|
|
|
WAKATI Waislamu wakizidi kulalamika kwamba wanakandamizwa na serikali ya awamu ya tatu kwa kunyimwa haki yao ya kikatiba ya kuabudu na kutangaza dini yao kwa uhuru. Mjadala wa Katiba umechukua sura mpya hapa nchini. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imetoa msimamo ambao kwa watu wenye mapenzi na demokrasia ya kweli wanauona siyo tu kwamba ni kielelezo cha dalili za utawala wa Kiimla bali pia ni kielelezo potovu juu ya maana ya Katiba. Kwa kuamua kutumia njia ya Waraka maalum (White Paper) kufanya marekebisho ya Katiba, serikali ya CCM ina lengo la kuwachagulia wananchi njia ya kurekebisha Katiba na hivyo kuufanya msimamo wa wale wanaotaka Katiba Mpya kufa kifo cha mende au wahaini. Kitu kimoja ni muhimu kuzingatiwa. Haya yote yanayotokea hivi sasa ni athari za muda mrefu za Chama kushika hatamu ambapo kiongozi wa chama na serikali (Practically) alikuwa siku zote juu ya Katiba na Katiba ilifuatwa pale ilipokubaliana na maslahi ya chama na serikali. Itakumbukwa pia kwamba Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 haikutokana na matakwa ya wananchi bali matakwa ya Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa chama na serikali. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 ambao pia ulizaliwa na fikra za Mwalimu Nyerere na Karume unasemekana kuwa ndiyo msingi mkuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977. Jambo la kushangaza ni kwamba mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa mwaka 1964 na Constituent Assembly Act ya 1964 ambazo ndizo zilizotowa nguvu za kisheria za kuwepo Katiba ya mpito (Interim constitution) ya 1965 na hatimaye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 pia zinaonekana kutawaliwa na fikra za Nyerere na Karume kuliko mtu yeyote. Katika mambo yaliyosaidia kwa serikali ya Tanzania kukubalika licha ya kutowashirikisha wananchi katika utengenezaji wa Katiba ni pamoja na nadharia ya siasa ya ujamaa na kujitegemea, umoja wa kitaifa, chama kushika hatamu, na kubwa zaidi ni sehemu kubwa ya wananchi kutokuwa na elimu ya Katiba hata kidogo. Hivi sasa wakati tunaingia katika mfumo wa siasa ya vyama vingi, mambo mengi yamejitokeza. Utawala wa Mwalimu Nyerere ulifikia ukingoni mwaka 1985 na Ali Hassan Mwinyi akashika usukani. Kiongozi huyu wa awamu ya pili tofauti na aliyemtangulia alijitahidi kuthamini utawala wa kisheria na kuheshimu haki za binadamu. Ni bahati nzuri sana kwamba mapema alipoingia madarakani (Bill of Rights) iliyoingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1984 ikaanza kutekelezwa rasmi mwaka 1985. "Bill of Rights" kimsingi ni nyaraka ya kisheria inayoorodhesha haki za msingi za binadamu na kuzipa nguvu za kisheria. Inapoingizwa katika Katiba inapewa hadhi ya juu kabisa katika sheria zote za nchi. Ni nukta ya muhimu kukumbuka kwamba Bill of Rights ilianzwa kuingizwa katika Katiba mpya ya Zanzibar mwaka 1984 kabla haijaingizwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Iwe itakavyokuwa, suala la kuingizwa Bill of Rights katika Katiba ya upande mmoja wa Jamhuri, lilifanya suala la kuingizwa sheria hiyo katika Katiba ya Muungano kuwa lisiloepukika. Kana kwamba haitoshi, utawala wa Mwinyi uliipelekea Tanzania katika Biashara Huria ambayo imesaidia sana kufunua mawazo ya wananchi. Vyombo vya mawasiliano vya kisasa vimekuwa vingi sana kiasi kwamba wananchi wanaweza kujionea kwa urahisi mambo yanayotokea sehemu nyingine duniani. Vile vile hali ya kimaisha kwa ujumla ilianza kuwa nzuri kiasi kwamba badala ya kukaa na kufikiria kesho utakula nini au badala ya kulala mapema ili kesho uwahi foleni ya unga wa mhogo (mkembe), mtu unawaza kufikiria siasa za nchi. Vyama vingi vya siasa vimeundwa, mashirika mengi yasiyo ya kiserikali nayo yameundwa yote haya yamechangia kuwaamsha wananchi kutoka katika usingizi mzito wa blanketi la ujamaa chini ya sera za Nyerere. Mpaka tunaingia katika awamu ya karne ya sayansi na teknolojia, historia inaanza kujirudia kidogo kidogo huku kwa upande mwingine watu wanazidi kuamka kidogo kidogo. Kwa upande mwingine jamii ya Kiislamu hapa nchini haikuonekana kuyapapatikia sana mageuzi ya kisiasa kama ilivyokuwa kwa watu wa dini nyingine ambako ibada zilitawaliwa na kampeni za kisiasa. Hata hivyo, kadiri serikali inavyoonyesha kutojali utawala wa kikatiba na kuheshimu matakwa ya watawaliwa ndivyo jamii ya Kiislamu inavyozidi kuona umuhimu wa kushirikiana na wenzao wa dini zingine katika kuleta mabadiliko kwa ajili ya maslahi ya Waislamu ambao wanaonekana kuwa raia wa daraja la chini. Matukio kama Waislamu kupigwa mabomu hadi Msikitini, Polisi kuingia Msikitini na viatu, binti zao na mama zao kudhalilishwa, kuzuiliwa kuhubiri dini kwa amani, upendeleo katika uteuzi wa Bodi mbalimbali mfano Parole na wananchi kuchomewa nyumba zao, yanatoa picha sahihi juu ya hali hii na hali ya baadaye. Katika serikali nyingi duniani ushahidi umeonyesha kuwa pale serikali inapoamua kujitafutia uhalali kwa njia ya mabavu bila kuheshimu matakwa ya watawaliwa mwisho wake huwa ni matatizo ya kisiasa. Mfano mzuri ni Algeria ambako wananchi wengi kwa kutumia njia za Kikatiba walionyesha mapenzi yao kutaka kutawaliwa na chama cha FIS lakini serikali kwa kuangalia maslahi yake ikafanya dhulma, matokeo yake yalikuwa machafuko ya kisiasa pia angalia Zaire na Kenya. Hivi sasa sehemu kubwa ya Watanzania wanataka Katiba Mpya na serikali haina haki ya kisheria kuwalazimisha kukubali kutumia njia ya White Paper kwani kifungu cha 8(1)(a) cha Katiba ya Jamhuri kinasema kuwa wananchi ndiyo msingi wa utawala. Serikali kama inataka kujihakikishia uhalali wake ni lazima Katiba Mpya iwepo ambayo itatungwa kwa kuwashirikisha wananchi wote kutokana katika vikundi mbalimbali vya kijamii, vyama vya kisiasa na viongozi wa kidini. Viongozi kutoa kauli za kimantiki zilizojengwa kwa premisiya lemavu
kwamba eti "White Paper" ni zao la serikali na serikali ni zao la wananchi
kwa hiyo "White Paper" ni zao la wananchi, huu ni uchokozi na msiba wa
kisiasa.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|