AN-NUUR 
Na.179 Shaaban  1419, Desemba 11 - 17, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Historia Form IV

Upinzani dhidi ya Serikali ya Kiislamu wakati wa Khalifa wa Kwanza  

Katika vita vya Daba adui alishindwa na uasi ukatokomezwa. Hadharamawti nako kulikuwa na uasi. Gavana wa jimbo hili alikuwa Mu hajir ambae alikwenda Madina, na nafasi yake ilishikiliwa na Ziad. Nyuma yake Ash’ath Ibn Qais chifu wa kabila la Kindi aliongoza maasi dhidi ya Ziad. Taarifa zilipofika Madina Muhajir alirudi na wapiganaji, akaungana na Ziad, na Ikrima aliyekuwa anatokea Oman na kumshinda Ashath ambae alikamatwa mateka na kupelekwa Madina alikoachiwa huru na Khalifa.52 

Mitume wa uongo nao ambao idadi yao ilikuwa wanne walinyamazishwa. Mitume bandia hawa ni Aswad Ausi, Tulaiha, Sajah bint Alharith na Musailamah Al-kadh-dhab. (mzandiki). Aswad alitangaza utume wake Yemen baada ya kukusanya jeshi kubwa. Mtume huyu wa uwongo aliyekuwa anajitanda uso wote hata akaitwa mtume anaejitanda aliuliwa na Qais ibn Makshuh aliyekuwa chifu wa Waarabu akishirikiana na Feroze Dailme na Darweih. Khalifa Abubakr alimteua Feroze kuwa kamanda wake - Yemen na wale wenzie wamsaidie. Lakini Qais alimuua Feroze na Darweih alikimbia kuokoa maisha yake, wakati huo huo jeshi la Waislamu lilikuwa linaelekea Yemen chini ya uongozi wa Muhajir. Qais na Amr waliungana kuzuia majeshi ya Khalifa lakini walishindwa walikamatwa mateka na kupelekwa kwa Khalifa Madina ambako walisamehewa.53 Kwa namna hii mtume wa uongo Aswad aliekufa na uasi ukazimwa katika jimbo la Yemen. Tulaiha anatoka katika kabila la Bani Asad kaskazini mwa Arabia. Mara baada ya kifo cha Mtume, alijiitangazia utume. Khalifa Abubakr alimtuma Khalid bin Walid kuzima uasi huu. Khalid alikuwa jemedari mwenye kipaji cha kupigana. anarekodiwa kuwa miongoni mwa majemadali wa dunia. Mtume (s.a.w.) kwa uhodari wake alimwita "Upanga wa Mwenyezi Mungu" 54 Khalid alishinda makabila yote yaliyokuwa yanamuunga mkono Tulaiha, wakiwemo Bani Tay, Bani Ghatfan na Bani Asad. Katika vita vilivyopiganiwa mahali paitwapo Bozakha, Jeshi la adui liliongozwa na Uyeina. Tulaiha alikimbilia Syria na mkewe, Uyeina alikamatwa mateka na kupelekwa Madina pamoja na watemi wengine wawili ambako baada ya kuomba msamaha walisamehewa. 

Sajah bint Al-Harith anatoka katika kabila la Bani Tamim. Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.) watemi wengi wa kabila hili waliritadi ndipo Sajah akajitangazia utume. Sajah alikusanya watu elfu nne tayari kuelekea Madina. Alipokuwa anakwenda Madina akapata habari za jeshi la Khalid bin Walid lilivyomuangamiza Tulaiha. Aliingiwa na khofu kwenda Madina. Kwa udhuru huu akamuandikia Musailimah mzandiki washirikiane ambae nae alikwisha tangaza utume wake. Sajah aliungana Musailamah mzandiki na kutambua utume wake. Wakati huo huo, Khalid bin Walid alifika makao makuu ya kabila la Bani Tamim na kutuliza uasi. Baada ya kutuliza fujo za kabila la Bani Tamim Khalid alimgeukia Musailimah Al-kadh-dhab. 

Kati ya Arabia ndipo penye kitongoji cha Yamama lilipokuwa linaishi kabila la Bani Hanifa. Bani Hanifa hawakusilimu. Katika siku za mwisho za Utume katika mwaka wa kumi hijra (10 A.H.) Musailimah alijitangazia utume na akamuandikia Mtume (s.a.w.) juu ya utume wake na kumtaka wagawane Dunia nusu kwa nusu katika kuiendesha. Mtume (s.a.w.) alimjibu, "Kutoka kwa Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Musailimah alkadhab mzandiki. Dunia iko chini ya ufalme wa Mwenyezi Mungu na humuachia kuitawala amtakae. Na mwisho mwema ni wa wakweli."55 Musailimah alikuwa na wafuasi wengi. Hivyo alikusanya jeshi la watu arobaini elfu 8 lililopigana na jeshi la Waislamu la watu elfu kumi na tatu liliongozwa na Khalid bin Walid. Ikrima na Shurahbil walitangulia lakini walishindwa. Kuwasili kwa Khalid kuliwapelekea kukusanya nguvu na kufikia askari kumi na tatu elfu dhidi ya adui aliyekuwa na jeshi la arubaini elfu. Pambano hili ambalo matokeo yake yalikuwa "Bustani ya Vifo: lilikuwa kali sana na lenye matokeo ya kuelemewa kwa adui. Waislamu waliwaangamiza Bani Hanifa na wasaidizi wao, wakawauwa adui 21,000 56 (ishirini na moja elfu) pamoja na Musailamah aliyeuliwa na Wahshiy aliyemuua Hamza katika vita vya Uhud. Waislamu waliouawa ni mia nane (800) wakiwemo maswahaba 360 (mia tatu sitini) wengi wao wakiwa wamehifadhi Qur’an 11. Vita hivi vilipiganwa mnamo mwaka 633 A.D. au 11 A.H. vilichukua miezi saba. Vita vya Yamama vilimalizia uasi wa Riddah na Dola ikarudia utulivu. 

