AN-NUUR  Na.174 Rajab 1419, Novemba 6 - 12, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Tafuteni ufalme wa kisiasa
 

HII ni makala yangu ya kwanza katika AN-NUUR. Inshaallah penye majaaliwa nakusudia kuendelea kuandika makala nyingine nyingi tu hapo siku zijazo. Wakati huu niandikapo, mimi ni Rais wa Baraza la Waislamu wa Tanzania waishio Marekani jijini Washington DC. Hali ambayo inanifanya nilazimike hapa hapa mwanzoni nifafanue kwa uwazi kuwa mawazo yote yaliyomo katika makala hii ni ya kwangu mimi mwenyewe binafsi na wala hayahusiani na Baraza hilo. Kufikiri, kuamua, kusema na kutenda ni haki yangu niliyozaliwa nayo. Ni uhuru wangu wa kuyafanya hayo unaolindwa na katiba siyo tu nchini mwangu bali na nchi zingine zote duniani zenye mfumo wa kidemokrasia ya kweli, ili muradi nisiwe nimevunja sheria zilizopo. Katika msingi huo huo, wasomaji nao wanayo haki sawa ya kukubaliana na kutokubaliana na fikra hizi. 

Nafurahi na kupongeza mwamko wa Waislamu nchini na nje ya Tanzania. Naona pia kuwa Waislamu tuna matatizo, malalamiko, masikitiko na maonevu. Kosa lililojitokeza kwangu ni kuwa wale tunaowategemea kutuondolea majanga yanayotufika wameyafungia macho na kuyatilia pamba masikioni. Ili muradi tunapuuzwa, tunadharauliwa na kunyanyaswa kama vile sisi ni raia wa daraja la pili nchini mwetu wenyewe. Hivi tutaendelea na hali hii mpaka lini? Wahenga walisema; "Aliyelala usimuamshe, ukimuamsha, utalala wewe." 

Wakoloni walituamsha Waafrika barani Afrika na matokeo yake kila mmoja anayajua, walizikunja bendera zao moja baada ya nyingine. Historia, kwa hakika, hujirudia yenyewe! 

Ni aibu na fedheha kubwa mtu kuwa omba omba nchini mwake mwenyewe, hasa ukijitambua kuwa uko huru na kuwa ati una serikali yako mwenyewe. Kila uchao tunapigishwa magoti kuiomba serikali itupe haki zetu. Haki za kuhubiri na kuhadhiri, haki za kuabudu bila kuingiliwa misikitini, haki za kulindiwa usalama wa maisha yetu na mali zetu bila ya kupigwa au kuuawa na ati askari zetu wenyewe, haki za kutofungwa mahabusini bila ya dhamana tukingojea uchunguzi usiokwisha, haki za kutochomewa nyumba zetu ziitwazo vidungu, haki ya kutopata mgao wa vyeo na madaraka unaowiana na idadi yetu katika chama tulichokianzisha wenyewe na serikali tuliyoidai wenyewe katika harakati za ukombozi wa nchi yetu kutoka kwa wakoloni. Ikumbukwe kuwa nchi hii haikukombolewa na juhudi za mtu mmoja kama inavyonadiwa. Mmoja huwa kiongozi na wengine huwa ni mwili. Na kiongozi hawezi kamwe kuwa mzuri kama hana wafuasi wazuri.Uzuri wa kiongozi ndio uzuri wa wanaoongozwa. Juhudi za kiongozi haziwi juhudi kama hakuna juhudi za wafuasi. 

Mlolongo wa haki za Waislamu tunazodhulumiwa ni mrefu mno kiasi kwamba unaweza kulijaza hili gazeti lote na kusaza.Ili muradi tafrani kem kem. 

Napenda hapa niwakumbushe Waislamu maneno ya Al Haj Marehemu Kighoma Ali Malima (Allah Subhanahu Wataala, amuweke miongoni mwa walio wema peponi Amin!), alisema; "Mtu haki yake haiombi, mtu haki yeke huichukua." Leo na mimi nasema, "swadakta!" Na wakati wa Waislamu kuichukua haki yetu ni hivi sasa. 

Kabla sijaendelea napenda tutahadhari sana wakati tunapoichukua haki yetu tusichukue na haki za wenzetu, tukifanya hivyo tutakuwa tumekwenda kinyume na maadili ya mafunzo ya Uislamu. Matokeo yake yatakuwa kuipa mwanya Historia ijirudie yenyewe kama CCM na Serikali yake ilivyotoa na inavyotoa mwanya katika miaka hii 37 ya utawala wake. 

Tunaambiwa tunapouona uchafu, ima tuuondowe kwa mikono yetu au tuukemee. Na tunaposhindwa kuyafanya hayo, basi tunune. Haya yanaonekana kama ni mambo matatu, lakini ukitafakari utaona kuwa hapa tunaambiwa jambo moja tu, nalo ni kuwa tutumie akili zetu kuepukana na uchafu huo. 

Kukubali kupuuzwa ni uchafu, kukubali kudharauliwa ni uchafu na kukubali kunyanyaswa pia ni uchafu wa hali ya juu. Si haya haya ndiyo yaliyotufanya tukamwambia mkoloni kuwa "sasa basi?" Kwa kuwa tumekwisha kukubaliana kuwa Historia hujirudia yenyewe, kinachotufanya tuseme leo maneno hayo hayo ni nini? Hakuna jambo chafu zaidi ya kukubali kukaa na uchafu bila ya kuchukua hatua kabambe za kuuondoa uchafu huo. 

Baba wa Taifa la Waafrika Weusi, aliyeikomboa Ghana (Gold Coast) kutoka kwa wakoloni na kuhamasisha ukombozi wa Afrika nzima, mwanaume wa kwanza aliyeuona na kuutetea mwanga wa muungano na umoja wa Afrika yote, Marehemu Kwame Nkrumah, alituambia, "Tafuteni kwanza UFALME wa KISIASA na falme nyingine zote zitafuata." Ukweli wa maneno yake leo uko wazi kwetu sisi Waislamu wa Tanzania. Ingawa wengi wetu ndio walioanzisha TAA, iliyomzaa TANU na kumjukuu CCM. Tulipoziachia tu hatamu za UFALME wa KISIASA, matokeo yake si tunayaona? Imekuwa sisi tulioanzisha harakatri za ukombozi wa Tanganyika, hatuwezi kupata mgao wa vyeo uwiano na idadi yetu, chamani wala serikali bado tuko nyuma. Kama hivi si vituko basi imekuwa mauzauza! Maneno haya hatukuambiwa sisi sote kwa pamoja na mkoloni wakati tukiudai uhuru wetu? Leo wenzetu mmetuacha saa ngapi? Hii siyo kuwa Historia inajirudia yenyewe? 

Hivi hawa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Mawaziri na Wasaidizi wao na wale wengine wote watufanyiao kazi za aina hizo wamesomea nini? Kwa kiwango gani? Na wanamzidi nani na nani? 

Hali hii inaonyesha kuwa iko haja kubwa kwa Waislamu kuzitafuta na kuzishikilia imara hatamu za UFALME wa KISIASA. Ni katika hali hiyo tu ndio tutaweza kupata haki sawa ndani ya vyama vyetu, ndani ya serikali yetu na pia nchini mwetu kwa jumla. Katika hali hiyo, hatutapuuzwa tena, hatutanyanyaswa tena na wala hatutadharauliwa kamwe! 

Tulipoupata uhuru wetu (kama tuliupata kweli), nilidhani kuwa tumeupata "ufalme wa kisiasa", lakini kumbe bado, maana kama tungeupata, falme zingine zingefuata, tungekuwa na flame za elimu, falme za uchumi na kadhalika, hasa baada ya miaka 37 ya utawala wetu wenyewe. Naona kuna njama za kutuhujumu, Nafurahi kuwa tumezigundua na kuzisitukia. 

Ndugu zangu Waislamu, nasema tena, kuna haja kubwa sana ya kuzikamata hatamu za kisiasa, aminini msiamini, zikwideni kanzu zenu na akina mama fungeni vibwebwe vyenu tuingie kazini. Hatuwezi kupata haki zetu kwa kupiga magoti na kuomba, au kwa kupiga kelele nyingi na kulia kwa mayowe, au kwa kuandika makala ndefu kama hii ya kwangu hapa. Tutumie akili zetu kwa kushirikiana na kushikamana tukapata KURA YA PAMOJA katika chaguzi. Najua sana kuwa hiyo ni kazi kubwa na nzito, tena ngumu mno. Lakini sote si tunajua kuwa hakuna kizuri kinachopatikana kwa urahisi? 

Hata hesabu zikigangwa kiasi gani, ukweli utabaki pale pale, sisi siku zote tuko wengi kuliko wengine wote nchini. Kinachokosekana ni umoja na ushirikiano. Tunasahau kuwa utengano ndio msingi wa udhaifu wetu hivi sasa. Katika hali ya utengano, tutapuuzwa mwanzo hadi mwisho, tena siku zote, daim kaim. Wakati ni huu! 

  

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI  
Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha 

Serikali yakumbushwa kujiunga OIC 
Na Mwandishi wetu 

Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi 

Wafungwa waomba Futari na Vikoi 

Macho ya shutuma 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Hoja pofu 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Tafuteni ufalme wa kisiasa 

Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 

'Vichupi' vya nini Kimiti? 
Na. Said Rajab 

Mjadala wa Katiba na haki za Waislamu 
Na Masoud Mohammed Mbogo 

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 3 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Waliochukuliwa utumwa Uarabuni 
Na Hassan Omar 

Madrasatul Maamury Islamiya 

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4) 
Na Hassan Omar 

Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito 

TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' 

Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa  

Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza 

Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga 

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa 

Barua za wasomaji  

Masomo ya dini ya Kiislam  

Chakula na lishe 

Mashairi 

Matangazo 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita