|
|
"LICHA ya kupigwa vita na wasomi kadhaa wa SUA Mazimbu Campus wakiwemo wasomi Waislamu, SUA Madrasat ikiwa na wanafunzi 50 hivi sasa imepita hatua moja mbele kuelekea kwenye kiini cha malengo yake". Hiyo ni kauli ya mwalimu Mohammed Abdallah Mazohanya Ustaadh wa Madrasa hiyo akilifamisha AN-NUUR hali halisi ya madrasa yake, Madrasat SUA Mazimbu Campas ilianzishwa mapema mwaka 1997 na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Morogoro kwa lengo la kutoa elimu ya msingi ya dini ya Kiislamu kwa wana watoto wa wafanyakazi wa chuo hicho na pembezoni mwake. Mazimbu Campas ilipo madrasa hiyo ni miongoni mwa sehemu chache za kitaaluma zenye wakazi wengi Waislamu mjini hapa, hivyo suala la kuwepo madrasa lilikuwa ni la lazima. Na hicho ndicho hasa kilichowapelekea wasomi hawa wa Kilimo kuanzisha shule hiyo. "Tulianza kwa taabu sana kutokana na wasomi wengi wa Kiislamu wenye fikra za kimagharibi kutuoona umuhimu wa watoto wao kufunzwa maarifa ya Kiislamu. Wanaona madrasa zanawaharibia masomo mengine ya shuleni watoto wao, hata hivyo mzee wetu Bw. Said Waziri Mbwana ametupatia darasa nyumbani kwake, tunamshukuru sana" alisema mwalimu Mohammed na kuongeza "kuna watoto wa familia tatu tu za wasomi wa hapa SUA, wengine wote wanatoka nje ya kambi, hili pia ni tatizo". Madrasa hiyo licha ya matatizo hayo inawafunza vijana hao wadogo maarifa ya Kiislamu, lugha ya Kiarabu, Kiswahili, Kuandika na wako mbioni kufunza lugha ya Kiingereza, Hisabati na Sayansi. Licha ya kuwa ina muda mfupi tangu kuasisiwa kwake, lakini wanafunzi wake wanaonyesha matumaini ya kufikia kwenye malengo. "Tunachohitaji ni ushirikiano mzuri na wazazi, hilo litatusaidia kutoka hapa tulipo na kufika pale tulipokusudia kwa mafanikio", alisema Mwalimu Mohamed. Mmoja wa wazazi na waasisi wa madrasa Dk. Ally Fungo ametoa mfano wa ushirikiano huo kwa kujitolea posho kwa mwalimu kila mwezi." Kuhusu suala la mtaala, mwalimu huyo alisema kuwa, mara kadhaa wamekuwa wakitumia mitaala ya nchi jirani ambayo mazingira yake ni tofauti kidogo na yetu, hivyo amefurahishwa sana kusikia habari njema ya mitaala mipya ya Kitanzania iliyoandaliwa na IPC kutolewa. "Lakini tunaisikia tu, bado hatujaipata wala kuiona katika maduka ya
vitabu. Tunaomba taasisi husika kutusambazia ‘silabasi’ hizo mapema iwezekanavyo
ili wakati usitiache nyuma", alimalizia kusema Mwalimu Mohamed Abdallah.
INASEMEKANA kwamba mwalimu aliyekuwa akifundisha dini kijijini Matui wilayani Kiteto amefukuzwa na hivyo kuwakosesha Waislamu darsa. Imeelezwa kwamba kufukuzwa kwa mwalimu huyo kumechochewa na baadhi ya watu wanaohisi wanaharibiwa biashara yao ya sihri na ramli kutokana na Waislamu wengi kuiva katika Tawhiid. Habari zaidi zimefahamisha kwamba, baada ya Waislamu wengi kuivishwa katika elimu ya Tawheed wamekuwa wakipinga mambo mengi ya shirki ambayo yalikuwa yamezoeleka kijijini hapo. Hali hiyo imeelezwa kwamba ndiyo iliyopelekea baadhi ya watu wasiotaka kuachana na jadi zao kujenga hoja kwamba Ustadh anafundisha kinyume na wao walivyosomeshwa zamani na Masheikh wao. Baadhi ya Waislamu waliongea na mwandishi wa habari hizi walisema kwamba mwenendo kama huo utapelekea Uislamu kuendelea kuwa kitu kigeni vijijini. Ustaadh Haruna J. Mdoe aliye miongoni mwa waathirika alisema kwamba si rahisi kumpata Sheikh kukubali kuishi kijijini ili awaelimishe watu. Kwa hiyo kufukuzwa kwa huyo ambaye tayari alikuwa amejitolea kuyakabili maisha ya kijijini ili Waislamu wanufaike na elimu yake ni dhahiri kutawakatisha tamaa hata wengine kuja. Ustaadh aliyefukuzwa ambaye hakupendelea jina lake litokee gazetini alisema kwamba yeye anaamini hakufanya lolote kinyume na Uislamu na pia taratibu za ufundishaji na hivyo anachofanya ni kuwasiliana na muajiri wake Ofisi ya Bakwata mkoa wa Arusha ili kujua hatma ya ajira yake. Kijiji cha Matui kina vitongoji sita ambavyo ni Azimio, Bwawani, Chapakazi, Juhudi, Kivukoni, Maweni na Soweto. Kijiji pekee chenye madrasa hivi sasa ni Azimio ambapo mamia ya watoto
husoma chini ya mwalimu mmoja tu Ustaadh Mohammed Kisisa.
Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha USTADHI mmoja (jina tunalihifadhi) anadaiwa kutoroka na mifuko 62 ya saruji ambayo ilitolewa na mfadhili mmoja kwa ajili ya ujenzi wa Madrasa ya Ngarenaro. Taarifa kutoka Msikiti Mkuu wa Ijumaa Ngarenaro zimeeleza kwamba Ustadh huyo alikabidhiwa mifuko hiyo 62 na mmoja wa wadhamini wa Msikiti huo lakini badala ya kuiwakilisha Msikitini akamuuzia mfanyabiashara mmoja kwa shilingi laki tatu. Ustadhi huyo ambaye pia ni mwalimu wa madrasa ya Msikiti huo, inasemekana ameiuza simenti hiyo kwa mfanyabiashara mmoja mwenye duka karibu na ofisi za Idara ya Maji Mkoa. Habari zaidi zimeeleza kwamba Ustadhi huyo alipohojiwa na uongozi wa Msikiti alikiri kosa na akaomba apewe watu wa kuandamana naye kwenda kuonyesha saruji hiyo ilipo. Hata hivyo, aliwatoroka watu aliofuatana nao walipofika maeneo ya Ol-Matejo na mpaka sasa hajulikani alipo. Sheikh na Imam Mkuu wa Msikiti wa Ngarenaro alipohojiwa na gazeti hili alikiri kuwepo kwa tukio hilo. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni suala hili lilikuwa halijafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa madai kwamba uongozi umempa muda mtuhumiwa ajirudi. |
YALIYOMO
Maoni Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani? Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha Serikali yagwaya kwa wafugaji
nguruwe
Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo:
Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Muhammad (s.a.w.) katika
Unabii wa Isaya (a.s.)
Ijue SUA Madrasa Moro
Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha Akina mama Muheza waungana kufanya
Daawa
Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata
uongozi
Je, hivi tuendelee kushika amri
za Mungu tena? - 2
Njia ya uzima ni nyembamba,
waionao ni wachache - 2
Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Sheikh Jongo aichachamalia
Uwawaru
Waamriwa kurejesha Mali ya
Mirathi
Waislamu Mlimba Moro mashakani
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|