AN-NUUR 
Na.179 Shaaban  1419, Desemba 11 - 17, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Tathmini
Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
 

Kipi Watanzania tunajivunia? 

Na Maalim Mwalimu 

MIAKA 37 iliyopita Watanganyika walikuwa wanasheherekea fungate ya uhuru. Matumaini na matazamio yao ndiyo yaliwafanya wawe katika hali ya kushereheka. 

Wakati ule watu walidhani nchi ilishapata uhuru, mambo kama kunyanyaswa, kubaguliwa, kutawaliwa, kipato duni, umaskini, maradhi, magonjwa na mengineyo yangekoma. 

Wale waliojaaliwa kushuhudia miaka 37 ya uhuru ule bila shaka tunaiona hali kama ilivyo, hali ambayo imejenga mazingira ambayo Mtanganyika anahitaji kusimama tena kujikomboa. 

Wakati wa ukoloni, huduma za jamii mfano elimu, afya, maji na usafiri ziligawanywa kulingana na tabaka la mtu. Ubora na kiasi cha huduma fulani kilitegemea rangi au taifa la mtu husika. Wazungu ndiyo waliofaidi zaidi, wakifuatiwa na Wahindi halafu watu weusi Wakristo. Uhuru ulitegemewa ulete usawa. Leo bado matabaka yapo. 

Wako Wazungu weusi. Huduma zao za afya, elimu, mawasiliano n.k. ni tofauti na wenzao. Kwa sababu wamo katika matabaka tofauti. Kimsingi hali zao za kijamii na kiuchumi ni bora zaidi kuliko wananchi wengine.  

Iliahidiwa vile vile kuwa watu wote wangeishi katika misingi ya usawa. Hapana ruhusa kubaguana na kuwa rasilimali za taifa zingetumika kwa faida ya wote. 

Katika miaka ya mwanzo ya uhuru vikaundwa vyama mbalimbali kama vile Jumuiya ya Wafanyakazi (NUTA), Jumuiya ya Wazazi (TAPA), Jumuiya ya Wanawake (UWT) na vyama vya ushirika kwa ajili ya wakulima na wafugaji. Wakati ule ilidaiwa kwamba "ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio huru na sawa". Ikatangazwa kuwa mali (njia kuu zote za uchumi) ni mali ya umma. Ikawa ni haramu mtu kumiliki majumba, viwanda, viwanja, mashamba n.k. huku akiwa kiongozi. Haya yakapigiwa debe mpaka wananchi wakaamini kuwa wanatawaliwa na viongozi bora wenye fikra sahihi na za kudumu! 

Leo wakati tunaadhimisha miaka 37 ya uhuru na tukiwa na takriban viongozi wale wale walioharamisha yaliyosemwa hapo juu nchi imekumbwa na ububu. Haisemwi tena kama ujamaa na kujitegemea ndiyo juu, juu juu zaidi! Na wala hatuambiwi iwapo tumeshakuwa huru na sawa! Hizo njia kuu zilizomilikiwa na umma sasa zinauzwa. Baadhi ya wanunuzi wake ni wale wale waliopiga debe hapo awali hadi wananchi wakadhania kuwa wanaongozwa na ‘Mitume’. 

Leo hii wakulima hawana mtetezi, vyama vyao vya ushirika vimefishwa. Wafanyakazi hali kadhalika. 

Cha kutisha zaidi ni kuwa wale waliopewa dhamana ya uongozi katika vyama, viwanda, mashirika, mashamba na sehemu nyingine wao wanaishi ndani ya mageti katika majumba ya kisasa, kitu kinachoashiria tofauti ya matabaka yao na wananchi. Wengine watoto wao wanasoma nje, wake zao huenda sokoni kwa magari, barabara za maeneo wanayoishi zina lami. 

Kwa nafasi zao wanaweza kukopa magari wapendavyo na pia kupatiwa mikopo katika mifuko ya wafanyakazi bila ya wale wanaochangia mifuko hiyo kujua. Kwa nafasi zao wanamiliki mashamba makubwa yenye maelfu ya ekari katika maeneo ya miji wakati wananchi wa kawaida wakikabiliwa na mafuriko mabondeni. 

Ilidaiwa wakati wa ujamaa kuwa sisi hatuwezi kuwa mabepari kwa sababu hatuna mtaji. Ukweli huu hadi leo upo pale pale, kilichobadilika ni kuwa wale waliokuwa wakiusema sana wamefunga midomo yao. Mpaka benki sasa inauzwa. Nchi inatawaliwa kwa sera kutoka kwa wale tulioambiwa kwamba wana sera za unyama, wanajali maendeleo ya vitu kuliko watu n.k. 

