|
|
|
UTANGULIZI
Sababu za kutaka kuunganisha kompyuta mbili au zaidi zipo nyingi. Kwa mfano unaweza kuwa na haja ya kuyafanya majalada au mafaili yaliyo kwenye kompyuta moja yaweze kusomeka kutoka kwenye kompyuta nyengine. Au unaweza kuwa unayo printa moja tu uliyoiunganisha na moja kati ya kompyuta zilizopo lakini ukataka kompyuta zaidi ya moja ziweze kuitumia printa hiyo. Au pia, unaweza kuwa unayo line moja tu ya simu uliyoiunganisha na moja kati ya kompyuta zilizopo, kompyuta ambayo ndio pekee yenye modem, lakini ukataka kompyuta nyengine ziweze kuitumia line hiyo hiyo ya simu na modem hiyo hiyo moja. Ukiwa na haja zilizoelezwa hapo juu, hapana shaka utahitaji kuziunganisha kompyuta zako kwa njia fulani. Sehemu tatu za mwanzo za makala hii zimejishughulisha zaidi na njia za kutimiza haja ya kuweza kuyasoma majalada ya kompyuta moja kutoka kwenye kompyuta nyengine. Lakini njia hizo hazitafaa kutimiza haja ya kuweza kutumia printa au modem iliyounganishwa na kompyuta moja wakati ukiwa unatumia kompyuta nyengine. Kwa haja kama hizo utahitaji njia maalum ya kuziunganisha kompyuta zako ili kwa pamoja ziweze kufanya kitu kinachoitwa Local Area Network, au kwa ufupi "LAN". LAN ziko za aina kadhaa, lakini katika makala hii tutaelezea jinsi ya kuziunganisha kompyuta zinazotumia Windows 95 (au Windows 98), kufanya aina ya LAN inayojuilikana kama "peer-to-peer", yaani kiungo kati ya kompyuta ya kawaida na kompyuta nyengine ya kawaida (PC-to-PC), na sio LAN ya kuunganisha kompyuta za kawaida na server. Kama unataka kuziunganisha kompyuta (PC) ili zifanye LAN, na moja kati
ya kompyuta hizo unataka iwe server ya kuzihudumia kompyuta nyengine,
basi kwenye hiyo kompyuta itakayofanya kazi kama server utahitaji
kutumia programu-mama ya utando (network operating system) kama
vile Linux, Windows NT au Novell Netware. LAN ya namna
hiyo hatutaizungumza kwenye makala hii. LAN ya aina ya peer-to-peer
inaweza kufanywa kirahisi kwa kutumia kompyuta zenye Windows 95
au Windows 98 kwani programu-mama (operating system) hizo
tayari zinao uwezo wa kutengeneza LAN za namna hiyo.
VIFAA VINAVYOHITAJIKA Kifaa muhimu kinachohitajika kuziunganisha kompyuta kufanya LAN ni kadi ya utando , kwa Kiingereza, "network interface card" (NIC). Kila kompyuta itahitaji kuwa na NIC yake. ![]() NIC pia zinatafautiana kwa aina za nyaya zinazoweza kuchomekewa. Kuna
ambazo zinaweza kutumika pamoja na nyaya za aina ya UTP (Unshielded
Twisted Pair) zenye plagi za aina ya RJ-45 (Registered Jack 45)
, na ziko nyengine ambazo zimetengenezwa kutumika pamoja na nyaya za aina
ya coax (yaani coaxial cable) zenye kiungo (connector)
cha aina ya BNC (Bayonet Nut Connector). Waya huu wa coax
unafanana na ule unaotumika pamoja na TV lakini tafauti yao ni kuwa waya
wa coax unaotumika kwenye LAN ni wa 50 ohms wa aina ya RG-58,
wakati ule unaotumika pamoja na TV ni wa 75 ohms. Hizo 50 ohms
na 75 ohms ni za kipimo maalum cha waya kinachoitwa kwa Kiingereza
"characteristic impedance". Kwa hivyo, characteristic impedance
ya waya unaotumika kwenye LAN ni 50 ohms.