Upinzani kutoka kwa Wakristo 

Chokochoko nyingine wakati wa uongozi wa Abubakr ulitoka kwa Wapeshia au Waajemi na Warumi au Dola ya Wakristu wa Kirumi. Upande wa kaskazini Dola ya Kiislamu ilipakana na uajemi (Persia) au Iraq. Jimbo hasa lililopakana na Dola ya Kiislamu linaitwa Chaldea na Hira 6 au Persia ya Sasanid. 

Miongoni mwa hoja zilizopelekea upinzani baina ya Persia na Dola ya Kiislamu ni kuutukana ujumbe wa Mtume uliotumwa kwa mfalme wa Persia Chosroes II aliyejulikana katika Historia ya Persia kwa jina la Khushraw Parwiz. Huu ni uchokozi ulio dhahiri si hivyo tu lakini Waajemi walisaidia waasi wa Bahrein. wakazi wa jimbo la Hira walikuwa Fellaheen ambao ni Waarabu, Banu Bakr, Denkans na Lakh-mite n.k. miongoni mwao yapo makabila yaliyosilimu kama Banu Bakr na Fellaheen na yapo makabila ambayo hayakusilimu. Katika uasi wa jimbo la Bahrein, Waajemi walisaidia waasi hao na huu ulikuwa uchokozi dhahiri kwa Dola ya Kiislamu. Uchokozi wa Waajemi hawa ambao walikuwa mushriks, haukuishia hapa lakini walikabiliana na Muthana bin al-Harithah chifu wa Banu shayban ukoo wa kabila la Banu Bakr ambao ni Waislamu. Hali hii ikapelekea kuzuka kwa vita baina ya Dola ya Kiislamu na uajemi. Kama kawaida Waislamu siku zote waliingizwa kwenye vita kutokana na uchokozi wa adui; haijatokea kupigana vita vya uchokozi. 

Muthana alipokabiliana na jeshi la Waajemi alilazimika kuomba msaada kutoka kwa Khalifa ambae baada ya kushauriana na shura yake alitumwa Khalid bin Walid na jeshi lake na wakakutana na kuungana na jeshi la muthanna mnamo mwaka 12 A.H. sawa na 633 A.C. mahali paitwapo Ubillah. 

Kama ilivyokwisha elezwa kuwa Waislamu huingizwa kwenye vita na uadui, lakini hata baada ya kuingizwa kwenye vita, kabla ya kupigana hujaribu kutafuta suluhu ya amani ama kwa kutumia wajumbe au barua. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Wapeshia. Generali Khalid Simba wa Mwenyezi Mungu kabla kuanza vita alimuandikia Hurmuz Generali maarufu wa kivita wa Waajemi aliyekuwa anaongoza jeshi la Waajemi kuwa: 

"Tumekuletea Neno la Mwenyezi Mungu Uislamu, Hatuna lengo la kupigana, ukubali Uislamu njia ya maisha ya amani, utakuwa salama. Kama hutaki, tupishe ili tuwafikishie watu wako maelezo ya njia hii ya maisha iliyo bora, ukikubali Uislamu unapaswa kulipa Jizya kwa Khalifa. Kama hukubali lolote kati ya haya, njia iliyosalia ni kutumia upanga. Kabla hujakubali kupigana uzingatie tu kuwa, ninakuletea wapiganaji wanaopenda kufa kuliko mnavyopenda maisha yenu"57

Waajemi walijiona sana, wao na Warumi walikuwa ndio mataifa yaliyokuwa yanatajika kivita, hivyo hawakutilia manani maelezo ya Khalid na wakaamua kupigana. 

Vita kubwa iliyopiganwa baina ya Waislamu na Waajemi ni vita vya mikufu iliyopiganiwa mahali paitwapo Hafir. Jeshi la adui lilikuwa kubwa kuliko la Waislamu, lakini kutokana na ahadi ya Mwenyezi Mungu kuwa kundi la Allah ndilo litakaloshinda na pia nguvu ya Muislamu mmoja ni sawa na watu ishirini. Waislamu waliibuka washindi. Lakini vita haikuwa hii tu, kwani April 633 na Machi 634 Khalid alipigana kishujaa kabisa na kuwashinda Waajemi katika mapigano kumi na tano 58 yakiwemo yale ya Ubullah, Mazar Walajah, Allis, Hirah, Anbar, Ayntamar na Dumatul-Jandal.59 Ushindi huu ulizima uchokozi wa Waajemi na kuifanya Dola ya Kiislamu kupanuka na kufikia Iraq (Uajemi) magharibi ya mto Tigris au Iraq ya kusini na sehemu kubwa ya Iraq kaskazini. 60 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani?

Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha

Serikali yagwaya kwa wafugaji nguruwe 
Na Muhibu Said

Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Na Maalim Mwalimu

Adabu katika swala

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Na Ally Said

Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya  (a.s.)
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe

Ijue SUA Madrasa Moro
Na Mussa Ally, Morogoro

Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli

Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha

Akina mama Muheza waungana kufanya Daawa
Na B. Mwakangwale

Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata uongozi
Na B.  Mwakangwale

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 2
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzima ni nyembamba,  waionao ni wachache - 2
Na Yasin Valerian Massawe

Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Jongo  aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki  A.

Waislamu Mlimba Moro mashakani
Na Q. Mataita

Sayansi na Teknolojia 
[Ielewe Modem yako] 
 
Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Futari ya Tende] 
 
Tangazo
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita