AN-NUUR 
Na.179 Shaaban  1419, Desemba 11 - 17, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: 

Batendi hakumuelewa Mkomidachi 

Na Ally Said 

KATIKA toleo Na. 177 Shaaban 1419 Novemba 27 - Desemba 2, 1998. Ndugu Elia Batendi bado hakumuelewa Ustaadh Mkomidachi kwa maelezo mazuri aliyotoa. 

Naomba nimjibu moja moja: Anasema Yesu ni Alfa na Omega Yoh 22:12-13 kama Yohana aliandika kwa ajili ya Uungu wa Yesu; Mungu katika kinywa cha Isaya anasema Isa 43:10-11 (BWANA) ni Mungu "Kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote; Omega; Baada - wala baada yangu mimi hatakuwepo mwingine. 

Na kama alimchukulia kama Mtume au Nabii; basi Mitume wengi wamepita kabla yake; Yesu alisema Mat 8:11 yaani akina Ibraimu, Isaka, Yakobo; pia kuna Musa, Elia, Ezekiel n.k. Omega pia Yesu alisema Mat 7:15-23 Mtawatambua kwa matunda yao yaani hao Manabii wajao. 

Na alisema Yn 16:7-14 Atakuja huyo Roho wa Kweli (sio Roho Mtakatifu) yaani Nabii wa kweli sio wa uwongo; Amekusudiwa mtu sio Mungu, malaika wala Roho ile ambyo ni utendaji wa kazi za Mungu ile aliyosema Yohana katika waraka wake wa kwanza 4:1 Zijaribuni kama zimetoka kwa Mungu. 

Anasema wakati wa Shahada tunamtaja Muhammad pekee. Ndiyo Mtume wa umma huu; pia Mitume iko 124000 kama utataja yote, sala itakuwa ndefu mno. 

Anasema kafara ya dunia: Sio kweli kwa Mtume wa Mungu awe ni kafara ya dhambi za watu. Soma Hos 6:6; Kumb 21:22-23; Eze 18:1-21, Kumb 24:16; pia Yesu anasema Mat 12:7, Mat 19:14 Wayahudi katika sheria. Yn 19:7 ambayo ndio ile katika Kumb 21:22-23. Na pia Yuda asingeitwa msaliti. 

Dhambi ya Asili: Rejea Kumb 24:16, Eze 18:1-21, Yer 31:29-30. 

Kulipiza kisasi: Soma Law 24:20; Qur Hud 11:126 sawa na Qur 5:45 lakini kusema Yesu katika Mat 5:46-47 ni sawa pia katika Qur 42:42 Maana kulipiza sio ubaya kama ulivyotendewa lakini kusamehe ni bora zaidi unapata thawabu kubwa. Yesu hakuja kuitengua Torati ndugu Elia bali kuitimiza haondoi hata yodi moja (Mat 5:17-20). 

Qur’an inategemea vitabu vya kale: Alitoa aya Yunus 10:37 pale Allah aliposema na, ni maelezo ya vitabu vilivyopita. Hiyo sio maana yake; hapo Allah anasema vilitiwa hitilafu nyingi na hao wafuasi wao, sasa katika Qur’an vinawekwa bayana vieleweke hivyo Qur 11:110; Yer 8:8 Injili Lk 1:1-3 soma tafadhali; Qur’an 18:1-2 maana pia ya Qur. 

Malaika kutomtii binadamu au Adamu: Mbona hukatai pale Yesu aliposema Mat 24:29-31 maana hata yeye ni mwana wa Adamu Lk 21:27. 

Mbinguni hakuna kuoa: Je! Adamu wakati anapewa Hawa awe mkewe alikuwa duniani au mbinguni? Soma Mwa 2:18-24; ndugu uelewe mke ni yule wa ndoa ndio maana mnatafsiri vibaya juu ya mti wa katikati, sio ule kama wengi mnavyodai bali ni mti katika miti ya peponi. 

Bali kuzaa ndio hakuna huko, ndio maana Adamu akaambiwa nendeni duniani mkazaane. Ndio maana ya kusudio la Mwenyezi Mungu tuzaane ili tumuabudu wengi na tuwatawale wanyama. Soma hiyo Mwa 2:24 utaona mke hapo, mke niyule wa ndoa. Labda tu uliza ndoa yake alitoa mahari gani? Na hiyo itahitaji muhadhara: Omba kibali ufahamishwe zaidi. 

Anasema kama Malaika anamtii Binadamu asingemkaba Mtume: Sio kama alimkaba bali ni kuminya na Mtume alikuwa akipewa elimu ambayo alikuwa hana, au ufahamu zaidi mbali na ule aliokuwa nao mdogo ili aweze kuongoza watu. Maarifa yalizidi kila alipokuwa anaminywa na Jibril. Soma Isa 28:9-11 na Isa 29:12 halafu utaona historia ya Mtume linganisha. 



Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya (a.s.) 

Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe 

KITABU cha Nabii Isaya (a.s.) ni kitabu pekee chenye maelezo kamili ya wazi kuhusu dini ya Kiislamu bila kuhitajia kuunganishwa na rejea za vitabu vingine. Baada ya kuona utabiri wa Nabii Isaya (a.s.) juu ya kuibuka kwa kuwa dini ya Kiislamu yenyewe (rejea makala yangu "utabiri sahihi wa kuibuka kwa Uislamu katika AN-NUUR Na. 171 Uk. 14 la Oktoba 16-22, 1998) hapa nakamilisha unabii wa Uislamu kwa rejea zinazomhusu Mtume Muhammad (s.a.w.) ndani ya kitabu hicho hicho cha Nabii Isaya (a.s.) 

Katika kitabu hicho, nabii Isaya (a.s.) amemtabiri mtu mmoja atakaye kuwa mtukufu kuliko watu wote. Wanatheolojia wanamwita mtu huyo "mtumishi wa Bwana". Mtu huyo anayo maelezo ambayo wanatheolojia wameyaita "nyimbo nne za mtumishi wa Bwana". 

Hapa nitanukuu "nyimbo" zote nne ili kuona kama zinafafanana na sifa za Mtume Muhammad (s.a.w.). Kwa kuwa maelezo ya "nyimbo" hizo yako wazi sana, nitafafanua pale tu penye ulazima wa kufanya hivyo. 

 

Wimbo wa kwanza: 

"Tazama Mtumishi nimtegemeaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njiaa kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hautazima, atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia wala hatakata tamaa hata atakapoweka hukumu duniani, na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu BWANA anena, Yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda; Yeye aliyetandaza nchi na mazao yake; Yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; Yeye awapaye roho wao waendao ndani yake. Mimi, BWANA, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa, kuyafunua macho ya vipofu (wapagani), kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa (yaani kuwakomboa watu na sheria za kibinadamu). Mimi ni BWANA ndilo jina langu, na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake". (Isaya 1-9) 

Wimbo wa pili 

"Nisikilizeni, enyi visiwa, tegeni masikio yenu tumboni, toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri, naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; akaniambia; wewe u mtumishi wangu, Israel, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa BWANA asema hivi; Yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimlete Yakobo tena na Israel wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya BWANA na Mungu wangu amekuza nguvu zangu). Naam, asema hivi, ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo na kuwarejeza watu wa Israel waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nikutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata mwisho wa dunia". (Isaya 49:1-6). Katika "wimbo" huu, neno "Israel" katika aya ya tatu halimo katika unabii wa asili (original), limewekwa na waandishi wa baadaye. 

  

Wimbo wa tatu 

"Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao (wanatheolojia), nipate kujua jinsi ya kumtegemea kwa maneno yake aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi, huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; na nami aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala. Ni nani miongoni mwenu amchaye BWANA, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la BWANA, na kumtegemea Mungu wake. Tazama, ninyi mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge, endeni ninyi katika mwali wa moto wenu, na katikati ya mienge mlioiwasha, mtayapata haya kwa mkono wangu, mtalala kwa huzuni." (Isaya 50:4-11). 

Wimbo huu unaonyesha kuwa, mtumishi huyo wa Mwenyezi Mungu hana elimu yoyote ya kidini (theolojia) wala ya kawaida (aya 4-5). Hili linasisitizwa na maneno yafuatayo: "Sikilizeni, enyi viziwi, tazameni, enyi vipofu mpate kuona. Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? AU aliye kiziwi, kama mjumbe wangu, nimtumaye? Nani kipofu kama mtumishi wa BWANA". (Isaya 42:18-19). 