Lakini watu wengi wanapendelea kutumia nyaya za aina ya UTP zenye plagi za RJ-45 kama zinacvyoonekana kwenye Picha 2, kwa vile ni rahisi kuzitumia. Waya wa aina ya UTP una jozi mbili za nyaya ndani yake – jozi moja kwa kupelekea data na ya pili kwa kupokelea data. Waya huo unaitwa "twisted pair" kwa vile jozi za waya zilizomo ndani yake zimezongwa pamoja kwa mtindo maalum ili zisiweze kuathirika na umeme ulio kwenye anga unaotoka kwenye vyanzo mbali mbali kama vile vifaa vya elektroniki na hata radi. Nyaya hizo unaweza kuzitumia kuunganishia kompyuta kwa masafa yasiyozidi mita 100 kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa. Ukitumia waya wa coax utahitaji pia kuwa na viungo vya "T" (yaani T-junction) kadhaa kutegemeana na idadi ya kompyuta ulizonazo, na pia utahitaji kuchomeka "50 ohm coaxial terminator" kwenye kila sehemu ya T-junction iliyokuwa haikuungwa na chochote. Huo ni udhia kidogo na ndio maana watu wengi wakapendelea waya za UTP zenye plagi za aina ya RJ-45. Lakini waya za coax zinakuruhusu kuunga kompyuta zako kwenye masafa marefu zaidi, ambayo yanaweza kufikia mpaka mita 185. Lakini masafa kati ya kompyuta mbili zilizoungwa kwa kutumia waya wa coax hayatakiwi kuwa chini ya nusu mita kwa mujibu wa viwango vilivyokubalika. NIC za aina ya 10Base-T, ambazo ni maarufu zaidi, zinaweza kupeleka au kupokea data kwa kasi ya juu ya 10 Mbps (megabits per second), yaani bit ("0" au "1") milioni 10 kwa sekunde moja! Hiyo ni kasi kubwa sana, lakini zipo NIC za aina ya 10/100Base-T zenye uwezo wa kupeleka au kupokea data kwa kasi ya juu ya 10 Mbps na pia 100 Mbps. Kama LAN ina kompyuta chache tu, NIC za aina ya 10Base-T zinatosha kukidhi haja. 10Base-T hasa ni aina moja ya LAN zinazotumia njia ya mawasiliano inayojuilikana kama Ethernet. Kwenye neno 10Base-T , "10" inamanisha "10 Mbits/sec" ambayo ni kasi ya juu ya data inayohimiliwa kwenye LAN ya aina hiyo, "Base" inawakilisha neno "Baseband" ambao ni mtindo wa kusafirisha data unaotumiwa na LAN ya aina ya Ethernet, mtindo ambao ni data za aina ya Ethernet pekee zinazosafirishwa. Herufi "T" inamaanisha "Twisted-pair", ambao ni aina ya waya unaotumiwa kwenye LAN za aina hiyo – LAN hizo zinajuilikana kama Twisted-pair Ethernet. Aina ya waya inaelekeza juu ya masafa ya juu yanayoweza kutumiwa pamoja na waya huo. Kama tulivyoeleza kabla masafa hayo ni mita 100 kwa waya wa aina ya Twisted-pair. LAN zinazotumia nyaya nyembamba za aina ya coax, zinajuilikana kama Thin Ethernet na hizo hujuilikana kama 10Base-2. Hiyo "2" ukizidisha mara 100 inakupa masafa ya juu yanayoweza kutumika kuungnaisha kompyuta kwenye LAN inayotumia nyaya za namna hiyo. Kwa 10Base-2 masafa hayo ni mita 200, lakini hayo ni makisio tu, masafa halisi ni mita 185 kama ilivyoelezwa kabla. LAN za aina ya 10Base-5 zinazotumia waya mnene wa aina ya coax, zinajuilikana kama Thick Ethernet, na zinaweza kutanda kwenye masafa marefu ya wastani wa mita 500. Ukihitaji kutengeneza LAN kuunganisha kompyuta mbili tu, utakachokihitaji ni NIC mbili na waya maalum unaojuilikana kama "crossover cable". Waya huo upo wa urefu mbali mbali mpaka futi 25 na bei yake ni kama US$10. Unaweza pia kutumia waya wa aina ya coax kama NIC zako zina kiungo cha aina ya BNC. Ukihitaji kutengeneza LAN kuunganisha kompyuta zaidi ya mbili, utahitaji nyaya za kawaida za LAN za aina ya Category 5 10Base-T, (bei yake ni wastani wa US$15 kwa urefu wa futi 25), na kifaa kinachoitwa "network hub" au "concentrator" au "repeater". Hicho ni kifaa ambacho kinatumika kuziunga pamoja nyaya za LAN zinazotoka kwenye kompyuta mbali mbali kufanya mtindo wa kuunganisha kompyuta kwenye LAN unaoitwa "star network". Kwa mfano, ukiwa na "hub" yenye "port" nne za aina ya RJ-45, utaweza kuziunganisha pamoja kwa mtindo wa star, kompyuta nne zilizoko kwenye LAN yako. Hub nazo ziko za kasi ya 10 Mbps na pia 100 Mbps. Hub ya 10 Mbps yenye port nne unaweza kuinunua kwa bei ya kama US$50 au zaidi kidogo; na yenye port nane bei yake ni kama US$70 hivi. Hub za kasi ya 100 Mbps bila shaka ni ghali zaidi, kama US$100 kwa hub yenye port nne. Mara nyingi, wanaotengeneza NIC ndio hao hao wanaotengeneza hub. Watengenezaji maarufu ni pamoja na 3COM, Asante, Compex, D-Link, SMC, Intel, na Bay Networks. Kuna baadhi ya makampuni yanauza vifaa vya LAN kamili kamili (LAN kit) kwa pamoja. Unaweza kununua LAN kit yenye NIC mbili za aina ya ISA, waya wa aina ya UTP wenye plagi za RJ-45, hub ya port nne, diskette zenye programu na driver zote zinazohitajika, pamoja na kitabu chenye maelezo kamili ya kutengeneza LAN kwa kutumia vifaa hivyo. LAN kit ya namna hiyo bei yake ni nafuu sana, kama US$120. Baada ya kuelewa vifaa vinavyohitajika, kwenye sehemu inayofuatia tutaelezea namna ya kuitayarisha LAN yenyewe. Inaendelea toleo lijalo |
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|