Leo baada ya miaka 37 ya uhuru Mtanzania anaweza akapigwa risasi na polisi katika mazingira ya chuki na ikawa basi na watawala wakasema jambo hili liko wazi na linafahamika. Leo baada ya miaka 37 ya uhuru wananchi wanachomewa nyumba zao na inakuwa basi. 

Leo baada ya miaka 37 ya uhuru Mtanzania anayeishi Dar es Salam (Tandika kwa mfano) analazimika kuishi gizani kwa kushindwa kumudu gharama za kufunga umeme katika nyumba yake. Mtoto wake haendi shule kwa vile hana shilingi 21,000 kwa ajili ya michango mbalimbali ili mwanaye aandikishwe shule ya msingi. 

Leo baada ya miaka 37 Printpak iko taabani, wafanyakazi hawajui pakwenda, serikali haioni hata haja ya kuhoji kulikoni! 

Leo baada ya miaka 37 ya uhuru Wakatamiwa Wasafa na Wandali kule Kilombero wanaishi maisha ya kama iliyokuwa Soweto, Afrika Kusini, kazi ngumu na mishahara duni yenye makato kibao! 

Leo baada ya miaka 37 ya uhuru mikoa ya Kigoma, Tabora, Singida, Lindi na Mtwara imetelekezwa, hakuna maendeleo, hali za wenyeji wake kimaisha za kusikitisha. Mpaka imefikia kujitangaza wao "sio wananchi wa nchi hii"! 

Leo baada ya miaka 37 upatikanaji wa maji ya matumizi nyumbani ni wa visimani. Hii ni katikati ya Jiji (mji mkuu wa nchi!) 

Leo baada ya miaka 37 wanachoweza wale tulowakabidhi dhamana nzito ni kusafiri huku na kule pasi na wananchi kufaidi matunda ya safari hizo. 

Baada ya miaka 37 ya uhuru wapo wananchi wanaoishi mitaani bila nyumba wala uhakika wa kula. Wanaishi wao na wake zao na watoto wao. 

Tuliambiwa pia kuwa ili tuendelee tunahitaji mambo manne: Watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. 

Miaka 37 baada ya uhuru imejitokeza haja ya kujiuliza tunahitaji watu wa aina gani? Ardhi ipo imewekwa na Mungu, viongozi na siasa katika mfumo wetu hapa nchini huwekwa na watu na hasa watu wa tabaka lile lenye wingi wa watu. 

Kwa bahati nzuri baadhi ya watu waliopigania uhuru huu uliotekwa nyara na wale waliopewa dhamana ya kuulinda bado wapo. Na pia ni bahati nzuri kuwa wengi wa Watanzania hawajafaidika ipasavyo na uhuru huu. Nasema ni bahati nzuri kwa sababu wakitaka nchi yao hakuna wa kuwazuia kwa vile wako wengi na sababu za kuitaka nchi yao wanazo. 

Msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi ni watu (wananchi) wanaojali utu wao. Wanaoheshimu haki za wengine na haki zao. Wananchi wasiopenda kudhulumu. Wananchi walio tayari kusimama kupinga dhuluma na kukataa kudhulumiwa. 

Tunachotakiwa kukifanya hivi sasa ni: Kuwaondoa wale walio warithi Wazungu katika kuendeleza sera za kuiba rasilimali ya taifa. 

Kuwaondoa wale waliopewa dhamana ya kuongoza na badala yake wakaamua kutawala na kujijengea himaya kama za kifalme katika nchi hii. 

Kuhakikisha ubaguzi unakomeshwa. Kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii zinatumika kwa faida ya wote. 

Mazingira yetu yanahitaji ukombozi kwa sababu wako watu wanaishi kama daraja la kwanza (first class) na wako watu wanaoishi kama wanyonge (lower class) katika Tanzania hii huru! 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani?

Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha

Serikali yagwaya kwa wafugaji nguruwe 
Na Muhibu Said

Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Na Maalim Mwalimu

Adabu katika swala

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Na Ally Said

Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya  (a.s.)
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe

Ijue SUA Madrasa Moro
Na Mussa Ally, Morogoro

Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli

Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha

Akina mama Muheza waungana kufanya Daawa
Na B. Mwakangwale

Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata uongozi
Na B.  Mwakangwale

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 2
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzima ni nyembamba,  waionao ni wachache - 2
Na Yasin Valerian Massawe

Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Jongo  aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki  A.

Waislamu Mlimba Moro mashakani
Na Q. Mataita

Sayansi na Teknolojia 
[Ielewe Modem yako] 
 
Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Futari ya Tende] 
 
Tangazo
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita