujiengua kwa Mrema kutoka NCCR-MAGEUZI hatimaye kulifanikiwa kuzima mgogoro ndani ya chama hicho. Tatizo tu ni kwamba kujiengua huko kumesababisha chama hicho kuhamwa na idadi kubwa ya wanachama wake ambao kimsingi utiifu wao kwa Mrema ulikuwa mkubwa zaidi kuliko kwa chama. Si hivyo tu, hata kwa wananchi tu wa kawaida ambao si wanachama wa chama chochote cha siasa wengi wao hivi sasa wanakizungumzia chama hicho kimashaka mashaka na kuna kila dalili kuwa hata sasa bado kuna kutokuelewana kwa viongozi na wanachama ndani ya chama hicho. Kwa kweli utakuwa ni muujiza mtupu kama NCCR-MAGEUZI kitaweza kutwaa madaraka ya nchi katika uchaguzi mkuu ujao. Tumaini pekee ililonalo ni kujitahidi kung'ang'ania isipoteze idadi kubwa ya viti vya bunge inavyovishikilia hivi sasa, japo kwa hali halisi ilivyo hata kazi hiyo itakuwa ni kibarua cha kutosha. Nina hisia kuwa baadhi ya wale wabunge wa NCCR-MAGEUZI ambao watapenda kurejea bungeni baada ya uchaguzi mkuu ujao watashawishika kukihama chama hicho na kuzamia katika baadhi ya vyama vingine vya upinzani. TLP ni chama ambacho hakikuwa na umaarufu wowote kabla mwenyekiti wake wa sasa, Bwana Agustino Lyatonga Mrema hajajiunga nacho baada ya kujiengua kutoka NCCR-MAGEUZI. Bwana Mrema si kwamba tu alijiunga na TLP, bali pia alikiletea mvua ya wanachama ambao walikuwa wameamua kujiengua kutoaka NCCR-MAGEUZI ili kumfuata. Kufuatia hatua hii ya Bwana Mrema TLP kimefanikiwa kubadilika kwa muda mfupi , kupanda chati na kuwa chama kinachotajika kitaifa. Hata hivyo mabadiliko haya ya ghafla yamepanda mbegu ya mgogoro katika chama hiki kwani baadhi ya wanachama wake walipinga hatua ya waliokuwa viongozi wa chama hicho kuukabidhi uongozi wa chama hicho kwa Mrema na wapambe wake 'kienyeji'. Baadhi ya wanachama hawa walifungua kesi mahakamani kupinga hatua hii jambo ambalo lilisababisha mahakama kumzuia kwa muda Mrema na viongozi wenzake wa 'papo kwa papo' kujishughulisha na shughuli za uongozi wa chama hicho. Hata hivyo baadaye mahakama iliwahalalisha Mrema na wenzake kuendelea na uongozi wa chama hicho. Mgogoro huu uliokuwa unachipua ndani ya TLP, japo kwa hivi sasa umefifia, lakini umeacha athari fulani mbaya kwa Mrema na TLP yenyewe. Watu wanajiuliza Mrema hakujifunza chochote kutokana na mgogoro uliomuondoa NCCR-MAGEUZI? Alitegemea nini zaidi ya mgogoro ndani ya chama chake kipya cha TLP iwapo ile kujiunga tu anaibuka akiwa amekabidhiwa madaraka ya uenyekiti katika mazingira ya kutatanisha? Inawezekana ikawa iko kwenye damu ya Mrema kuwa shida yake kubwa ni madaraka? Maswali ya aina hii pamoja na matamshi yake ya mara kwa mara yasiochujwa, ikiwa ni pamoja na 'kulipua mabomu' ambayo hayajafanyiwa utafiti wa kutosha yamesababisha zianze kujitokeza hisia kuwa hana subira, siyo makini, na ni mtu anayeabudu umaarufu. Hisia hizi ambazo zinasambaa haraka zimewafanya watu wengi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya waliokuwa wapenzi wake wa damu wakiri kimya kimya kuwa Mrema huenda hafai kuwa mkuu wa nchi. Katika uchaguzi mkuu uliopita Mrema kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, alikuwa ni mshindi wa pili nyuma ya rais Benjamin William Mkapa kwa kupata asilimia ishirini na tisa ya kura. Tukumbuke kuwa Mrema alianza kampeni iliyomzungusha nchi nzima miezi kadhaa kabla ya kipindi rasmi cha kampeni, kwa kutumia kivuli cha kujitambulisha rasmi kwa wananchi baada ya kujiengua CCM na kujiunga na NCCR-MAGEUZI. Na kama tutakuwa wakweli na nafsi zetu, inabidi tukiri kwamba katika kipindi hiki Mrema alikuwa amefikia juu kileleni katika chati yake ya umaarufu. Hali kadhalika lazima tukiri kuwa uwezo wa kioganaizesheni uliionyeshwa na NCCR-MAGEUZI kipindi kile hauna dalili yoyote ya kufikiwa na TLP hata kwa mbali katika kipindi hiki tulipo. Sasa inabidi tujiulize, je, kama Mrema mbali ya yote haya aliishia na kupata asilimia ishirini na tisa tu ya kura, vipi nafasi yake leo hii? Binafsi naamini kabisa kuwa Mrema katika uchaguzi huu ujao nafasi yake ya kufanya vizuri ni ndogo zaidi kuliko hata katika uchaguzi uliopita. Hata hivyo anaweza kuchakarika na kufanikiwa kurejea bungeni yeye binafsi na kusaidia kuwapigia debe baadhi ya wanachama wenzake ndani ya TLP kunyakua ubunge katika baadhi ya majimbo. Ingekuwa ni vizuri kama Mrema na wenzake ndani ya TLP wangechagua kujiunga na umoja uliokusudiwa na vyama vya CUF, UDP na CHADEMA unaokusudia kuteua mgombea mmoja tu wa kiti cha urais kupambana na atakayekuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao. Chama Cha Wananchi-CUF kikanuni ndicho chama kikuu cha upinzani katika jamhuri ya muungano wa Tanzania. Nasema kikanuni kwa sababu mbali ya kwamba ndicho chama cha upinzani chenye idadi kubwa ya wabunge ndani ya bunge- na hivyo kisheria kupata fursa ya kuunda serikali kivuli bungeni, hakuna hata mmoja miongoni mwao anayetoka Tanzania bara. Moja wapo ya sababu zilizopelekea hali hii ni ukweli kwamba wakati uchaguzi mkuu wa Oktoba 1995 unaingia, ndio kwanza chama hiki kilikuwa kimetoka kuibuka katika mgogoro mkubwa wa kiuongozi. Hatima ya mgogoro huu ilikuwa ni kuondolewa na wanachama katika uongozi viongozi wengi akiwemo aliyekuwa mwenyekiti, Bwana James Mapalala. Huu ni mgogoro ambao uliuathiri upande wa bara kwa kiasi kikubwa kwani mbali ya Mapalala, wengi wa viongozi wengine walioondolewa walitokea bara. Hivyo basi wakati uchaguzi mkuu unaingia ndio kwanza CUF upande wa bara ilikuwa inajaribu kujijenga upya kiungozi, na kwa kweli kulikuwa hakuna maandalizi yoyote ya maana ambayo yangepelekea chama hiki kishiriki kikamilifu katika uchaguzi. Kwa kutambua tatizo hili CUF iliingia katika makubaliano na NCCR-MAGEUZI na CHADEMA kumuunga mkono Agustino Lyatonga Mrema katika kinyang'anyiro cha kura ya urais, makubaliano ambayo hata hivyo yalivunjwa na NCCR-MAGEUZI siku chache kabla ya siku ya mwisho ya kuwasilisha majina ya wagombea urais wa kila chama kwa tume ya uchaguzi. Kufuatia kuvunjika kwa makubaliano haya CUF iliamua pamoja na kuwa na maandalizi duni, kuingiza mgombea wake katika kinyang'anyiro cha kiti cha urais; na kumteua mwanachama wa kawaida- Profesa Ibrahim Harun Lipumba kuwania kiti hicho akisaidiwa na mwanachama mwingine wa kawaida, Bwana Juma Duni Haji kama mgombea mwenza,. Ni uamuzi ambao nadhani CUF hawatakaa waujutie kamwe. Uamuzi huu ndio chanzo cha umaarufu mkubwa iliyonayo CUF hivi sasa na kwa kweli umekuwa ni kama kaa la moto kwenye mfumo wa neva wa CCM. Kutokana na mchanganyiko wa sababu mbalimbali, miongoni mwa vyama vyote vya upinzani CCM inaiona CUF kuwa ndiyo adui namba moja na tishio kubwa kwake kisiasa. Kwanza kabisa ni kutokana na ukweli kuwa kwa kiasi kikubwa kisiasa CCM imeipoteza Zanzibar kwa CUF na uwezekano wa kugeuza mwelekeo wa kisiasa kwa njia za kidemokrasia unaonekana ni finyu. Pili, ni tatizo ambalo kimsingi ni la kisera na lina uwezo mkubwa wa kuifanya CCM iipoteze bara kwa CUF kisiasa. Sera zote za CUF zimeegemezwa katika sera kuu mbili- yaani: HAKI SAWA KWA WOTE NA UTAJIRISHO. Kwa bahati mbaya sana kwa CCM, haya ni maeneo ambayo chama hicho kina rekodi mbaya, mbaya, mbaya. Ni mtu mpumbavu tu anayeweza kusimama hadharani na akatetea kwa dhati kuwa haki za raia wote wa Tanzania zinalindwa kwa kiwango kilekile- yaani bila kujali tabaka lake kiuchumi, imani ya dini yake, au mwelekeo wake kisiasa. Hali kadhalika hakuna mtu ambaye akiwa na akili zake timamu kabisa anaweza kwa dhati yake kukanusha ukweli kwamba watanzania wanaishi katika dimbwi la umasikini na kuwa kwa kiwango kikubwa umasikini huu unafanya kufugwa. Hivyo basi sera hizi mbili za CUF zina hatari ya kipekee kwa CCM. Mfano halisi wa jinsi CCM inavyotishwa na sera hizi za CUF unajidhihirisha vizuri zaidi katika suala la Uislamu na waislam nchini. Kwa miaka nenda rudi kundi kubwa la wananchi wa Tanzania - waislamu, wamekuwa wakipiga kelele kwamba hawatendewi haki . Serikali ya CCM au imechagua wakati mwingine kukaa kimya na kuwapuuza, au wakati mwingine kutoa majibu ya kejeli, au wakati mwingine inaposhindwa kuvumilia 'kero' hizo za waislam kutumia nguvu za dola. CCM kwa kuona hatari iliyopo ndani ya sera ya CUF ya 'haki sawa kwa wote'kuwa inaweza kuwa ni kivutio kikubwa kwa waislam ambao idadi yao inatosha kabisa kuifanya CUF iipate bara bila msaada wa chama kingine chochote, imeamua kuanzisha vita ya kisaikologia- vita ambayo kutokana na aina ya silaha CCM ilizochagua kutumia, ni chafu na ya hatari kabisa- si kwa chama hicho pinzani tu, bali hata kwa mustakabali wa baadaye wa taifa hili. Kwa msaada wa mtandao wa vyombo vya habari unaojumuisha vile vya CCM yenyewe na jumuia zake, vya serikali na vya makampuni binafsi, CCM inatumia nguvu nyingi na gharama kubwa kuuhadaa umma wa Tanzania na ulimwengu kwa ujumla kuwa CUF inatumia misikiti kama majukwaa ya kisiasa. Mbinu hii ina malengo makubwa matatu. Kwanza imelenga katika kuijengea CUF mazingira ya kupoteza muda mwingi kujitetea- na mtu yeyote anayepoteza muda mwingi kila mara kujitetea katika tuhuma fulani ambazo kila mara ni yeye tu zinaelekezwa kwake- kwenye macho ya watu wengi moja kwa moja mtu huyo ni anageuka kuwa mhalifu. Pili, imelenga katika kuwafanya viongozi wa CUF waingie hofu, hivyo wawe wanajiuma uma tu 'haki sawa kwa wote inapoingia kwenye suala la waislam', na hivyo kuwafanya waislam wasiwaamini. Na tatu, imelenga katika kuwatisha wakiristo waone kwamba maisha na maslahi yao yako hatarini sana na tumaini lao pekee ni kutogawa nguvu yao na potelea mbali hata kama CCM wengine hawaipendi, bora waiunge mkono iwe nusu shari kuliko shari kamili. Mbinu hii ya hatari hadi sasa imefanya kazi kwa mafanikio makubwa. Imewafanya wakristo wengi na hata baadhi ya waislam- hasa wale wavivu kufikiri, waiangalie CUF kwa macho ya woga. Hata hivyo mbinu hii ina mapungufu makubwa mawili ambayo kama CUF itayaona na iyatumie kikamilifu basi CCM itakuwa imejikaanga kwa mafuta yake yenyewe. Kwanza kabisa viongozi wa CUF wanaweza waamue kuivaa CCM kichwa kichwa na waseme wazi kwamba watakapoingia madarakani miongoni mwa mambo ya kwanza kuyafanya ni 'kuunda tume huru ya kitaalamu' kwa mfano wa ile ya Africa Kusini chini ya askofu Tutu- kuchunguza na kuthibitisha au kukanusha, madai ya waislam, wakiristo, au kundi jingine lolote linalohisi lina madai yake- kama njia pekee ya uhakika ya kuhakikisha kwamba ukweli unajulikana, haki inatendeka na hivyo kuondoa mazingira ya kushawishi kuvunjika kwa amani na kuondoka kwa utulivu. Pili, CCM kabla ya kuanzisha vita hii ilitakiwa isimame kwenye kioo kirefu ijikague kwa makini toka utosini hadi kwenye dole gumba la mguu. Kwa sababu gani? Sababu ni kwamba CCM ndicho chama pekee cha siasa hapa Tanzania ambacho kiko kwenye rekodi zilizofanyiwa utafiti wa kina , kuonyeshwa kuwa kimekuwa kikichanganya siasa na dini kikamilifu kwa nia ya kuendeleza maslahi ya wakiristo na kudidimiza yale ya waislamu katika kipindi chote ambacho imekaa madarakani. Kwa kuwa si kazi kubwa kupata rekodi hizo na kuwa nazo mkononi, CCM inapaswa kujiuliza ni kitu gani itakivuna iwapo watafiti wa CUF watazipata rekodi hizi na viongozi wao wasione kinyaa kuzitumia majukwaani. Kwa upande wa sera ya utajirisho, CUF imepata bahati mara mbili- na ambayo ni nuksi mara mbili kwa CCM. Kwanza kabisa hivi sasa watanzania wengi ni maskini mno(CCM haiwezi hata kidogo kukwepa lawama) kiasi ambacho ni wakati mzuri mno wa kuuza sera kama hiyo. Pili, CUF kwa kiasi kikubwa sana inaweza ikaaminika ikitamba na sera kama hiyo kwa sababu wana nyenzo muhimu inayoweza kuibadili sera hiyo kutoka kwenye makaratasi tu kuwa kweli!- Profesa Lipumba. Lipumba si tu kuwa ni Profesa wa uchumi- hawa wako wengi, bali ni mchumi mwenye sifa za kimataifa. Canada, Marekani, Japani, Finland, Uingereza, Brazili, Uganda, Zimbabwe, U.N n.k., ni baadhi tu ya maeneo ambayo Lipumba ameshawahi kutoa ushauri wake katika masuala ya uchumi. Kwa kifupi ni kwamba, kama ni kompyuta ambayo tungeiomba ituchagulie rais kwenye uchaguzi mkuu ujao katika misingi ya yule ambaye ana uwezekano mkubwa wa kututoa katika lindi la umasikini linalotuzunguka hivi sasa- kompyuta haipokei rushwa wala haisikilizi propaganda za kipumbavu- bila kuchelewa ingetutolea jibu kwamba kwa asilimia mia moja rais huyo ni Lipumba! Mbali ya yote haya, je Lipumba na CUF wana uwezo wa kutwaa madaraka ya nchi katika uchaguzi mkuu ujao na kuunda serikali? Awali nilisema kuwa siamini kuwa CUF itakaa iujutie uamuzi wake wa kumsimamisha Lipumba katika uchaguzi mkuu uliopita. Sababu yenyewe ni rahisi. Kwanza Lipumba aliingia kwenye uchaguzi ule akiwa hajulikani kabisa kisiasa. Pili, yeye na mwenzake, Juma Duni ndio waliooendesha kampeni kimaskini kuliko wagombea wote ( mapostas ya photocopy nyeusi na nyeupe, magari ya kuazima, uwezo sifuri wa kutoa matangazo, uwezo mdogo mno wa kugharamia mawakala, n.k.) na hata hivyo walifanikiwa- kwa mujibu wa matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi -kupata asilimia sita ya kura na kushika nafasi ya tatu kati ya wagombea wanne! Kilichotokea ni kwamba muda mfupi tu baada ya kampeni kuanza ilidhihirika wazi kwa kila mtu kuwa kati ya wagombea wote Lipumba alikuwa bora zaidi.Alikuwa ndiye mgombea pekee aliyeweza kuyaelezea kwa ufasaha matatizo yetu na kuelezea ni kitu gani kinahitajika kifanywe ili kuyatatua. Alikuwa ndiye mgombea pekee aliyeruhusu kuulizwa maswali katika mikutano ya kampeni naye akayajibu kwa uaminifu. Mathalani, katika mkutano uliofanyika katika chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) wanafunzi ambao awali walivaa sura zilizojaa uadui walijikuta wanachangamka ghafla baada ya kukuta maswali yao yote yanapata majibu ya kutosheleza, wakachomoa notibuku zao na kuanza kuchukua notes! Tatizo kwa watu wengi kwa mujibu wa maelezo yao wenyewe ni kwamba walisita kumpa kura zao eti kwa kuwa walikuwa hawamjui! Sababu hii ukichanganya na maandalizi duni ya CUF kwenye uchaguzi ule vilichanagia sana kumpotezea Lipumba kura nyingi za wazi kabisa. Lipumba baada ya uchaguzi mkuu alilazimika kuondoka nchini kwa muda kufuatia chuo kikuu cha Dar es salaam- ambacho ndicho kilichokuwa mwajiri wake, kumwachisha kazi. Ni kiasi gani hali hii ililetwa na shinikizo za kisiasa ni utawala pekee wa chuo hicho unaoweza kutubainishia. Vyovyote iwavyo, Lipumba hakuwa na jinsi. Mbali ya kwamba sasa hakuwa na njia ya uhakika ya kujipatia riziki - naye kutokuwa tayari kusubiri kuvizia vizia ruzuku ya chama- mataifa mengi ya nje yalimbembeleza aende kuyasaidia. Hivyo basi Lipumba kwa kipindi cha karibu miaka mitatu baada ya uchaguzi wa Oktoba 1995, ukiondoa mawasiliano ya karibu yaliyokuwepo kati yake na chama chake, alitoweka katika uwanja wa siasa za Tanzania. Mwaka mmoja uliopita Lipumba alirejea nchini na kuanza tena rasmi harakati za kisiasa. Mwaka mmoja ni muda mfupi sana lakini Lipumba amedhihirisha kuwa yeye si mchumi mahiri tu, bali ni mwanasiasa mwenye kipaji cha hali ya juu. Katika kipindi hiki kifupi tu ameweza kuigeuza CUF bara kutoka kuwa chama cha maofisini ( kama vilivyo vyama vingi vingine) na kukikabidhi kwa wananchi tena katika sura ya kitaifa hasa- hatua ambayo ilipelekea wanachama wa chama hicho kumchagua kuwa mwenyekiti wao kwa kauli moja kufuatia aliyekuwa mwenyekiti, mzee Msobi Mageni kuamua kustaafu shughuli za uongozi. Matokeo ya chaguzi ndogo za Ubungo na Temeke na ule wa serikali za mitaa hivi karibuni unatoa ushahidi ni jinsi gani CUF katika kipindi kifupi sana imekuwa ni mali ya wananchi . Ni wazi kabisa kuwa kati ya sasa na Oktoba kabla ya uchaguzi Lipumba ana uwezo kabisa wa kuunganisha sehemu kubwa ya watanzania nyuma yake tayari kwa kuiondoa CCM madarakani. Makubaliano ya Cheyo, Makani, na Lipumba ya kuunganisha nguvu zao katika uchaguzi mkuu ujao ni ya kuungwa mkono kwani yatazidi kuibana CCM. Hata hivyo ushauri wangu kwa viongozi hao ni kuwa ni muhimu wananchi tumjue watakayempa nafasi hiyo ya kugombea mapema, na huo uteuzi uzingatie sifa na mahitaji ya taifa hivi sasa na si vinginevyo. Inabidi wawe waangalifu hasa wasije wakaunda umoja ambao utasusiwa na wapiga kura. |
YALIYOMO
Tahariri:
Serikali inakwamisha barabara ya Kibiti-Lindi -CUF Waislamu kuadhimisha mauaji ya Mwembechai J’pili Wazanzibar sasa wataka kuuona Mkataba wa Muungano Wanawake wa Kiislamu watakiwa kupinga unyanyasaji wa kijinsia Rufaa za chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji MAKALA
MAKALA
Kalamu
ya Mwandishi
Makala
USHAURI
NASAHA
MAKALA
LISHE
Michuano ya soka Mataifa ya Afrika |
|
|
|
|