|
|
| Adabu
katika swala
ALHAMDULILLAH. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu (sw.) kwa kutuwezesha kukamilisha toleo Nambari 1, linalohusu utaratibu unaofaa kuukaribisha mwezi wa Ramadhani. Katika toleo hilo tuliweza kuona kwa ufupi hekima aliyoikusudia Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kututunukia mwezi wa Ramadhani na kutulazimisha kufunga katika mwezi huo ili tuweze kumcha au kuwa na Taqwa. Pia tuliweza kuona mambo yanayofaa na yale yasiyofaa katika kujiandaa kwa funga ya Ramadhani. Inshaalah, katika toleo hili tutaiangalia nafasi ya swala katika Uislamu
na vipi itekelezwe. Pia tutaweza kuona jinsi nguzo ya swala inavyohusiana
na nguzo nynginezo za Uislamu. Na hatimaye tutatoa tathmini ya swala zetu
kwa kuiangalia swala ya Sunnah ya Taraweih inayoswaliwa katika mwezi wa
Ramadhani.
Nafasi wa swala katika Uislamu "Ibn Umar (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema Uislamu umejengewa juu ya nguzo tano: Kushuhudia kuwa hapana Mola ila Allah, na kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allah, Kusimamisha Swala, Kutoa zaka, kufunga Ramadhani na kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo". (Bukhari na Muslim) Katika Hadithi tuliyoirejea hapo juu, Mtume (s.a.w.) amesema: "Uislamu umejengwa juu ya nguto tano". Je, hii ina maana sawa na kusema Uislamu ni nguzo tano? Ama ni sawa na kusema kuwa Uislamu unakamilika kwa kutekeleza nguzo tano? Jawabu la swali hili ni kuwa, kuna mambo mengine ya ziada ya kutekeleza ili kukamilisha Uislamu mbali na nguzo tano. Hivyo, nguzo tano hapa zinakusudiwa kuwa ni nyenzo za kutuandaa ili tuweze kuutekeleza Uislamu wetu kwa ukamilifu. Yaani, tuweze kuutekeleza kwa masaa yote 24 ya kila siku katika maisha yetu. Nguzo tano ni sawa na taasisi ama vyuo ambamo mwanaadamu anaandaliwa ili akitoka nje ya vyuo hivi abakie kuwa ni mtumishi mwema kwa kuyafanyia kazi yale aliyojifunza vyuoni. Baada ya ufafanuzi huo, sasa tuiangalie nafasi ya swala katika nguzo tano za Uislamu. Swala imetajwa ya pili baada ya matamshi ya kushuhudia (yaani kukiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kuwa hapana Mola ila Allah na kuwa Muhammad ni Mtume wa Allah). Kwa maneno mengine ni kusema kuwa, swala inafuata mara tu baada ya mja kuwa na imani ya Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (s.a.w.). Mwenyezi Mungu (s.w.) amemueleza Nabii Muhammad (s.a.w.) kuwa: "Waambie waja wangu walioamini wasimamishe swala..." (Qur’an 14:31) Naye Mtume Muhammad (s.a.w.) akabainisha uzito wa kusimamisha swala katika hadith ifuatayo: "Swala ndiyo NGUZO KUBWA ya dini: Mwenye kusimamisha swala amesimamisha dini na mwenye kuvunja swala amevunja dini". Katika Hadith hii, tunaiona nafasi ya Swala miongoni mwa nguzo tano za Uislamu kuwa ndiyo NGUZO KUBWA ya dini. Hivyo, hatuwezi kutekeleza nguzo nyingine bila ya kusimamisha swala na tukawa ni wenye mafanikio; bali itakuwa ni kinyume chake kuwa ni wenye hasara. Hapa inafaa tuzingatie nukta muhimu katika funga yetu ya Ramadhani kuwa, wale wanaofunga Ramadhani bila ya kusimamisha swala, tusitarajie kupata malipo yoyote kwa funga zetu hizo bali ni sharti yote mawili tuyafanye sambamba. Bwana Mtume (s.a.w.) anaendelea kusema kuwa: "Swala ndio ufunguo wa kila kheri". Hadithi hii inatufahamisha kwamba, sharti la kupata malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ibada yoyote au wema wowote tuufanyao ni kama tutakuwa na ufunguo wa kuweza kuifungua kheri hiyo; yaani, ni kama tutakuwa tumesimamisha swala. Pia ametupa kipimo cha kumtambua Muislamu na asiyekuwa Muislamu kuwa si jina wala mavazi ya mtu bali ni kusimamisha swala pale alipoeleza kuwa: "Tofauti iliyopo kati yetu ( Waislamu) na wengine (wasiokuwa Waislamu) ni swala". (Ahmad, Abu Daud, An- Nisai, Tirmidh) Kama hii ndiyo nafasi ya swala katika Uislamu, je ni vipi tuitekeleze ili tuwe ni wenye kufaulu, yaani, ili tuweze kufunguliwa milago yote ya kheri tunayoikusudia na kupata yaliyomo ndani? Jawabu la swali hili ni kwamba tunachotakiwa ni kusimamisha swala. Kusimamisha swala ni tofauti na kuswali. Kusimamisha swala ni kuiswali swala kwa kufuata barabara sharti na nguzo zake zote; kunyenyekea na kuihudhurisha nafsi katika swala. Ukiacha moja katika haya utakuwa hujasimamisha swala bali utakuwa umeswali tu. Wenye kuswali tu bila ya kusimamisha swala wanaahidiwa kupata adhabu kali ya moto. "... Basi, adhabu (kali) itawathibitikia wanaoswali ambao wanapuuza swala zao (hawazisimamishi)". (Qur’an 107:4-5) Kupuuza swala ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo sharia za swala, nguzo za swala na kutokuwa na Khushui (unyenyekevu) wakati wa swala. Wale wenye kusimamisha swala wameahidiwa malipo makubwa ya pepo na wametangaziwa kufuzu kama anavyotufahamisha Mwenyezi Mungu (s.w.) pale aliposema: "Hakika wamefuzu waumini ambao katika swala zao ni wanyenyekevu... na ambao swala zao wanazihifadhi". (Qur’ani 23:-1-2, 9). Tathmini ya swala zetu Alhamdulillah.Kwa ufupi tumekwishaona nafasi ya swala katika Uislamu; hivyo ni jukumu letu kufanya tathmini ya kina katika swala zetu zote ziwe za faradhi ama za sunnah. Tukusudie/tuazimie kuzitekeleza ipasavyo ili tuweze kupata mafanikio yake. Tukifanya vinginevyo, tutakuwa ni wenye kuipuuza swala na hivyo kuwa ni wenye kuangamia. Tuzipime swala zetu kama zinatuepusha na mambo machafu ama bado tunaswali na huku tunayaelekea maovu. Allah (s.w.) ametupa kipimio pale aliposema: "Soma uliyoletewa Wahyi, Bila shaka Kitabu (hiki ulicholetewa) na usimamishe swala. Bila shaka swala (ikiswaliwa vilivyo) humzuilia (huyo mwenye kuswali na) mambo machafu na maovu, na kwa yakini ndani ya swala kuna kumkumbuka Mwenyezi Mungu kukubwa, na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda". (Qur’an 29:45) Swala ya Taraweih Katika swala nyingi za sunnah ya Tareweih watu tunaswali kwa haraka sana kiasi cha kushindwa kuutuliza mwili wote sehemu tunapopaswa kufanya hivyo. Baadhi ya Maamuma tunawatangulia Maimamu wetu katika vitendo ama tunakwenda sambamba nao. Baadhi ya Maimamu wetu wanasoma sura fupi fupi kwa haraka (kama vile Suratul-Ikhlasw) na kuwafanya maamuma/wanaowafuata washindwe kumaliza kuisoma Suratul-Fatiha. Hata pale zinaposomwa sura ndefu kwa lengo la kumaliza juzuu, zinasomwa kwa haraka haraka bila ya adabu. Baadhi yetu tunakwenda mbio mbio kukimbilia swala baada ya kuwa tumechelewa. Kwa kifupi ni kwamba, katika swala nyingi za Taraweih hakuna unyenyekevu isipokuwa tunadokoa dokoa tu nguzo mbalimbali katika swala nzima. Utaratibu wote huu wa kuswali tuliouorodhesha ni kuipuuza swala na hiini hatari kubwa sana kama tulivyokwisha kuona hapo awali. Kuhusu kutokujituliza katika swala mahala inapopasa, kutokukamilisha visomo vyetu, na kadhalika; matendo yanayosababishwa na kuswali mbio mbio, Bwana Mtume (s.a.w.) anatuonya katika Hadithi zifuatazo: "Mwizi mkubwa kabisa katika watu ni yule mwenye kuiba katika swala yake. Alipoulizwa; vipi mtu anaiba katika swala yake? Akajibu kuwa hatimizi rukuu wala sijida zake wala hatimizi kisomo chake katika swala hiyo" Abu Hurairah (r.a.) amemsikia Bwana Mtume (s.a.w.) akisema: "Mwenyezi Mungu hatamuangalia mtu ambaye hasimamishi uti wake wa mgongo baina ya rukui yake na sijida yake" (Imepokelewa na Imamu Ahmad) Seyyidna Abu Musa (r.a.) amesema: "Siku moja Bwana Mtume (s.a.w.) aliswali na Maswahaba zake, kisha akakaa. Basi, akaingia mtu Msikitini akasimama anaswali. Akawa anarukuu na anadonoa-donoa sijida yake. Kuona hivyo, Bwana Mtume (s.a.w.) akasema: (Mnamuona mtu huyu, lau kama atakufa basi atakufa nje ya Uislamu - yaani atakufa nje ya mila ya Muhammad (s.a.w.), anadonoa-donoa swala yake kama kunguru anavyodonoa kipande cha nyama?" Kuhusu kufuata sawa sawa na Imamu ama kumtangulia katika vitendo ndani ya swala, Bwana Mtume (s.a.w.) pia anatuonya katika Hadith zifuatazo: Seyyidna Anas (r.a.) amemsikia Bwana Mtume (s.a.w.) akisema: Enyi watu, mimi ni Imamu wenu. Hivyo, msinitangulie katika Rukui, wala katika sijida, wala katika kisimamo, wala katika kitako (cha At-tahiyyatu) na wala msinitangulie katika kutoa salamu. (Imepokelewa na Imamu Muslim) Pia amesema: "Je, haogopi mmoja wenu kunyanyua kichwa chake kabla ya Imamu, Mwenyezi Mungu kumgeuza kichwa chake, sura ya kichwa cha punda, au kuigeuza sura yake ikawa sura ya punda? Alhamdulillah. Haya ndiyo aliyotuwezesha Mwenyezi Mungu (s.w.) kuyafikisha kwenu katika toleo hilo la pili. Yaliyo muhimu miongoni mwa adabu za swala ni mengi hatuwezi kuyamaliza. Kheri ya kidogo chenye kuzingatiwa kuliko kingi kinachosahaulika. Inshaallah, katika toleo lijalo, tutaangalia kuhusu "Kuanza na Kwisha kwa Mwezi wa Ramadhani". Kwa maoni, maswali au mapendekezo, tafadhali tuandikie:
|
YALIYOMO
Maoni Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani? Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha Serikali yagwaya kwa wafugaji
nguruwe
Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo:
Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Muhammad (s.a.w.) katika
Unabii wa Isaya (a.s.)
Ijue SUA Madrasa Moro
Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha Akina mama Muheza waungana kufanya
Daawa
Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata
uongozi
Je, hivi tuendelee kushika amri
za Mungu tena? - 2
Njia ya uzima ni nyembamba,
waionao ni wachache - 2
Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Sheikh Jongo aichachamalia
Uwawaru
Waamriwa kurejesha Mali ya
Mirathi
Waislamu Mlimba Moro mashakani
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|