|
|
| Maoni
Waislamu tunakusudiwa kufanywa
watumwa wa nani?
KWA kipindi kirefu sasa Waislamu wameshuhudia kamata kamata ya viongozi wao wa dini kwa visingizio mbalimbali. Waislamu wasingekuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi kama kamata kamata hiyo ingekuwa inafanyika pale ambapo vyombo husika vimeona lipo kosa au zipo sababu za msingi za kujenga tuhuma. Lakini aliyekuwa akifuatilia kamata kamata hii toka mwaka 1993 atakuwa amegundua kwamba imekuwepo kawaida ya kuvumisha uzushi ili kujenga dhana kwamba lipo jambo zito katika jamii linalohitaji kuchukuliwa hatua nzito na za haraka. Uvumi huo huzungukwa na vishindo vyenye kujenga hoja ya kufanya ubaya ambao utatafsiriwa kama hatua za lazima zipasazo kuchukuliwa ili kupambana na wanaodaiwa kuwa ni wahalifu. Mwaka 1993 Waziri wa seirkali ambaye ana mtandao wa vyombo vyenye kumpa habari sahihi za hali ya nchi; aliibuka na madai kwamba wapo watu wameingiza masanduku makubwa makubwa ya silaha. Vyombo vya habari vikazipokea tarifa hizi kwa kuzipigia zumari. Sambamba na madai hayo ikajengwa hoja kwamba wapo Masheikh wenye malengo ya kisiasa, wanaotumiwa na watu wa nje kuhatarisha amani ya nchi. Ikadaiwa kwamba wengine hutumia Misikti na dini huku wakiendesha biashara za madawa ya kulevya. Uzushi huu baada ya kupambwa sana na vyombo vya habari ulipelekea Masheikh wengi na Waislamu wengine kukamatwa; baadhi ya taasisi za Kiislamu kufutwa; na Masheikh wa kigeni kadhaa kufukuzwa nchini kwa kishindo. Masheikh waliishia rumande kwa miezi kadhaa, wengine wakatoka jela wakiwa dhaifu kiafya na kufa muda mfupi baadaye. Mpaka leo serikali haijatoa ushahidi wowote wa kuthibitisha kuingizwa kwa silaha hizo nchini kama ilivyodaiwa na Waziri wake, na wala haijaona umuhimu wa kuwataka radhi Waislamu juu ya uzushi huo uliopeleka madhila makubwa katika jamii yao. Kana kwamba serikali imeruhusu kujengeka kwa utamaduni maalum wa kuwazushia fitna Waislamu, lilipotokea janga la Shauritanga baadhi ya Wabunge waliowahi kushika nyadhifa kubwa serikalini hawakuwa mbali kupeleka Bungeni utamaduni huu wa uzushi dhidi ya Waislamu. Mbunge huyo hakuona vibaya kusimama Bungeni na kutoa kauli zilizoashiria kuwazushia Waislamu kuhusika na janga lile. Linalotia khofu Bunge lilikaa kimya kuhusu tuhuma hizo na wala serikali haikusema lolote, utadhani mwelekeo huu wa kuwazushia Waislamu majanga ndio mwelekeo rasmi wa serikali. Katika hali inayoelekea kuimarika utamaduni huu wa kuwazushia Waislamu majanga, katika kipindi hicho hicho, Waziri wa serikali akaja tena na fitna kwamba walikuwepo Waislamu wanaovinjari na mabomu ndani ya hijabu zao kwa lengo la kulipua Makanisa na taasisi zake. Historia ya ulimwengu inashuhudia kwamba wakati mwingine watu wenye chuki binafsi dhidi ya raia wengine kama ilivyokuwa kwa Hitler na Wayahudi huweza kuzusha fitna kwa lengo la kuhalalisha maangamizi dhidi ya raia wenziwao. Leo inajulikana kuwa madai ya Hitler dhidi ya Wayahudi yalikuwa ni uzushi mtupu. Lakini uzushi huu ulileta maangamizi makubwa. Tunajua kuwa serikali yetu inavyo vyombo vyake vya upelelezi. Kwa kuuacha uzushi huu dhidi ya Waislamu kuenea, lipi linalokusudiwa? Katika tukio la Mwembechai, uzushi ulisukwa, ikapatikana sababu ya kutumwa jeshi la polisi lenye silaha kuvamia Msikiti kwa kishindo kikubwa. Msikiti ukavunjwa, watu walipigwa mabomu ya machozi, ambayo yawaathiri watu wengi na baadhi ya watoto kufariki dunia, baadhi ya Waislamu wakauliwa kwa kupigwa risasi, watu zaidi ya 200 wakakamatwa wakiwemo wanawake miongoni mwao vikongwe ambao walipigwa, waliteswa, walinyanyaswa na kudhalilishwa. Miongoni mwa walioteswa rumande walikuwemo wagonjwa walionyimwa haki ya kupata matibabu. Baadhi ya wagonjwa hao walifia rumande. Waislamu na baadhi ya wananchi wakiwemo Wabunge wameitaka serikali iunde tume kuchunguza mauaji ya Mwembechai. Hilo halijafanywa. Isipokuwa kilichofanyika ni Waziri Mkuu kutoa kauli Bungeni ya kupongeza yale yaliyofanywa na polisi Mwembechai. Katika mlolongo huu wa uzushi na dhulma dhidi ya Waislamu, yupo mtoto wa shule mkazi wa Mwembechai aliyepigwa risasi wakati akielekea nyumbani kwao. Mtoto huyo Chuki Athumani kapewa kilema cha maisha. Katika hali inayopelekea kuhalalisha dhulma hii, Waziri wa serikali alidai tena Bungeni kwamba mtoto yule alipigwa risasi kwa sababu alikuwa kabeba makaratasi ya uchochezi. Hadi leo Waziri hajawafahamisha wananchi kama mtoto yule aliyekuwa akipita njia; askari polisi walimpiga risasi ili wajue kama ya uchochezi au walimpekua kwanza anayomakaratasi wakayaona ndipo wakampiga risasi? Hivi serikali haioni kuwa hali hii inaweza kupelekea Waislamu kuanza kuamini kwamba kuandamwa huku kuna kusudio la kuwaangamiza? Miongoni mwa Masheikh waliokamatwa mara tu baada ya tukio la Mwembechai na kuteseka jela bila kuhukumiwa ni Sheikh Juma Mbukuzi. Baadhi ya Masheikh walioteseka jela pamoja na Sheikh Mbukuzi na wakatoka wakiwa na hali mbaya kiafya, Mwenyezi Mungu ameshawachukua. Lakini Sheikh Juma Mbukuzi bado anaendelea kukamatwa kamatwa mara kwa mara kwa madai mbalimbali. Kuandamwa kwa Sheikh Mbukuzi kunaonyesha sura ile ile ya jinsi Waislamu na viongozi wao wanavyoandamwa kwa uzushi. Moja ya visingizio vinavyotumiwa kujenga uzushi dhidi ya Waislamu ni hiki cha kulinda amani na utulivu. Kimsingi miongoni mwa wanaohatarisha amani na utulivu ni wazushi wa mambo mazito kama haya tuliyoyataja. Katika tukio la Mwembechai, yuko Paroko anayejulikana ambaye uzushi wake ulipelekea fitna ya Mwembechai. Uzushi huo uliungwa mkono na kuchochewa zaidi na radio moja ya kidini na kudakiwa na baadhi ya magazeti. Hatuamini kuwa serikali haiwajui wazushi hao. Lakini hatuoni hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Hali inayopelekea kudhihirisha kuwepo kwa mambo mahususi dhidi ya Waislamu, ambao pia kuna dalili zinazoonyesha kuwa yapo Makanisa yanayoujua na hivyo kuushadidia. Hivi karibuni kiongozi mkubwa wa Kanisa moja amekuwa akipita sehemu mbalimbali nchini akitoa matamshi ya kichochezi yenye lengo la kuishinikiza serikali iendelee kuwadhalilisha Waislamu. Katika matamshi yake amekuwa akidai kwamba Waislamu waliodhulumiwa Mwembechai ni wahuni na yaliyowakuta ni stahiki yao. Serikali inayodai kuwa inataka kuhakikisha amani na utulivu nchini na kisha serikali hiyo hiyo ikamwachia mtu wa aina hii kueneza uchochezi huu nchi nzima inataka wananchi na hasa Waislamu waelewe vipi? Hatudhani kwamba serikali hii inataka kuwafanya baadhi ya raia katika nchi hii wajihisi kuwa ni watumwa katika nchi yao. Mwaka 1781 meli ya Uingereza ilikuwa imebeba watumwa kuelekea Amerika. Katikati ya bahari ya Atlantiki nahodha akaona kwamba akiba ya chakula na maji haitatosha hadi kufika. Akaamuru watumwa 133 watoswe baharini. Baadaye baadhi ya watumwa waliochukizwa na unyama huo walifungua kesi ya mauaji dhidi ya nahodha yule. Jaji katika kesi hiyo akadai kwamba sana sana muhusika anaweza kuchekwa tu kwamba kaharibu mali yake (watumwa), lakini sio kumtia hatiani kwamba kaua. Meli ni yake, watumwa ni wake na chakula kilikuwa chake. Hiyo ilikuwa ndio hali ya madhalimu walioanzisha biashara ya utumwa. Baadhi ya watu walidhani dunia hii ni haki yao peke yao na wana uwezo wa kumiliki hata roho za wengine, waziangamize wazitakazo na kuziacha hai wazitakazo kwa maslahi yao. Leo mwaka 1998 katika nchi huru yenye katiba inayotoa haki ya uhai kwa watu wote; nchi yenye raia wasio kuwa utumwani, nchi inayotawaliwa na serikali inayochaguliwa na wananchi katika zama ambazo kampeni kubwa hufanywa kutetea haki za binadamu; watu wameuliwa, hata kesi zao kufikishwa mahakamani inaonekana haijuzu! Watumwa wale walitoswa baharini ili kupunguza idadi ya watumwa ilingane na chakula kilichopo, Hawa waliouliwa kwa amri ya "piga yule" nao tatizo lilikuwa nini? Mbona hatuelezwi? Kinyume chake ni akina Sheikh Mbukuzi kukamatwa kila leo. Mbona hatuelezwi? Kinyume chake tunaona ni wanasiasa na viongozi wa Kanisa kujenga fungamano la kudai wale ni wahuni, wanatumiwa kisiasa n.k. Leo mwaka 1998 Waislamu wanapigwa risasi na kuuliwa hadharani licha ya kuwepo katiba na sheria zinazolinda haki za raia wote, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Waislamu katika nchi hii ni watu wa nani? Nahodha yule aliwatosa watumwa mwaka 1781 angalau alifikishwa mahakamani. Waliouwa Mwembechai mwaka 1998 katika Tanzania huru badala ya kufikishwa mahakamani na kujibu mashitaka ya mauaji wanatetewa na kupongezwa nje ya mahakama. Waislamu wa Tanzania ni watumwa wa aina gani? Serikari yetu inadai kuwa inafuata utawala wa haki na sheria. Muislamu Abu Azizi kamwandikia mwanasheria mkuu wa serikali kumtaka achukue hatua za haki na kisheria kuhusu suala la Mwembechai kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi. Mwanasheria mkuu mpaka leo hajajibu wala kuchukua hatua zozote. Hata
waheshimiwa Majaji ambao ni walinzi wa sheria hizo hatujawasikia kuhusu
waliouliwa Mwembechai. Lakini tumelisikia karipio lao alipouliwa mbwa "Immigration"
japo hawakuombwa rasmi. Na juzi hapa tumeambiwa kwamba dereva mmoja kapewa
nishani baada ya kupata ajali na kufa akimkwepa mbwa. Je! Serikali na vyombo
vyake inataka Waislamu wajihisi vipi katika nchi hii? Na wakishapata hisia
hiyo iwe nini? Haya yote yanafanywa kwa maslahi ya nani?
|
YALIYOMO
Maoni Waislamu tunakusudiwa kufanywa watumwa wa nani? Wananchi waingiwa na hofu kuhusu silaha Serikali yagwaya kwa wafugaji
nguruwe
Hakuna njama za kupindua Bakwata - Sheikh Yahya MARADHI YA KISAIKOLOJIA:: VOYEURISM
Tathmini: Miaka 37 ya uhuru wa Tanganyika
Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo:
Batendi hakumuelewa Mkomidachi
Muhammad (s.a.w.) katika
Unabii wa Isaya (a.s.)
Ijue SUA Madrasa Moro
Kiteto wakosa darsa kwa kupinga Ramli Ustadh ayeyuka na saruji ya Msikiti mjini Arusha Akina mama Muheza waungana kufanya
Daawa
Wanafunzi Waislamu Mbeya wapata
uongozi
Je, hivi tuendelee kushika amri
za Mungu tena? - 2
Njia ya uzima ni nyembamba,
waionao ni wachache - 2
Waandishi andikeni ukweli - Kamati
Sheikh Jongo aichachamalia
Uwawaru
Waamriwa kurejesha Mali ya
Mirathi
Waislamu Mlimba Moro mashakani
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|