Angalia pia Isaya 29:11-14. Aidha anaishi katika mazingira ya kipagani yaani "giza" (aya ya 10) katika ya aya 11 onyo kwa wasomi wa kidini (wanatheolojia) na wataalamu wengine (wawashao moto), kuwa atawafedhehesha kwa elimu yake kubwa ajabu . Kwa ufafaunzi zaidi wa hili soma pia Luka 10:21, 1Kor 1:18-19. 

Muujiza huu mkubwa wa uongozi bora na mafanikio makubwa bila elimu, umewashangaza hata wasomi wasio Waislamu wa karne hii. Mmoja wa wasomi hao, Bwana Maurice Guadefroy - emonyness katika kitabu chake "Muslim Institutions", London, 1950, ukurasa 20, anasema: "Muhammad was a Prophet, not a theologian, a fact so evident that one is loathe to state it. The men who surrounded him and constituted the influantial elite of the primitive Muslim community, contended themselves with obeying the that he had prochaimed in the name of Allah and with following his teaching and example. They had a simple, robust faith that was satified with a small number of formulae and a few rites". 

Wimbo wa nne 

"Tazama mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyostaajabia. (uso wake ulikuwa umeharibikiwa sana zaidi ya mtu yeyote, na umbo lake zaidi ya wanaadamu). Ndivyo atakakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu". (Isaya 52:13-15). 

Wimbo huu unaonyesha kuwa mtu huyo atakuzwa sana kuliko watu wote. Aidha dola (falme) zitasalimu amri kwake. "Wafalme watamfumbia vinywa vyao". (aya ya 15) 

Tukiangalia "nyimbo" hizo, na kulinganisha na sifa za Mtume Muhammad (s.a.w.), inatudhihirishia wazi kuwa, "mtumishi wa Bwana", ni Mtume Muhammad (s.a.w.). Aidha tukiunganisha unabii huu wa Nabii Isaya (a.s.) na utabiri wa Nabii Yesu (a.s.) uhusuo kuja kwa Parakletos (Roho Mtakatifu) katika Yohana 16:7-13, tunaona kuwa Muhammad (s.a.w.) ndiye nabii aliyeitwa na Wayahudi "Nabii yule" (tazama Yohana 1:19-25) aliyetabiriwa na nabii Musa (a.s.) kama ifuatavyo: "BWANA akaniambia, wametenda wema kusema walivyosema. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa NDUGU ZAO (sio miongoni mwao Wayahudi wenyewe) mfano wako wewe (Musa) nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu (Bi-ismi-llah), nitalitaka kwake (nitamwadhibu vikali)" (Kumbukumbu la Torati 18:17-19) 

Namalizia kwa aya ya Qur’an ifuatayo: "Sema (Ewe Nabii Muhamamd): Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote; (Mungu) ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi, hapana aabudiwaye (kwa haki) ila Yeye; Yeye ndiye ahuishaye na ndiye afishaye. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake aliye Nabii Ummy (asiyejua kusoma na wala kuandika) ambaye huamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na Mfuateni Yeye ili Mpate Kuongoka". (Qur. 7:158). 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani?

Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha

Serikali yagwaya kwa wafugaji nguruwe 
Na Muhibu Said

Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Na. Abu Halima Sachangwa

Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Na Maalim Mwalimu

Adabu katika swala

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo: Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Na Ally Said

Muhammad (s.a.w.) katika Unabii wa Isaya  (a.s.)
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa, Korogwe

Ijue SUA Madrasa Moro
Na Mussa Ally, Morogoro

Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli

Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha

Akina mama Muheza waungana kufanya Daawa
Na B. Mwakangwale

Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata uongozi
Na B.  Mwakangwale

Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? - 2
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

Njia ya uzima ni nyembamba,  waionao ni wachache - 2
Na Yasin Valerian Massawe

Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Jongo  aichachamalia Uwawaru
Na Badru Kimwaga

Waamriwa kurejesha Mali ya Mirathi
Na Njuki  A.

Waislamu Mlimba Moro mashakani
Na Q. Mataita

Sayansi na Teknolojia 
[Ielewe Modem yako] 
 
Mafundisho ya Quran

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Futari ya Tende] 
 
Tangazo
Vitabu na Mihutasari ya Maarifa ya Uislamu
 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita